Mwanzo 16:1-16

  • Hagari na Ishmaeli (1-16)

16  Sasa Sarai mke wa Abramu hakuwa amemzalia mtoto yeyote,+ lakini alikuwa na mtumishi Mmisri aliyeitwa Hagari.+  Basi Sarai akamwambia Abramu: “Sasa tafadhali! Yehova amenizuia nisizae watoto. Tafadhali, lala na mtumishi wangu. Huenda nikapata watoto kupitia yeye.”+ Kwa hiyo Abramu akasikiliza maneno ya Sarai.  Baada ya Abramu kuishi katika nchi ya Kanaani kwa miaka kumi, Sarai mke wa Abramu akamchukua Hagari, mtumishi wake Mmisri na kumpa Abramu mumewe awe mke wake.  Basi Abramu akalala na Hagari, naye akapata mimba. Alipogundua kwamba ana mimba, alianza kumdharau bimkubwa wake.  Ndipo Sarai akamwambia Abramu: “Ni wewe uliyesababisha madhara ninayotendewa. Ni mimi niliyemweka mtumishi wangu mikononi mwako,* lakini alipogundua kwamba ana mimba, alianza kunidharau. Yehova na awe mwamuzi kati yangu na wewe.”  Basi Abramu akamwambia Sarai: “Tazama! Mtumishi wako yuko chini ya mamlaka yako. Mtendee lolote unaloona ni jema.” Kisha Sarai akamfedhehesha Hagari, naye akamkimbia.  Baadaye malaika wa Yehova akamkuta kwenye chemchemi ya maji nyikani, chemchemi iliyo njiani kuelekea Shuri.+  Naye akamuuliza: “Hagari, mtumishi wa Sarai, umetoka wapi na unaenda wapi?” Ndipo akajibu: “Ninamkimbia Sarai, bimkubwa wangu.”  Basi malaika wa Yehova akamwambia: “Rudi kwa bimkubwa wako na ujinyenyekeze chini ya mkono wake.” 10  Kisha malaika wa Yehova akasema: “Nitawazidisha sana wazao wako, hivi kwamba watakuwa wengi sana wasiweze kuhesabiwa.”+ 11  Malaika wa Yehova akaendelea kusema: “Sasa una mimba, nawe utazaa mwana, nawe unapaswa kumpa jina Ishmaeli,* kwa maana Yehova amesikia mateso yako. 12  Atakuwa mtu aliye kama pundamwitu.* Mkono wake utapigana na kila mtu, na mkono wa kila mtu utapigana naye, naye atakaa akielekeana na ndugu zake wote.”* 13  Ndipo akaliitia jina la Yehova, aliyekuwa akizungumza naye: “Wewe ni Mungu anayeona,”+ kwa kuwa alisema: “Je, ni kweli kwamba nimemwona hapa yeye ambaye huniona?” 14  Ndiyo sababu kisima hicho kiliitwa Beer-lahai-roi.* (Kiko kati ya Kadeshi na Beredi.) 15  Basi Hagari akamzalia Abramu mwana, naye Abramu akamwita huyo mwanawe ambaye Hagari alimzaa, Ishmaeli.+ 16  Abramu alikuwa na umri wa miaka 86 Hagari alipomzaa Ishmaeli.

Maelezo ya Chini

Tnn., “kifuani pako.”
Maana yake “Mungu Husikia.”
Baadhi ya watu hudhani ni pundamilia. Yaelekea ametumiwa kurejelea mtazamo wa kujitegemea.
Au labda, “naye ataishi kwa uhasama na ndugu zake wote.”
Maana yake “Kisima cha Aliye Hai Ambaye Huniona.”