Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SURA YA 82

Huduma ya Yesu Huko Perea

Huduma ya Yesu Huko Perea

LUKA 13:22–14:6

  • KUJITAHIDI KUINGIA KUPITIA MLANGO MWEMBAMBA

  • LAZIMA YESU AFE HUKO YERUSALEMU

Yesu amekuwa akifundisha na kuwaponya watu huko Yudea na Yerusalemu. Kisha anavuka Mto Yordani ili akafundishe kutoka jiji hadi jiji katika wilaya ya Perea. Hata hivyo, baada ya muda mfupi atarudi Yerusalemu.

Yesu akiwa huko Perea, mtu fulani anamuuliza: “Bwana, je, wale watakaookolewa ni wachache?” Huenda mtu huyo anajua jinsi viongozi wa kidini wanavyojadili kuhusu idadi ya watu watakaookolewa, kama ni wengi au ni wachache. Badala ya kuzungumzia kuhusu idadi ya watakaookolewa, Yesu anazungumzia jambo ambalo watu wanapaswa kufanya ili waokolewe. Anasema: “Jitahidini sana ili mwingie kupitia mlango mwembamba.” Wanahitaji kujitahidi, naam, kupambana. Kwa nini? Yesu anaeleza: “Ninawaambia wengi watajaribu kuingia lakini hawataweza.”—Luka 13:23, 24.

Yesu anatoa mfano ili kuonyesha umuhimu wa kujitahidi sana, anasema: “Mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, mtakuwa nje mkibisha mlangoni, mkisema, ‘Bwana, tufungulie.’ . . . Lakini atawaambia, ‘Sijui mnatoka wapi. Ondokeni kwangu, ninyi nyote watenda maovu!’”—Luka 13:25-27.

Mfano huo unaonyesha hali inayompata mtu anayechelewa—inaonekana anakuja wakati unaomfaa yeye—na anapata mlango ukiwa umefungwa. Alipaswa kuja mapema, hata ikiwa muda huo haukumfaa. Hali hiyo inafanana na ya wengi ambao wangenufaika kwa sababu Yesu yuko hapo akiwafundisha. Lakini hawakutumia nafasi hiyo kufanya ibada ya kweli iwe jambo kuu maishani mwao. Wengi wa wale ambao Yesu alitumwa kwao, hawajakubali maandalizi ya Mungu ya wokovu. Yesu anasema kwamba ‘watalia na kusaga meno yao’ watakapotupwa nje. Hata hivyo, watu kutoka “mashariki na magharibi, na kutoka kaskazini na kusini,” naam, kutoka mataifa yote, “wataketi mezani katika Ufalme wa Mungu.”—Luka 13:28, 29.

Yesu anaeleza: “Kuna wale wa mwisho [kama vile watu wasio Wayahudi na Wayahudi wa hali ya chini] watakaokuwa wa kwanza, na kuna wale wa kwanza [Wayahudi walio na vyeo vya kidini ambao wanajivunia kuwa wazao wa Abrahamu] watakaokuwa wa mwisho.” (Luka 13:30) Kuwa “wa mwisho” kunamaanisha kwamba watu hao wasio na shukrani hawatakuwa kamwe katika Ufalme wa Mungu.

Sasa, baadhi ya Mafarisayo wanamjia Yesu na kumshauri: “Ondoka hapa uende mahali pengine, kwa sababu Herode [Antipa] anataka kukuua.” Labda Mfalme Herode ndiye aliyeanzisha habari hizo za uwongo ili kumfanya Yesu akimbie eneo hilo. Huenda Herode anahofia kuhusika katika kifo cha nabii mwingine, kama alivyohusika kumuua Yohana Mbatizaji. Lakini Yesu anawaambia  Mafarisayo: “Nendeni mkamwambie mbweha huyo, ‘Tazama! Ninawafukuza roho waovu na kuwaponya watu leo na kesho, na siku ya tatu nitakuwa nimemaliza.’” (Luka 13:31, 32) Anapomwita Herode mbweha, huenda Yesu anarejelea jinsi mbweha walivyo wajanja. Hata hivyo, Yesu hataongozwa au kuharakishwa na Herode au mtu mwingine yeyote. Atafanya kazi ambayo Baba yake alimpa, akifuata ratiba ya Mungu, bali si ya mwanadamu.

Yesu anaendelea na safari yake ya kurudi Yerusalemu kwa sababu, kama anavyosema, “haiwezekani nabii kuuawa nje ya Yerusalemu.” (Luka 13:33) Hakuna unabii wa Biblia unaosema kwamba lazima Masihi afe katika jiji hilo, basi kwa nini Yesu anasema atafia huko? Kwa sababu Yerusalemu ndilo jiji kuu, lina mahakama ya Sanhedrini yenye washiriki 71, na wale wanaoshtakiwa kuwa manabii wa uwongo huhukumiwa huko. Isitoshe, huko ndiko dhabihu za wanyama hutolewa. Kwa hiyo, Yesu anatambua kwamba hapaswi kuuawa akiwa sehemu nyingine yoyote.

Yesu anaomboleza: “Yerusalemu, Yerusalemu, muuaji wa manabii na aliyewapiga mawe wale waliotumwa kwake—nilijaribu mara ngapi kuwakusanya watoto wako, kama vile kuku anavyokusanya vifaranga wake chini ya mabawa yake! Lakini hamkutaka. Tazama! Mmeachiwa nyumba yenu.” (Luka 13:34, 35) Taifa hilo linamkataa Mwana wa Mungu basi lazima lipate matokeo mabaya!

Kabla Yesu hajafika Yerusalemu, kiongozi fulani wa Mafarisayo anamwalika nyumbani kwake kwa ajili ya mlo siku ya Sabato. Wale walioalikwa wanatazama kwa makini ili kuona Yesu atamfanyia nini mwanamume aliye hapo ambaye ana ugonjwa wa kuvimba mwili (umajimaji mwingi unaokusanyika hasa katika miguu na nyayo). Yesu anawauliza Mafarisayo na wataalamu wa Sheria: “Je, ni halali au si halali kumponya mtu siku ya Sabato?”—Luka 14:3.

Hakuna anayejibu. Yesu anamponya mtu huyo kisha anawauliza: “Ni nani kati yenu ambaye mwana wake au ng’ombe wake akianguka ndani ya kisima siku ya Sabato, hatamtoa humo mara moja?” (Luka 14:5) Kwa mara nyingine tena, wanashindwa kupinga sababu nzuri anazotoa.