Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SURA YA 66

Akiwa Yerusalemu kwa Ajili ya Sherehe ya Vibanda

Akiwa Yerusalemu kwa Ajili ya Sherehe ya Vibanda

YOHANA 7:11-32

  • YESU AFUNDISHA HEKALUNI

Yesu anajulikana sana tangu alipobatizwa. Maelfu ya Wayahudi wameona miujiza yake na habari kuhusu kazi zake zimeenea kotekote nchini. Sasa, wengi waliohudhuria Sherehe ya Vibanda huko Yerusalemu, wanamtafuta.

Watu wana maoni mbalimbali kumhusu Yesu. Wengine wanasema: “Yeye ni mtu mwema.” Nao wengine wanasema: “Hapana. Anaupotosha umati.” (Yohana 7:12) Mazungumzo hayo ya chinichini yanafanywa katika siku za kwanza za sherehe. Lakini hakuna mtu aliye na ujasiri wa kumtetea Yesu hadharani kwa sababu wengi wanahofia jinsi viongozi wa Kiyahudi watakavyotenda.

Yesu anakuja hekaluni sherehe ikiwa inaendelea. Watu wengi wanashangazwa na uwezo wake wa pekee wa kufundisha. Yesu hajawahi kusoma kwenye shule za kirabi, basi Wayahudi wanashangaa: “Mtu huyu alipataje ujuzi wa Maandiko, ingawa hajafundishwa shuleni?”—Yohana 7:15.

Yesu anawaambia: “Mambo ninayofundisha si yangu, bali ni ya yule aliyenituma. Mtu yeyote anayetamani kufanya mapenzi ya Mungu, atajua kama mafundisho haya yanatoka kwa Mungu au ninasema mambo niliyojitungia.” (Yohana 7:16, 17) Mafundisho ya Yesu yanapatana na Sheria ya Mungu, basi inapaswa kuwa wazi kwamba Yesu anatafuta utukufu wa Mungu bali si wake mwenyewe.

Kisha Yesu anasema: “Musa aliwapa Sheria, sivyo? Lakini hakuna yeyote kati yenu anayetii Sheria. Kwa nini mnataka kuniua?” Baadhi ya watu katika umati, labda wageni kutoka maeneo mengine, hawajui kuhusu jambo hilo. Kwa maoni yao, haiwezekani kwamba mtu yeyote anataka kumuua mwalimu kama huyo. Basi wanakata shauri kwamba lazima Yesu ana tatizo fulani ndio maana anasema hivyo. Wanamwambia: “Wewe una roho mwovu. Ni nani anayetaka kukuua?”—Yohana 7:19, 20.

Kwa kweli mwaka mmoja na nusu mapema, viongozi wa dini ya Kiyahudi walitaka kumuua Yesu alipomponya mtu siku ya Sabato. Sasa Yesu anatoa sababu yenye kuchochea fikira na kufunua kwamba hawana usawaziko. Anawakumbusha kwamba kulingana na Sheria, mtoto wa kiume anapaswa kutahiriwa siku ya nane, hata kama ni siku ya Sabato. Kisha anauliza: “Ikiwa mtu hutahiriwa siku ya sabato ili Sheria ya Musa isivunjwe, mbona mnanikasirikia kwa sababu nilimponya mtu siku ya sabato naye akapona kabisa? Acheni kuhukumu kwa kutazama sura ya nje tu, bali hukumuni kwa uadilifu.”—Yohana 7:23, 24.

Wakaaji wa Yerusalemu wanaojua hali hiyo wanasema: “Huyu ndiye mtu [ambaye watawala wanataka] kumuua, sivyo? Na bado oneni! anazungumza hadharani, na hawamwambii chochote. Je, kweli watawala wametambua kwa hakika kwamba huyu ndiye Kristo?” Basi, kwa nini watu hawaamini kwamba Yesu ndiye Kristo? Wanasema: “Tunajua mtu huyu ametoka wapi; lakini Kristo atakapokuja, hakuna mtu atakayejua alikotoka.”—Yohana 7:25-27.

Papo hapo hekaluni, Yesu anawajibu: “Ninyi mnanijua na pia mnajua nilikotoka. Nami sikuja kwa uamuzi wangu mwenyewe, lakini yule aliyenituma ni halisi, nanyi hammjui. Mimi ninamjua, kwa sababu mimi ni mwakilishi kutoka kwake, naye Ndiye aliyenituma.” (Yohana 7:28, 29) Wanaposikia maneno hayo yaliyo wazi wanajaribu kumkamata Yesu ili wamtupe gerezani au wamuue. Hata hivyo wanashindwa kumkamata kwa sababu bado muda haujafika wa Yesu kufa.

Hata hivyo, kwa kufaa wengi wanamwamini Yesu. Ametembea juu ya maji, ametuliza  upepo, amewalisha maelfu ya watu kimuujiza kwa mikate michache na samaki, amewaponya wagonjwa, amewawezesha vilema kutembea, amefungua macho ya vipofu, amewaponya wenye ukoma na hata akawafufua wafu. Naam, wana sababu nzuri ya kuuliza: “Kristo atakapokuja, je, atafanya ishara nyingi kuliko alizofanya mtu huyu?”—Yohana 7:31.

Mafarisayo wanaposikia umati ukisema mambo hayo, wao pamoja na wakuu wa makuhani wanawatuma watu wakamkamate Yesu.