Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SURA YA 115

Pasaka ya Mwisho ya Yesu Yakaribia

Pasaka ya Mwisho ya Yesu Yakaribia

MATHAYO 26:1-5, 14-19 MARKO 14:1, 2, 10-16 LUKA 22:1-13

  • YUDA ISKARIOTE ALIPWA ILI AMSALITI YESU

  • MITUME WAWILI WAFANYA MATAYARISHO YA PASAKA

Akiwa kwenye Mlima wa Mizeituni, Yesu anamaliza kuwafundisha wale mitume wanne na kujibu swali lao kuhusu kuwapo kwake wakati ujao na umalizio wa mfumo wa mambo.

Nisani 11 imekuwa siku yenye shughuli nyingi sana! Huenda wakiwa wanarudi Bethania ili kulala huko, Yesu anawaambia mitume wake hivi: “Mnajua kwamba baada ya siku mbili kutakuwa na Pasaka, naye Mwana wa binadamu atatolewa ili auawe kwenye mti.”—Mathayo 26:2.

Inaonekana Yesu anatumia siku inayofuata, yaani, Jumatano, pamoja na mitume wake tu. Siku ya Jumanne, alikuwa amewakemea viongozi wa kidini na kufunua uovu wao hadharani. Wanataka kumuua. Kwa hiyo, hajionyeshi waziwazi Nisani 12 ili chochote kisimzuie kusherehekea Pasaka pamoja na mitume wake baada ya jua kutua jioni ya siku inayofuata, Nisani 14 inapoanza.

Lakini wakuu wa makuhani na wanaume wazee wa watu wana shughuli nyingi kabla ya Pasaka. Wanakusanyika katika ua wa kuhani mkuu, Kayafa. Kwa nini? Wamekasirika kwa sababu Yesu amekuwa akifunua matendo yao. Sasa wanapanga njama pamoja “ili kumkamata Yesu kwa hila na kumuua.” Watafanya hivyo wakati gani na jinsi gani? Wanasema: “Si kwenye sherehe, ili watu wasifanye ghasia.” (Mathayo 26:4, 5) Wanaogopa kwa sababu watu wengi wanampenda Yesu.

Wakati huohuo, viongozi hao wa kidini wanapata mgeni. Wanashangaa kuona kwamba ni Yuda Iskariote, mmoja wa mitume wa Yesu. Shetani amepanda ndani yake wazo la kumsaliti Bwana wake! Yuda anawauliza: “Mtanipa nini ili nimsaliti kwenu?” (Mathayo 26:15) Wanafurahishwa sana na jambo hilo, nao ‘wanakubaliana kumpa fedha.’ (Luka 22:5) Kiasi gani?  Wanakubaliana kumpa vipande 30 vya fedha. Kumbuka kwamba bei ya mtumwa ni shekeli 30. (Kutoka 21:32) Hivyo, viongozi wa kidini wanaonyesha jinsi wanavyomdharau Yesu, kwamba ana thamani ndogo. Sasa Yuda anaanza “kutafuta nafasi nzuri ya kumsaliti kwao bila umati kuwapo.”—Luka 22:6.

Nisani 13 inaanza Jumatano jua linapotua, na huu ndio usiku wa sita na wa mwisho ambao Yesu analala Bethania. Siku inayofuata, matayarisho ya mwisho yatahitaji kufanywa kwa ajili ya Pasaka. Wanahitaji kumpata mwanakondoo ili wamchinje na kumchoma akiwa mzima baada ya Nisani 14 kuanza. Watakula mlo huo wapi, na ni nani atakayeutayarisha? Yesu hajawaambia habari hizo. Basi, Yuda hawezi kuwajulisha wakuu wa makuhani.

Inaonekana kwamba mapema Alhamisi alasiri, Yesu anawatuma Petro na Yohana akiwa Bethania, akisema: “Nendeni mkatutayarishie Pasaka tule.” Wanamuuliza: “Unataka tuitayarishe wapi?” Yesu anawaeleza: “Mtakapoingia jijini, mtakutana na mwanamume akiwa amebeba mtungi wa maji. Mfuateni mwingie katika nyumba atakayoingia. Mwambieni mwenye nyumba hiyo, ‘Mwalimu anasema: “Kiko wapi chumba cha wageni ambamo ninaweza kula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu?”’ Mtu huyo atawaonyesha chumba kikubwa cha juu chenye vifaa. Tayarisheni humo.”—Luka 22:8-12.

Bila shaka, mwenye nyumba hiyo ni mwanafunzi wa Yesu. Huenda anatarajia kwamba Yesu ataomba kutumia nyumba yake kwa ajili ya sherehe hiyo. Mitume hao wawili wanapofika Yerusalemu, wanapata kila kitu kama Yesu alivyowaambia. Basi wanahakikisha kwamba mwanakondoo yuko tayari, na kwamba matayarisho mengine kwa ajili ya mlo wa Pasaka yamekamilika na yatawatosha watu 13—Yesu na mitume wake 12.