Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SURA YA 86

Mwana Aliyepotea Arudi

Mwana Aliyepotea Arudi

LUKA 15:11-32

  • MFANO WA MWANA ALIYEPOTEA

Yesu amesimulia mfano wa kondoo aliyepotea na mfano wa sarafu ya drakma iliyopotea inaelekea bado akiwa huko Perea, mashariki ya Mto Yordani. Mifano hiyo miwili inatufundisha kwamba tunapaswa kushangilia mtenda dhambi anapotubu na kumrudia Mungu. Mafarisayo na waandishi wamekuwa wakimshutumu Yesu kwa sababu anawakaribisha watu kama hao. Lakini je, Mafarisayo na waandishi wanajifunza kutokana na mifano hiyo miwili ya Yesu? Je, wanaelewa jinsi Baba yetu aliye mbinguni anavyohisi kuwaelekea watenda dhambi wanaotubu? Sasa Yesu anasimulia mfano unaogusa moyo ambao unakazia somo hilo muhimu.

Mfano huo unamhusu baba aliye na wana wawili, mwana mdogo ndiye mhusika mkuu katika mfano huo. Mafarisayo na waandishi, na pia watu wengine wanaomsikiliza Yesu, wanapaswa kujifunza kutokana na mambo yanayosemwa kumhusu yule mwana mdogo. Hata hivyo, hatupaswi kupuuza mambo ambayo Yesu anasema kumhusu yule baba na yule mwana mkubwa, kwa maana tunaweza kujifunza kutokana na mtazamo wao. Basi wafikirie wanaume hao watatu Yesu anaposimulia mfano huo:

Yesu anaanza hivi: “Mtu fulani alikuwa na wana wawili. Yule mdogo akamwambia baba yake, ‘Baba, nipe sehemu ya urithi ambayo ni yangu.’ Basi akawagawia wanawe mali yake.” (Luka 15:11, 12) Ona kwamba yule mwana mdogo haombi apewe urithi kwa sababu baba yake amekufa. Bado baba yake yuko hai. Lakini mwana huyo anataka fungu lake sasa ili awe na uhuru na kutumia urithi huo kama apendavyo. Naye anafanya nini?

“Baada ya siku chache,” Yesu anaeleza, “yule mwana mdogo akakusanya vitu vyake vyote akasafiri kwenda nchi ya mbali, akiwa huko akatumia vibaya mali yake kwa kuishi maisha ya anasa.” (Luka 15:13) Badala ya kufurahia usalama nyumbani, pamoja na baba anayewajali wanawe na kuwatunza, mwana huyo anahamia nchi nyingine. Akiwa huko anaharibu urithi wake kwa kuishi maisha ya raha, anasa, na uasherati.  Kisha anaanza kuteseka, kama Yesu anavyoendelea kusimulia:

“Alipokuwa ametumia kila kitu, njaa kali sana ikatokea katika nchi hiyo yote, naye hakuwa na chochote. Hata alienda kuajiriwa na raia mmoja wa nchi hiyo, ambaye alimpeleka kwenye mashamba yake akalishe nguruwe. Naye alitamani kujishibisha kwa maganda ya karuba ambayo nguruwe walikuwa wakila, lakini hakuna mtu aliyempa chochote.”—Luka 15:14-16.

Kulingana na Sheria ya Mungu, nguruwe ni mnyama asiye safi, lakini mwana huyo anafanya kazi ya kulisha kundi la nguruwe. Anapatwa na njaa kali, naye anatamani kula chakula ambacho kwa kawaida huliwa na wanyama, yaani, nguruwe anaowalisha. Akiwa katika hali hiyo ya kuteseka na inayokatisha tamaa, ‘anarudiwa na fahamu.’ Sasa anafanya nini? Anajiambia: “Baba yangu ameajiri wafanyakazi wengi nao wana mkate kwa wingi, lakini mimi ninakufa njaa! Nitafunga safari kwenda kwa baba yangu na kumwambia: ‘Baba, nimetenda dhambi dhidi ya mbingu na dhidi yako. Sistahili tena kuitwa mwanao. Naomba niwe mmoja wa wafanyakazi wako.’” Kisha anaondoka na kwenda kwa baba yake.—Luka 15:17-20.

Baba yake atatendaje? Je, atakasirika na kuanza kumkemea kuhusu upumbavu wa kuondoka nyumbani? Je, baba huyo atampuuza na kukataa kumkaribisha? Kama ingekuwa wewe, ungetendaje? Namna gani kama ni mwana au binti yako?

 MWANA ALIYEPOTEA APATIKANA

Yesu anafafanua jinsi yule baba anavyohisi na kutenda: “[Yule mwana] akiwa mbali, baba yake akamwona na kumsikitikia, akakimbia, akamkumbatia na kumbusu kwa wororo.” (Luka 15:20) Hata ikiwa yule baba amesikia kuhusu maisha mapotovu ya mwanawe, anamkaribisha mwanawe. Je, viongozi wa Kiyahudi, wanaodai kumjua na kumwabudu Yehova, wataona kutokana na mfano huo jinsi baba yetu wa mbinguni anavyohisi kuwaelekea watenda dhambi wanaotubu? Je, watatambua pia kwamba Yesu amekuwa akionyesha roho kama hiyo ya ukaribishaji?

Baba huyo mwenye utambuzi anaweza kuona kwamba mwanawe ametubu kwa kutazama uso wake wenye huzuni. Lakini hatua ambayo baba anachukua kwanza ya kumsalimia inafanya iwe rahisi kwa mwanawe kutubu dhambi zake. Yesu anasimulia hivi: “Kisha yule mwana akamwambia, ‘Baba, nimetenda dhambi dhidi ya mbingu na dhidi yako. Sistahili tena kuitwa mwanao.’”—Luka 15:21.

Yule baba anawaagiza watumwa wake hivi: “Leteni upesi kanzu bora zaidi na kumvika, pia mvisheni pete mkononi na viatu miguuni. Vilevile, leteni ndama aliyenoneshwa, mchinjeni, nasi tule na tusherehekee, kwa sababu huyu mwanangu alikuwa amekufa na sasa yuko hai; alikuwa amepotea naye amepatikana.” Kisha wanaanza “kusherehekea.”—Luka 15:22-24.

Wakati huo, mwana mkubwa wa yule baba yuko shambani. Yesu anasema hivi kumhusu: “Alipokuwa akirudi na kukaribia nyumba, akasikia sauti ya muziki na dansi. Basi akamwita mtumishi mmoja akamuuliza kilichokuwa kikiendelea. Akamjibu, ‘Ndugu yako amerudi, kwa hiyo baba yako amechinja ndama aliyenoneshwa kwa sababu amerudi akiwa na afya njema.’ Lakini akakasirika na kukataa kuingia ndani. Basi baba yake akatoka nje akaanza kumbembeleza. Akamjibu baba yake, ‘Tazama! nimekutumikia kwa miaka mingi na sijawahi kuvunja amri  yako hata mara moja, lakini hujawahi kunipa hata mara moja mwanambuzi ili nijifurahishe pamoja na rafiki zangu. Lakini mara tu alipofika huyu mwanao aliyetumia vibaya mali yako na makahaba, ulimchinjia ndama aliyenoneshwa.’”—Luka 15:25-30.

Ni nani ambao kama yule mwana mkubwa wamekuwa wakimshutumu Yesu kwa kuonyesha rehema na kushirikiana na watu wa kawaida na watenda dhambi? Ni waandishi na Mafarisayo. Yesu ametoa mfano huo kwa kuwa wanamshutumu kwa sababu ya kuwakaribisha watenda dhambi. Bila shaka, mtu yeyote anayemshutumu Mungu kwa kuonyesha rehema anapaswa kujifunza kutokana na mfano huo.

Yesu anamalizia mfano huo kwa kutaja ombi la baba kwa yule mwana mkubwa: “Mwanangu, umekuwa pamoja nami sikuzote, na vitu vyangu vyote ni vyako. Lakini ilibidi tusherehekee na kushangilia, kwa maana ndugu yako alikuwa amekufa lakini sasa yuko hai; alikuwa amepotea naye amepatikana.”—Luka 15:31, 32.

Yesu hasemi jambo ambalo mwishowe yule mwana mkubwa anafanya. Hata hivyo, baada ya Yesu kufa na kufufuliwa, “umati mkubwa wa makuhani wakawa waamini.” (Matendo 6:7) Huenda walitia ndani baadhi ya wale waliomsikia Yesu akisimulia mfano huo unaogusa moyo kuhusu mwana aliyepotea. Naam, iliwezekana kwao kurudiwa na fahamu, kutubu, na kumrudia Mungu.

Tangu siku hiyo, wanafunzi wa Yesu wanaweza na wanapaswa kujifunza masomo muhimu aliyotaja katika mfano huo bora. Somo la kwanza ni kwamba ni jambo la hekima kubaki katika usalama wa watu wa Mungu, chini ya utunzaji wa Baba yetu anayetupenda na kututunza, badala ya kwenda kutafuta raha katika “nchi ya mbali.”

Somo lingine ni kwamba yeyote kati yetu akiiacha njia ya Mungu, anapaswa kurudi kwa unyenyekevu kwa Baba yetu ili afurahie tena kibali chake.

Pia, somo lingine linaonekana kupitia tofauti kati ya mtazamo wa baba aliyemkaribisha na kumsamehe mwanawe na mtazamo wa mwana mkubwa aliyeweka kinyongo na kukataa kumkaribisha ndugu yake. Bila shaka, watumishi wa Mungu wanapaswa kumsamehe na kumkaribisha mtu aliyekuwa amepotea ambaye anatubu na kurudi kwenye ‘nyumba ya baba.’ Acheni tushangilie kwamba ndugu yetu ‘aliyekuwa amekufa sasa yuko hai’ na kwamba ‘aliyekuwa amepotea amepatikana.’