Mwanzo 9:1-29

  • Maagizo kwa wanadamu wote (1-7)

    • Sheria kuhusu damu (4-6)

  • Agano la upinde (8-17)

  • Unabii mbalimbali kuhusu wazao wa Noa (18-29)

9  Basi Mungu akambariki Noa na wanawe na kuwaambia: “Zaeni muwe wengi na kuijaza dunia.+  Kila kiumbe aliye hai duniani na kila kiumbe anayeruka angani na kila kiumbe anayetambaa ardhini na samaki wote wa baharini wataendelea kuwaogopa na kuwahofu ninyi. Sasa nimewatia mikononi mwenu.*+  Kila mnyama aliye hai anayetembea anaweza kuwa chakula chenu.+ Kama nilivyowapa mimea, ninawapa hao wote wawe chakula chenu.+  Ila tu nyama pamoja na uhai wake*—damu yake+—hampaswi kula.+  Zaidi ya hayo, nitadai muwajibike kwa sababu ya damu ya uhai wenu.* Nitadai kila kiumbe aliye hai awajibike; nami nitamdai kila mwanadamu awajibike kwa sababu ya uhai wa ndugu yake.+  Yeyote anayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake mwenyewe itamwagwa+ na mwanadamu, kwa maana Mungu alimuumba mwanadamu+ kwa mfano Wake.  Lakini ninyi, zaeni muwe wengi, mwongezeke kwa wingi na kujaa+ duniani.”  Kisha Mungu akamwambia Noa na wanawe:  “Sasa ninafanya agano langu pamoja nanyi+ na pamoja na wazao wenu baada yenu, 10  na pamoja na kila kiumbe aliye hai ambaye yupo* pamoja nanyi, ndege, wanyama, na viumbe wote walio hai duniani pamoja nanyi, wote waliotoka ndani ya safina—kila kiumbe aliye hai duniani.+ 11  Naam, ninafanya agano langu pamoja nanyi: Viumbe wote* hawataangamizwa tena kamwe kwa maji ya gharika, na gharika haitaiharibu+ dunia tena kamwe.” 12  Na Mungu akaendelea kusema: “Hii ndiyo ishara ya agano ninalofanya pamoja nanyi na pamoja na kila kiumbe hai aliye pamoja nanyi, kwa vizazi vyote vijavyo. 13  Ninauweka upinde wangu wa mvua mawinguni, nao utakuwa ishara ya agano nililofanya na dunia. 14  Kila mara ninapoleta mawingu juu ya dunia, kwa hakika upinde wa mvua utaonekana mawinguni. 15  Nami hakika nitakumbuka agano langu nililofanya pamoja nanyi na pamoja na kila aina ya kiumbe aliye hai; na kamwe hakutakuwa tena na gharika ya maji itakayowaangamiza viumbe wote.+ 16  Na upinde wa mvua utatokea mawinguni, nami hakika nitauona na kukumbuka agano la milele ambalo mimi Mungu nilifanya pamoja na kila aina ya kiumbe hai duniani.” 17  Mungu akarudia kumwambia Noa: “Hii ndiyo ishara ya agano ninalofanya pamoja na viumbe wote walio duniani.”+ 18  Hawa ndio wana wa Noa waliotoka ndani ya safina: Shemu, Hamu, na Yafethi.+ Baadaye Hamu akamzaa Kanaani.+ 19  Hao watatu walikuwa wana wa Noa, na watu wote duniani walitokana nao na kuenea kotekote.+ 20  Sasa Noa akaanza kulima, akapanda shamba la mizabibu. 21  Alipokunywa divai, alilewa, naye akavua nguo ndani ya hema lake. 22  Hamu, baba ya Kanaani, akamwona baba yake akiwa uchi, akawaambia ndugu zake wawili waliokuwa nje. 23  Kwa hiyo Shemu na Yafethi wakachukua nguo na kuiweka mabegani mwao na kuingia ndani kinyumenyume. Basi wakaufunika uchi wa baba yao huku nyuso zao zikitazama pembeni, nao hawakuuona uchi wa baba yao. 24  Divai ilipomtoka Noa, naye akasikia jambo ambalo mwanawe mdogo alimtendea, 25  akasema: “Alaaniwe Kanaani.+ Na awe mtumwa wa hali ya chini kabisa kwa ndugu zake.”+ 26  Pia akasema: “Asifiwe Yehova, Mungu wa Shemu,Acha Kanaani awe mtumwa wake.+ 27  Mungu na ampe Yafethi nafasi ya kutosha,Na akae katika mahema ya Shemu. Kanaani na awe mtumwa wake pia.” 28  Noa akaendelea kuishi miaka 350 baada ya Gharika.+ 29  Basi siku zote za maisha ya Noa zilikuwa miaka 950, kisha akafa.

Maelezo ya Chini

Au “nimewaweka chini ya mamlaka yenu.”
Au “nafsi yake.”
Au “damu ya nafsi zenu.”
Au “nafsi iliyo hai iliyo.”
Au “Viumbe wote walio hai.”