Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SURA YA 27

Mathayo Aitwa

Mathayo Aitwa

MATHAYO 9:9-13 MARKO 2:13-17 LUKA 5:27-32

  • YESU AMWITA MATHAYO, MKUSANYA KODI

  • YESU ANASHIRIKIANA NA WATENDA DHAMBI ILI AWASAIDIE

Muda mfupi baada ya kumponya mtu aliyepooza, Yesu anabaki katika eneo la Kapernaumu kando ya Bahari ya Galilaya. Umati unamjia tena, naye anaanza kuwafundisha. Akiwa anatembea anamwona Mathayo, ambaye pia anaitwa Lawi, akiwa ameketi kwenye ofisi ya kodi. Yesu anampa mwaliko wa pekee: “Njoo uwe mfuasi wangu.”—Mathayo 9:9.

Kama ilivyokuwa kwa Petro, Andrea, Yakobo, na Yohana, huenda tayari Mathayo anajua kwa kadiri fulani mafundisho ya Yesu na miujiza aliyofanya katika eneo hilo. Kama wao, Mathayo anakubali mara moja. Mathayo anaeleza jambo hilo katika Injili yake akisema: “Mara moja [Mathayo mwenyewe] akasimama na kumfuata” Yesu. (Mathayo 9:9) Hivyo, Mathayo anaacha kazi yake ya kukusanya kodi na kuwa mwanafunzi wa Yesu.

Baadaye, labda ili kuonyesha shukrani kwa ajili ya mwaliko huo wa pekee kutoka kwa Yesu, Mathayo anaandaa karamu kubwa katika nyumba yake. Ni nani wengine wanaoalikwa zaidi ya Yesu na wanafunzi wake? Mathayo amewaalika marafiki wake wengi wa zamani, ambao ni wakusanya kodi. Wanakusanya kodi kwa ajili ya serikali ya Roma inayochukiwa, kodi hiyo inatia ndani kodi za meli zinazokuja bandarini, kodi za misafara kwenye barabara kuu, na kodi za bidhaa zilizoingizwa nchini. Kwa kawaida, Wayahudi wanawaonaje wakusanya kodi hao? Watu wanawachukia kwa sababu mara nyingi wanadai pesa nyingi kuliko kiasi kilichowekwa cha kodi. Katika karamu hiyo pia kuna ‘watenda dhambi’ ambao wanajulikana kwa kutenda maovu.—Luka 7:37-39.

Wanapoona Yesu akiwa na watu hao katika karamu, Mafarisayo walio hapo ambao wanajiona kuwa waadilifu, wanawauliza wanafunzi wake: “Kwa nini mwalimu wenu anakula pamoja na wakusanya kodi na watenda dhambi?” (Mathayo 9:11) Yesu anapowasikia anajibu hivi: “Watu wenye afya hawahitaji daktari, lakini wagonjwa wanamhitaji. Nendeni, basi, mkajifunze maana ya maneno haya, ‘Ninataka rehema, si dhabihu.’ Kwa maana sikuja kuwaita watu waadilifu, bali watenda dhambi.” (Mathayo 9:12, 13; Hosea 6:6) Mafarisayo si wanyoofu wanapomwita Yesu “mwalimu,” hata hivyo wanaweza kujifunza kutoka kwake kuhusu mambo yaliyo sawa.

Inaonekana kwamba Mathayo amewaalika wakusanya kodi na watenda dhambi hao nyumbani kwake ili wamsikilize Yesu na waponywe kiroho, “kwa maana wengi wao walikuwa wakimfuata.” (Marko 2:15) Yesu anataka kuwasaidia wawe na uhusiano mzuri pamoja na Mungu. Tofauti na Mafarisayo wanaojiona kuwa waadilifu, Yesu hawadharau watu kama hao. Anachochewa na huruma na rehema; akiwa daktari wa kiroho, anaweza kuwahudumia wote ambao ni wagonjwa kiroho.

Yesu anawahurumia wakusanya kodi na watenda dhambi, hafanyi hivyo ili kupuuza dhambi zao, bali anawaonyesha hisia nyororo kama alivyowaonyesha watu waliokuwa wagonjwa kimwili. Kwa mfano, kumbuka alivyomgusa kwa wororo mtu mwenye ukoma, akisema: “Ninataka! Takasika.” (Mathayo 8:3) Je, hatupaswi kuwa na mtazamo huohuo wa huruma na kuwasaidia watu walio na uhitaji, hasa kwa njia ya kiroho?