Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SURA YA 42

Yesu Awakemea Mafarisayo

Yesu Awakemea Mafarisayo

MATHAYO 12:33-50 MARKO 3:31-35 LUKA 8:19-21

  • YESU AZUNGUMZIA “ISHARA YA YONA”

  • WANAFUNZI NI WATU WA KARIBU KULIKO FAMILIA

Waandishi na Mafarisayo wanapopinga kwamba Yesu anafukuza roho waovu kwa kutumia nguvu za Mungu, wako katika hatari ya kukufuru roho takatifu. Basi, watakuwa upande wa nani—wa Mungu au wa Shetani? Yesu anasema: “Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake yawe mazuri, au muufanye mti uoze na matunda yake yaoze, kwa maana mti hujulikana kwa matunda yake.”—Mathayo 12:33.

Ni upumbavu kudai kwamba tunda zuri la kufukuza roho waovu ni matokeo ya Yesu kumtumikia Shetani. Kama Yesu alivyofafanua katika Mahubiri yake ya Mlimani, ikiwa tunda ni zuri, basi mti ni mzuri, haujaoza. Hivyo, tunda la Mafarisayo, yaani mashtaka yao ya upuuzi dhidi ya Yesu, yanathibitisha nini? Kwamba wameoza. Yesu anawaambia: “Uzao wa nyoka, mnawezaje kusema mambo mema, wakati ninyi ni waovu? Kwa maana kinywa husema mambo yaliyojaa moyoni.”—Mathayo 7:16, 17; 12:34.

Naam, maneno yetu hufunua hali ya mioyo yetu nayo huweka msingi wa hukumu. Hivyo, Yesu anasema: “Ninawaambia kwamba katika Siku ya Hukumu watu watatoa hesabu kuhusu kila neno lisilofaa wanalosema; kwa maneno yako utatangazwa kuwa mwadilifu, na kwa maneno yako utahukumiwa.”—Mathayo 12:36, 37.

Licha ya miujiza ambayo Yesu anafanya, waandishi na Mafarisayo wanadai mengi zaidi: “Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako.” Iwe walimwona akifanya miujiza au la, kuna mashahidi wengi waliojionea mambo anayofanya. Hivyo Yesu anaweza kuwaambia hivi viongozi hao wa Kiyahudi: “Kizazi kiovu na chenye uzinzi kinaendelea kutafuta ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ishara ya nabii Yona.”—Mathayo 12:38, 39.

Yesu hataki wabaki wakijiuliza alimaanisha nini, basi anasema: “Kama vile Yona alivyokuwa katika tumbo la samaki mkubwa kwa siku tatu mchana na usiku, ndivyo Mwana wa binadamu atakavyokuwa katika moyo wa ardhi siku tatu mchana na usiku.” Yona alimezwa na samaki mkubwa lakini baadaye alitoka kana kwamba amefufuliwa. Hivyo, Yesu anatabiri kwamba yeye mwenye atakufa na siku ya tatu atafufuliwa. Baadaye, inapotukia hivyo, viongozi wa Kiyahudi wanapinga ‘ishara ya Yona,’ wakikataa kutubu na kugeuka. (Mathayo 27:63-66; 28:12-15) Tofauti na hilo, “watu wa Ninawi” walitubu baada ya Yona kuwahubiria. Basi watakihukumu kizazi hiki. Yesu pia anasema kwamba vilevile Malkia wa Sheba kupitia mfano wake atawashutumu. Alitamani kusikia hekima ya Sulemani na  alishangazwa nayo. Sasa Yesu anasema, “hapa pana mtu mkuu kuliko Sulemani.”—Mathayo 12:40-42.

Yesu analinganisha hali ya kizazi hiki kiovu na mtu ambaye anatokwa na roho mwovu. (Mathayo 12:45) Kwa sababu mtu huyo hajazi vitu vyema kwenye nafasi iliyoachwa, yule roho mwovu anarudi akiwa na roho wengine saba waovu zaidi yake na kumwingia. Vivyo hivyo, taifa la Israeli lilikuwa limesafishwa na kubadilika—kama yule mtu aliyetokwa na roho mwovu. Lakini taifa hilo liliwakataa manabii wa Mungu, kufikia hatua ya kumpinga yule ambaye ni wazi kwamba ana roho ya Mungu, yaani, Yesu. Hilo linaonyesha kwamba hali ya taifa hili ni mbaya kuliko mwanzoni.

Yesu akiwa anaongea, mama yake na ndugu zake wanafika na kusimama karibu na umati. Baadhi ya wale walioketi karibu naye wanasema: “Mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kukuona.” Kisha Yesu anaonyesha jinsi alivyo na uhusiano wa karibu na wanafunzi wake, ambao ni kama ndugu, dada, na mama zake halisi. Ananyoosha mkono wake kuelekea wanafunzi wake na kusema: “Mama yangu na ndugu zangu ni hawa wanaosikia neno la Mungu na kulitenda.” (Luka 8:20, 21) Hivyo anaonyesha kuwa licha ya kwamba uhusiano wake na watu wake wa ukoo una thamani sana, uhusiano na wanafunzi wake una thamani hata zaidi. Inaburudisha sana kuwa na uhusiano kama huo na ndugu zetu wa kiroho, hasa wengine wanapotilia shaka au kutushutumu sisi na matendo yetu mazuri!