Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SURA YA 77

Yesu Atoa Ushauri Kuhusu Utajiri

Yesu Atoa Ushauri Kuhusu Utajiri

LUKA 12:1-34

  • MFANO WA MTU TAJIRI

  • YESU AZUNGUMZA KUHUSU KUNGURU NA MAYUNGIYUNGI

  • “KUNDI DOGO” KUWA KATIKA UFALME

Yesu akiwa anakula katika nyumba ya Farisayo, umati unakusanyika nje ukimsubiri. Tukio kama hilo lilitokea akiwa huko Galilaya. (Marko 1:33; 2:2; 3:9) Sasa akiwa Yudea, watu wengi wanataka kumwona na kumsikia, wana mtazamo tofauti na ule wa Mafarisayo walio kwenye mlo.

Jambo ambalo Yesu anasema kwanza lina maana ya pekee kwa wanafunzi wake: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, ambayo ni unafiki.” Yesu aliwapa onyo hilo hapo awali, lakini mambo aliyoona katika mlo yanaonyesha jinsi ushauri huo ulivyo muhimu. (Luka 12:1; Marko 8:15) Mafarisayo wanaweza kujaribu kuficha uovu wao kwa kujionyesha kuwa waadilifu, lakini wao ni hatari na wanapaswa kufunuliwa. Yesu anafafanua hivi: “Hakuna jambo lolote lililofunikwa kwa uangalifu ambalo halitafunuliwa, na hakuna siri yoyote ambayo haitafichuliwa.”—Luka 12:2.

Labda umati uliokusanyika kumzunguka Yesu ni Wayudea ambao hawakumsikia akifundisha huko Galilaya. Basi Yesu anarudia mambo makuu aliyozungumzia hapo awali. Anawahimiza wote wanaomsikiliza: “Msiwaogope wale wanaoua mwili na baada ya hilo hawawezi kufanya jambo lolote zaidi.” (Luka 12:4) Kama alivyofanya hapo awali, anakazia umuhimu wa wafuasi wake kuamini kwamba Mungu atawategemeza. Pia, wanapaswa kumtambua Mwana wa binadamu na kuelewa kwamba Mungu anaweza kuwasaidia.—Mathayo 10:19, 20, 26-33; 12:31, 32.

Kisha mtu fulani katika umati anamwambia shida aliyo nayo: “Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane urithi.” (Luka 12:13) Sheria inasema kwamba mwana wa kwanza anapaswa kupata mafungu mawili ya urithi, basi malalamiko hayapaswi kuwapo. (Kumbukumbu la Torati 21:17) Hata hivyo, inaonekana mwanamume huyo, anataka kupata zaidi ya kiwango ambacho sheria inaruhusu. Kwa hekima Yesu anakataa kuunga mkono upande wowote. Yesu anauliza: “Ni nani aliyeniweka niwe mwamuzi au mpatanishi kati yenu wawili?”—Luka 12:14.

Kisha Yesu anawapa wote ushauri huu: “Endeleeni kufungua macho yenu na mjilinde na kila aina ya pupa, kwa sababu hata mtu anapokuwa na vitu vingi, uhai wake hautokani na vitu alivyo navyo.” (Luka 12:15) Hata mtu akiwa na mali nyingi sana, je, wakati hautafika ambapo atakufa na kuacha kila kitu? Yesu anakazia jambo hilo kwa kutumia mfano unaokumbukwa ambao pia unaonyesha thamani ya kujifanyia jina zuri pamoja na Mungu:

“Shamba la tajiri fulani lilizaa vizuri. Basi akaanza kuwaza moyoni, ‘Nitafanya nini kwa sababu sina mahali pa kuhifadhi mazao yangu?’ Kisha akasema, ‘Nitafanya hivi: Nitabomoa maghala yangu na kujenga makubwa zaidi, kisha nitahifadhi humo nafaka yangu na vitu vyangu vyote, kisha nitajiambia: “Una vitu vingi vizuri ulivyokusanya kwa miaka mingi; starehe, ule, unywe, na ujifurahishe.”’ Lakini Mungu akamwambia, ‘Wewe mpumbavu, usiku huu wanautaka uhai wako. Basi, vitu ulivyohifadhi vitakuwa vya nani?’ Hivyo ndivyo huwa kwa mtu anayejiwekea hazina lakini si tajiri kwa Mungu.”—Luka 12:16-21.

Wanafunzi wa Yesu na wote wanaomsikiliza wanaweza kunaswa na mtego wa kutafuta au kujirundikia mali. Au mahangaiko ya maisha yanaweza kuwakengeusha wasimtumikie Yehova. Kwa hiyo, Yesu anarudia shauri zuri alilowapa mwaka mmoja na nusu hivi uliopita katika Mahubiri ya Mlimani:

“Acheni kuhangaikia uhai wenu kuhusu kile mtakachokula au miili yenu kuhusu kile mtakachovaa. . . . Waangalieni kunguru: Hawapandi mbegu wala hawavuni; hawana bohari wala ghala; lakini Mungu huwalisha. Je, ninyi si wenye thamani kuliko ndege? . . . Angalieni jinsi mayungiyungi yanavyokua: Hayafanyi kazi wala hayasokoti; lakini ninawaambia hata Sulemani katika utukufu wake wote hakupambwa kama maua hayo. . . . Basi acheni kutafuta kile mtakachokula au mtakachokunywa, na acheni kuhangaika kwa wasiwasi . . . Baba yenu anajua mnahitaji vitu hivi. . . . Endeleeni kuutafuta Ufalme wake, nanyi mtaongezewa vitu hivyo.”—Luka 12:22-31; Mathayo 6:25-33.

Ni nani watakaoutafuta Ufalme wa Mungu? Yesu anafunua kwamba idadi ndogo, “kundi dogo,” la wanadamu waaminifu ndio watakaokuwa wakifanya hivyo. Baadaye itafunuliwa kwamba idadi yao ni 144,000 tu. Wanatarajia kupata nini? Yesu anawahakikishia hivi: “Baba yenu amekubali kuwapa Ufalme.” Hao hawatakazia fikira kujiwekea hazina duniani, ambako wezi wanaweza kuiba. Badala yake mioyo yao itakazia “hazina isiyopungua huko mbinguni,” ambako watatawala na Kristo.—Luka 12:32-34.