Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SURA YA 4

Maria​—Ana Mimba Lakini Hajaolewa

Maria​—Ana Mimba Lakini Hajaolewa

MATHAYO 1:18-25 LUKA 1:56

  • YOSEFU AGUNDUA KWAMBA MARIA ANA MIMBA

  • MARIA AOLEWA NA YOSEFU

Maria amekuwa na mimba kwa miezi minne. Unakumbuka kwamba katika miezi ya kwanza ya mimba yake alikaa pamoja na Elisabeti mtu wake wa ukoo kwenye vilima vya Yudea huko kusini. Lakini sasa Maria amerudi nyumbani huko Nazareti. Akiwa huko, watu wote watajua kwamba ana mimba. Wazia jinsi hali hiyo inavyompa wasiwasi!

Hali ni mbaya zaidi kwa sababu Maria ni mchumba wa seremala aitwaye Yosefu anayeishi katika eneo hilo. Na Maria anajua kwamba kulingana na Sheria ya Mungu kwa Israeli, mwanamke ambaye anachumbiwa na mwanamume lakini anafanya ngono kimakusudi na mwanamume mwingine anapaswa kupigwa mawe na kuuawa. (Kumbukumbu la Torati 22:23, 24) Kwa hiyo, ingawa Maria hajafanya uasherati, huenda anawaza jinsi anavyoweza kumweleza Yosefu kuhusu mimba yake na kile kitakachotokea.

Maria hajakuwapo kwa miezi mitatu, basi tuna hakika kwamba Yosefu anatamani kumwona. Wanapokutana, inaelekea Maria anamwambia kuhusu hali yake, akijitahidi kabisa kueleza kwamba amepata mimba kupitia roho takatifu ya Mungu. Lakini, kama unavyojua, ni vigumu sana kwa Yosefu kuelewa na kuamini jambo hilo.

Yosefu anajua kwamba Maria ni mwanamke mzuri na kwamba anaheshimiwa. Naye anampenda sana Maria. Lakini bado, licha ya maelezo yake, Yosefu anaona kwamba angeweza tu kupata mimba kupitia mwanamume mwingine. Yosefu hataki apigwe mawe na kuuawa au kuabishwa hadharani; basi, anaamua kumtaliki kisiri. Siku hizo wachumba walionwa kama watu  waliofunga ndoa, na talaka ilihitajiwa ili kuvunja uchumba.

Baadaye, Yosefu akiwa anatafakari mambo hayo, analala usingizi. Malaika wa Yehova anamtokea katika ndoto na kumwambia: “Usiogope kumpeleka Maria mke wako nyumbani, kwa sababu amepata mimba kupitia roho takatifu. Atamzaa mwana, nawe utamwita jina Yesu, kwa maana atawaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao.”—Mathayo 1:20, 21.

Yosefu anapoamka, anafurahi kwa sababu anaelewa jambo hilo vizuri zaidi! Hakawii kufanya kama alivyoagizwa na malaika. Anampeleka Maria nyumbani kwake. Hili ni tendo la hadharani ambalo, kwa hakika, ni sherehe ya ndoa, na linaonyesha kwamba Yosefu na Maria sasa wamefunga ndoa. Hata hivyo, Yosefu hafanyi ngono na Maria akiwa na mimba ya Yesu.

Miezi kadhaa baadaye, Yosefu na Maria, ambaye anakaribia kujifungua, wanapaswa kujiandaa kusafiri kwenda mbali na nyumbani kwao Nazareti. Wanapaswa kwenda wapi wakati ambao Maria anakaribia kujifungua?