Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SURA YA 46

Aponywa kwa Kugusa Vazi la Yesu

Aponywa kwa Kugusa Vazi la Yesu

MATHAYO 9:18-22 MARKO 5:21-34 LUKA 8:40-48

  • MWANAMKE APONYWA KWA KUGUSA VAZI LA YESU

Habari kwamba Yesu amerudi kutoka Dekapoli zinaenea miongoni mwa Wayahudi wanaoishi katika ufuo wa kaskazini magharibi wa Bahari ya Galilaya. Inawezekana wengi wamesikia kwamba wakati wa dhoruba ya hivi karibuni, Yesu alituliza upepo na maji, na huenda wengine wanajua kwamba aliwaponya wale watu waliokuwa na roho waovu. Kwa hiyo, “umati mkubwa” unakusanyika kando ya bahari, huenda ni katika eneo la Kapernaumu, ili kumkaribisha Yesu. (Marko 5:21) Anapofika kwenye ufuo, wanamtarajia kwa hamu.

Miongoni mwa watu wanaotamani kumwona Yesu ni Yairo, msimamizi wa sinagogi, labda ni sinagogi la Kapernaumu. Anaanguka miguuni pa Yesu na kumsihi tena na tena: “Binti yangu mdogo ni mgonjwa sana. Tafadhali njoo uweke mikono yako juu yake ili apone na kuishi.” (Marko 5:23) Yesu ataitikiaje ombi la Yairo la kumsaidia binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka 12 na anayempenda sana?—Luka 8:42.

Yesu akiwa njiani kuelekea nyumbani kwa Yairo, anakabiliana na tukio lingine linalogusa hisia. Watu wengi walioandamana na Yesu wamesisimka, wanajiuliza ikiwa watamwona akifanya muujiza mwingine. Hata hivyo, mwanamke fulani katika umati anakazia fikira hali yake mbaya ya kiafya.

Mwanamke huyu Myahudi amekuwa na ugonjwa wa kutokwa na damu kwa miaka 12. Ametafuta msaada kutoka kwa madaktari mbalimbali, akitumia pesa zake zote katika matibabu waliyopendekeza. Lakini hajapona. Badala yake, hali yake ‘imezidi kuwa mbaya.’—Marko 5:26.

Huenda unaelewa kwamba mbali na ugonjwa wake kumdhoofisha, unamwaibisha na kumfedhehesha. Kwa kawaida mtu hazungumzii tatizo kama hilo hadharani. Isitoshe, chini ya Sheria ya Musa, kutokwa na damu kulimfanya mwanamke asiwe safi kisherehe. Yeyote anayemgusa mwanamke huyo au mavazi yake yenye damu anapaswa kuoga na hatakuwa safi hadi jioni.—Mambo ya Walawi 15:25-27.

Mwanamke huyu ‘amesikia habari kuhusu Yesu,’ na sasa anamtamfuta. Kwa kuwa yeye si safi, anapita katikati ya umati kimyakimya, akijiambia: “Nikiyagusa tu mavazi yake ya nje, nitapona.” Anapogusa upindo wa vazi la Yesu, mara moja anahisi kwamba damu imeacha kutiririka! “Amepona ule ugonjwa mbaya.”—Marko 5:27-29.

Kisha Yesu anauliza: “Ni nani aliyenigusa?” Unafikiri mwanamke huyo anahisije anaposikia maneno hayo? Petro analalamika na kumkaripia Yesu kwa njia isiyo ya moja kwa moja: “Umati umekuzunguka na kukusonga.” Basi kwa nini Yesu aliuliza, “Ni nani aliyenigusa?” Yesu anaeleza: “Mtu fulani amenigusa, kwa maana ninajua nguvu zimenitoka.” (Luka 8:45, 46) Naam, Yesu ametokwa na nguvu baada ya yule mwanamke kuponywa.

Anapogundua kwamba hawezi kujificha, yule mwanamke anaanguka mbele ya Yesu, akiwa na hofu huku akitetemeka. Mbele ya watu wote, anamwambia Yesu ukweli kuhusu ugonjwa wake na kwamba sasa ameponywa. Yesu anamfariji kwa fadhili: “Binti yangu, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, umepona ugonjwa wako mbaya.”—Marko 5:34.

Kwa kweli, yule ambaye amechaguliwa na Yehova kuitawala dunia, ni mtu mchangamfu, mwenye huruma, na anayewajali watu na pia ana nguvu za kuwasaidia!