Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SURA YA 40

Somo Kuhusu Msamaha

Somo Kuhusu Msamaha

LUKA 7:36-50

  • MWANAMKE MTENDA DHAMBI AMIMINA MAFUTA KWENYE MIGUU YA YESU

  • AFUNDISHA KUHUSU MSAMAHA AKITUMIA MFANO WA MTU MWENYE DENI

Watu wanaitikia kwa njia tofauti mambo ambayo Yesu anasema na kufanya, ikitegemea hali ya moyo wao. Hilo linaonekana wazi katika nyumba fulani huko Galilaya. Farisayo anayeitwa Simoni anamkaribisha Yesu kwenye mlo, labda ili amwone kwa ukaribu mtu anayefanya kazi hizo za ajabu. Huenda Yesu anakubali kwa sababu anaona hiyo ni nafasi ya kuwahubiria wale waliopo, kama alivyokubali pindi nyingine alipoalikwa kula pamoja na wakusanya kodi na watenda dhambi.

Hata hivyo, Yesu hakaribishwi kwa uchangamfu kama ilivyo kawaida kuwatendea wageni. Kwenye barabara zenye vumbi huko Palestina, miguu iliyovaa viatu vya kanda au vya wazi hupata joto na vumbi, kwa hiyo kuna desturi ya ukarimu ya kuosha miguu ya mgeni kwa maji baridi. Yesu hatendewi hivyo. Wala hakaribishwi kwa busu, kama ilivyo kawaida. Desturi nyingine ni kumimina mafuta kwenye nywele za mgeni ili kuonyesha fadhili na ukarimu. Yesu hatendewi hivyo pia. Je, kweli amekaribishwa?

Mlo unaanza baada ya wageni kuketi mezani. Wanapoendelea kula, mwanamke fulani anaingia kimyakimya katika chumba hicho bila kualikwa. Mwanamke huyo ‘anajulikana jijini kuwa mtenda dhambi.’ (Luka 7:37) Wanadamu wote wasio wakamilifu ni watenda dhambi, lakini inaonekana mwanamke huyo anaishi maisha yaliyopotoka, labda ni kahaba. Inawezekana alisikia mafundisho ya Yesu, kutia ndani mwaliko wa ‘wote waliolemewa na mizigo waje kwake ili wapate burudisho.’ (Mathayo 11:28, 29) Huenda akichochewa na maneno na matendo ya Yesu, mwanamke huyo amemtafuta Yesu.

Anakuja nyuma ya Yesu mezani na kupiga magoti miguuni pake. Macho yake yanadondosha machozi kwenye miguu ya Yesu, naye anaifuta kwa nywele zake. Anaibusu miguu yake kwa wororo na kuimiminia mafuta yenye marashi ambayo ameleta. Simoni anatazama huku akiwa amechukizwa na jambo hilo, na kusema: “Kama kweli mtu huyu angekuwa nabii, angejua ni nani na ni mwanamke wa aina gani anayemgusa, kwamba ni mtenda dhambi.”—Luka 7:39.

Yesu anapotambua jambo ambalo Simoni anawaza, anasema: “Simoni, ninataka kukuambia jambo.” Simoni anajibu: “Sema, mwalimu!” Yesu anaendelea: “Mtu fulani aliwakopesha watu wawili pesa, mmoja deni la dinari 500, na mwingine 50. Waliposhindwa kumlipa, akawasamehe kwa hiari wote wawili. Kwa hiyo, ni nani kati yao atakayempenda zaidi?” Simoni anajibu hivi, labda akiwa hapendezwi sana: “Nadhani ni yule aliyesamehewa zaidi.”—Luka 7:40-43.

Yesu anakubali. Kisha akimtazama yule mwanamke, anamwambia Simoni: “Unamwona mwanamke huyu? Niliingia katika nyumba yako; hukunipa maji ya kuosha miguu yangu. Lakini mwanamke huyu aliiosha miguu yangu kwa machozi yake na kuifuta kwa nywele zake. Wewe hukunibusu, lakini mwanamke huyu hajaacha kuibusu miguu yangu kwa wororo tangu nilipoingia. Hukunipaka mafuta kichwani, lakini mwanamke huyu ameipaka miguu yangu mafuta yenye marashi.” Yesu aliona kuwa mwanamke huyo alikuwa akithibitisha kwamba ametubu kutoka moyoni kwa sababu ya maisha yake yaliyopotoka. Basi anamalizia hivi: “Kwa hiyo, ninakuambia ingawa dhambi zake ni nyingi, amesamehewa, kwa sababu amependa sana. Lakini anayesamehewa kidogo, hupenda kidogo.”—Luka 7:44-47.

Yesu hakubaliani na maisha yaliyopotoka. Badala yake anaonyesha huruma kwa kuwaelewa watu wanaofanya dhambi nzito lakini ambao wanaonyesha kwamba wanasikitika na kumgeukia Kristo ili kupata kitulizo. Na mwanamke huyo anapata kitulizo kikubwa Yesu anaposema: “Umesamehewa dhambi zako. . . . Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani.”—Luka 7:48, 50.