Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SURA YA 23

Yesu Afanya Miujiza Huko Kapernaumu

Yesu Afanya Miujiza Huko Kapernaumu

MATHAYO 8:14-17 MARKO 1:21-34 LUKA 4:31-41

  • YESU AMFUKUZA ROHO MWOVU

  • MAMA MKWE WA PETRO APONYWA

Yesu amewaalika wanafunzi wanne—Petro, Andrea, Yakobo, na Yohana—wawe wavuvi wa watu. Ni siku ya Sabato na wote wanaenda kwenye sinagogi fulani huko Kapernaumu. Yesu anafundisha katika sinagogi, na kwa mara nyingine tena watu wanashangazwa na njia yake ya kufundisha. Anafundisha kama mtu mwenye mamlaka na si kama waandishi wao.

Siku hii ya Sabato mtu fulani aliye na roho mwovu amehudhuria. Papo hapo katika sinagogi, mtu huyo anapaza sauti na kusema: “Kwa nini unatusumbua, wewe Yesu Mnazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninajua wewe ni nani, Mtakatifu wa Mungu!” Yesu anamkemea roho mwovu anayemwongoza mtu huyo kwa kusema: “Nyamaza, na umtoke!”—Marko 1:24, 25.

Papo hapo, yule roho mwovu anamwangusha mtu huyo chini na kumfanya agaegae na kupiga kelele kwa sauti kubwa. Lakini yule roho mwovu anamtoka mtu huyo “bila kumuumiza.” (Luka 4:35) Watu waliomzunguka katika sinagogi wanashangaa sana! “Ni jambo gani hili?” wanaulizana. “Hata anawaamuru roho waovu kwa mamlaka, nao wanamtii!” (Marko 1:27) Inaeleweka kwamba habari kuhusu tukio hilo la kushangaza zinaenea katika Galilaya yote.

Baada ya kutoka katika sinagogi, Yesu na wanafunzi wake wanaenda nyumbani kwa Simoni, yaani, Petro. Mama mkwe wa Petro ni mgonjwa sana, anaugua homa kali. Wanamwomba Yesu amsaidie. Basi Yesu anamkaribia, anamshika mkono, na kumwinua. Mara moja anaponywa na kuanza kumhudumia Yesu na wanafunzi walio pamoja naye, labda anawaandalia chakula.

Inapokaribia jioni, watu kutoka kila mahali wanakuja nyumbani kwa Petro wakiwa na wagonjwa. Baada ya muda mfupi ni kana kwamba jiji lote limekusanyika mlangoni. Kwa nini? Wanataka kuponywa. Kwa kweli, ‘wote waliokuwa na watu wenye magonjwa mbalimbali wanawaleta kwake. Anawaponya kwa kuweka mikono yake juu ya kila mgonjwa.’ (Luka 4:40) Naam, hata wawe na ugonjwa gani, Yesu anawasaidia, kama ilivyotabiriwa. (Isaya 53:4) Hata anawaweka huru wale walio na roho waovu. Roho waovu wanapotoka, wanapaza sauti: “Wewe ndiye Mwana wa Mungu.” (Luka 4:41) Lakini Yesu anawakemea na hawaruhusu wazungumze tena. Wanajua kwamba Yesu ndiye Kristo, naye hataki waonekane kana kwamba wanamtumikia Mungu wa kweli.