Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SURA YA 58

Afanya Mikate Iongezeke Kimuujiza na Kuonya Kuhusu Chachu

Afanya Mikate Iongezeke Kimuujiza na Kuonya Kuhusu Chachu

MATHAYO 15:32–16:12 MARKO 8:1-21

  • YESU ALISHA WANAUME 4,000

  • AONYA KUHUSU CHACHU YA MAFARISAYO

Umati mkubwa umemjia Yesu katika eneo la Dekapoli, mashariki ya Bahari ya Galilaya. Wamekuja kumsikiliza na kuponywa, pia wamekuja na vikapu vikubwa vya chakula.

Hata hivyo, baada ya muda Yesu anawaambia wanafunzi wake: “Ninausikitikia umati, kwa sababu tayari wamekaa pamoja nami siku tatu nao hawana chakula. Nikiwaacha waende nyumbani wakiwa na njaa, watazimia njiani, na baadhi yao wametoka mbali.” Wanafunzi wanauliza: “Tutapata wapi mikate ya kuwatosha watu hawa mahali hapa pasipo na watu?”—Marko 8:2-4.

Yesu anauliza: “Mna mikate mingapi?” Wanafunzi wanajibu: “Saba, na samaki wachache wadogo.” (Mathayo 15:34) Kisha Yesu anawaambia watu waketi chini. Anachukua ile mikate na samaki, anasali kwa Mungu na kuwapa wanafunzi wake waigawe. Ajabu ni kwamba, wote wanakula na kushiba. Mikate inayobaki inapokusanywa inajaza vikapu saba vikubwa, hata ingawa wanaume 4,000 hivi na pia wanawake na watoto wamekula!

Baada ya kuuaga umati, Yesu na wanafunzi wake wanavuka kwa mashua kwenda Magadani, ufuo wa magharibi wa Bahari ya Galilaya. Akiwa hapo, Mafarisayo na baadhi ya wale wa dhehebu la Masadukayo wanamjaribu Yesu, wanamwomba awaonyeshe ishara kutoka mbinguni.

Akitambua mawazo yao, Yesu anawajibu: “Inapofika jioni ninyi husema, ‘Hali ya hewa itakuwa nzuri kwa maana anga ni jekundu,’ na asubuhi mnasema: ‘Leo kutakuwa na baridi kali na mvua, kwa maana anga ni jekundu na lina mawingu mazito.’ Mnajua jinsi ya kufafanua hali ya anga, lakini hamwezi kufafanua ishara za nyakati.” (Mathayo 16:2, 3) Kisha Yesu anawaambia Mafarisayo na Masadukayo kwamba hawatapewa ishara yoyote isipokuwa ishara ya Yona.

Yesu na wanafunzi wake wanapanda mashua na kuelekea Bethsaida kwenye ufuo wa kaskazini mashariki wa bahari. Wakiwa safarini wanafunzi wanagundua kwamba wamesahau kubeba mikate ya kutosha. Wana mkate mmoja tu. Anapokumbuka jinsi ambavyo hivi karibuni alikabiliana na Mafarisayo na Masadukayo ambao ni wafuasi wa Herode, Yesu anaonya hivi: “Endeleeni kuwa macho; jihadharini na chachu ya Mafarisayo na ya Herode.” Wanafunzi wanafikiri kimakosa kuwa anapotaja chachu anamaanisha kwamba wamesahau mikate. Anapotambua wamekosea, Yesu anasema: “Kwa nini mnabishana kuhusu kutokuwa na mikate?”—Marko 8:15-17.

Hivi karibuni Yesu aliandaa mikate kwa ajili maelfu ya watu. Basi wanafunzi wanapaswa kujua kwamba Yesu hazungumzii mkate halisi. “Je hamkumbuki nilipoimega ile mikate mitano kwa  ajili ya wale wanaume 5,000, mlikusanya vipande vilivyobaki mkajaza vikapu vingapi?” Wanajibu: “Kumi na viwili.” Yesu anaendelea kusema: “Nilipoimega ile mikate saba kwa ajili ya wale wanaume 4,000, mlikusanya vipande vilivyobaki mkajaza vikapu vikubwa vingapi?” Wanajibu: “Saba.”—Marko 8:18-20.

Yesu anauliza: “Kwa nini hamwelewi kwamba sikuongea nanyi kuhusu mikate?” Anaongezea hivi: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”—Mathayo 16:11.

Mwishowe wanafunzi wanaelewa. Chachu hutumiwa kuchachisha na kufanya mkate uumuke. Yesu anatumia chachu kumaanisha upotovu. Anawaonya wanafunzi wake wajihadhari na “mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo,” ambayo yamepotoka.—Mathayo 16:12.