Mwanzo 11:1-32

  • Mnara wa Babeli (1-4)

  • Yehova avuruga lugha (5-9)

  • Kuanzia Shemu hadi Abramu (10-32)

    • Familia ya Tera (27)

    • Abramu ahama Uru (31)

11  Sasa dunia yote iliendelea kuwa na lugha moja na maneno yaleyale.*  Walipokuwa wakisafiri kuelekea mashariki, waligundua bonde tambarare katika nchi ya Shinari,+ wakaanza kuishi huko.  Kisha wakaambiana: “Njooni! Tufyatue matofali na kuyachoma.” Basi wakatumia matofali badala ya mawe, na lami badala ya saruji.  Sasa wakasema: “Haya! Na tujijengee jiji na mnara ambao kilele chake kitafika mbinguni, na tujijengee jina maarufu, ili tusitawanyike katika dunia yote.”+  Kisha Yehova akashuka ili aone jiji na mnara ambao wanadamu walikuwa wamejenga.  Ndipo Yehova akasema: “Tazama! Watu hawa ni kitu kimoja na wanazungumza lugha moja,+ na hili ndilo jambo waliloanza kufanya. Sasa hakuna jambo lolote wanalokusudia kufanya litakalowashinda.  Njooni! Tushuke+ huko na kuvuruga lugha yao ili kila mmoja wao asiielewe lugha ya mwenzake.”  Basi Yehova akawatawanya duniani pote+ kutoka huko, na hatua kwa hatua wakaacha kujenga jiji hilo.  Ndiyo sababu liliitwa Babeli,*+ kwa sababu huko ndiko Yehova alikovuruga lugha ya dunia yote, na kutoka huko Yehova aliwatawanya duniani pote. 10  Hii ndiyo historia ya Shemu.+ Shemu alikuwa na umri wa miaka 100 alipomzaa Arpakshadi+ miaka miwili baada ya Gharika. 11  Baada ya kumzaa Arpakshadi, Shemu aliishi miaka 500. Akazaa wana na mabinti.+ 12  Arpakshadi alipokuwa na umri wa miaka 35, alimzaa Shela.+ 13  Baada ya kumzaa Shela, Arpakshadi aliishi miaka 403. Akazaa wana na mabinti. 14  Shela alipokuwa na umri wa miaka 30, alimzaa Eberi.+ 15  Baada ya kumzaa Eberi, Shela aliishi miaka 403. Akazaa wana na mabinti. 16  Eberi alipokuwa na umri wa miaka 34, alimzaa Pelegi.+ 17  Baada ya kumzaa Pelegi, Eberi aliishi miaka 430. Akazaa wana na mabinti. 18  Pelegi alipokuwa na umri wa miaka 30, alimzaa Reu.+ 19  Baada ya kumzaa Reu, Pelegi aliishi miaka 209. Akazaa wana na mabinti. 20  Reu alipokuwa na umri wa miaka 32, alimzaa Serugi. 21  Baada ya kumzaa Serugi, Reu aliishi miaka 207. Akazaa wana na mabinti. 22  Serugi alipokuwa na umri wa miaka 30, alimzaa Nahori. 23  Baada ya kumzaa Nahori, Serugi aliishi miaka 200. Akazaa wana na mabinti. 24  Nahori alipokuwa na umri wa miaka 29, alimzaa Tera.+ 25  Baada ya kumzaa Tera, Nahori aliishi miaka 119. Akazaa wana na mabinti. 26  Tera alipokuwa na umri wa miaka 70, alimzaa Abramu,+ Nahori,+ na Harani. 27  Hii ndiyo historia ya Tera. Tera alimzaa Abramu, Nahori, na Harani; naye Harani akamzaa Loti.+ 28  Tera, baba yake, alipokuwa bado hai, Harani alikufa katika nchi alimozaliwa, katika jiji la Uru+ la Wakaldayo.+ 29  Abramu na Nahori wakapata wake. Mke wa Abramu aliitwa Sarai,+ na mke wa Nahori aliitwa Milka, binti ya Harani, baba ya Milka+ na Iska. 30  Sasa Sarai alikuwa tasa;+ hakuwa na mtoto. 31  Kisha Tera akamchukua Abramu mwanawe na Loti mjukuu wake,+ mwana wa Harani, na Sarai binti mkwe wake, mke wa Abramu mwanawe, wakaondoka pamoja naye katika jiji la Uru la Wakaldayo ili kwenda katika nchi ya Kanaani.+ Baada ya muda wakafika Harani+ na kuanza kukaa huko. 32  Tera aliishi miaka 205. Kisha Tera akafa huko Harani.

Maelezo ya Chini

Au “msamiati uleule.”
Maana yake “Vurugu.”