Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 SURA YA 8

Wanaokoka Kutoka kwa Mtawala Mwovu

Wanaokoka Kutoka kwa Mtawala Mwovu

MATHAYO 2:13-23

  • FAMILIA YA YESU INAKIMBILIA MISRI

  • YOSEFU ANAIHAMISHIA FAMILIA YAKE NAZARETI

Yosefu anamwamsha Maria ili kumpa habari fulani muhimu. Hivi punde tu malaika wa Yehova amemtokea katika ndoto akimwambia: “Simama, mchukue huyo mtoto na mama yake mkimbilie Misri, mkae huko mpaka nitakapokwambia, kwa maana Herode yuko karibu kumtafuta huyo mtoto ili amuue.”—Mathayo 2:13.

Bila kukawia, Yosefu, Maria na mwana wao wanaondoka usiku. Wanaondoka wakati unaofaa, kwa sababu Herode amegundua kwamba wanajimu wamemdanganya. Alikuwa amewaambia wampelekee jibu. Badala yake waliondoka bila kumwambia. Herode amekasirika sana. Akiwa bado anataka kumuua Yesu, anatoa amri ya kuwaua wavulana wote wenye umri wa kuanzia miaka miwili kushuka chini walio Bethlehemu na maeneo yaliyo karibu. Anakadiria umri huo kwa kutegemea mambo aliyokuwa ameambiwa na wanajimu waliokuja kutoka Mashariki.

Ni jambo linalochukiza sana kuwaua wavulana wote! Hatuwezi kujua ni wavulana wangapi waliouawa, lakini kilio cha uchungu na maombolezo ya akina mama waliofiwa yanatimiza unabii wa Biblia uliotabiriwa na Yeremia, nabii wa Mungu.—Yeremia 31:15.

Wakati huohuo, Yosefu na familia yake wamekimbilia Misri, nao wanaendelea kuishi huko. Kisha usiku mmoja malaika wa Yehova anamtokea tena Yosefu katika ndoto. Malaika anasema: “Simama, umchukue mtoto na mama yake, nanyi mrudi katika nchi ya Israeli, kwa sababu wale waliotaka kumuua mtoto wamekufa.” (Mathayo 2:20) Kwa hiyo Yosefu anaamua kwamba familia inaweza kurudi katika nchi yao. Kwa njia hiyo unabii mwingine wa Biblia unatimizwa—Mwana wa Mungu anaitwa kutoka Misri.—Hosea 11:1.

 Inaonekana, Yosefu anapanga familia yake ikae Yudea, labda karibu na mji wa Bethlehemu, ambako walikuwa wanaishi kabla ya kukimbilia Misri. Lakini anagundua kwamba Arkelao mwana mwovu wa Herode ndiye mfalme wa Yudea. Katika ndoto nyingine, Mungu anamwonya Yosefu kuhusu hatari hiyo. Basi, Yosefu na familia yake wanasafiri kwenda kaskazini na kuishi katika jiji la Nazareti lililo katika eneo la Galilaya, mbali na kitovu cha maisha ya dini ya Kiyahudi. Yesu analelewa katika jamii hii, jambo hilo linatimiza unabii mwingine: “Ataitwa Mnazareti.”—Mathayo 2:23.