Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SURA YA 108

Yesu Apangua Njama za Kumtega

Yesu Apangua Njama za Kumtega

MATHAYO 22:15-40 MARKO 12:13-34 LUKA 20:20-40

  • VITU VYA KAISARI KWA KAISARI

  • JE, KUTAKUWA NA NDOA KATIKA UFUFUO?

  • AMRI KUU ZAIDI

Viongozi wa kidini ambao ni maadui za Yesu wamekasirika. Ametoka tu kusimulia mifano inayofunua uovu wao. Sasa Mafarisayo wanapanga njama ili kumnasa. Wanajaribu kumfanya aseme jambo litakalofanya wamkabidhi kwa gavana Mroma, basi wanawalipa baadhi ya wanafunzi wao ili wamtege.—Luka 6:7.

Wanasema: “Mwalimu, tunajua wewe husema na kufundisha kwa usahihi na huna ubaguzi, bali unafundisha njia ya Mungu kupatana na kweli: Je, ni halali au si halali kwetu kumlipa Kaisari kodi?” (Luka 20:21, 22) Yesu hapumbazwi wanapomsifu-sifu, kwa maana wamejaa unafiki na hila moyoni. Akisema, ‘Hapana, si halali kulipa kodi,’ anaweza kushtakiwa kwa uchochezi dhidi ya Roma. Lakini akisema, ‘Ndiyo, lipeni kodi hiyo,’ watu waliochoshwa kuwa chini ya utawala wa Roma, wanaweza kumwelewa vibaya na kuanza kumshambulia. Basi anajibuje?

Yesu anajibu hivi: “Kwa nini mnanijaribu, ninyi wanafiki? Nionyesheni sarafu ya kodi.” Wanaleta dinari, kisha anawauliza: “Sura hii na maandishi haya ni ya nani?” Wanajibu: “Ni ya Kaisari.” Kisha Yesu anatoa mwongozo huu thabiti: “Basi, mlipeni Kaisari vitu vya Kaisari, na Mungu vitu vya Mungu.”—Mathayo 22:18-21.

Watu hao wanashangazwa na maneno ya Yesu. Wakiwa wamenyamazishwa baada ya Yesu kuwajibu kwa ustadi, wanaondoka. Lakini bado siku haijaisha, wala jitihada za kumnasa  hazijakwisha. Mafarisayo wanapokosa kufanikiwa, viongozi wa kikundi kingine cha kidini wanamkaribia Yesu.

Masadukayo, ambao husema hakuna ufufuo, wanauliza swali linalohusu ufufuo na desturi ya mtu kuoa mke wa ndugu yake aliyekufa. Wanauliza hivi: “Mwalimu, Musa alisema: ‘Mtu yeyote akifa bila kupata watoto, ndugu yake anapaswa kumwoa mke wake ili kumwinulia ndugu yake uzao.’ Basi kulikuwa na ndugu saba kati yetu. Wa kwanza akaoa kisha akafa, na kwa sababu hakuwa na watoto, akamwachia ndugu yake mke wake. Ikawa vivyo hivyo kwa yule wa pili na wa tatu, na kwa wote saba. Mwishowe, yule mwanamke akafa. Basi, katika ufufuo, atakuwa mke wa nani kati ya wale saba? Kwa maana aliolewa na wote.”—Mathayo 22:24-28.

Akirejelea maandishi ya Musa, ambayo Masadukayo wanayakubali, Yesu anajibu hivi: “Ninyi mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko wala nguvu za Mungu. Kwa maana wanapofufuliwa kutoka kwa wafu, wanaume hawaoi wala wanawake hawaolewi, bali wao ni kama malaika mbinguni. Lakini kuhusu kufufuliwa kwa wafu, je, hamkusoma katika kitabu cha Musa, simulizi kuhusu kile kichaka cha miiba kwamba Mungu alimwambia: ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo’? Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Mmekosea sana.” (Marko 12:24-27; Kutoka 3:1-6) Umati unashangazwa na jibu lake.

Yesu amewanyamazisha Mafarisayo na Masadukayo, basi wapinzani hao wa kidini wanaungana kisha wanakuja kumjaribu tena. Mwandishi mmoja anauliza: “Mwalimu, ni amri gani iliyo kuu zaidi katika Sheria?”—Mathayo 22:36.

Yesu anajibu: “Ya kwanza ni hii, ‘Sikilizeni, enyi Waisraeli, Yehova Mungu wetu ni Yehova mmoja, nawe lazima umpende Yehova Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa nafsi yako yote na kwa akili yako yote na kwa nguvu zako zote.’ Ya pili ni hii, ‘Lazima umpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’ Hakuna amri nyingine iliyo kubwa kuliko amri hizi.”—Marko 12:29-31.

Yule mwandishi anaposikia jibu hilo anasema: “Mwalimu, umesema vema kupatana na kweli, ‘Yeye ni Mmoja, na hakuna mwingine isipokuwa yeye’; na kumpenda Mungu kwa moyo wote na kwa uelewaji wote na kwa nguvu zote na pia mtu kumpenda jirani yake kama anavyojipenda mwenyewe ni bora kuliko matoleo yote mazima ya kuteketezwa na dhabihu.” Yesu anapoona kwamba mwandishi huyo amejibu kwa kutumia akili, anamwambia hivi: “Wewe huko mbali na Ufalme wa Mungu.”—Marko 12:32-34.

Kwa siku tatu (Nisani 9, 10, na 11) Yesu amekuwa akifundisha hekaluni. Baadhi ya watu, kama vile mwandishi huyo, wamefurahia kumsikiliza. Lakini sivyo kwa viongozi wa kidini ambao sasa ‘hawathubutu tena kumuuliza swali.’