Mwanzo 14:1-24

  • Abramu amwokoa Loti (1-16)

  • Melkizedeki ambariki Abramu (17-24)

14  Sasa katika siku za Amrafeli mfalme wa Shinari,+ Arioko mfalme wa Elasari, Kedorlaoma+ mfalme wa Elamu,+ na Tidali mfalme wa Goiimu,  wafalme hawa walikwenda kupigana vita na Bera mfalme wa Sodoma,+ Birsha mfalme wa Gomora,+ Shinabu mfalme wa Adma, Shemeberi mfalme wa Seboiimu,+ na mfalme wa Bela, yaani, Soari.  Hao wote waliungana pamoja katika Bonde la* Sidimu,+ yaani, Bahari ya Chumvi.+  Walikuwa wamemtumikia Kedorlaoma kwa miaka 12, lakini wakaasi katika mwaka wa 13.  Kwa hiyo katika mwaka wa 14, Kedorlaoma na wafalme waliokuwa pamoja naye wakaja na kuwashinda Warefaimu waliokuwa Ashteroth-karnaimu, Wazuzi waliokuwa Hamu, Waemi+ waliokuwa Shave-kiriathaimu,  na Wahori+ katika mlima wao wa Seiri+ na kuteremka mpaka El-parani, eneo lililo nyikani.  Kisha wakarudi nyuma na kwenda En-mishpati, yaani, Kadeshi,+ wakashinda eneo lote la Waamaleki+ na pia Waamori+ waliokuwa wakiishi Hasason-tamari.+  Ndipo mfalme wa Sodoma akapiga mwendo, na pia mfalme wa Gomora, mfalme wa Adma, mfalme wa Seboiimu, na mfalme wa Bela, yaani, Soari, nao wakajipanga kivita ili kupigana nao katika Bonde la* Sidimu,  ili kupigana na Kedorlaoma mfalme wa Elamu, Tidali mfalme wa Goiimu, Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari+—wafalme wanne dhidi ya wale watano. 10  Sasa Bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami, na wafalme wa Sodoma na Gomora walijaribu kutoroka lakini wakaanguka humo, na wale waliobaki wakakimbilia eneo lenye milima. 11  Kisha washindi wakachukua mali zote za Sodoma na Gomora na chakula chao chote na kwenda zao.+ 12  Pia wakamchukua Loti, mwana wa ndugu ya Abramu ambaye alikuwa akikaa Sodoma,+ na vilevile wakachukua mali zake, wakaenda zao. 13  Baada ya hayo mtu mmoja aliyetoroka akaja na kumletea habari Abramu Mwebrania. Wakati huo alikuwa akiishi karibu na miti mikubwa ya Mamre yule Mwamori,+ ndugu ya Eshkoli na Aneri.+ Wanaume hao walikuwa marafiki wa Abramu. 14  Hivyo Abramu akasikia kwamba mtu wake wa ukoo*+ alikuwa ametekwa. Kwa hiyo akawakusanya wanaume wake waliozoezwa, watumishi 318 waliozaliwa nyumbani mwake, wakawafuatia mpaka Dani.+ 15  Wakati wa usiku, akavigawa vikosi vyake, yeye na watumishi wake wakawashambulia na kuwashinda. Naye akawafuatia mpaka Hoba, upande wa kaskazini wa Damasko. 16  Alipata mali zote zilizochukuliwa, na pia akamwokoa Loti mtu wake wa ukoo, mali zake, wanawake, na watu wengine. 17  Abramu aliporudi baada ya kumshinda Kedorlaoma na wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma alienda kukutana na Abramu kwenye Bonde la* Shave, yaani, Bonde la Mfalme.+ 18  Na Melkizedeki+ mfalme wa Salemu+ akaleta mkate na divai; alikuwa kuhani wa Mungu Aliye Juu Zaidi.+ 19  Kisha akambariki Abramu na kumwambia: “Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye Juu Zaidi,Muumba wa mbingu na dunia; 20  Na asifiwe Mungu Aliye Juu Zaidi,Ambaye amewatia mikononi mwako wale wanaokukandamiza!” Na Abramu akampa sehemu ya kumi ya vitu vyote.+ 21  Baada ya hayo mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu: “Nipe hao watu, lakini chukua mali.” 22  Lakini Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma: “Ninauinua mkono wangu na kuapa kwa Yehova, Mungu Aliye Juu Zaidi, Muumba wa mbingu na dunia, 23  kwamba sitachukua kitu chochote ambacho ni chako, kuanzia uzi mpaka kamba ya kiatu, ili usije ukasema, ‘Nilimtajirisha Abramu.’ 24  Sitachukua chochote isipokuwa kile ambacho wanaume hawa vijana wamekula tayari. Lakini kuhusu fungu la watu walioenda pamoja nami, Aneri, Eshkoli, na Mamre+—acha wachukue fungu lao.”

Maelezo ya Chini

Au “Nchi Tambarare ya Chini ya.”
Au “Nchi Tambarare ya Chini ya.”
Tnn., “ndugu yake.”
Au “Nchi Tambarare ya Chini ya.”