Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SURA YA 41

Anafanya Miujiza kwa Nguvu za Nani?

Anafanya Miujiza kwa Nguvu za Nani?

MATHAYO 12:22-32 MARKO 3:19-30 LUKA 8:1-3

  • YESU AANZA SAFARI YA PILI YA KUHUBIRI

  • AFUKUZA ROHO WAOVU NA KUONYA KUHUSU DHAMBI ZISIZOSAMEHEWA

Muda mfupi baada ya kuzungumza kuhusu kusamehe katika nyumba ya Farisayo anayeitwa Simoni, Yesu anaanza safari nyingine ya kuhubiri huko Galilaya. Ni mwaka wa pili wa huduma yake, naye hasafiri akiwa peke yake. Yuko na wale mitume 12, na pia wanawake fulani ambao ‘aliwatoa roho waovu na kuwaponya magonjwa.’ (Luka 8:2) Miongoni mwao ni Maria Magdalene, Susana, na Yoana, ambaye mume wake ni ofisa wa Mfalme Herode Antipa.

Kadiri watu wengi wanavyomfahamu Yesu, ndivyo maswali mengi kuhusu kazi zake yanavyozuka. Jambo hilo linaonekana wazi mtu fulani mwenye roho waovu, ambaye ni kipofu na bubu anapoletwa kwa Yesu naye anaponywa. Sasa mwanamume huyo hasumbuliwi tena na roho waovu na anaweza kuona na kuongea. Watu wanashangaa sana, wakisema: “Je, inawezekana kwamba huyu ndiye Mwana wa Daudi?”—Mathayo 12:23.

Umati uliozunguka nyumba ambayo Yesu anakaa ni mkubwa sana hivi kwamba Yesu na wanafunzi wake hawawezi hata kula. Hata hivyo si wote wanaofikiri Yesu ndiye “Mwana [aliyeahidiwa] wa Daudi.” Baadhi ya waandishi na Mafarisayo wamekuja kutoka mbali sana, huko Yerusalemu—hawakuja kujifunza wala kumuunga mkono. Wanawaambia watu hivi: “Ana Beelzebuli” na hivyo anashirikiana na “mtawala wa roho waovu.” (Marko 3:22) Watu wa ukoo wa Yesu wanaposikia kuhusu vurugu hizo, wanakuja kumshika. Kwa nini?

Kwa kweli, kufikia sasa ndugu za Yesu hawaamini kwamba yeye ni Mwana wa Mungu. (Yohana 7:5) Yesu anayeonekana kusababisha vurugu hizo, si kama yule Yesu waliyemfahamu walipokuwa wakikua pamoja huko Nazareti. Wanafikiri  kwamba ana tatizo la akili, nao wanasema: “Amerukwa na akili.”—Marko 3:21.

Hata hivyo, ushahidi unathibitisha nini? Hivi punde Yesu amemponya mwanamume aliyekuwa na roho waovu, na sasa anaweza kuona na kuongea. Hakuna mtu anayeweza kupinga jambo hilo. Sasa waandishi na Mafarisayo wanajaribu kumharibia sifa Yesu kwa mashtaka ya uwongo. Wanasema: “Mtu huyu anawafukuza roho waovu kwa nguvu za Beelzebuli, mtawala wa roho waovu.”—Mathayo 12:24.

Yesu anajua mawazo ya waandishi na Mafarisayo, kwa hiyo anawaambia: “Kila ufalme uliogawanyika dhidi yake wenyewe utaangamia, na kila jiji au nyumba iliyogawanyika dhidi yake yenyewe haitasimama. Vivyo hivyo, ikiwa Shetani anamfukuza Shetani, amegawanyika dhidi yake mwenyewe; basi, ufalme wake utawezaje kusimama?”—Mathayo 12:25, 26.

Ukweli huo hauwezi kupingwa! Mafarisayo wanajua kwamba baadhi ya Wayahudi wana mazoea ya kufukuza roho waovu. (Matendo 19:13) Basi Yesu anauliza: “Ikiwa ninawafukuza roho waovu kupitia Beelzebuli, wana wenu wanawafukuza kupitia nani?” Kwa maneno mengine, shutuma zao zinawahusu wao pia. Yesu anaendelea kusema hivi: “Lakini ikiwa ninawafukuza roho waovu kupitia roho ya Mungu, kwa kweli Ufalme wa Mungu umewafikia ninyi ghafla.”—Mathayo 12:27, 28.

Ili kuonyesha kwamba uwezo wake wa kufukuza roho waovu unathibitisha ana nguvu kuliko Shetani, Yesu anasema: “[Mtu] yeyote anawezaje kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuchukua mali zake isipokuwa kwanza amfunge mtu huyo? Hapo ndipo anaweza kuipora nyumba yake. Yeyote asiye upande wangu ananipinga, na yeyote asiyekusanya pamoja nami anatawanya.” (Mathayo 12:29, 30) Kwa kweli waandishi na Mafarisayo wanampinga Yesu, na hivyo kuonyesha kwamba wanatumiwa na Shetani. Wanawatawanya watu kutoka kwa Mwana wa Mungu, ambaye kazi yake inaungwa mkono na Yehova.

Yesu anawaonya hivi wapinzani hao wa kishetani: “Wanadamu watasamehewa mambo yote, hata ziwe dhambi gani au maneno ya kukufuru wanayosema. Lakini yeyote anayekufuru roho takatifu hatasamehewa milele, bali atakuwa na hatia ya dhambi ya milele.” (Marko 3:28, 29) Fikiria maana ya maneno hayo kwa wale wanaosema kuwa Shetani anafanya mambo ambayo ni wazi kwamba yanafanywa na roho ya Mungu!