Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SURA YA 101

Mlo Katika Nyumba ya Simoni Huko Bethania

Mlo Katika Nyumba ya Simoni Huko Bethania

MATHAYO 26:6-13 MARKO 14:3-9 YOHANA 11:55–12:11

  • YESU ARUDI BETHANIA, KARIBU NA YERUSALEMU

  • MARIA AMMIMINIA YESU MAFUTA YENYE MARASHI

Yesu anaondoka Yeriko na kuelekea Bethania. Safari hiyo inahusisha kupanda mwinuko wa kilomita 20, akipita sehemu ambazo si rahisi kupitia. Mji wa Yeriko uko karibu mita 250 chini ya usawa wa bahari, nacho kijiji cha Bethania kiko karibu mita 610 juu ya usawa wa bahari. Lazaro na dada zake wawili wanaishi katika kijiji kidogo cha Bethania kilicho karibu kilomita 3 kutoka Yerusalemu, kwenye mteremko wa upande wa mashariki wa Mlima wa Mizeituni.

Tayari Wayahudi wengi wamefika Yerusalemu kwa ajili ya Pasaka. Wamefika mapema ili “wajitakase kisherehe” iwapo wamegusa maiti au kitu kingine kinachofanya wasiwe safi. (Yohana 11:55; Hesabu 9:6-10) Baadhi ya wale wanaofika mapema wanakusanyika hekaluni. Wanaulizana ikiwa Yesu atakuja kwenye Pasaka au la.—Yohana 11:56.

Watu wanabishana sana kumhusu Yesu. Baadhi ya viongozi wa kidini wanataka kumkamata ili wamuue. Hata wametoa maagizo kwamba yeyote akijua mahali alipo Yesu, awajulishe “ili wamkamate.” (Yohana 11:57) Tayari viongozi hao walijaribu kumuua Yesu alipomfufua Lazaro. (Yohana 11:49-53) Inaeleweka kwa nini wengine wanatilia shaka iwapo Yesu atajitokeza hadharani.

Yesu anawasili Bethania Ijumaa, “siku sita kabla ya Pasaka.” (Yohana 12:1) Siku mpya (Sabato, Nisani 8) inaanza jua linapotua. Kwa hiyo, amemaliza safari kabla ya Sabato. Hangeweza kusafiri kutoka Yeriko siku ya Sabato—kuanzia jua linapotua Ijumaa hadi jua linapotua Jumamosi—kwa sababu sheria ya Wayahudi inakataza kusafiri wakati huo. Inaelekea Yesu anaenda nyumbani kwa Lazaro, kama alivyofanya pindi nyingine.

Simoni ambaye pia anaishi Bethania anamwalika Yesu na wenzake, kutia ndani Lazaro, kwa ajili ya mlo Jumamosi jioni. Simoni anaitwa “mwenye ukoma” labda kwa sababu alikuwa na ukoma mwanzoni naye Yesu akamponya. Kama kawaida yake, Martha anaonyesha bidii kwa kuwahudumia wageni. Maria anamkazia fikira hasa Yesu, pindi hii anafanya hivyo kwa njia inayotokeza mabishano.

Maria anafungua chupa ya alabasta ambayo ina “ratili moja ya mafuta yenye marashi, nardo halisi.” (Yohana 12:3) Mafuta hayo ni yenye thamani sana, thamani yake (dinari 300) ni sawa na mshahara wa mwaka mzima! Maria anamimina mafuta juu ya kichwa na miguu ya Yesu kisha anaifuta kwa nywele zake. Harufu ya marashi inajaa nyumba nzima.

Wanafunzi wanakasirika na kuuliza: “Kwa nini mafuta haya ya marashi yapotezwe bure?” (Marko 14:4) Yuda Iskariote anauliza: “Kwa nini mafuta haya yenye marashi hayangeuzwa  kwa dinari 300 na maskini wapewe pesa hizo?” (Yohana 12:5) Kwa kweli, si kwamba Yuda anawahangaikia maskini. Amekuwa akiiba pesa kutoka kwenye sanduku la pesa analotunza kwa ajili ya wanafunzi.

Yesu anamtetea Maria, akisema: “Kwa nini mnataka kumsumbua mwanamke huyu? Amenitendea jambo jema. Kwa maana maskini mnao sikuzote, lakini mimi hamtakuwa nami sikuzote. Alipomimina mafuta haya yenye marashi kwenye mwili wangu, alifanya hivyo ili kunitayarisha kwa ajili ya mazishi. Kwa kweli ninawaambia, popote ambapo hii habari njema itahubiriwa ulimwenguni, jambo alilofanya mwanamke huyu litatajwa pia ili kumkumbuka.”—Mathayo 26:10-13.

Yesu amekuwa Bethania kwa zaidi ya siku moja, na habari zinaenea kwamba yuko katika eneo hilo. Wayahudi wengi wanakuja nyumbani kwa Simoni si kumwona Yesu tu bali pia kumwona Lazaro “aliyekuwa amefufuliwa kutoka kwa wafu.” (Yohana 12:9) Sasa wakuu wa makuhani wanapanga njama ili kumuua Yesu na pia Lazaro. Viongozi hao wa kidini wanahisi kwamba watu wengi wanamwamini Yesu kwa sababu Lazaro yuko hai tena. Viongozi hao wa kidini ni waovu sana!