Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SURA YA 2

Yesu Aheshimiwa Kabla Hajazaliwa

Yesu Aheshimiwa Kabla Hajazaliwa

LUKA 1:34-56

  • MARIA AMTEMBELEA ELISABETI MTU WAKE WA UKOO

Baada ya malaika Gabrieli kumwambia mwanamke kijana Maria kwamba atazaa mwana atakayeitwa Yesu na ambaye atatawala akiwa Mfalme milele, Maria anauliza: “Hilo litawezekanaje, kwa kuwa sina uhusiano wa kingono na mwanamume?”—Luka 1:34.

Gabrieli anajibu: “Roho takatifu itakuja juu yako, na nguvu za Aliye Juu Zaidi zitakufunika. Kwa hiyo yule atakayezaliwa ataitwa mtakatifu, Mwana wa Mungu.”—Luka 1:35.

Labda ili kumsaidia Maria aelewe ujumbe huo, Gabrieli anaongezea hivi: “Tazama! Hata Elisabeti mtu wako wa ukoo, ingawa amezeeka ana mimba ya miezi sita, yule anayejulikana kuwa tasa; kwa sababu kwa Mungu hakuna tangazo lisilowezekana.”—Luka 1:36, 37.

Maria anakubali maneno aliyosema Gabrieli kama tunavyoona katika jibu lake. Anasema: “Tazama! Kijakazi wa Yehova! Na itendeke kwangu kulingana na tangazo lako.”—Luka 1:38.

Baada ya Gabrieli kuondoka, Maria anajitayarisha kumtembelea Elisabeti, ambaye anaishi na Zekaria mume wake, karibu na Yerusalemu kwenye vilima vya Yudea. Kutoka nyumbani kwa Maria huko Nazareti, safari hiyo huenda ikachukua siku tatu au nne.

Mwishowe Maria anafika kwenye nyumba ya Zekaria. Anapoingia anamsalimia Elisabeti ambaye ni mtu wake wa ukoo. Papo hapo, Elisabeti anajazwa roho takatifu, na kumwambia Maria: “Umebarikiwa kati ya wanawake, na uzao wa tumbo lako umebarikiwa! Imekuwaje nimependelewa hivi kwamba mama ya Bwana wangu amenitembelea? Kwa maana tazama! niliposikia salamu zako, mtoto aliye tumboni mwangu aliruka kwa shangwe.”—Luka 1:42-44.

Kisha Maria anajibu kwa shukrani kutoka moyoni: “Nafsi yangu inamtukuza Yehova, na roho yangu haitaacha kumshangilia Mungu Mwokozi wangu, kwa sababu ametazama hali ya chini ya kijakazi wake. Tazama! tangu sasa vizazi vyote vitanitangaza kuwa mwenye furaha, kwa sababu Mwenye nguvu amenitendea mambo makuu.” Tunaona kwamba ingawa Maria amependelewa, anaelekeza utukufu wote kwa Mungu. Anasema: “Jina lake ni takatifu, naye huwaonyesha rehema wale wanaomwogopa, kizazi baada ya kizazi.”—Luka 1:46-50.

Akitumia maneno ya kinabii yaliyoongozwa na roho, Maria anaendelea kumsifu Mungu, akisema: “Amefanya mambo makuu kwa mkono wake, amewatawanya wenye majivuno katika nia ya mioyo yao. Amewashusha watu wenye nguvu kutoka kwenye viti vya ufalme na kuwainua watu wa hali ya chini; amewashibisha kabisa wenye njaa kwa vitu vyema na kuwafukuza mikono mitupu wale waliokuwa na mali. Amekuja kumsaidia Israeli mtumishi wake, amekumbuka rehema zake, kama alivyowaahidi mababu zetu, Abrahamu na uzao wake, milele.”—Luka 1:51-55.

Maria anakaa pamoja na Elisabeti kwa miezi mitatu hivi, inaelekea anamsaidia katika majuma hayo ya mwisho kabla Elisabeti hajajifungua. Inapendeza kwamba wanawake hao wawili, ambao kila mmoja amepata mimba kwa msaada wa Mungu, wanaweza kuwa pamoja wakati huu katika maisha yao!

Pia, kumbuka jinsi Yesu alivyoheshimiwa hata kabla hajazaliwa. Elisabeti alimwita “Bwana wangu,” na yule mtoto aliye tumboni mwake ‘akaruka kwa shangwe’ Maria alipoingia. Hilo ni tofauti sana na jinsi baadaye wengine wanavyomtendea Maria na mtoto wake ambaye bado hajazaliwa, kama tutakavyoona.