Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SURA YA 64

Umuhimu wa Kusamehe

Umuhimu wa Kusamehe

MATHAYO 18:21-35

  • JE, INATOSHA KUSAMEHE MARA SABA?

  • MFANO WA MTUMWA ASIYE NA REHEMA

Petro amesikia ushauri wa Yesu kuhusu jinsi ya kusuluhisha kutoelewana kati ya ndugu, yaani kujitahidi kusuluhisha bila kuwahusisha watu wengine. Lakini inaonekana Petro anataka kujua idadi hususa ya mara ambazo mtu anapaswa kusamehe.

Petro anauliza: “Bwana, ndugu yangu atanitendea dhambi mara ngapi nami nimsamehe? Mpaka mara saba?” Viongozi fulani wa kidini wanafundisha kwamba mtu anapaswa kusamehe hadi mara tatu. Basi huenda Petro akahisi kwamba atakuwa mkarimu sana ikiwa atamsamehe ndugu yake “mpaka mara saba.”—Mathayo 18:21.

Hata hivyo, wazo la kuweka hesabu ya mara ambazo mtu amekukosea halipatani na mafundisho ya Yesu. Basi anamrekebisha Petro: “Ninakuambia, si mpaka mara saba, bali mpaka mara 77.” (Mathayo 18:22) Kwa maneno mengine, anamaanisha hakuna mwisho. Hakuna idadi hususa ya mara ambazo Petro anapaswa kumsamehe ndugu yake.

Kisha Yesu anamsimulia Petro na wale wengine mfano ili kusisitiza wajibu walio nao wa kuwasamehe wengine. Unahusu mtumwa anayekataa kumwiga bwana wake mwenye rehema. Mfalme anataka kufanya hesabu na watumwa wake. Mtumwa mmoja aliye na deni kubwa la talanta 10,000 [dinari 60,000,000] analetwa kwake. Kwa kweli, hana uwezo wa kulipa deni hilo. Basi mfalme anaagiza kwamba mtumwa huyo, mke wake, na watoto wake wauzwe ili kulipia deni hilo. Anaposikia hivyo, mtumwa huyo anaanguka miguuni pa bwana wake na kumsihi: “Naomba univumilie, nitakulipa kila kitu.”—Mathayo 18:26.

Mfalme anamwonea huruma na kwa rehema anafuta deni kubwa la mtumwa huyo. Baada ya mfalme kufanya hivyo, mtumwa huyo anaenda na kumpata mtumwa mwenzake aliye na deni lake la dinari 100. Anamshika na kuanza  kumkaba koo akisema: “Nilipe ninachokudai.” Lakini mtumwa huyo anaanguka miguuni pa mtumwa anayemdai na kumsihi: “Naomba univumilie, nami nitakulipa.” (Mathayo 18:28, 29) Hata hivyo mtumwa ambaye deni lake lilifutwa na mfalme hamwigi bwana wake. Anaagiza mtumwa mwenzake aliyekuwa na deni dogo kuliko lake atupwe gerezani hadi atakapolipa deni hilo.

Kisha, Yesu anasimulia kwamba watumwa wengine ambao wanaona tendo hilo lisilo la rehema wanaenda na kumweleza bwana wao, ambaye kwa hasira anamwita mtumwa huyo na kumwambia: “Mtumwa mwovu, nilifuta deni lako lote uliponisihi. Je, hukupaswa pia kumwonyesha rehema mwenzako kama nilivyokuonyesha rehema?” Kisha mfalme akiwa amekasirika anamkabidhi mtumwa huyo asiye na rehema kwa walinzi wa jela hadi atakapolipa deni lote. Yesu anamalizia kwa kusema: “Baba yangu wa mbinguni atawatendea ninyi vivyo hivyo ikiwa kila mmoja wenu hatamsamehe ndugu yake kutoka moyoni.”—Mathayo 18:32-35.

Tunajifunza somo muhimu sana kuhusu kusamehe kutokana na mfano huo! Mungu ametusamehe deni kubwa la dhambi. Makosa yoyote ambayo Mkristo mwenzetu anaweza kututendea ni madogo zaidi. Na Yehova anatusamehe si mara moja tu bali mara nyingi sana. Je, hatuwezi kumsamehe ndugu yetu mara kadhaa, hata tunapokuwa na sababu ya kulalamika? Kama Yesu alivyofundisha katika Mahubiri ya Mlimani, Mungu ‘atatusamehe madeni yetu, kama vile tunavyowasamehe wadeni wetu.’—Mathayo 6:12.