Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kamusi ya Maneno ya Biblia

  A     B     C     D     E     F     G     H     I     J     K     L     M     N     O     P     R     S     T     U     V     W     Y     Z  

A

 • Abi.

  Jina la mwezi wa 5 katika kalenda takatifu ya Wayahudi baada ya kutoka uhamishoni Babiloni na jina la mwezi wa 11 katika kalenda iliyotumiwa na watu wote. Mwezi huo ulianzia katikati ya mwezi wa Julai mpaka katikati ya mwezi wa Agosti. Jina la mwezi huo halitajwi katika Biblia; unarejelewa tu kuwa “mwezi wa tano.” (Hes 33:38; Ezr 7:9)—Angalia Nyongeza B15.

 • Abibu.

  Jina asilia la mwezi wa kwanza katika kalenda takatifu ya Wayahudi na mwezi wa saba katika kalenda iliyotumiwa na watu wote. Jina hilo linamaanisha “Masuke Mabichi (ya Nafaka)” na mwezi huo ulianzia katikati ya mwezi wa Machi mpaka katikati ya mwezi wa Aprili. Baada ya Wayahudi kurudi kutoka uhamishoni, mwezi huo uliitwa Nisani. (Kum 16:1)—Angalia Nyongeza B15.

 • Abiso.

  Neno hili linatokana na neno la Kigiriki aʹbys·sos, linalomaanisha “-enye kina kirefu sana” au “bila mwisho, bila mipaka.” Linatumiwa katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo kumaanisha mahali au hali ya kuwa kifungoni. Linamaanisha pia kaburi lakini lina maana pana zaidi.—Lu 8:31; Ro 10:7; Ufu 20:3.

 • Adari.

  Jina la mwezi wa 12 katika kalenda takatifu ya Wayahudi baada ya kutoka uhamishoni Babiloni na jina la mwezi wa 6 katika kalenda iliyotumiwa na watu wote. Mwezi huo ulianzia katikati ya mwezi wa Februari mpaka katikati ya mwezi wa Machi. (Est 3:7)—Angalia Nyongeza B15.

 • Agano.

  Makubaliano rasmi, au mkataba, kati ya Mungu na wanadamu au kati ya wanadamu wawili ya kufanya au kutofanya jambo fulani. Nyakati fulani ni upande mmoja tu uliokuwa na jukumu la kutekeleza masharti ya agano hilo (agano la upande mmoja ambalo kimsingi lilikuwa ahadi). Nyakati nyingine pande zote mbili zilipaswa kutimiza masharti fulani (agano la pande mbili). Mbali na maagano ambayo Mungu alifanya na wanadamu, Biblia hutaja pia maagano kati ya wanadamu, makabila, mataifa, au vikundi vya watu. Miongoni mwa maagano ambayo yamekuwa na manufaa makubwa sana ni agano ambalo Mungu alifanya na Abrahamu, Daudi, taifa la Israeli (agano la Sheria), na Israeli wa Mungu (agano jipya).—Mwa 9:11; 15:18; 21:27; Kut 24:7; 2Nya 21:7.

 • Akaya.

  Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, Akaya ni mkoa wa Roma uliokuwa kusini mwa Ugiriki, na jiji kuu lilikuwa Korintho. Mkoa wa Akaya ulitia ndani eneo lote la Peloponesi na eneo la kati la bara nchini Ugiriki. (Mdo 18:12)—Angalia Nyongeza B13.

 • Alabasta.

  Jina la chupa ndogo za manukato ambazo awali zilitengenezwa kwa jiwe lililopatikana karibu na Alabastroni, Misri. Kwa kawaida chupa hizo zilitengenezwa zikiwa na shingo nyembamba ambayo ingeweza kuzibwa ili kuzuia manukato hayo yenye thamani yasivuje. Hatimaye jiwe hilo lilijulikana kwa jina hilo.—Mk 14:3.

 • Alamothi.

  Neno la kimuziki linalomaanisha “Wanawali; Wanawake Vijana,” huenda linarejelea sauti za juu (soprano) za wanawake vijana. Inaelekea lilitumiwa kuonyesha kwamba muziki ulipaswa kuimbwa au ala ilipaswa kuchezwa kwa sauti ya juu.—1Nya 15:20; Zb 46:Utangulizi.

 • Alfa na Omega.

  Ni herufi ya kwanza na herufi ya mwisho katika alfabeti ya Kigiriki; maneno hayo yanatumiwa pamoja mara tatu katika kitabu cha Ufunuo kurejelea cheo cha Mungu. Katika Maandiko hayo, maneno hayo yanamaanisha “wa kwanza na wa mwisho” na “mwanzo na mwisho.”—Ufu 1:8; 21:6; 22:13.

 • Amina.

  “Na iwe hivyo,” au “bila shaka.” Neno hili linatokana na shina la Kiebrania ʼa·manʹ, linalomaanisha “kuwa mwaminifu, kuaminika.” Neno “Amina” lilisemwa ili kukubali kiapo, sala, au taarifa fulani. Katika Ufunuo, linatumiwa likiwa cheo cha Yesu.—Kum 27:26; 1Nya 16:36; Ufu 3:14.

 • Andiko (Maandiko).

  Maandishi matakatifu ya Neno la Mungu. Neno hilo linapatikana tu katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo.—Lu 24:27; 2Ti 3:16.

 • Aramu; Waaramu.

  Wazao wa Aramu mwana wa Shemu ambao waliishi hasa katika maeneo ya Milima ya Lebanoni mpaka Mesopotamia na kuanzia Milima ya Taurusi upande wa kaskazini na kushuka mpaka Damasko na mbele zaidi upande wa kusini. Eneo hilo, linaloitwa Aramu katika Kiebrania, baadaye liliitwa Siria, na wakaaji wake waliitwa Wasiria.—Mwa 25:20; Kum 26:5; Ho 12:12.

 • Areopago.

  Kilima kirefu kilicho katika jiji la Athene, upande wa kaskazini magharibi wa Akropoli. Lilikuwa pia jina la baraza au mahakama iliyofanyia mikutano huko. Wanafalsafa Wastoa na Waepikurea walimleta Paulo Areopago ili afafanue mambo aliyoamini.—Mdo 17:19.

 • Aselgeia.​

  Tazama MWENENDO MPOTOVU.

 • Ashtorethi.

  Mungu wa kike wa Wakanaani, wa vita na uzazi, mke wa Baali.—1Sa 7:3.

 • Asia.

  Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, Asia ni jina la mkoa wa Roma ambao ulitia ndani eneo ambalo sasa ni eneo la magharibi nchini Uturuki, na pia visiwa fulani vya pwani, kama vile Samosi na Patmo. Jiji kuu lilikuwa Efeso. (Mdo 20:16; Ufu 1:4)—Angalia Nyongeza B13.

 • Azazeli.

  Jina la Kiebrania ambalo huenda linamaanisha “Mbuzi Anayetoweka.” Katika Siku ya Kufunika Dhambi, mbuzi aliyechaguliwa kuwa wa Azazeli alipelekwa na kuachiliwa nyikani, na hivyo kwa njia ya mfano alibeba dhambi za taifa za mwaka uliopita na kwenda nazo.—Law 16:8, 10.

 • B

 • Baali.

  Mungu wa Wakanaani aliyeonwa kuwa mmiliki wa anga na mpaji wa mvua na uzazi. Neno “Baali” lilitumiwa pia kurejelea miungu mingine midogo. Katika Kiebrania neno hilo linamaanisha “Mmiliki; Bwana.”—1Fa 18:21; Ro 11:4.

 • Bathi.

  Kipimo cha vitu vya majimaji kinachokadiriwa kuwa sawa na lita 22 hivi, kulingana na uchunguzi wa vigae vya kale vya magudulia vilivyokuwa na neno hilo. Katika Biblia, vipimo vingine vingi vikavu na vya vitu vya majimaji vinahesabiwa kulingana na ujazo uliokadiriwa wa kipimo cha bathi. (1Fa 7:38; Eze 45:14)—Angalia Nyongeza B14.

 • Beelzebubu au Beelzebuli.

  Jina linalotumiwa kumrejelea Shetani, ambaye ni mkuu, au mtawala, wa roho waovu. Huenda ni Baal-zebubu—jina la Baali aliyeabudiwa na Wafilisti kule Ekroni—ambalo limebadilishwa kidogo.—2Fa 1:3; Mt 12:24.

 • Buli.

  Jina la mwezi wa nane katika kalenda takatifu ya Wayahudi na jina la mwezi wa pili katika kalenda iliyotumiwa na watu wote. Jina hilo linatokana na neno linalomaanisha “tokeza mazao; zaa” na mwezi huo ulianzia katikati ya mwezi wa Oktoba mpaka katikati ya mwezi wa Novemba. (1Fa 6:38)—Angalia Nyongeza B15.

 • C

 • Chachu.

  Kitu kilichoongezwa kwenye unga uliokandwa au kwenye vitu vya majimaji ili kuvichachisha; hasa donge lililohifadhiwa la unga uliokandwa na kuchachuka. Mara nyingi chachu hutumiwa katika Biblia kufananisha dhambi na upotovu, hutumiwa pia kurejelea ukuzi unaoenea bila kuonekana.—Kut 12:20; Mt 13:33; Gal 5:9.

 • D

 • Dagoni.

  Mungu wa Wafilisti. Chanzo cha neno hili hakijulikani vizuri, lakini baadhi ya wasomi wanalihusianisha na neno la Kiebrania dagh (samaki).—Amu 16:23; 1Sa 5:4.

 • Dariki.

  Sarafu ya Kiajemi ya dhahabu yenye uzito wa gramu 8.4. (1Nya 29:7)—Angalia Nyongeza B14.

 • Dekapoli.

  Kikundi cha majiji ya Kigiriki, ambayo awali yalikuwa majiji kumi (kutokana na neno la Kigiriki deʹka, linalomaanisha “kumi,” na poʹlis, linalomaanisha “jiji”). Pia lilikuwa jina la eneo lililokuwa upande wa mashariki wa Bahari ya Galilaya na Mto Yordani, eneo lililokuwa na mengi ya majiji hayo. Majiji hayo yalikuwa vituo vya utamaduni wa Wagiriki na biashara. Yesu alipitia katika eneo hilo, lakini hakuna maandishi yoyote yanayoonyesha kwamba alitembelea mojawapo ya majiji hayo. (Mt 4:25; Mk 5:20)—Angalia Nyongeza A7 na B10.

 • Dhabihu ya dhambi.

  Dhabihu iliyotolewa kwa ajili ya dhambi iliyofanywa bila kukusudia kwa sababu ya udhaifu wa mwili usio mkamilifu. Dhabihu za wanyama mbalimbali, kuanzia ng’ombe dume mpaka njiwa, zilitolewa, kulingana na cheo na hali za yule ambaye dhambi zake zingefunikwa.—Law 4:27, 29; Ebr 10:8.

 • Dhabihu ya hatia.

  Dhabihu ya dhambi za mtu binafsi. Ilitofautiana kidogo na dhabihu nyingine za dhambi kwa sababu ilitolewa ili kutimiza au kurudisha haki fulani za agano ambazo mtenda dhambi aliyetubu alikuwa amepoteza kwa sababu ya dhambi na ili kumletea kitulizo kutokana na adhabu.—Law 7:37; 19:22; Isa 53:10.

 • Dhabihu ya kuteketezwa.

  Dhabihu ya mnyama aliyeteketezwa juu ya madhabahu na kutolewa kwa Mungu akiwa dhabihu nzima; mwabudu hakuchukua sehemu yoyote ya mnyama huyo (ng’ombe dume, kondoo dume, mbuzi dume, njiwa tetere, au huwa mchanga).—Kut 29:18; Law 6:9.

 • Dhabihu ya nadhiri.

  Ni dhabihu ya hiari iliyoambatana na nadhiri fulani.—Law 23:38; 1Sa 1:21.

 • Dhabihu ya shukrani.

  Ni dhabihu ya ushirika iliyokusudiwa kumsifu Mungu kwa sababu ya maandalizi yake na upendo wake mshikamanifu. Nyama ya mnyama aliyetolewa dhabihu ililiwa pamoja na mikate yenye chachu na mikate isiyo na chachu. Nyama hiyo ilipaswa kuliwa siku hiyohiyo.—2Nya 29:31.

 • Dhabihu ya ushirika.

  Dhabihu iliyotolewa kwa Yehova ili kuomba uhusiano wa amani pamoja naye. Mwabudu na watu wa nyumbani mwake, kuhani aliyehudumu, na makuhani waliokuwa na zamu walishiriki wote kuila. Ni kana kwamba Yehova alipokea moshi unaopendeza wa mafuta yaliyokuwa yakiteketea. Alipewa pia damu ambayo huwakilisha uhai. Ni kana kwamba makuhani na waabudu waliketi na kula pamoja na Yehova, kuonyesha kwamba walikuwa na uhusiano wenye amani.—Law 7:29, 32; Kum 27:7.

 • Dhabihu.

  Kitu ambacho mtu anamtolea Mungu ili kumshukuru, kukiri hatia, na kurudisha uhusiano mzuri pamoja naye. Kuanzia Abeli, wanadamu walitoa dhabihu mbalimbali za hiari, kutia ndani wanyama, mpaka agano la Sheria ya Musa lilipofanya kutoa dhabihu hizo kuwa jambo la lazima. Dhabihu za wanyama hazikuhitajika tena Yesu alipotoa uhai wake mwenyewe kuwa dhabihu kamilifu, ingawa Wakristo wanaendelea kumtolea Mungu dhabihu za kiroho.—Mwa 4:4; Ebr 13:15, 16; 1Yo 4:10.

 • Dhiki kuu.

  Neno la Kigiriki linalotafsiriwa “dhiki” linatoa wazo la taabu au mateso yanayosababishwa na mikazo inayoletwa na hali. Yesu alizungumza kuhusu “dhiki kuu” isiyo na kifani ambayo ingekumba jiji la Yerusalemu na hasa dhiki ambayo baadaye itawakumba wanadamu ‘atakapokuja akiwa na utukufu’ wakati ujao. (Mt 24:21, 29-31) Paulo alifafanua kwamba dhiki hiyo ni tendo la uadilifu la Mungu dhidi ya “wale wasiomjua Mungu na wale wasiotii habari njema” kumhusu Yesu Kristo. Kitabu cha Ufunuo sura ya 19 kinaonyesha kwamba Yesu ndiye anayeyaongoza majeshi ya mbinguni kupigana na “yule mnyama-mwitu na wafalme wa dunia na majeshi yao.” (2Th 1:6-8; Ufu 19:11-21) “Umati mkubwa” unaonekana ukiokoka dhiki hiyo. (Ufu 7:9, 14)—Tazama HAR-MAGEDONI.

 • Dinari.

  Sarafu ya fedha ya Kiroma iliyokuwa na uzito wa gramu 3.85 hivi na ilikuwa na picha ya Kaisari upande mmoja. Dinari ilikuwa mshahara wa siku moja wa kibarua na sarafu ya “kodi ya kichwa” ambayo Wayahudi walitozwa na Waroma. (Mt 22:17; Lu 20:24)—Angalia Nyongeza B14.

 • Drakma.

  Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, neno hili linarejelea sarafu ya fedha ya Kigiriki, ambayo wakati huo ilikuwa na uzito wa gramu 3.4. Maandiko ya Kiebrania yanataja sarafu ya drakma ya dhahabu ya enzi za Waajemi ambayo inalinganishwa na dariki. (Ne 7:70; Mt 17:24)—Angalia Nyongeza B14.

 • E

 • Edomu.

  Jina lingine alilopewa Esau, mwana wa Isaka. Wazao wa Esau (Edomu) walimiliki eneo la Seiri, eneo lenye milima kati ya Bahari ya Chumvi na Ghuba ya ‘Aqaba. Baadaye liliitwa Edomu. (Mwa 25:30; 36:8)—Angalia Nyongeza B3 na B4.

 • Efa.

  Kipimo cha vitu vikavu, na pia chombo kilichotumiwa kupimia nafaka. Kilikuwa sawa na kipimo cha bathi cha vitu vya majimaji, kwa hiyo kilikuwa sawa na lita 22. (Kut 16:36; Eze 45:10)—Angalia Nyongeza B14.

 • Efodi.

  Vazi linalofanana na kizibao lililovaliwa na makuhani. Kuhani mkuu alivaa efodi ya pekee, na upande wa mbele wa efodi hiyo ulikuwa na kifuko cha kifuani kilichokuwa na mawe 12 yenye thamani. (Kut 28:4, 6)—Angalia Nyongeza B5.

 • Efraimu.

  Jina la mwana wa pili wa Yosefu; baadaye mojawapo ya makabila ya Israeli liliitwa kwa jina hilo. Baada ya Israeli kugawanyika, Efraimu, ambalo lilikuwa kabila maarufu zaidi, liliwakilisha ufalme wote wa makabila kumi.—Mwa 41:52; Yer 7:15.

 • Efrati.

  Mto mrefu zaidi na muhimu zaidi kusini magharibi mwa Asia, na mojawapo ya mito miwili mikubwa Mesopotamia. Unatajwa kwa mara ya kwanza katika Mwanzo 2:14 ukiwa mojawapo ya mito minne ya Edeni. Kwa kawaida unaitwa “ule Mto.” (Mwa 31:21) Ulikuwa mpaka wa kaskazini wa eneo ambalo Waisraeli walipewa. (Mwa 15:18; Ufu 16:12)—Angalia Nyongeza B2.

 • Eluli.

  Jina la mwezi wa 6 katika kalenda takatifu ya Wayahudi baada ya kutoka uhamishoni Babiloni na jina la mwezi wa 12 katika kalenda iliyotumiwa na watu wote. Mwezi huo ulianzia katikati ya mwezi wa Agosti mpaka katikati ya mwezi wa Septemba. (Ne 6:15)—Angalia Nyongeza B15.

 • Ethanimu.

  Jina la mwezi wa saba katika kalenda takatifu ya Wayahudi na jina la mwezi wa kwanza katika kalenda iliyotumiwa na watu wote. Mwezi huo ulianzia katikati ya mwezi wa Septemba mpaka katikati ya mwezi wa Oktoba. Baada ya Wayahudi kurudi kutoka Babiloni, uliitwa Tishri. (1Fa 8:2)—Angalia Nyongeza B15.

 • Ethiopia.

  Taifa la kale lililo upande wa kusini wa Misri. Lilitia ndani upande wa kusini kabisa wa nchi ya sasa ya Misri na nusu ya upande wa kaskazini wa nchi ambayo sasa inaitwa Sudan. Jina hilo hutumiwa nyakati nyingine badala ya jina “Kushi” la Kiebrania.—Est 1:1.

 • F

 • Fadhili zisizostahiliwa.

  Maneno haya yametafsiriwa kutokana na neno la Kigiriki ambalo wazo lake kuu ni kitu kinachokubalika na kinachopendeza. Mara nyingi neno hilo hutumiwa kurejelea zawadi ya fadhili au utoaji wenye fadhili. Linaporejelea fadhili zisizostahiliwa za Mungu, neno hilo humaanisha zawadi ya bure inayotolewa na Mungu kwa ukarimu, bila kutarajia alipwe chochote. Basi, maneno “fadhili zisizostahiliwa” yanaonyesha jinsi Mungu anavyotoa kwa wingi sana na pia upendo wake mwingi na fadhili zake nyingi sana kuwaelekea wanadamu. Neno la Kigiriki hutafsiriwa pia kwa maneno kama vile “kibali” na “zawadi ya fadhili.” Ni zawadi ambayo mtu hupewa bila kuifanyia kazi na ambayo hastahili; mtoaji huitoa akichochewa tu na ukarimu wake.—2Ko 6:1; Efe 1:7.

 • Fanya kosa; Kosa.

  Kufanya kosa ni kukiuka sheria iliyowekwa; kosa ni tendo la ukiukaji wa sheria. Katika Biblia, kosa ni kisawe cha “dhambi.”—Zb 51:3; Ro 5:14.

 • Farao.

  Jina la cheo walilopewa wafalme wa Misri. Mafarao watano wanatajwa katika Biblia (Shishaki, So, Tirhaka, Neko, na Hofra), lakini wengine hawatajwi, kutia ndani wale walioshughulika sana na Abrahamu, Musa, na Yosefu.—Kut 15:4; Ro 9:17.

 • Fidia.

  Bei inayolipwa ili kumweka mtu huru kutoka katika utekwa, adhabu, mateso, dhambi, au hata wajibu fulani. Bei hiyo haikulipwa kwa pesa tu sikuzote. (Isa 43:3) Fidia ilihitaji kutolewa kwa ajili ya hali mbalimbali. Kwa mfano, wazaliwa wote wa kwanza wa kiume au wa wanyama dume walikuwa wa Yehova, na fidia, au bei ya ukombozi, ilihitaji kulipwa ili kuwaweka huru wasihudumu tu katika utumishi wa Yehova. (Hes 3:45, 46; 18:15, 16) Ikiwa ng’ombe dume hatari aliyeachiliwa alimuua mtu, mwenye ng’ombe dume huyo alitozwa fidia ili kumweka huru kutokana na adhabu ya kifo aliyostahili. (Kut 21:29, 30) Hata hivyo, fidia haikukubaliwa kamwe kwa ajili ya muuaji wa kukusudia. (Hes 35:31) Jambo muhimu zaidi ni kwamba Biblia inakazia fidia ambayo Kristo alilipa kupitia kifo chake cha kidhabihu ili kuwaweka huru wanadamu watiifu kutoka katika dhambi na kifo.—Zb 49:7, 8; Mt 20:28; Efe 1:7.

 • Fimbo ya ufalme.

  Kirungu au fimbo iliyobebwa na mtawala kama ishara ya mamlaka ya kifalme.—Mwa 49:10; Ebr 1:8.

 • G

 • Gari la vita.

  Gari lenye magurudumu mawili lililokokotwa na farasi na kutumiwa hasa vitani.—Kut 14:23; Amu 4:13; Mdo 8:28.

 • Gehena.

  Neno la Kigiriki linalorejelea Bonde la Hinomu, lililokuwa upande wa kusini magharibi wa jiji la kale la Yerusalemu. (Yer 7:31) Neno hilo lilitumiwa kinabii kurejelea mahali ambapo maiti zilitupwa. (Yer 7:32; 19:6) Hakuna uthibitisho kwamba wanyama au wanadamu walitupwa katika Gehena ili wateswe au kuchomwa moto wakiwa hai. Kwa hiyo mahali hapo hapangeweza kufananisha mahali pasipoonekana ambapo nafsi za wanadamu zinateswa milele katika moto halisi. Badala yake, Yesu na wanafunzi wake walitumia neno “Gehena” kufananisha adhabu ya milele ya “kifo cha pili,” yaani, maangamizi ya milele, uharibifu.—Ufu 20:14; Mt 5:22; 10:28.

 • Gera.

  Uzito uliolingana na gramu 0.57. Gera moja ilikuwa sehemu 1 ya 20 ya shekeli. (Law 27:25)—Angalia Nyongeza B14.

 • Gileadi.

  Lilikuwa hasa eneo lenye rutuba lililokuwa upande wa mashariki wa Mto Yordani, nalo lilifika upande wa kaskazini na upande wa kusini wa Bonde la Yaboki. Nyakati nyingine neno hilo lilitumiwa kurejelea eneo lote la Waisraeli lililokuwa upande wa mashariki wa Yordani, mahali ambapo makabila ya Rubeni, Gadi, na nusu ya kabila la Manase yaliishi. (Hes 32:1; Yos 12:2; 2Fa 10:33)—Angalia Nyongeza B4.

 • Gitithi.

  Neno la kimuziki ambalo maana yake haijulikani vizuri, ingawa inaonekana kwamba linatokana na neno la Kiebrania gath. Baadhi ya watu wanaamini kwamba huenda ni sauti ya muziki inayohusiana na nyimbo zinazoimbwa wakati wa kutengeneza divai, kwa sababu neno gath linamaanisha shinikizo la divai.—Zb 81:Utangulizi.

 • H

 • Habari njema.

  Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo maneno hayo yanarejelea habari njema ya Ufalme wa Mungu na ya wokovu unaotegemea imani katika Yesu Kristo.—Lu 4:18, 43; Mdo 5:42; Ufu 14:6.

 • Hadesi.

  Neno la Kigiriki lenye maana sawa na neno la Kiebrania “Sheoli.” Linatafsiriwa kuwa “Kaburi” (kwa herufi kubwa), ili kuonyesha kwamba ni kaburi la wanadamu wote kwa ujumla.—Tazama KABURI.

 • Har–Magedoni.

  Neno hili linatokana na neno la Kiebrania Har Meghid·dohnʹ, linalomaanisha “Mlima wa Megido.” Neno hilo linahusianishwa na “vita vya siku kuu ya Mungu Mweza-Yote” wakati ambapo “wafalme wa dunia nzima inayokaliwa” watakusanyika kupigana vita dhidi ya Yehova. (Ufu 16:14, 16; 19:11-21)—Tazama DHIKI KUU.

 • Hekalu.

  Jengo la kudumu jijini Yerusalemu lililokuwa kitovu cha ibada ya Waisraeli ambalo lilichukua mahali pa hema la ibada lililokuwa likibebwa. Hekalu la kwanza lilijengwa na Sulemani na liliharibiwa na Wababiloni. Hekalu la pili lilijengwa na Zerubabeli baada ya Wayahudi kurudi kutoka uhamishoni Babiloni na baadaye lilijengwa upya na Herode Mkuu. Katika Maandiko, kwa kawaida hekalu linaitwa “nyumba ya Yehova.” (Ezr 1:3; 6:14, 15; 1Nya 29:1; 2Nya 2:4; Mt 24:1)—Angalia Nyongeza B8 na B11.

 • Hema la ibada.

  Ni hema la ibada lililoweza kusafirishwa ambalo lilitumiwa na Waisraeli baada ya Kutoka Misri. Sanduku la agano la Yehova ambalo liliwakilisha uwepo wa Mungu liliwekwa humo, na hema hilo lilikuwa pia mahali pa kutolea dhabihu na kuabudu. Nyakati nyingine linaitwa “hema la mkutano.” Lilijengwa kwa viunzi vya mbao na kufunikwa kwa vitambaa vya kitani vilivyotariziwa kwa michoro ya makerubi. Liligawanywa katika vyumba viwili, cha kwanza kiliitwa Patakatifu, na cha pili, Patakatifu Zaidi. (Yos 18:1; Kut 25:9)—Angalia Nyongeza B5.

 • Hema la mkutano.

  Maneno hayo yanatumiwa kurejelea hema la Musa na pia hema takatifu la ibada ambalo mwanzoni lilipigwa nyikani.—Kut 33:7; 39:32.

 • Herme.

  Mungu wa Ugiriki, mwana wa Zeu. Kule Listra, Paulo aliitwa kimakosa Herme wakifikiria jukumu ambalo walidhani mungu huyo anatimiza akiwa mjumbe wa miungu na mungu wa ufasaha wa kuzungumza.—Mdo 14:12.

 • Herode, wafuasi wa chama cha.

  Wanajulikana pia kuwa Waherode. Walikuwa wanachama wazalendo waliounga mkono malengo ya kisiasa ya Maherode walipokuwa wakitawala chini ya Waroma. Huenda baadhi ya Masadukayo walikuwa wafuasi wa chama hicho. Waherode walijiunga na Mafarisayo kumpinga Yesu.—Mk 3:6.

 • Herode.

  Jina la ukoo la wafalme waliowekwa na Roma ili kuwatawala Wayahudi. Mfalme wa kwanza alikuwa Herode Mkuu, aliyejulikana kwa kulijenga upya hekalu la Yerusalemu na kuagiza watoto wachinjwe katika jitihada ya kumwangamiza Yesu. (Mt 2:16; Lu 1:5) Herode Arkelao na Herode Antipa, wana wa Herode Mkuu, waliwekwa ili kusimamia maeneo fulani katika milki ya baba yao. (Mt 2:22) Antipa alikuwa mmojawapo wa viongozi wanne wadogo, naye alijulikana kuwa “mfalme” na alitawala wakati wa huduma ya Kristo ya miaka mitatu na nusu kufikia kipindi cha Matendo 12. (Mk 6:14-17; Lu 3:1, 19, 20; 13:31, 32; 23:6-15; Mdo 4:27; 13:1) Kisha, malaika wa Mungu alimuua Herode Agripa wa Kwanza, mjukuu wa Herode Mkuu, baada ya kutawala kwa kipindi kifupi. (Mdo 12:1-6, 18-23) Mwanawe, Herode Agripa wa Pili, akawa mtawala, naye alitawala mpaka wakati wa uasi wa Wayahudi dhidi ya Roma.—Mdo 23:35; 25:13, 22-27; 26:1, 2, 19-32.

 • Higayoni.

  Neno la kitaalamu la kuongozea muziki. Katika Zaburi 9:16, neno hilo linaweza kumaanisha pumziko katika uimbaji wakati ambapo kinubi kilipigwa kwa sauti nzito ya chini au kituo cha kuwaza kwa uzito kinachomwezesha mtu kutafakari.

 • Hini.

  Ni kipimo cha vitu vya majimaji na pia chombo cha kupimia Hini. Ilikuwa sawa na lita 3.67 kulingana na maelezo ya mwanahistoria Yosefo aliyesema kwamba hini ilikuwa sawa na choe mbili za Kiathene. (Kut 29:40)—Angalia Nyongeza B14.

 • Hisopo.

  Mmea wenye matawi na majani laini, uliotumiwa kunyunyiza damu au maji kwenye sherehe za kutakasa. Huenda ulikuwa mmea wa marjoram (Origanum maru; Origanum syriacum). Katika Yohana 19:29, huenda ulikuwa mmea wa marjoram ulio kwenye tawi au mmea wa dura, aina fulani ya mtama wa kawaida (Sorghum vulgare), kwa maana huenda mmea huo ulikuwa na kijiti kirefu vya kutosha kubeba sifongo ya divai kali na kuifikisha kwenye kinywa cha Yesu.—Kut 12:22; Zb 51:7.

 • Homeri.

  Kipimo cha vitu vikavu kinacholingana na kori. Kilikuwa sawa na lita 220, kulingana na ujazo uliokadiriwa wa kipimo cha bathi. (Law 27:16)—Angalia Nyongeza B14.

 • Horebu; Mlima Horebu.

  Eneo lenye milima kuzunguka Mlima Sinai. Jina lingine la Mlima Sinai. (Kut 3:1; Kum 5:2)—Angalia Nyongeza B3.

 • I

 • Ibilisi.

  Jina linalomfafanua Shetani katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, linamaanisha “Mchongezi.” Shetani alipewa jina Ibilisi kwa sababu yeye ndiye mchongezi mkuu na wa kwanza kabisa na mshtaki wa uwongo dhidi ya Yehova, neno Lake zuri, na jina Lake takatifu.—Mt 4:1; Yoh 8:44; Ufu 12:9.

 • Ilirikamu.

  Mkoa wa Roma ulio upande wa kaskazini magharibi wa Ugiriki. Paulo alisafiri mpaka huko katika huduma yake, lakini Biblia haitaji ikiwa alihubiri Ilirikamu au alifika tu karibu na mkoa huo. (Ro 15:19)—Angalia Nyongeza B13.

 • Ishara.

  Kitu, tendo, hali, au tukio lisilo la kawaida ambalo ni muhimu na ni dalili ya jambo litakalotokea, wakati uliopo au wakati ujao.—Mwa 9:12, 13; 2Fa 20:9; Mt 24:3; Ufu 1:1.

 • Isiyo na chachu.

  Maneno haya yanatumiwa kuhusu mikate iliyookwa bila chachu.—Kum 16:3; Mk 14:12; 1Ko 5:8.

 • Israeli.

  Jina ambalo Mungu alimpa Yakobo. Baadaye liliwarejelea wazao wake wote kwa ujumla, katika kipindi chochote kile. Kwa kawaida, wazao wa wana 12 wa Yakobo waliitwa wana wa Israeli, nyumba ya Israeli, watu (wanaume) wa Israeli, au Waisraeli. Pia, jina Israeli lilitumiwa kurejelea ufalme wa kaskazini wa makabila kumi ambao ulitengana na ufalme wa kusini, na baadaye lilitumiwa kuwarejelea Wakristo watiwa-mafuta, “Israeli wa Mungu.”—Gal 6:16; Mwa 32:28; 2Sa 7:23; Ro 9:6.

 • J

 • Jiji la Daudi.

  Jiji la Yebusi liliitwa jina hilo baada ya Daudi kulishinda na kujenga makao yake ya kifalme humo. Linaitwa pia Sayuni. Ni sehemu ya kusini mashariki ya Yerusalemu ambayo pia ni ya kale zaidi.—2Sa 5:7; 1Nya 11:4, 5.

 • Jiwe la kusagia.

  Jiwe la mviringo lililowekwa juu ya jiwe lingine linalofanana nalo na kutumiwa kusaga nafaka iwe unga. Mchi uliotiwa katikati ya jiwe la chini la kusagia ulishikilia jiwe la juu la kusagia. Katika nyakati za Biblia, mawe ya mkononi ya kusagia yalitumiwa na wanawake katika nyumba nyingi. Kwa kuwa familia ilitegemea jiwe la mkononi la kusagia ili kupata mkate wa kila siku, Sheria ya Musa iliwakataza watu wasichukue kwa lazima jiwe la chini la kusagia au jiwe la juu kuwa dhamana. Mawe makubwa zaidi ya kusagia yenye muundo huohuo yalizungushwa na wanyama.—Kum 24:6; Mk 9:42.

 • Jiwe la pembeni.

  Jiwe linalowekwa kwenye pembe, au kona, ya jengo mahali ambapo kuta mbili zinakutana, lilikuwa muhimu sana katika kuziunganisha na kuzifunga kuta pamoja. Jiwe la msingi la pembeni ndilo lililokuwa jiwe kuu la pembeni; kwa kawaida jiwe ambalo lilikuwa imara lilichaguliwa kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya umma na kuta za jiji. Neno hilo linatumiwa kwa njia ya mfano kuhusiana na kuwekwa kwa msingi wa dunia, na Yesu anarejelewa kuwa “jiwe la msingi la pembeni” la kutaniko la Kikristo, ambalo linafananishwa na nyumba ya kiroho.—Efe 2:20; Ayu 38:6.

 • K

 • Kabi.

  Kipimo cha vitu vikavu cha lita 1.22, kulingana na ujazo uliokadiriwa wa kipimo cha bathi. (2Fa 6:25)—Angalia Nyongeza B14.

 • Kaburi la ukumbusho.

  Mahali pa kuzikia ambamo mtu aliyekufa aliwekwa. Neno hili linatafsiriwa kutokana na neno la Kigiriki mne·meiʹon, linalotokana na kitenzi “kukumbusha,” kinachodokeza kwamba mtu aliyekufa anakumbukwa.—Yoh 5:28, 29.

 • Kaburi.

  Neno hili linapoanza kwa herufi ndogo, linarejelea kaburi ambamo mtu huzikwa; linapoanza kwa herufi kubwa, linarejelea kaburi la wanadamu kwa ujumla, ambalo katika Kiebrania ni “Sheoli” na katika Kigiriki “Hadesi.” Katika Biblia, linafafanuliwa kuwa mahali pa mfano au hali ambamo mtu hawezi kutenda jambo lolote na fahamu zake zote zinakoma.—Mwa 47:30; Mhu 9:10; Mdo 2:31.

 • Kahaba.

  Mtu anayefanya ngono nje ya kifungo cha ndoa, hasa ili apate pesa. (Neno la Kigiriki linalotafsiriwa “kahaba,” porʹne, linatokana na neno ambalo kimsingi linamaanisha “kuuza.”) Mara nyingi neno kahaba hutumiwa kumhusu mwanamke, ingawa wanaume makahaba wanatajwa pia katika Biblia. Sheria ya Musa ilikataza ukahaba, na malipo ya kahaba hayakukubaliwa kutolewa kuwa mchango wa mahali patakatifu pa Yehova, tofauti kabisa na zoea la wapagani la kuwatumia makahaba wa hekaluni kuwa chanzo cha mapato. (Kum 23:17, 18; 1Fa 14:24) Biblia hutumia pia neno hilo kwa njia ya mfano, kuwarejelea watu, mataifa, au mashirika yanayojihusisha na aina fulani ya ibada ya sanamu huku yakidai kumwabudu Mungu. Kwa mfano, milki ya kidini inayoitwa “Babiloni Mkubwa” inafafanuliwa katika kitabu cha Ufunuo kuwa kahaba kwa sababu imeshirikiana na watawala wa ulimwengu huu kupata mamlaka na utajiri.—Ufu 17:1-5; 18:3; 1Nya 5:25.

 • Kaisari.

  Jina la familia ya Kiroma ambalo lilikuja kuwa jina la cheo la maliki Waroma. Biblia inawataja Augusto, Tiberio, na Klaudia kwa majina, na ingawa haimtaji Nero kwa jina, yeye pia alikuwa Kaisari. Jina “Kaisari” linatumiwa pia katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo kufananisha mamlaka za kiraia, au Serikali.—Mk 12:17; Mdo 25:12.

 • Kanaani.

  Mjukuu wa Noa, na mwana wa nne wa Hamu. Makabila 11 yaliyotokana na Kanaani hatimaye yaliishi katika eneo la mashariki kando ya Mediterania kati ya Misri na Siria. Eneo hilo liliitwa “nchi ya Kanaani.” (Law 18:3; Mwa 9:18; Mdo 13:19)—Angalia Nyongeza B4.

 • Kemoshi.

  Mungu mkuu wa Wamoabu.—1Fa 11:33.

 • Kiapo.

  Taarifa inayotolewa kwa kuapa ili kuthibitisha kwamba jambo fulani ni la kweli, au ahadi nzito ya kwamba mtu atafanya au hatafanya jambo fulani. Kwa kawaida ni nadhiri inayotolewa kwa mtu mwenye mamlaka, hasa kwa Mungu. Yehova aliliimarisha agano lake pamoja na Abrahamu kwa kiapo.—Mwa 14:22; Ebr 6:16, 17.

 • Kiaramu.

  Lugha ya Kisemiti inayokaribiana sana na Kiebrania, inayotumia alfabeti ya Kiebrania. Awali ilizungumzwa na Waaramu lakini baadaye ikawa lugha ya kimataifa ya biashara na mawasiliano katika milki ya Ashuru na milki ya Babiloni. Pia ilikuwa lugha rasmi ya serikali katika Milki ya Uajemi. (Ezr 4:7) Sehemu fulani za kitabu cha Ezra, Yeremia, na Danieli ziliandikwa katika Kiaramu.—Ezr 4:8–6:18; 7:12-26; Yer 10:11; Da 2:4b–7:28.

 • Kida.

  Bidhaa hii inatokana na gome la mti wa kida (Cinnamomum cassia), ambao uko katika jamii moja na mti wa mdalasini. Kida ilitumiwa kama manukato na kama mojawapo ya viungo vya mafuta matakatifu yaliyotumiwa kutia mafuta.—Kut 30:24; Zb 45:8; Eze 27:19.

 • Kifuko cha kifuani.

  Kifuko kilichopambwa kwa vito ambacho kilivaliwa na kuhani mkuu wa Israeli juu ya moyo wake wakati wowote alipoingia Patakatifu. Kiliitwa “kifuko cha kifuani cha maamuzi” kwa sababu kilikuwa na Urimu na Thumimu, vitu ambavyo vilitumiwa kufunua maamuzi ya Yehova. (Kut 28:15-30)—Angalia Nyongeza B5.

 • Kifuniko cha nguzo.

  Kilikuwa kifuniko maridadi kilichokuwa juu ya nguzo za hekalu. Nguzo mbili zilizoitwa Yakini na Boazi zilikuwa upande wa mbele wa hekalu la Sulemani. (1Fa 7:16)—Angalia Nyongeza B8.

 • Kifuniko cha upatanisho.

  Kifuniko cha sanduku la agano; mbele ya kifuniko hicho kuhani mkuu alinyunyiza damu ya dhabihu za dhambi Siku ya Kufunika Dhambi. Kimsingi, neno hilo katika Kiebrania linatokana na kitenzi kinachomaanisha “kufunika (dhambi)” au labda “kufutilia mbali (dhambi).” Kifuniko hicho chote kilitengenezwa kwa dhahabu, na kilikuwa na makerubi wawili, mmoja upande huu na mwingine upande wa pili. Nyakati nyingine kinaitwa tu “kifuniko.” (Kut 25:17-22; 1Nya 28:11; Ebr 9:5)—Angalia Nyongeza B5.

 • Kigiriki.

  Lugha inayozungumzwa na watu wa Ugiriki; mwenyeji wa Ugiriki au mtu ambaye asili ya familia yake ni Ugiriki. Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, neno hilo lina maana pana, linarejelea watu wote ambao si Wayahudi au watu walioathiriwa na lugha na utamaduni wa Ugiriki.—Yoe 3:6; Yoh 12:20.

 • Kilemba.

  Kitambaa kinachovaliwa kwa kuzungushwa kichwani. Kuhani mkuu alivaa kilemba cha kitani bora, kilichokuwa na bamba la dhahabu lililofungwa upande wa mbele kwa uzi wa bluu. Mfalme alivaa kilemba ndani ya taji lake. Ayubu alitumia neno hilo kwa njia ya mfano alipofananisha haki yake na kilemba.—Kut 28:36, 37; Ayu 29:14; Eze 21:26.

 • Kilima.

  Sehemu ya kijiografia au sehemu iliyojengwa katika Jiji la Daudi. Huenda kilima hicho kilikuwa kuta za kutegemeza zenye matuta au kitegemezi cha aina nyingine.—2Sa 5:9; 1Fa 11:27.

 • Kilomita.

  Kipimo cha umbali kinachotajwa mara moja tu katika maandishi ya awali ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo kwenye Mathayo 5:41, labda kinarejelea maili au kilomita ya Kiroma ambayo ilikuwa sawa na mita 1,479.5 (futi 4,854). Maandiko mengine matatu yanayotaja “kilomita,” yaani, Luka 24:13, Yohana 6:19, na Yohana 11:18 yanarejelea kipimo kilichokubalika cha kilomita kilichopatikana kwa kubadilisha kipimo cha kale cha stadia kinachotajwa katika maandishi ya awali.—Angalia Nyongeza B14.

 • Kiongozi.

  Linapotumiwa katika Zaburi, inaonekana kwamba neno hilo katika Kiebrania linamrejelea mtu ambaye kwa njia fulani alitunga nyimbo na kuongoza uimbaji wa nyimbo hizo, aliwafundisha na kuwazoeza waimbaji Walawi, na hata aliongoza uimbaji katika pindi rasmi. Tafsiri nyingine zinatafsiri neno hilo kuwa “mwimbaji mkuu” au “kiongozi wa muziki.”—Zb 4:Utangulizi; 5:Utangulizi.

 • Kiriba cha divai.

  Chupa ya ngozi iliyotengenezwa kwa ngozi ya mnyama, kama vile mbuzi au kondoo, ambayo ilitumiwa kuwekea divai. Divai iliwekwa katika viriba vipya vya divai, kwa sababu divai inapochacha, hutokeza gesi ya kaboni dioksidi inayosababisha shinikizo kubwa ndani ya chupa hizo za ngozi. Ngozi mpya hupanuka; ngozi ngumu zilizozeeka hupasuka shinikizo linapoongezeka.—Yos 9:4; Mt 9:17.

 • Kislevu.

  Jina la mwezi wa tisa katika kalenda takatifu ya Wayahudi baada ya kutoka uhamishoni Babiloni na jina la mwezi wa tatu katika kalenda iliyotumiwa na watu wote. Mwezi huo ulianzia katikati ya mwezi wa Novemba mpaka katikati ya mwezi wa Desemba. (Ne 1:1; Zek 7:1)—Angalia Nyongeza B15.

 • Kitabu cha kukunjwa.

  Ukurasa mrefu wa ngozi au mafunjo, uliokuwa na maandishi upande mmoja, ambao kwa kawaida ulikunjwa kwenye kijiti. Maandiko yaliandikwa na kunakiliwa katika vitabu vya kukunjwa; vitabu hivyo vilikuwa vikitumiwa kwa ukawaida wakati Biblia ilipokuwa ikiandikwa.—Yer 36:4, 18, 23; Lu 4:17-20; 2Ti 4:13.

 • Kitabu cha ngozi.

  Ngozi ya kondoo, mbuzi, au ndama iliyotayarishwa ili itumiwe kama karatasi ya kuandikia. Ilidumu kwa muda mrefu kuliko mafunjo na ilitumiwa kutengeneza vitabu vya kukunjwa vya Biblia. Huenda vitabu vya ngozi ambavyo Paulo alimwomba Timotheo amletee vilikuwa sehemu fulani za Maandiko ya Kiebrania. Baadhi ya Vitabu ya Kukunjwa vya Bahari ya Chumvi vilikuwa vya ngozi.—2Ti 4:13.

 • Kiti cha hukumu.

  Kwa kawaida lilikuwa jukwaa lililoinuliwa ambalo lilikuwa nje; lilikuwa na ngazi, na maofisa walioketi kwenye kiti hicho wangeweza kuuhutubia umati wa watu na kutangaza maamuzi yao. Maneno “kiti cha hukumu cha Mungu” na “kiti cha hukumu cha Kristo” ni maneno ya mfano yanayomaanisha mpango wa Yehova wa kuwahukumu wanadamu.—Ro 14:10; 2Ko 5:10; Yoh 19:13.

 • Koleo.

  Vifaa vilivyotengenezwa kwa dhahabu, ambavyo huenda vilifanana na mikasi; vilitumiwa katika hema la ibada na hekaluni kuzima taa.—Kut 37:23.

 • Komamanga.

  Tunda lenye umbo la tofaa, ambalo lina ua au taji upande mmoja. Ndani ya ganda lake gumu kuna punje nyingi ndogo zilizojaa umajimaji, na kila punje ina mbegu ndogo ya rangi ya waridi au nyekundu. Mapambo yenye umbo la komamanga yalipamba upindo wa joho la bluu lisilo na mikono la kuhani mkuu na pia vifuniko vya nguzo zilizoitwa Yakini na Boazi zilizokuwa mbele ya hekalu.—Kut 28:34; Hes 13:23; 1Fa 7:18.

 • Kombeo.

  Mkanda wa ngozi au mkanda uliosukwa wa kano za wanyama, matete, au manyoya ya wanyama. Kwa kawaida jiwe au kitu kilichopaswa kurushwa kiliwekwa katika sehemu pana ya katikati. Mwisho mmoja wa kombeo ulifungiliwa mkononi au kwenye kitanga cha mkono, na mwisho wa pili ulishikwa na kuachiliwa kombeo lilipozungushwa. Mataifa ya kale yalikuwa na wanajeshi waliorusha mawe kwa kombeo.—Amu 20:16; 1Sa 17:50.

 • Kori.

  Kipimo cha vitu vikavu na vya majimaji. Kilikuwa sawa na lita 220, kulingana na ujazo uliokadiriwa wa kipimo cha bathi. (1Fa 5:11)—Angalia Nyongeza B14.

 • Korongo.

  Bonde au sakafu ya kijito ambayo kwa kawaida huwa kavu isipokuwa katika majira ya mvua; neno hilo linaweza pia kurejelea kijito chenyewe. Vijito fulani havikukauka kwa sababu maji yake yalitoka katika chemchemi. Katika Maandiko fulani, korongo linaitwa “bonde.”—Mwa 26:19; Hes 34:5; Kum 8:7; 1Fa 18:5; Ayu 6:15.

 • Kristo.

  Jina la cheo la Yesu linalotokana na neno la Kigiriki Khri·stosʹ, ambalo ni sawa na neno la Kiebrania linalotafsiriwa kuwa “Masihi,” au “Mtiwa-Mafuta.”—Mt 1:16; Yoh 1:41.

 • Kufunga.

  Kujizuia kula vyakula vya aina yote kwa kipindi fulani. Waisraeli walifunga katika Siku ya Kufunika Dhambi, nyakati za taabu, na walipohitaji mwongozo kutoka kwa Mungu. Wayahudi walikuwa na pindi nne za kufunga kila mwaka ili kukumbuka pindi za misiba katika historia yao. Kufunga si takwa kwa Wakristo.—Ezr 8:21; Isa 58:6; Lu 18:12.

 • Kufunika dhambi.

  Katika Maandiko ya Kiebrania, tendo hilo lilihusiana na dhabihu zilizotolewa ili kuwawezesha watu wamkaribie Mungu na kumwabudu. Chini ya Sheria ya Musa, dhabihu zilitolewa, hasa katika Siku ya kila mwaka ya Kufunika Dhambi, ili watu waweze kupatanishwa na Mungu licha ya dhambi za mtu mmoja-mmoja na taifa zima. Dhabihu hizo zilifananisha dhabihu ya Yesu, ambayo ilifunika kabisa dhambi za wanadamu mara moja kwa wakati wote, na hivyo kuwapa wanadamu nafasi ya kupatanishwa na Yehova.—Law 5:10; 23:28; Kol 1:20; Ebr 9:12.

 • Kuhani mkuu.

  Chini ya Sheria ya Musa, alikuwa kuhani mwenye cheo cha juu aliyewawakilisha watu mbele za Mungu na kuwasimamia makuhani wengine. Anaitwa pia “mkuu wa makuhani.” (2Nya 26:20; Ezr 7:5) Ni yeye peke yake aliyeruhusiwa kuingia Patakatifu Zaidi, chumba cha ndani zaidi cha hema la ibada na baadaye chumba cha ndani zaidi cha hekalu. Alifanya hivyo wakati tu wa Siku ya kila mwaka ya Kufunika Dhambi. Maneno “kuhani mkuu” yanatumiwa pia kumhusu Yesu Kristo.—Law 16:2, 17; 21:10; Mt 26:3; Ebr 4:14.

 • Kuhani.

  Mwakilishi rasmi wa Mungu mbele za watu aliowatumikia, naye aliwafundisha kumhusu Mungu na sheria zake. Pia, makuhani waliwawakilisha watu mbele za Mungu, wakitoa dhabihu na pia kuwatetea na kuwaombea watu msamaha. Kabla ya kuanzishwa kwa Sheria ya Musa, kichwa cha familia alitumikia akiwa kuhani wa familia yake. Chini ya Sheria ya Musa, wanaume wa familia ya Haruni katika kabila la Lawi walikuwa makuhani. Wanaume wengine Walawi walikuwa wasaidizi wao. Wakati wa uzinduzi wa agano jipya, taifa la kiroho la Israeli likawa taifa la makuhani, Yesu Kristo akiwa Kuhani Mkuu.—Kut 28:41; Ebr 9:24; Ufu 5:10.

 • Kuokota masalio.

  Ni tendo la kukusanya mazao yoyote ambayo wavunaji waliacha kimakusudi au bila kukusudia. Sheria ya Musa iliwaagiza watu wasivune kabisa kingo za mashamba yao wala kuchukua zeituni zote au zabibu zote. Mungu alimpa maskini, mtu anayeteseka, mkaaji mgeni, yatima, na mjane haki ya kuokota masalio yoyote baada ya mavuno.—Ru 2:7.

 • Kupeleka uhamishoni.

  Tendo la kumwondoa mtu kwa lazima katika nchi alimozaliwa au katika makao yake, kwa kawaida washindi walitoa agizo hilo. Neno la Kiebrania linamaanisha “kuondoka.” Katika pindi mbili, Waisraeli wengi sana walipelekwa uhamishoni. Ufalme wa kaskazini wa makabila kumi ulipelekwa uhamishoni na Waashuru, na baadaye ufalme wa kusini wa makabila mawili ulipelekwa uhamishoni na Wababiloni. Wahamishwa waliobaki katika pindi zote mbili walirudishwa katika nchi yao chini ya utawala wa Koreshi, mtawala wa Uajemi.—2Fa 17:6; 24:16; Ezr 6:21.

 • Kupura; Uwanja wa kupuria.

  Kupura ni kuondoa nafaka katika bua lake na katika makapi; kazi hiyo ilifanywa kwenye uwanja wa kupuria. Nafaka ilipurwa kwa mkono kwa kutumia fimbo, au kiasi kikubwa zaidi cha nafaka kilipurwa kwa vifaa vya pekee, kama vile kifaa cha kupuria nafaka au magurudumu ya kupuria yaliyovutwa na wanyama. Vifaa hivyo vilipitishwa juu ya nafaka iliyotandazwa kwenye uwanja wa kupuria, yaani, eneo tambarare la mviringo ambalo kwa kawaida lilikuwa sehemu iliyoinuka iliyopigwa na upepo.—Law 26:5; Isa 41:15; Mt 3:12.

 • Kura.

  Vijiwe vya mviringo au vipande vidogo vya mbao vilivyotumiwa kufanya maamuzi. Vitu hivyo vilitiwa katika mikunjo ya nguo au katika chombo na kutikiswa. Kura iliyoanguka nje au kutolewa humo ndiyo iliyochaguliwa. Kwa kawaida sala zilitolewa wakati wa kupiga kura. Neno “kura” linatumiwa kihalisi na kwa njia ya mfano kumaanisha “sehemu” au “fungu.”—Yos 14:2; Zb 16:5; Met 16:33; Mt 27:35.

 • Kusanyiko.

  Kundi la watu waliokusanyika kuitikia mwito. Katika Maandiko ya Kiebrania, mara nyingi neno hili linatumiwa kuwarejelea watu wa taifa la Israeli waliokusanyika kwa ajili ya sherehe za kidini au matukio muhimu ya kitaifa.—Kum 16:8; 1Fa 8:5.

 • Kusemethi.

  Aina fulani ya ngano ya hali ya chini (Triticum spelta), ambayo mbegu yake haiwezi kutenganishwa kwa urahisi na makapi.—Kut 9:32.

 • Kutaniko.

  Kikundi cha watu waliokusanyika pamoja kwa kusudi maalumu au kazi fulani. Katika Maandiko ya Kiebrania, kwa ujumla neno hilo linarejelea taifa la Israeli. Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, linarejelea kutaniko mojamoja la Wakristo lakini kwa kawaida linarejelea kutaniko la Kikristo kwa ujumla.—1Fa 8:22; Mdo 9:31; Ro 16:5.

 • Kuvu.

  Mojawapo ya magonjwa mengi ya mimea yanayosababishwa na ukungu. Imesemwa kwamba ugonjwa wa kuvu unaotajwa katika Biblia ni kizimwili (Puccinia graminis).—1Fa 8:37.

 • Kuwapo.

  Katika baadhi ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, neno hili linarejelea kuwapo kwa Yesu Kristo akiwa mfalme kuanzia wakati alipowekwa kuwa Mfalme wa Kimasihi bila kuonekana na kuendelea mpaka katika siku za mwisho za mfumo huu wa mambo. Kuwapo kwa Kristo si tukio la kuja na kisha kuondoka haraka; badala yake, kuwapo kwake kunadumu kwa kipindi kilichowekwa cha wakati.—Mt 24:3.

 • Kuwasiliana na roho.

  Imani ya kwamba roho za wanadamu waliokufa huendelea kuishi baada ya mwili kufa na kwamba zinaweza kuwasiliana na watu walio hai, nazo huwasiliana nao, hasa kupitia mtu (anayewasiliana na roho) anayeweza kutumiwa na roho hizo. Neno la Kigiriki linalotafsiriwa kuwa “mazoea ya kuwasiliana na roho” ni phar·ma·kiʹa, ambalo kihalisi linamaanisha “ulevi wa dawa.” Neno hilo linahusiana na kuwasiliana na roho kwa sababu katika nyakati za kale, dawa zilitumiwa kuleta nguvu za roho waovu ili kufanya ulozi.—Gal 5:20; Ufu 21:8.

 • Kuweka mikono juu ya.

  Mikono iliwekwa juu ya mtu ili kumweka rasmi kwa ajili ya kazi ya pekee au kumchagua apate baraka, maponyo, au zawadi ya roho takatifu. Nyakati nyingine mikono iliwekwa juu ya wanyama kabla hawajatolewa dhabihu.—Kut 29:15; Hes 27:18; Mdo 19:6; 1Ti 5:22.

 • L

 • Laana.

  Kumtisha au kumtakia uovu mtu au kitu. Neno hilo halipaswi kueleweka kuwa matusi au hasira kali. Kwa kawaida laana ni tangazo rasmi la kiapo au la kumtabiria uovu mtu au kitu, na laana hiyo inapotamkwa na Mungu au na mtu aliyepewa mamlaka inakuwa na uzito na nguvu kama unabii.—Mwa 12:3; Hes 22:12; Gal 3:10.

 • Lawi; Mlawi.

  Mwana wa tatu wa Yakobo aliyezaliwa na mke wake Lea; pia ni jina la kabila linaloitwa kwa jina lake. Wanawe watatu walianzisha vikundi vitatu vikuu vya makuhani Walawi. Nyakati nyingine, neno “Walawi” linarejelea kabila zima, lakini kwa kawaida halitii ndani familia ya kikuhani ya Haruni. Kabila la Lawi halikugawiwa ardhi katika Nchi ya Ahadi lakini lilipewa majiji 48 katika ardhi ambayo makabila mengine yaligawiwa.—Kum 10:8; 1Nya 6:1; Ebr 7:11.

 • Lebanoni, safu ya Milima ya.

  Mojawapo ya safu mbili za milima nchini Lebanoni. Safu ya milima ya Lebanoni iko upande wa magharibi, na safu ya milima iliyo ng’ambo ya milima ya Lebanoni iko upande wa mashariki. Bonde refu lenye rutuba linatenganisha safu hizo mbili. Safu ya milima ya Lebanoni imeinuka juu kana kwamba ni moja kwa moja kutoka kwenye pwani ya Mediterania, na vilele vyake vimeinuka kufikia urefu wa kati ya mita 1,800 na 2,100 (futi 6,000 na 7,000) kwa wastani. Katika nyakati za kale, nchi ya Lebanoni ilifunikwa na miti mirefu sana ya mierezi, na mataifa jirani yaliiona miti hiyo kuwa yenye thamani kubwa sana. (Kum 1:7; Zb 29:6; 92:12)—Angalia Nyongeza B7.

 • Leptoni.

  Katika enzi za Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, Leptoni ilikuwa sarafu ndogo zaidi ya Kiyahudi ya shaba au shaba nyekundu. Tafsiri fulani za Biblia zinaiita “sarafu ndogo.” (Mk 12:42; Lu 21:2; maelezo ya chini.)—Angalia Nyongeza B14.

 • Leviathani.

  Ni mnyama fulani ambaye kwa kawaida inasemekana kwamba anakaa majini. Katika Ayubu 3:8 na 41:1, inaonekana ni mamba au mnyama mwingine wa majini ambaye ni mkubwa sana na ana nguvu nyingi. Katika Zaburi 104:26, huenda ni aina fulani ya nyangumi. Katika Maandiko mengine neno hilo linatumiwa kwa njia ya mfano na halihusiani na mnyama fulani hususa.—Zb 74:14; Isa 27:1.

 • Liwali (wa Babiloni na Uajemi).

  Mwakilishi wa mfalme, au gavana wa mkoa, katika milki ya Babiloni na ya Uajemi. Liwali aliwekwa na mfalme kuwa mtawala mkuu.—Ezr 8:36; Da 6:1.

 • Liwali (wa Roma).

  Gavana mkuu wa mkoa uliokuwa chini ya usimamizi wa Baraza la Roma. Alikuwa na mamlaka ya kuhukumu na ya kijeshi, na ingawa Baraza la Roma lilikuwa na haki ya kuchunguza matendo yake, alikuwa na mamlaka kubwa sana katika mkoa.—Mdo 13:7; 18:12.

 • Logi.

  Kipimo kidogo zaidi cha vitu vya majimaji kinachotajwa katika Biblia. Talmudi ya Wayahudi inasema kwamba logi ni sehemu 1 ya 12 ya hini, basi kwa msingi huo, logi ingekuwa sawa na lita 0.31. (Law 14:10)—Angalia Nyongeza B14.

 • M

 • Madhabahu.

  Sehemu iliyoinuliwa au jukwaa lililotengenezwa kwa udongo, mawe, mawe yaliyochongwa, au mbao zilizofunikwa kwa chuma; sehemu hiyo ilitumiwa kutoa dhabihu au uvumba wakati wa ibada. Katika chumba cha kwanza cha hema la ibada na cha hekalu, kulikuwa na ‘madhabahu ndogo ya dhahabu’ ya kufukizia uvumba. Ilitengenezwa kwa mbao zilizofunikwa kwa dhahabu. ‘Madhabahu kubwa zaidi ya shaba’ iliyotumiwa kutolea dhabihu za kuteketezwa ilikuwa nje katika ua. (Kut 27:1; 39:38, 39; Mwa 8:20; 1Fa 6:20; 2Nya 4:1; Lu 1:11)—Angalia Nyongeza B5 na B8.

 • Madhehebu.

  Kikundi cha watu wanaofuata imani fulani au kiongozi fulani na walio na mafundisho yao wenyewe. Neno hili linatumiwa kurejelea vikundi viwili maarufu vya dini ya Kiyahudi, yaani, Mafarisayo na Masadukayo. Watu wasio Wakristo waliuita pia Ukristo “madhehebu” au “madhehebu ya Wanazareti,” labda waliwaona kuwa farakano la dini ya Kiyahudi. Hatimaye, madhehebu yalisitawi katika kutaniko la Kikristo; “madhehebu ya Nikolao” yanatajwa kihususa katika kitabu cha Ufunuo.—Mdo 5:17; 15:5; 24:5; 28:22; Ufu 2:6; 2Pe 2:1.

 • Mafarisayo.

  Dhehebu maarufu la dini ya Kiyahudi katika karne ya kwanza W.K. Hawakuwa wa uzao wa kikuhani, lakini waliifuata sana Sheria, hata mambo madogo zaidi ya Sheria, nao waliyakweza mapokeo yaliyopitishwa kwa mdomo na kuyaona kuwa kama Sheria. (Mt 23:23) Walipinga uvutano wowote wa utamaduni wa Ugiriki, na wakiwa wasomi wa Sheria na mapokeo, walikuwa na mamlaka kubwa juu ya watu. (Mt 23:2-6) Baadhi yao walikuwa pia washiriki wa Sanhedrini. Kwa kawaida walimpinga Yesu kuhusiana na kushika Sabato, mapokeo, na kwa sababu alishirikiana na watenda dhambi na wakusanya kodi. Baadhi yao walikuja kuwa Wakristo, kutia ndani Sauli wa Tarso.—Mt 9:11; 12:14; Mk 7:5; Lu 6:2; Mdo 26:5.

 • Mafunjo.

  Mmea wa majini unaofanana na matete uliotumiwa kutengenezea vikapu, vyombo, na mashua. Ulitumiwa pia kutengeneza karatasi za mafunjo za kuandikia na vitabu vingi vya kukunjwa.—Kut 2:3.

 • Mahakimu.

  Katika serikali ya Babiloni, mahakimu-askari walikuwa maofisa wa raia katika wilaya za utawala waliojua sheria na walikuwa na kiasi fulani cha mamlaka ya kuhukumu. Katika makoloni ya Roma, mahakimu wa raia walikuwa wasimamizi wa serikali. Majukumu yao yalitia ndani kudumisha utaratibu, kudhibiti matumizi ya fedha, kuwahukumu waliovunja sheria, na kuagiza adhabu itekelezwe.—Da 3:2; Mdo 16:20.

 • Mahalathi.

  Ni wazi kwamba neno hili ni la kimuziki, nalo linapatikana katika utangulizi wa Zaburi 53 na 88. Huenda linahusiana na kitenzi cha Kiebrania ambacho kimsingi kinamaanisha “kudhoofika; kuwa mgonjwa,” na kwa hiyo kitenzi hicho kinadokeza sauti ya simanzi na huzuni ambayo inapatana na mambo ya kuhuzunisha yanayotajwa katika nyimbo hizo mbili.

 • Mahali pa juu.

  Mahali pa ibada ambapo kwa kawaida palikuwa juu ya kilima, mlima, au jukwaa lililotengenezwa na watu. Ingawa nyakati nyingine watu walitumia mahali pa juu kumwabudia Mungu, mara nyingi panahusianishwa na ibada ya kipagani ya miungu ya uwongo.—Hes 33:52; 1Fa 3:2; Yer 19:5.

 • Mahali patakatifu.

  Kwa ujumla, ni mahali palipotengwa kwa ajili ya ibada, mahali patakatifu. Hata hivyo, mara nyingi neno hilo linamaanisha hema la ibada au hekalu lililokuwa Yerusalemu. Neno hilo linatumiwa pia kurejelea makao ya Mungu mbinguni.—Kut 25:8, 9; 2Fa 10:25; 1Nya 28:10; Ufu 11:19.

 • Majiji ya makimbilio.

  Majiji ya Walawi ambamo mtu aliyeua bila kukusudia angeweza kukimbilia ili asiuawe na mtu anayelipiza kisasi cha damu. Majiji sita ya makimbilio, yaliyoenea kotekote katika Nchi ya Ahadi, yalichaguliwa na Musa na baadaye na Yoshua, chini ya mwongozo wa Yehova. Baada ya kufika katika jiji la makimbilio, mtu aliyekuwa akikimbilia humo aliwaambia kesi yake wazee waliokuwa katika lango la jiji hilo, kisha walimkaribisha humo. Ili kuwazuia watu waliowaua wengine kimakusudi wasiutumie vibaya mpango huo, mtu aliyekimbilia usalama katika jiji la makimbilio alipaswa kufika mbele ya waamuzi katika jiji ambamo mauaji yalifanyika ili athibitishe kwamba hana hatia ya kuua kimakusudi. Ilipothibitishwa kwamba hana hatia, alirudishwa katika jiji la makimbilio, ambamo alipaswa kuishi ndani ya mipaka ya jiji hilo maisha yake yote au mpaka kuhani mkuu alipokufa.—Hes 35:6, 11-15, 22-29; Yos 20:2-8.

 • Makapi.

  Maganda yanayotenganishwa na sehemu inayoliwa ya nafaka wakati wa kupura na kupepeta. Makapi hutumiwa katika tamathali za usemi kufananisha kitu kisicho na thamani na kisichotamanika.—Zb 1:4; Mt 3:12.

 • Makedonia.

  Eneo lililo upande wa kaskazini wa Ugiriki ambalo lilipata umaarufu wakati wa Aleksanda Mkuu na kuendelea kuwa huru mpaka liliposhindwa na Waroma. Makedonia ilikuwa mkoa wa Roma mtume Paulo alipotembelea Ulaya kwa mara ya kwanza. Paulo alitembelea eneo hilo mara tatu. (Mdo 16:9)—Angalia Nyongeza B13.

 • Makerubi.

  Malaika wa cheo cha juu wenye majukumu ya pekee. Wao ni tofauti na maserafi.—Mwa 3:24; Kut 25:20; Isa 37:16; Ebr 9:5.

 • Malaika mkuu.

  Maana yake “mkuu wa malaika.” Ufafanuzi huo, pamoja na ukweli wa kwamba Biblia inatumia tu hali ya umoja inapomrejelea “malaika mkuu,” huthibitisha kwamba kuna malaika mkuu mmoja tu. Biblia inataja jina la huyo malaika mkuu, inamtambulisha kuwa Mikaeli.—Da 12:1; Yud 9; Ufu 12:7.

 • Malaika.

  Linatokana na neno la Kiebrania mal·ʼakhʹ na neno la Kigiriki agʹge·los. Maneno yote mawili kihalisi yanamaanisha “mjumbe” lakini yanatafsiriwa kuwa “malaika” yanapowahusu wajumbe wenye miili ya roho. (Mwa 16:7; 32:3; Yak 2:25; Ufu 22:8) Malaika ni viumbe wa roho walio na nguvu, ambao Mungu aliwaumba kabla ya wanadamu. Katika Biblia wanaitwa pia “makumi ya maelfu ya watakatifu,” “wana wa Mungu,” na “nyota za asubuhi.” (Kum 33:2; Ayu 1:6; 38:7) Hawakuumbwa wakiwa na uwezo wa kuzaa malaika wengine lakini waliumbwa mmoja mmoja. Idadi yao inazidi milioni mia moja. (Da 7:10) Biblia inaonyesha kwamba kila malaika ana jina lake na utu wake, hata hivyo wanakataa kwa unyenyekevu kuabudiwa, na wengi hata hukataa kufunua majina yao. (Mwa 32:29; Lu 1:26; Ufu 22:8, 9) Wana vyeo mbalimbali na wamepewa majukumu mbalimbali, kama vile kuhudumu mbele ya kiti cha Ufalme cha Yehova, kupeleka jumbe zake, kuwasaidia watumishi wa Yehova walio duniani, kutekeleza hukumu za Mungu, na kuunga mkono kazi ya kuhubiri habari njema. (2Fa 19:35; Zb 34:7; Lu 1:30, 31; Ufu 5:11; 14:6) Wakati ujao watajiunga na Yesu kupigana vita vya Har–Magedoni.—Ufu 19:14, 15.

 • Malkamu.

  Huenda ni sawa na neno Moleki, mungu mkuu wa Waamoni. (Sef 1:5)—Tazama MOLEKI.

 • Malkia wa Mbinguni.

  Jina la cheo la mungu wa kike aliyeabudiwa na Waisraeli waasi imani katika siku za Yeremia. Baadhi ya watu wanadai kwamba linarejelea mungu wa kike wa Babiloni aliyeitwa Ishtari (Astarte). Jina la mungu wa kike wa Wasumeri aliyekuwepo awali, Inanna, linamaanisha “Malkia wa Mbinguni.” Hakuhusianishwa tu na mbingu, bali pia alikuwa mungu wa kike wa uzazi. Astarte anaitwa pia “Bimkubwa wa Mbinguni” katika maandishi yaliyochongwa ya Wamisri.—Yer 44:19.

 • Mana.

  Chakula kikuu ambacho Waisraeli walikula kwa miaka 40 waliyokuwa nyikani. Kiliandaliwa na Yehova. Kilitokea kimuujiza kwenye ardhi chini ya tabaka la umande kila asubuhi isipokuwa siku ya Sabato. Waisraeli walipokiona kwa mara ya kwanza waliulizana, “Ni nini hiki?” au, katika Kiebrania, “man huʼ?” (Kut 16:13-15, 35) Katika Maandiko mengine, kinaitwa “nafaka ya mbinguni” (Zb 78:24), “mkate kutoka mbinguni” (Zb 105:40), na “mkate wa wenye nguvu” (Zb 78:25). Yesu alirejelea mana kwa njia ya mfano.—Yoh 6:49, 50.

 • Manemane.

  Utomvu unaonata wenye manukato unaotokana na vichaka mbalimbali vya miiba au miti midogo ya jamii ya Commiphora. Manemane ni mojawapo ya viungo vilivyotumiwa kutengeneza mafuta matakatifu ya kutia mafuta. Ilitumiwa kutia mavazi au vitanda marashi, na iliongezwa kwenye mafuta yaliyotumiwa kukanda mwili na mafuta ya kujipaka. Manemane pia ilitumiwa kuitayarisha miili kabla ya kuizika.—Kut 30:23; Met 7:17; Yoh 19:39.

 • Maombolezo.

  Huzuni inayoonyeshwa waziwazi kwa sababu ya kifo au msiba mwingine. Katika nyakati za Biblia, ilikuwa desturi kuomboleza kwa kipindi fulani. Mbali na kulia kwa sauti kubwa, waombolezaji walivaa mavazi ya pekee, walitia majivu kichwani, wakararua mavazi yao, na kujipigapiga kifuani. Nyakati nyingine waombolezaji waliolipwa walialikwa mazishini.—Mwa 23:2; Est 4:3; Ufu 21:4.

 • Marijani.

  Kitu kigumu kinachofanana na jiwe kinachofanyizwa na mifupa ya wanyama wadogo wa baharini. Kinapatikana baharini kikiwa na rangi mbalimbali, kama vile nyekundu, nyeupe, na nyeusi. Marijani yalikuwa mengi sana hasa katika Bahari Nyekundu. Katika nyakati za Biblia, marijani yenye rangi nyekundu yalikuwa na thamani kubwa sana na yalitumiwa kutengenezea shanga na mapambo mengine.—Met 8:11.

 • Masadukayo.

  Madhehebu maarufu ya dini ya Kiyahudi ambayo washiriki wake walikuwa watu maarufu walio matajiri na makuhani waliokuwa na mamlaka kubwa kuhusiana na utendaji wa hekaluni. Walikataa mapokeo mengi yaliyopitishwa kwa mdomo ambayo yalifuatwa na Mafarisayo na mafundisho mengine ya Kifarisayo. Hawakuamini ufufuo wala kuwepo kwa malaika. Walimpinga Yesu.—Mt 16:1; Mdo 23:8.

 • Maserafi.

  Viumbe wa roho waliosimama kuzunguka kiti cha ufalme cha Yehova mbinguni. Neno la Kiebrania sera·phimʹ kihalisi linamaanisha “wanaowaka moto.”—Isa 6:2, 6.

 • Masihi.

  Neno hili linatokana na neno la Kiebrania linalomaanisha “mtiwa-mafuta” au “aliyetiwa mafuta.” Katika Kigiriki neno hili linatafsiriwa kuwa “Kristo.”—Da 9:25; Yoh 1:41.

 • Maskili.

  Ni neno la Kiebrania linalopatikana katika tangulizi za zaburi 13 ambalo maana yake haijulikani vizuri. Huenda linamaanisha “shairi la kutafakari.” Baadhi ya watu wanafikiri kwamba neno sawa na hilo, linalotafsiriwa kuwa ‘kutumikia kwa busara,’ huenda lina maana sawa na neno hilo.—2Nya 30:22; Zb 32:Utangulizi.

 • Matunda ya kwanza.

  Mazao ya kwanza kabisa katika majira ya mavuno; kitu kinachopatikana kwanza au malimbuko ya kitu chochote. Yehova alitaka taifa la Israeli limtolee matunda ya kwanza au uzao wa kwanza wa mwanadamu, mnyama, au mazao ya nchi. Wakiwa taifa, Waisraeli walimtolea Mungu matunda ya kwanza wakati wa Sherehe ya Mikate Isiyo na Chachu na wakati wa Pentekoste. Usemi “matunda ya kwanza” ulitumiwa pia kwa njia ya mfano kumrejelea Kristo na wafuasi wake watiwa-mafuta.—1Ko 15:23; Hes 15:21; Met 3:9; Ufu 14:4.

 • Mbashiri; Mwaguzi.

  Mtu anayedai kuwa anaweza kutabiri matukio ya wakati ujao. Makuhani wachawi, wapiga ramli, wanajimu, na wengine wanatajwa katika Biblia kuwa wabashiri au waaguzi.—Law 19:31; Kum 18:11; Mdo 16:16.

 • Mchokoo.

  Fimbo ndefu yenye ncha kali ya chuma, iliyotumiwa na wakulima kumwongoza mnyama kwa kumdungadunga nayo. Maneno ya mtu mwenye hekima yanayomchochea msikilizaji kutii ushauri wenye hekima yanafananishwa na mchokoo. “Kuipiga teke michokoo” ni maneno yanayoleta taswira ya ng’ombe dume mkaidi anayekataa kufuata mwongozo wa mchokoo kwa kuupiga teke, na hivyo kujiumiza mwenyewe.—Mdo 26:14; Amu 3:31.

 • Merodaki.

  Mungu mkuu wa jiji la Babiloni. Baada ya mfalme wa Babiloni na mtunga sheria Hamurabi kulifanya Babiloni kuwa jiji kuu la Babilonia, umaarufu wa Merodaki (au, Marduki) uliongezeka, na hatimaye akachukua mahali pa miungu kadhaa iliyokuwepo awali, akawa mungu mkuu kati ya miungu yote ya Wababiloni. Baadaye, jina la cheo “Belu” (“Mmiliki”) lilianza kutumiwa badala ya Merodaki (au, Marduki), na kwa kawaida watu walimrejelea Merodaki kwa jina Beli.—Yer 50:2.

 • Methali.

  Msemo wa hekima au hadithi fupi inayofundisha somo au kufafanua ukweli muhimu kwa maneno machache sana. Methali ya Biblia inaweza kuwa fumbo au kitendawili. Methali huwasilisha ukweli kwa lugha inayovutia, mara nyingi kupitia mifano. Misemo fulani ilianza kutumiwa kama semi za kuwadhihaki au kuwadharau watu fulani.—Mhu 12:9; 2Pe 2:22.

 • Mfinyanzi.

  Mtengenezaji wa vyungu, mabakuli, na vyombo vingine vya udongo. Neno la Kiebrania linalotafsiriwa mfinyanzi kihalisi linamaanisha “anayeumba.” Mara nyingi mamlaka ambayo mfinyanzi anayo juu ya udongo hutumiwa kuonyesha mamlaka ya enzi kuu ambayo Yehova anayo juu watu mmojammoja na mataifa.—Isa 64:8; Ro 9:21.

 • Mfumo wa (Mifumo ya) mambo.

  Neno la Kigiriki ai·onʹ hutafsiriwa kwa maneno hayo linaporejelea hali ya sasa ya mambo au matukio yanayobainisha kipindi fulani cha wakati, enzi, au zama. Biblia hutumia maneno “mfumo wa mambo wa sasa,” kurejelea hali ya sasa ya ulimwengu kwa ujumla na njia ya kilimwengu ya maisha. (2Ti 4:10) Kupitia agano la Sheria, Mungu alianzisha mfumo wa mambo ambao baadhi ya watu wanaweza kuuita enzi ya Waisraeli au Wayahudi. Kupitia dhabihu yake ya fidia, Yesu Kristo alitumiwa na Mungu kuanzisha mfumo tofauti wa mambo, ambao msingi wake ni kutaniko la Wakristo watiwa-mafuta. Huo ulikuwa mwanzo wa enzi mpya, wakati ambapo mambo halisi yaliyokuwa yameonyeshwa mapema katika agano la Sheria yalianza kutimia. Maneno hayo yanapotumiwa katika wingi yanarejelea mifumo mbalimbali ya mambo, au hali mbalimbali zilizopo sasa, ambazo zimekuwapo au zitakazokuwapo.—Mt 24:3; Mk 4:19; Ro 12:2; 1Ko 10:11.

 • Mgeuzwa imani.

  Katika Maandiko, neno hili linamaanisha mtu aliyejiunga na dini ya Kiyahudi, na ikiwa ni mwanamume alitahiriwa.—Mt 23:15; Mdo 13:43.

 • Mikasi ya kukatia tambi za taa.

  Vifaa vilivyotumiwa katika hema la ibada na hekaluni, ambavyo vilitengenezwa kwa dhahabu au shaba. Huenda vifaa hivyo vilifanana na mikasi na vilitumiwa kukata tambi za taa.—2Fa 25:14.

 • Mikatale.

  Kifaa kilichotumiwa kumfunga mtu ili kumwadhibu. Mikatale fulani ilifunga miguu peke yake, na mingine iliupinda mwili kwa njia inayochosha, labda kwa kufunga miguu, mikono, na shingo.—Yer 20:2; Mdo 16:24.

 • Mikate ya toleo.

  Tazama MIKATE YA WONYESHO.

 • Mikate ya wonyesho.

  Mikate 12 iliyowekwa katika safu mbili, mikate sita katika kila safu, kwenye meza katika chumba cha Patakatifu kilichokuwa katika hema la ibada na hekaluni. Inaitwa pia “mikate ya tabaka” na “mikate ya toleo.” Kila siku ya Sabato, mikate hiyo ambayo iliwekwa mbele za Mungu iliondolewa na mikate mipya kuwekwa kwenye meza hiyo. Kwa kawaida mikate iliyoondolewa ililiwa na makuhani tu. (2Nya 2:4; Mt 12:4; Kut 25:30; Law 24:5-9; Ebr 9:2)—Angalia Nyongeza B5.

 • Miktamu.

  Neno la Kiebrania linalotumiwa katika tangulizi sita za zaburi (Zb 16, 56-60). Ni neno la kitaalamu ambalo maana yake haijulikani vizuri, ingawa huenda linahusiana na maneno “maandishi yaliyochongwa.”

 • Milkomu.

  Mungu aliyeabudiwa na Waamoni, labda ndiye mungu anayeitwa Moleki. (1Fa 11:5, 7) Sulemani alipokaribia mwisho wa utawala wake alimjengea mungu huyu wa uwongo mahali pa juu.—Tazama MOLEKI.

 • Mina.

  Huitwa pia mane katika kitabu cha Ezekieli. Kipimo cha uzito kilichotumika pia kama pesa. Kwa kutegemea uthibitisho wa vitu vya kale unaoonyesha kwamba mina ilikuwa sawa na shekeli 50, na shekeli ilikuwa na uzito wa gramu 11.4, katika Maandiko ya Kiebrania mina ilikuwa na uzito wa gramu 570. Huenda pia kulikuwa na mina ya kifalme, kama kulivyokuwa na kipimo cha kifalme cha mkono. Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, mina ilikuwa sawa na drakma 100. Ilikuwa sawa na uzito wa gramu 340. Mina 60 zilikuwa sawa na talanta moja. (Ezr 2:69; Lu 19:13)—Angalia Nyongeza B14.

 • Miujiza; Kazi zenye nguvu.

  Matendo au matukio yanayozidi nguvu zote zinazojulikana na wanadamu na ambayo yamesababishwa na chanzo kinachozidi uwezo wa wanadamu. Maneno kama vile “ishara,” “dalili,” na “maajabu” hutumiwa nyakati nyingine katika Biblia kumaanisha jambo lilelile.—Kut 4:21; Mdo 4:22; Ebr 2:4.

 • Mkono.

  Kipimo cha urefu ambacho kwa wastani kinaanzia kwenye kiwiko mpaka kwenye ncha ya kidole cha kati. Kwa kawaida Waisraeli walitumia kipimo cha mkono chenye urefu wa sentimita 44.5 hivi (inchi 17.5), lakini walitumia pia kipimo cha mkono mrefu zaidi ambacho kilizidi mkono wa kawaida kwa upana wa kitanga cha mkono, sentimita 51.8 hivi (inchi 20.4). (Mwa 6:15; Lu 12:25)—Angalia Nyongeza B14.

 • Mkristo.

  Jina ambalo Mungu aliwapa wafuasi wa Yesu Kristo.—Mdo 11:26; 26:28.

 • Mkuu wa makuhani.

  Jina lingine la “kuhani mkuu” katika Maandiko ya Kiebrania. Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, ni wazi kwamba usemi “wakuu wa makuhani” ulirejelea wanaume walioongoza katika ukuhani, huenda walitia ndani makuhani wowote wakuu walioondolewa na pia viongozi wa vile vikundi 24 vya makuhani.—2Nya 26:20; Ezr 7:5; Mt 2:4; Mk 8:31.

 • Mlinzi.

  Mtu anayewalinda watu au mali kutokana na madhara, kwa kawaida wakati wa usiku, na ambaye anaweza kupiga king’ora aonapo hatari. Kwa kawaida walinzi waliwekwa juu ya kuta na minara ya jiji ili kuwatazama watu wakiwa mbali kabla hawajalikaribia jiji. Mlinzi ambaye ni mwanajeshi huitwa askari mlinzi. Kwa njia ya mfano, manabii walitumikia wakiwa walinzi wa taifa la Israeli, walitoa onyo kuhusu uharibifu uliokuwa ukija.—2Fa 9:20; Eze 3:17.

 • Mlo wa Jioni wa Bwana.

  Mlo halisi wa mikate isiyo na chachu na divai, vitu ambavyo vinafananisha mwili wa Kristo na damu yake; navyo ni ukumbusho wa kifo cha Yesu. Kwa kuwa huu ni mwadhimisho ambao Maandiko yanasema Wakristo wanapaswa kuuadhimisha, kwa kufaa unaitwa “Ukumbusho.”—1Ko 11:20, 23-26.

 • Mnadhiri.

  Linatokana na neno la Kiebrania linalomaanisha “Aliyetengwa,” “Aliyewekwa Wakfu,” “Aliyewekwa Kando.” Kulikuwa na vikundi viwili vya Wanadhiri: wale waliojitolea na wale waliowekwa na Mungu kuwa Wanadhiri. Mwanamume au mwanamke angeweza kuweka nadhiri ya pekee kwa Yehova ili aishi akiwa Mnadhiri kwa kipindi fulani. Wale waliojitolea kuweka nadhiri hiyo walihitaji kuzingatia vizuizi vitatu vikuu: hawakupaswa kunywa kileo chochote wala kula zao lolote la mzabibu, hawakupaswa kunyoa nywele zao, na hawakupaswa kugusa maiti. Wale waliowekwa na Mungu kuwa Wanadhiri walibaki Wanadhiri maisha yao yote, na Yehova alitaja matakwa hususa waliyopaswa kutii.—Hes 6:2-7; Amu 13:5.

 • Mnajimu.

  Mtu anayechunguza mizunguko ya jua, mwezi, na nyota ili atabiri matukio ya wakati ujao.—Da 2:27; Mt 2:1.

 • Mnazareti.

  Jina la Yesu, linaloonyesha kwamba alitoka katika mji wa Nazareti. Huenda linahusiana na neno la Kiebrania linalotafsiriwa “chipukizi” katika Isaya 11:1. Baadaye neno hilo lilitumiwa pia kuwahusu wafuasi wa Yesu.—Mt 2:23; Mdo 24:5.

 • Moleki.

  Mungu wa Waamoni; labda ndiye mungu anayeitwa Malkamu, Milkomu, na Moloki. Huenda ni jina la cheo wala si jina la mungu fulani hususa. Sheria ya Musa ilisema kwamba mtu yeyote aliyewatoa dhabihu watoto wake kwa Moleki alistahili adhabu ya kifo.—Law 20:2; Yer 32:35; Mdo 7:43.

 • Moloki.

  Tazama MOLEKI.

 • Mpatanishi.

  Mtu anayeingilia kati ili kuvipatanisha vikundi viwili. Katika Maandiko, Musa ni mpatanishi wa agano la Sheria na Yesu ni mpatanishi wa agano jipya.—Gal 3:19; 1Ti 2:5.

 • Mpinga-Kristo.

  Neno la Kigiriki lina maana mbili. Linarejelea chochote ambacho ni kinyume cha, au kinachompinga Kristo. Linaweza pia kurejelea Kristo wa uwongo, yule anayechukua nafasi ya Kristo. Watu wote, mashirika, au vikundi vinavyodai kwa uwongo kumwakilisha Kristo au vinavyodai kuwa Masihi au vinavyompinga Kristo na wanafunzi wake vinaweza kwa kufaa kuitwa wapinga-Kristo.—1Yo 2:22.

 • Mshindio.

  Katika ufumaji, mshindio ni nyuzi za kitambaa zinazotoka kushoto kwenda kulia. Nyuzi hizi zilipita juu na chini ya mtande, yaani, nyuzi ndefu zilizotoka juu kwenda chini.—Law 13:59.

 • Msimamizi.

  Ofisa wa cheo cha chini kuliko liwali katika serikali ya Babiloni. Katika Biblia, wasimamizi hawa waliwasimamia watu wenye hekima katika makao ya mfalme wa Babiloni. Wasimamizi wanatajwa pia wakati wa utawala wa Mfalme Dario wa Umedi.—Da 2:48; 6:7.

 • Mtande.

  Katika ufumaji, mtande ni nyuzi ndefu zinazotoka juu kwenda chini katika kitambaa. Nyuzi zinazopita juu na chini ya mtande kutoka kushoto kwenda kulia zinaitwa mshindio.—Amu 16:13.

 • Mti (Nguzo).

  Mlingoti ulio wima ambao juu yake mtu aliyeadhibiwa alitundikwa. Ulitumiwa katika mataifa fulani kuwaua watu na/au kuanika maiti ili kuwaonya wengine au kumfedhehesha mtu hadharani. Waashuru, waliojulikana kwa sababu ya vita vyao vya kikatili, waliingiza miti yenye ncha kali kwenye tumbo la mateka wao mpaka kifuani na kuiacha miili ya mateka hao ikining’inia juu ya miti hiyo. Hata hivyo, katika Sheria ya Wayahudi, watu waliokuwa na hatia ya kufanya makosa mazito kama vile kukufuru au kuabudu sanamu waliuawa kwanza kwa kupigwa mawe au kwa njia nyingine, kisha maiti zao zilitundikwa kwenye nguzo, au miti, ili kuwaonya wengine. (Kum 21:22, 23; 2Sa 21:6, 9) Nyakati fulani Waroma waliwafunga tu wakosaji kwenye mti au nguzo, kwa hiyo mkosaji angeishi kwa siku kadhaa na hatimaye kufa kwa sababu ya uchungu, kiu, njaa, na kuchomwa na jua. Nyakati nyingine, kama Yesu alivyouawa, walimtundika mshtakiwa mtini kwa kuipigilia misumari mikono na miguu yake. (Lu 24:20; Yoh 19:14-16; 20:25; Mdo 2:23, 36)—Tazama MTI WA MATESO.

 • Mti mtakatifu.

  Neno la Kiebrania (ʼashe·rahʹ) linarejelea (1) mlingoti mtakatifu unaomwakilisha Ashera, mungu wa kike wa uzazi wa Wakanaani, au (2) sanamu ya mungu huyo wa kike Ashera. Inaonekana kwamba milingoti hiyo ilisimama wima na kwa sehemu ilitengenezwa kwa mbao. Huenda zilikuwa nguzo ambazo hazikuwa zimechongwa, au hata miti.—Kum 16:21; Amu 6:26; 1Fa 15:13.

 • Mti wa mateso.

  Maneno hayo yametafsiriwa kutokana na neno la Kigiriki stau·rosʹ, linalomaanisha nguzo iliyo wima au mlingoti, kama ule ambao Yesu aliuawa juu yake. Hakuna uthibitisho kwamba neno hilo la Kigiriki lilimaanisha msalaba, kama ule uliotumiwa na wapagani kuwa nembo ya kidini kwa karne nyingi kabla ya Kristo kuja. Maneno “mti wa mateso” yanawasilisha maana kamili ya neno la awali, kwa kuwa Yesu pia alitumia neno stau·rosʹ kuonyesha mateso, dhiki, na fedheha ambayo wafuasi wake wangekumbana nayo. (Mt 16:24; Ebr 12:2)—Tazama MTI (NGUZO).

 • Mti wa ujuzi wa mema na mabaya.

  Ni mti uliokuwa katika bustani ya Edeni uliotumiwa na Mungu kuwakilisha haki yake ya kuwawekea wanadamu viwango vya “mema” na “mabaya.”—Mwa 2:9, 17.

 • Mti wa uzima.

  Ni mti uliokuwa katika bustani ya Edeni. Biblia haisemi kwamba kiasili matunda yake yalikuwa na uwezo fulani wa kuendeleza uhai; badala yake, mti huo uliwakilisha uhakikisho wa kwamba Mungu angewapa uzima wa milele wale ambao angewaruhusu kula matunda yake.—Mwa 2:9; 3:22.

 • Mtu aliye huru; Mtu aliyewekwa huru.

  Wakati wa utawala wa Roma, “mtu aliye huru” ni mtu aliyezaliwa akiwa huru, akiwa na haki kamili za raia. Kinyume chake, “mtu aliyewekwa huru” ni mtumwa aliyefunguliwa kutoka utumwani. Mtumwa aliyefunguliwa rasmi kutoka utumwani alipata uraia wa Roma, lakini hakustahili kugombea cheo cha kisiasa. Mtumwa ambaye hakufunguliwa rasmi alipata uhuru lakini hakupata haki kamili za raia.—1Ko 7:22.

 • Mtu anayewasiliana na roho.

  Mtu anayedai kwamba anazungumza na watu waliokufa.—Law 20:27; Kum 18:10-12; 2Fa 21:6.

 • Mtume.

  Kimsingi neno hili linamaanisha “aliyetumwa,” nalo linatumiwa kumhusu Yesu na watu fulani waliotumwa kuwatumikia wengine. Mara nyingi, linatumiwa kuwahusu wanafunzi ambao Yesu mwenyewe aliwachagua wakiwa kikundi cha wawakilishi 12 waliowekwa rasmi.—Mk 3:14; Mdo 14:14.

 • Mtumishi wa huduma.

  Ni tafsiri ya neno la Kigiriki di·aʹko·nos, ambalo mara nyingi hutafsiriwa kuwa “mhudumu” au “mtumishi.” “Mtumishi wa huduma” ni yule anayetumikia akiwa msaidizi wa baraza la wazee kutanikoni. Ni lazima atimize viwango vya Biblia ili astahili kupata pendeleo hilo la utumishi.—1Ti 3:8-10, 12.

 • Muhuri.

  Kifaa kilichotumiwa kutia alama (kwa kawaida katika udongo wa mfinyanzi au nta), alama ambayo ilionyesha umiliki, uhalisia, au makubaliano. Mihuri ya kale ilitengenezwa kwa kitu kigumu (kama vile jiwe, pembe ya tembo, au ubao) nayo ilikuwa na herufi zilizochongwa au michoro iliyoandikwa kurudi nyuma. Muhuri unatumiwa kwa njia ya mfano kurejelea kitu kilichothibitishwa kuwa cha kweli, au kuwa alama ya umiliki, au kitu kilichofichwa au siri.—Kut 28:11; Ne 9:38; Ufu 5:1; 9:4.

 • Mungu wa kweli.

  Katika Kiebrania maneno hayo hutafsiriwa kuwa “yule Mungu.” Mara nyingi, matumizi ya kibainishi dhahiri katika Kiebrania huonyesha kwamba Yehova peke yake ndiye Mungu wa kweli tofauti na miungu ya uwongo. Maneno “Mungu wa kweli” huwasilisha maana kamili kabisa ya maneno hayo ya Kiebrania katika maandiko yenye maneno hayo.—Mwa 5:22, 24; 46:3; Kum 4:39.

 • Musa, Sheria ya.

  Sheria ambayo Yehova aliwapa Waisraeli kupitia Musa katika nyika ya Sinai mwaka wa 1513 K.W.K. Kwa kawaida vitabu vya kwanza vitano vya Biblia huitwa Sheria.—Yos 23:6; Lu 24:44.

 • Muth-labeni.

  Usemi unaopatikana katika utangulizi wa Zaburi 9. Kulingana na desturi, maana yake ni “kuhusu kifo cha mwana.” Baadhi ya watu wanasema kwamba lilikuwa jina au labda maneno ya kwanza ya wimbo uliojulikana ambayo yangetumiwa kuimba zaburi hiyo.

 • Mwadhimisho wa Miaka 50.

  Mwadhimisho uliofanywa kila mwaka wa 50, kuanzia wakati ambapo Waisraeli waliingia katika Nchi ya Ahadi. Nchi haikupaswa kulimwa katika mwaka wa Mwadhimisho huo, na watumwa Waebrania walipaswa kuwekwa huru. Ardhi za urithi zilizokuwa zimeuzwa zilirudishwa. Kwa njia fulani, mwaka mzima wa Mwadhimisho huo ulikuwa mwaka wa sherehe, mwaka wa uhuru ambao ulilirudisha taifa katika hali waliyofurahia wakati Mungu alipolianzisha taifa hilo mwanzoni.—Law 25:10.

 • Mwana wa binadamu.

  Maneno hayo yanapatikana mara 80 hivi katika vitabu vya Injili. Yanamhusu Yesu Kristo na yanaonyesha kwamba kwa kuzaliwa akiwa na mwili wa nyama, alikuja kuwa mwanadamu, wala hakuwa kamwe kiumbe wa roho aliyejivika mwili wa kibinadamu. Maneno hayo yanaonyesha pia kwamba Yesu angetimiza unabii wa Danieli 7:13 na 14. Katika Maandiko ya Kiebrania, maneno hayo yalitumiwa kumhusu Ezekieli na Danieli, yakikazia tofauti iliyopo kati ya wasemaji hao wanaoweza kufa na Mungu ambaye ni Chanzo cha ujumbe wao.—Eze 3:17; Da 8:17; Mt 19:28; 20:28.

 • Mwana wa Daudi.

  Kwa kawaida maneno hayo hutumiwa kumrejelea Yesu, yakikazia kwamba yeye ndiye Mrithi wa agano la Ufalme ambalo lingetimizwa na mtu fulani katika ukoo wa Daudi.—Mt 12:23; 21:9.

 • Mwandishi.

  Mtu aliyenakili Maandiko ya Kiebrania. Kufikia wakati ambapo Yesu alikuja duniani, neno hilo lilimaanisha watu waliokuwa na ujuzi wa Sheria. Waandishi walimpinga Yesu.—Ezr 7:6, maelezo ya chini; Mk 12:38, 39; 14:1.

 • Mwangalizi.

  Mwanamume ambaye jukumu lake la msingi ni kulilinda na kulichunga kutaniko. Wazo kuu la neno la Kigiriki e·piʹsko·pos ni kuangalia kwa kusudi la kulinda. Maneno “mwangalizi” na “mzee” (pre·sbyʹte·ros) yanarejelea wadhifa uleule katika kutaniko la Kikristo; neno “mzee” linaonyesha kwamba mtu aliyewekwa rasmi kuwa mzee ana sifa za ukomavu, na neno “mwangalizi” linakazia majukumu yanayofungamana na wadhifa huo.—Mdo 20:28; 1Ti 3:2-7; 1Pe 5:2.

 • Mwebrania.

  Neno lililotumiwa mwanzoni kumrejelea Abramu (Abrahamu), na hivyo kumtofautisha na majirani wake Waamori. Baadaye lilitumiwa kuwahusu wazao wa Abrahamu kupitia Yakobo mjukuu wake na pia lilitumiwa kurejelea lugha yao. Kufikia siku za Yesu, lugha ya Kiebrania ilikuwa na maneno mengi ya Kiaramu na ndiyo lugha iliyozungumzwa na Kristo na wanafunzi wake.—Mwa 14:13; Kut 5:3; Mdo 26:14.

 • Mwenendo mpotovu.

  Usemi huo unatokana na neno la Kigiriki a·selʹgei·a ambalo linahusiana na matendo yanayokiuka kabisa sheria za Mungu na ambayo yanadhihirisha mtazamo wa ufidhuli au mtazamo unaochukiza usio wa aibu; roho ya kudharau au hata kuchukia mamlaka, sheria, na viwango. Usemi huo haurejelei mwenendo usiofaa unaohusu makosa madogo.—Gal 5:19; 2Pe 2:7.

 • Mwezi mpya.

  Ni siku ya kwanza ya kila mwezi katika kalenda ya Wayahudi, ambayo iliadhimishwa ikiwa siku ya kukusanyika pamoja, kufanya karamu, na kutoa dhabihu za pekee. Baadaye, siku hiyo ilikuja kuwa siku muhimu ya kitaifa ya sherehe, na watu hawakufanya kazi siku hiyo.—Hes 10:10; 2Nya 8:13; Kol 2:16.

 • Mwonaji.

  Mtu aliyewezeshwa na Mungu kutambua mapenzi ya Mungu; mtu ambaye macho yake yalifunguliwa ili yaone au kuelewa mambo ambayo wanadamu kwa ujumla hawakuona. Neno la Kiebrania linatokana na neno ambalo kimsingi linamaanisha “kuona,” iwe ni kihalisi au kwa njia ya mfano. Watu walimfikia mwonaji ili kupata ushauri wenye hekima kuhusu matatizo waliyokabili.—1Sa 9:9.

 • Mwovu au yule Mwovu.

  Usemi huu hutumiwa kumhusu Shetani Ibilisi, anayempinga Mungu na viwango vyake vya uadilifu.—Mt 6:13; 1Yo 5:19.

 • Myahudi.

  Neno linalotumiwa kumrejelea mtu wa kabila la Yuda baada ya kuanguka kwa ufalme wa Israeli wa makabila kumi. (2Fa 16:6) Baada ya Waisraeli kutoka uhamishoni Babiloni, lilitumiwa kuwarejelea Waisraeli wa makabila mbalimbali waliorudi Israeli. (Ezr 4:12) Baadaye, lilitumiwa kotekote ulimwenguni kuwatofautisha Waisraeli na watu wasio Waisraeli. (Est 3:6) Mtume Paulo analitumia pia neno hilo kwa njia ya mfano anapofafanua kwamba taifa la mtu si muhimu katika kutaniko la Kikristo.—Ro 2:28, 29; Gal 3:28.

 • Mzaliwa wa kwanza.

  Neno hilo linamaanisha hasa mtoto mkubwa wa kiume wa baba (badala ya mtoto wa kwanza anayezaliwa na mama). Katika nyakati za Biblia, mwana mzaliwa wa kwanza aliheshimiwa katika familia, naye alipewa jukumu la kuwa kichwa cha familia baba yake alipokufa. Usemi huo unamhusu pia mnyama dume anayezaliwa kwanza.—Kut 11:5; 13:12; Mwa 25:33; Kol 1:15.

 • Mzee; Mwanamume mzee.

  Mwanamume mwenye umri mkubwa, lakini katika Maandiko, maneno hayo yanarejelea mtu ambaye hasa ana wadhifa wa mamlaka na majukumu katika jamii au taifa. Maneno hayo hutumiwa pia kuwahusu viumbe wa mbinguni katika kitabu cha Ufunuo. Neno la Kigiriki pre·sbyʹte·ros linatafsiriwa kuwa “mzee” linapowarejelea wale walio na jukumu la kuongoza kutanikoni.—Kut 4:29; Met 31:23; 1Ti 5:17; Ufu 4:4.

 • N

 • Nabii.

  Mtu anayetumiwa kutangaza makusudi ya Mungu. Manabii walikuwa wasemaji wa Mungu, hawakutabiri tu bali pia waliwasilisha mafundisho ya Yehova, amri zake, na hukumu zake.—Am 3:7; 2Pe 1:21.

 • Nadhiri.

  Ahadi takatifu ambayo mtu anamwahidi Mungu kwamba atafanya jambo fulani, atatoa dhabihu au zawadi fulani, ataanza utumishi fulani, au atajiepusha na vitu fulani ambavyo kimsingi havijakatazwa. Nadhiri ilikuwa na uzito kama kiapo.—Hes 6:2; Mhu 5:4; Mt 5:33.

 • Nafsi.

  Tafsiri iliyozoeleka ya neno la Kiebrania neʹphesh na neno la Kigiriki psy·kheʹ. Uchunguzi wa jinsi maneno hayo yanavyotumika katika Biblia, unaonyesha wazi kwamba kimsingi maneno hayo yanamaanisha (1) watu, (2) wanyama, au (3) uhai wa mtu au wa mnyama. (Mwa 1:20; 2:7; Hes 31:28; 1Pe 3:20; pia maelezo ya chini.) Tofauti na jinsi neno “nafsi” linavyotumiwa katika mafundisho mengi ya kidini, Biblia inaonyesha kwamba maneno yote mawili neʹphesh na psy·kheʹ, yanapotumiwa kuwahusu viumbe walio duniani, yanarejelea kitu kilicho halisi, kinachoweza kuguswa, kinachoonekana, na kinachoweza kufa. Katika tafsiri hii ya Biblia, mara nyingi maneno hayo ya lugha za awali yametafsiriwa kulingana na maana yake katika kila muktadha, kwa maneno kama vile “uhai,” “kiumbe,” “mtu,” au kama kiwakilishi nafsi (kwa mfano, “mimi” kuwakilisha “nafsi yangu”). Mara nyingi, maelezo ya chini hutaja neno “nafsi” linaloweza pia kutumika. Neno “nafsi” linapotumiwa, katika maandishi makuu au katika maelezo ya chini, linapaswa kueleweka kulingana na ufafanuzi huo. Maneno “kufanya jambo fulani kwa nafsi yote” yanamaanisha kulifanya kwa mwili wote, moyo wote, au kwa uhai wote wa mtu. (Kum 6:5; Mt 22:37) Katika Maandiko mengine, maneno hayo ya lugha za awali yanaweza kutumiwa kumaanisha tamaa au hamu ya kiumbe aliye hai. Yanaweza pia kumaanisha mtu aliyekufa au maiti.—Hes 6:6; Met 23:2; Isa 56:11; Hag 2:13.

 • Nardo.

  Mafuta ghali yenye manukato yaliyokuwa na rangi nyekundu hafifu, yaliyotengenezwa kutokana na mmea wa nardo (Nardostachys jatamansi). Kwa kuwa yalikuwa ghali, kwa kawaida mafuta ya nardo yalichanganywa na mafuta mengine yasiyo bora sana, na nyakati nyingine watu walitengeneza mafuta bandia ya nardo. Haishangazi kwamba Marko na Yohana wanasema kwamba Yesu alimiminiwa “nardo halisi.”—Mk 14:3; Yoh 12:3.

 • Ndoa ya ndugu mkwe.

  Ni desturi ambayo iliongezwa baadaye katika Sheria ya Musa, iliyomruhusu mwanamume kumuoa mjane wa ndugu yake aliyekufa bila mwana ili mwanamume huyo azae watoto na kuendeleza kizazi cha ndugu yake.—Mwa 38:8; Kum 25:5.

 • Nehilothi.

  Neno linalopatikana katika utangulizi wa Zaburi ya 5 ambalo maana yake haijulikani vizuri. Baadhi ya watu huamini kwamba linarejelea ala fulani inayopulizwa, nao wanalihusianisha neno hilo na neno la Kiebrania ambalo kimsingi linahusiana na neno cha·lilʹ (filimbi). Hata hivyo, linaweza kumaanisha sauti ya wimbo.

 • Nguo za magunia.

  Zilitengenezwa kwa kitambaa kigumu kinachotumiwa kutengenezea magunia, au mifuko, kama ile inayobeba nafaka. Kwa kawaida nguo hizo zilifumwa kwa kutumia manyoya ya mbuzi yaliyokolea rangi, nazo zilikuwa nguo za kitamaduni za maombolezo.—Mwa 37:34; Lu 10:13.

 • Nguzo takatifu.

  Nguzo iliyo wima, kwa kawaida ilikuwa ya mawe; ni wazi kwamba ilikuwa sanamu ya uume ya Baali au ya miungu mingine ya uwongo.—Kut 23:24.

 • Nguzo.

  Mhimili au mnara au kitu kinachofanana na nguzo. Baadhi ya nguzo zilijengwa ili kuwakumbusha watu mambo au matukio fulani ya kihistoria. Nguzo za kutegemeza jengo zilitumiwa katika hekalu na katika majengo mbalimbali ya kifalme yaliyojengwa na Sulemani. Wapagani walisimamisha nguzo takatifu kwa ajili ya dini yao ya uwongo, na nyakati nyingine Waisraeli waliiga zoea hilo. (Amu 16:29; 1Fa 7:21; 14:23)—Tazama KIFUNIKO CHA NGUZO.

 • Nira.

  Kipande cha mti kilichowekwa juu ya mabega ya mtu na mizigo kuning’inizwa kila upande, au ubao au kiunzi kilichowekwa juu ya shingo za wanyama wawili waliovuta mizigo (kwa kawaida ng’ombe); wanyama hao walifungiwa nira walipovuta kifaa cha kulimia au gari la kukokotwa. Kwa kuwa mara nyingi watumwa walitumia nira kubeba mizigo mizito, nira ilitumiwa kwa njia ya mfano kufananisha utumwa au kujitiisha chini ya mtu mwingine, na pia ukandamizaji na mateso. Kuondoa au kuvunja nira kulimaanisha kumweka mtu huru kutoka kifungoni, kutoka katika ukandamizaji, na dhuluma.—Law 26:13; Mt 11:29, 30.

 • Nisani.

  Jina jipya la mwezi wa Abibu, mwezi wa kwanza katika kalenda takatifu ya Wayahudi baada ya kutoka uhamishoni Babiloni na jina la mwezi wa saba katika kalenda iliyotumiwa na watu wote. Mwezi huo ulianzia katikati ya mwezi wa Machi mpaka katikati ya mwezi wa Aprili. (Ne 2:1)—Angalia Nyongeza B15.

 • Njia.

  Usemi huu unatumiwa kwa njia ya mfano katika Maandiko kumaanisha matendo au mwenendo unaokubaliwa au usiokubaliwa na Yehova. Wale waliokuja kuwa wafuasi wa Yesu Kristo waliitwa watu wa “Ile Njia,” yaani, waliishi kwa njia iliyotegemea imani katika Yesu Kristo, wakifuata mfano wake.—Mdo 19:9.

 • Nyara.

  Vitu vya kibinafsi au vya nyumbani, mifugo, au vitu vingine vyenye thamani vinavyochukuliwa kutoka kwa adui aliyeshindwa.—Yos 7:21; 22:8; Ebr 7:4.

 • Nyota ya asubuhi.

  Tazama NYOTA YA MCHANA.

 • Nyota ya mchana.

  Ni sawa na “nyota ya asubuhi.” Ndiyo nyota ya mwisho kuchomoza kwenye upeo wa mashariki kabla ya jua kuchomoza, na hivyo kutangaza kupambazuka kwa siku mpya.—Ufu 22:16; 2Pe 1:19.

 • Nzige.

  Jamii mbalimbali za panzi wanaohama katika makundi makubwa. Katika Sheria ya Musa, walionwa kuwa safi na wangeweza kuliwa. Makundi makubwa ya nzige yanayotafuna kila kitu kokote yanakopita na kusababisha uharibifu mkubwa, yalionwa kuwa pigo.—Kut 10:14; Mt 3:4.

 • O

 • Omeri.

  Kipimo cha vitu vikavu kilichokuwa sawa na lita 2.2, au sehemu moja ya kumi ya efa. (Kut 16:16, 18)—Angalia Nyongeza B14.

 • P

 • Pakanga.

  Vijiti vya mimea mbalimbali vyenye ladha chungu sana na harufu kali inayovutia. Pakanga hutumiwa kwa njia ya mfano katika Biblia kufafanua matokeo machungu ya uasherati, utumwa, ukosefu wa haki, na uasi imani. Katika Ufunuo 8:11, “pakanga” humaanisha kitu kichungu chenye sumu, kinachoitwa pia absinthe.Kum 29:18; Met 5:4; Yer 9:15; Am 5:7.

 • Paradiso.

  Bustani maridadi, au shamba lililo kama bustani. Paradiso ya kwanza ilikuwa Edeni, ambayo Yehova aliwatayarishia wanadamu wawili wa kwanza. Yesu alipokuwa akizungumza na mmoja wa wahalifu waliotundikwa kando yake kwenye mti wa mateso, alidokeza kwamba dunia itakuwa paradiso. Katika andiko la 2 Wakorintho 12:4, ni wazi kwamba neno hilo linarejelea paradiso ya wakati ujao, na katika Ufunuo 2:7, linarejelea paradiso ya kimbingu.—Wim 4:13; Lu 23:43.

 • Pasaka.

  Sherehe ya kila mwaka iliyofanywa siku ya 14 ya mwezi wa Abibu (baadaye mwezi huo uliitwa Nisani) ili kuadhimisha ukombozi wa Waisraeli kutoka Misri. Iliadhimishwa kwa kumchinja na kumchoma mwanakondoo (au mbuzi), na kumla kwa mboga chungu na mikate isiyo na chachu.—Kut 12:27; Yoh 6:4; 1Ko 5:7.

 • Patakatifu Zaidi.

  Chumba cha ndani zaidi katika hema la ibada na hekaluni, ambamo sanduku la agano liliwekwa; panaitwa pia Patakatifu pa Patakatifu. Mbali na Musa, ni kuhani mkuu peke yake aliyeruhusiwa kuingia Patakatifu Zaidi, naye angeweza kuingia humo siku moja tu katika Siku ya kila mwaka ya Kufunika Dhambi.—Kut 26:33; Law 16:2, 17; 1Fa 6:16; Ebr 9:3.

 • Patakatifu.

  Chumba cha kwanza kikubwa zaidi katika hema la ibada au katika hekalu, nacho ni tofauti na chumba cha ndani zaidi, yaani, Patakatifu Zaidi. Katika hema la ibada, Patakatifu palikuwa na kinara cha taa cha dhahabu, madhabahu ya uvumba ya dhahabu, meza ya mikate ya wonyesho, na vyombo vitakatifu; katika hekalu, mahali hapo palikuwa na madhabahu ya dhahabu, vinara kumi vya taa vya dhahabu, na meza kumi za mikate ya wonyesho. (Kut 26:33; Ebr 9:2)—Angalia Nyongeza B5 na B8.

 • Pazia.

  Kitambaa kilichofumwa kwa njia maridadi na kutariziwa kwa michoro ya makerubi ambacho kilitenganisha Patakatifu na Patakatifu Zaidi katika hema la ibada na pia hekaluni. (Kut 26:31; 2Nya 3:14; Mt 27:51; Ebr 9:3)—Angalia Nyongeza B5.

 • Pembe za madhabahu.

  Sehemu zilizochomoza kama pembe kwenye kona nne za madhabahu fulani. (Law 8:15; 1Fa 2:28)—Angalia Nyongeza B5 na B8.

 • Pembe.

  Neno hili linarejelea pembe za wanyama, ambazo zilitumiwa kama vyombo vya kunywea, vyombo vya mafuta, vyombo vya wino na vipodozi, na ala za muziki au za kutoa ishara fulani. (1Sa 16:1, 13; 1Fa 1:39; Eze 9:2) “Pembe” hutumiwa mara nyingi kwa njia ya mfano kumaanisha nguvu na ushindi.—Kum 33:17; Mik 4:13; Zek 1:19.

 • Pentekoste.

  Sherehe ya pili kati ya sherehe tatu kuu ambazo wanaume wote Wayahudi walipaswa kusherehekea kule Yerusalemu. Neno Pentekoste, linalomaanisha “(Siku) ya Hamsini,” ndilo neno linalotumiwa katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo kurejelea Sherehe ya Mavuno au Sherehe ya Majuma inayotajwa katika Maandiko ya Kiebrania. Sherehe hiyo ilifanywa siku ya 50 kuanzia Nisani 16.—Kut 23:16; 34:22; Mdo 2:1.

 • Pete ya muhuri.

  Aina ya muhuri uliovaliwa kwenye kidole au kutiwa kwenye kamba, na huenda ulivaliwa shingoni. Pete hiyo ilikuwa ishara ya mamlaka ya mtawala au ofisa. (Mwa 41:42)—Tazama MUHURI.

 • Pigo.

  Katika Maandiko ya Kiebrania, kwa kawaida neno hili linamaanisha tauni, ugonjwa, au adhabu ya msiba kutoka kwa Yehova. Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo linamaanisha kupiga kwa kiboko au mjeledi wenye vifundo au ncha kali.—Hes 16:49; Yoh 19:1.

 • Pima.

  Kipimo cha urefu kinachotumiwa kupima kina cha maji, ni sawa na mita 1.8 (futi 6). (Mdo 27:28)—Angalia Nyongeza B14.

 • Pimu.

  Kipimo cha uzito na pia bei ambayo Wafilisti walitoza ili kunoa vifaa mbalimbali vya chuma. Mawe kadhaa ya kupimia uzito yaliyopatikana katika machimbo ya vitu vya kale katika nchi ya Israel yana konsonanti za kale za Kiebrania za neno “pimu”; kwa wastani yana uzito wa gramu 7.8, ambao ni karibu theluthi mbili za shekeli.—1Sa 13:20, 21.

 • Porneia.

  Tazama UASHERATI.

 • Purimu.

  Sherehe ya kila mwaka iliyofanywa siku ya 14 na ya 15 katika mwezi wa Adari. Inaadhimishwa ili kukumbuka jinsi Wayahudi walivyokombolewa ili wasiangamizwe katika siku za Malkia Esta. Neno pu·rimʹ ambalo si la Kiebrania linamaanisha “kura.” Sherehe ya Purimu, au Sherehe ya Kura, iliitwa hivyo kwa sababu ya tendo la Hamani la kupiga Puri (Kura) ili kuamua siku ambayo angetekeleza njama yake ya kuwaangamiza Wayahudi.—Est 3:7; 9:26.

 • R

 • Rahabu.

  Jina linalotumiwa kwa njia ya mfano katika kitabu cha Ayubu, Zaburi, na Isaya (si mwanamke Rahabu anayetajwa katika kitabu cha Yoshua). Katika kitabu cha Ayubu, muktadha unafunua kwamba huyu Rahabu ni mnyama mkubwa sana wa baharini; katika maandiko mengine mnyama huyu mkubwa sana wa baharini anatumiwa kufananisha Misri.—Ayu 9:13; Zb 87:4; Isa 30:7; 51:9, 10.

 • Rehani.

  Kitu kinachomilikiwa na mkopaji ambacho anampa mkopeshaji ili kumhakikishia kwamba atalipa mkopo. Kitu hicho kiliitwa pia dhamana ya mkopo. Sheria ya Musa ilikuwa na maagizo yaliyohusu rehani ambayo yaliwalinda maskini na raia wa taifa hilo ambao hawakuwa na mtetezi.—Kut 22:26; Eze 18:7.

 • Roho takatifu.

  Kani ya utendaji isiyoonekana inayotumiwa na Mungu kutimiza mapenzi yake. Ni takatifu kwa sababu inatoka kwa Yehova, ambaye ni safi na mwadilifu kwa kiwango cha juu zaidi, na kwa sababu ndiyo njia anayotumia Mungu kutimiza mambo matakatifu.—Lu 1:35; Mdo 1:8.

 • Roho waovu.

  Viumbe waovu wa roho wasioonekana wenye nguvu zinazozidi za wanadamu. Kwa kuwa wanaitwa “wana wa Mungu wa kweli” katika Mwanzo 6:2 na “malaika” katika Yuda 6, hawakuumbwa wakiwa waovu; badala yake, walikuwa malaika waliojifanya wenyewe kuwa maadui wa Mungu kwa kutomtii katika siku za Noa na kujiunga na Shetani katika kumwasi Yehova.—Kum 32:17; Lu 8:30; Mdo 16:16; Yak 2:19.

 • Roho.

  Neno la Kiebrania ruʹach na neno la Kigiriki pneuʹma, ambayo kwa kawaida hutafsiriwa kuwa “roho” yana maana kadhaa. Yote mawili yanarejelea kitu ambacho macho ya wanadamu hayawezi kuona na huthibitisha kuwapo kwa nguvu inayotenda. Maneno hayo ya Kiebrania na Kigiriki hutumiwa kurejelea (1) upepo, (2) nguvu ya uhai inayotenda ndani ya viumbe walio duniani, (3) nguvu za msukumo zinazotoka katika moyo wa mfano na kumfanya mtu aseme na kutenda mambo kwa njia fulani, (4) maneno yaliyoongozwa na roho yanayotoka katika chanzo kisichoonekana, (5) Mungu na viumbe wa roho, na (6) nguvu za utendaji za Mungu, au roho takatifu.—Kut 35:21; Zb 104:29; Mt 12:43; Lu 11:13.

 • S

 • Sabato.

  Neno hili linatokana na neno la Kiebrania linalomaanisha “kupumzika; kukoma.” Ni siku ya saba katika juma la Kiyahudi (ilianza Ijumaa baada ya jua kutua mpaka Jumamosi baada ya jua kutua). Siku nyingine za sherehe katika mwaka ziliitwa pia siku za sabato, kutia ndani mwaka wa 7 na mwaka wa 50. Katika siku ya Sabato, hakuna kazi iliyopaswa kufanywa isipokuwa utumishi wa makuhani katika mahali patakatifu. Katika miaka ya Sabato, nchi haikupaswa kulimwa na Waebrania hawakupaswa kuwalazimisha Waebrania wenzao walipe madeni. Sheria ya Musa ilikuwa na usawaziko kuhusu mambo yaliyokatazwa siku ya Sabato, lakini viongozi wa kidini waliongeza mambo hayo hatua kwa hatua hivi kwamba kufikia siku za Yesu ilikuwa vigumu kwa watu kuyashika mambo hayo.—Kut 20:8; Law 25:4; Lu 13:14-16; Kol 2:16.

 • Safi.

  Katika Biblia, neno hili halimaanishi tu usafi wa kimwili bali pia linamaanisha kudumisha au kurudisha katika hali isiyo na dosari, doa, na kuwa huru kutokana na kitu chochote kinachochafua, kinachotia unajisi, au kupotosha kimaadili au kiroho. Chini ya Sheria ya Musa, neno hilo linamaanisha kuwa safi kisherehe.—Law 10:10; Zb 51:7; Mt 8:2; 1Ko 6:11.

 • Safu ya Nguzo za Sulemani.

  Katika siku za Yesu, safu hiyo ilikuwa njia iliyofunikwa upande wa mashariki wa ua wa nje, na wengi waliamini kwamba ilikuwa safu iliyobaki ya hekalu la Sulemani. Yesu alitembea kwenye safu hiyo “wakati wa majira ya baridi kali,” na Wakristo wa mapema walikutana kwenye eneo hilo kwa ajili ya ibada. (Yoh 10:22, 23; Mdo 5:12)—Angalia Nyongeza B11.

 • Samaria.

  Kwa miaka 200, lilikuwa jiji kuu la ufalme wa kaskazini wa Israeli wa makabila kumi, na pia lilikuwa jina la eneo lote la makabila hayo. Jiji hilo lilijengwa juu ya mlima uliokuwa na jina hilo. Katika siku za Yesu, Samaria lilikuwa jina la wilaya ya Roma iliyokuwa kati ya Galilaya upande wa kaskazini na Yudea upande wa kusini. Kwa kawaida Yesu aliepuka kuhubiri katika eneo hilo katika safari zake, lakini nyakati nyingine alipitia humo na kuzungumza na wakaaji wa eneo hilo. Petro alitumia ufunguo wa pili wa mfano wa Ufalme Wasamaria walipopokea roho takatifu. (1Fa 16:24; Yoh 4:7; Mdo 8:14)—Angalia Nyongeza B10.

 • Sanamu; Ibada ya sanamu.

  Sanamu ni mfano wa kitu chochote, kitu halisi au cha kuwaziwa, ambacho huenda kikatumiwa na watu katika ibada. Kuabudu sanamu ni kustahi, kupenda, kuabudu, au kuihusudu sanamu.—Zb 115:4; Mdo 17:16; 1Ko 10:14.

 • Sanduku la agano.

  Sanduku lililotengenezwa kwa mbao za mshita na kufunikwa kwa dhahabu, ambalo liliwekwa Patakatifu Zaidi katika hema la ibada na baadaye Patakatifu Zaidi katika hekalu lililojengwa na Sulemani. Lilikuwa na kifuniko cha dhahabu tupu na makerubi wawili walioelekeana. Vitu vya msingi vilivyokuwemo ni yale mabamba mawili yaliyokuwa na zile Amri Kumi. (Kum 31:26; 1Fa 6:19; Ebr 9:4)—Angalia Nyongeza B5 na B8.

 • Sanhedrini.

  Mahakama kuu ya Wayahudi iliyokuwa Yerusalemu. Katika siku za Yesu, ilikuwa na washiriki 71, kutia ndani kuhani mkuu na watu wengine ambao awali walikuwa makuhani wakuu, washiriki wa familia za makuhani, wazee, viongozi wa makabila na koo, na waandishi.—Mk 15:1; Mdo 5:34; 23:1, 6.

 • Sayuni; Mlima Sayuni.

  Ni jina la jiji la Wayebusi lenye ngome lililoitwa Yebusi ambalo lilikuwa kwenye kilima kilichokuwa upande wa kusini mashariki wa Yerusalemu. Baada ya Daudi kuliteka, alijenga makao yake ya kifalme huko, na jiji hilo likaanza kuitwa “Jiji la Daudi.” (2Sa 5:7, 9) Mlima Sayuni ukawa mlima mtakatifu hasa kwa Yehova wakati Daudi alipohamishia huko sanduku la agano. Baadaye, jina hilo lilitia ndani eneo la hekalu kwenye Mlima Moria, na nyakati nyingine jiji lote la Yerusalemu. Mara nyingi jina “Sayuni” hutumiwa kwa njia ya mfano katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo.—Zb 2:6; 1Pe 2:6; Ufu 14:1.

 • Sea.

  Kipimo cha vitu vikavu. Kulingana na kipimo cha bathi cha ujazo wa vitu vya majimaji, sea ilikuwa sawa na lita 7.33. (2Fa 7:1)—Angalia Nyongeza B14.

 • Sehemu ya kumi.

  Sehemu ya kumi, au asilimia 10, ilitolewa au kulipwa ikiwa ushuru, hasa kwa ajili ya makusudi ya kidini. (Mal 3:10; Kum 26:12; Mt 23:23) Chini ya Sheria ya Musa, kila mwaka Walawi walipewa sehemu ya kumi ya mazao ya nchi na sehemu ya kumi ya ongezeko la mifugo ili kuwategemeza. Walawi waliwapa makuhani wa ukoo wa Haruni sehemu ya kumi ya sehemu hiyo ya kumi ili kuwategemeza. Kulikuwa pia na sehemu nyingine za kumi. Wakristo hawako chini ya takwa la kutoa sehemu ya kumi.

 • Sela.

  Neno la kitaalamu linalohusiana na muziki au kukariri linalopatikana katika kitabu cha Zaburi na Habakuki. Linaweza kumaanisha kituo katika uimbaji au muziki, au mambo yote mawili, kwa kusudi la kutafakari kimyakimya au kuyafanya maneno yaliyotoka kuimbwa yawe wazi. Katika Septuajinti ya Kigiriki neno hilo linatafsiriwa kuwa di·aʹpsal·ma, linalomaanisha “pumziko la muziki.”—Zb 3:4; Hab 3:3.

 • Shebati.

  Jina la mwezi wa 11 katika kalenda takatifu ya Wayahudi baada ya kutoka uhamishoni Babiloni na jina la mwezi wa 5 katika kalenda iliyotumiwa na watu wote. Mwezi huo ulianzia katikati ya mwezi wa Januari mpaka katikati ya mwezi wa Februari. (Zek 1:7)—Angalia Nyongeza B15.

 • Shekeli.

  Kipimo cha msingi cha uzito kilichotumiwa na Waebrania na pia kilitumika kama pesa. Kipimo hicho kilikuwa na uzito wa gramu 11.4. Huenda maneno “shekeli ya mahali patakatifu” yalitumiwa kukazia kwamba kipimo hicho kilipaswa kuwa sahihi kabisa au kilipaswa kulingana kabisa na kipimo cha kawaida cha uzito kilichowekwa katika hema la ibada. Huenda kulikuwa na shekeli ya kifalme (iliyokuwa tofauti na shekeli ya kawaida) au kipimo cha kawaida cha uzito kilichowekwa katika makao ya mfalme.—Kut 30:13.

 • Sheminithi.

  Neno la kimuziki ambalo kihalisi linamaanisha “ya nane” ambayo huenda ni sauti ya chini zaidi au mtindo wa chini. Lilipotumiwa kuhusu ala, huenda neno hilo lilimaanisha ala zilizotoa sauti nzito katika muziki. Lilipotumiwa kuhusu nyimbo, inaelekea kwamba lilirejelea ala zilizopigwa kwa sauti nzito za chini zikiambatana na nyimbo zilizoimbwa kwa sauti hizo.—1Nya 15:21; Zb 6:Utangulizi; 12:Utangulizi.

 • Sheoli.

  Neno la Kiebrania lenye maana sawa na neno la Kigiriki “Hadesi.” Linatafsiriwa kuwa “Kaburi” (kwa herufi kubwa), ili kuonyesha kwamba ni kaburi la wanadamu wote kwa ujumla wala si kaburi moja.—Mwa 37:35; Zb 16:10; Mdo 2:31 (maelezo ya chini).

 • Sherehe ya Mavuno; Sherehe ya Majuma.

  Tazama PENTEKOSTE.

 • Sherehe ya Mikate Isiyo na Chachu.

  Sherehe ya kwanza kati ya sherehe tatu kubwa za kila mwaka zilizofanywa na Waisraeli. Ilianza tarehe 15 ya mwezi wa Nisani, siku iliyofuata siku ya Pasaka, na kuendelea kwa siku saba. Ni mikate isiyo na chachu tu iliyopaswa kuliwa, ili kuwakumbusha safari yao ya Kutoka Misri.—Kut 23:15; Mk 14:1.

 • Sherehe ya Vibanda.

  Iliitwa pia Sherehe ya Mahema, au Sherehe ya Kukusanya. Ilifanywa tarehe 15-21 ya mwezi wa Ethanimu. Waisraeli walisherehekea pindi ya mavuno mwishoni mwa mwaka wa kilimo katika Israeli na ulikuwa wakati wa kushangilia na kushukuru kwa sababu Yehova alibariki mazao yao. Siku za sherehe hiyo, watu walikaa katika vibanda, au mabanda yenye umbo la paa, ili kuwakumbusha safari yao ya Kutoka Misri. Ilikuwa kati ya sherehe tatu ambazo wanaume walipaswa kwenda Yerusalemu kuadhimisha.—Law 23:34; Ezr 3:4.

 • Sherehe ya Wakfu.

  Ilikuwa sherehe ya kila mwaka ya kukumbuka kutakaswa kwa hekalu baada ya kuchafuliwa na Antioko Epifane. Sherehe hiyo ilianza tarehe 25 ya mwezi wa Kislevu na kuendelea kwa siku nane.—Yoh 10:22.

 • Sheria.

  Neno hili linapoandikwa kwa herufi kubwa, linamaanisha Sheria ya Musa au vitabu vya kwanza vitano vya Biblia. Linapoandikwa kwa herufi ndogo, linaweza kumaanisha sheria moja moja katika Sheria ya Musa au kanuni fulani ya sheria.—Hes 15:16; Kum 4:8; Mt 7:12; Gal 3:24.

 • Shetani.

  Ni neno la Kiebrania linalomaanisha “Mpinzani.” Neno hilo linapotumiwa na kibainishi dhahiri katika lugha za awali, linamrejelea Shetani Ibilisi, Adui mkuu wa Mungu.—Ayu 1:6; Mt 4:10; Ufu 12:9.

 • Shinikizo la divai.

  Kwa kawaida shinikizo la divai lilitengenezwa kwa kuchimba mashimo mawili katika jiwe la chokaa, shimo moja lilikuwa juu kuliko lingine, na mashimo hayo yaliunganishwa kwa mfereji mdogo. Zabibu ziliposhinikizwa katika shimo la juu, maji ya zabibu yalitiririka katika shimo la chini. Maneno hayo yanatumiwa kwa njia ya mfano kurejelea hukumu ya Mungu.—Isa 5:2; Ufu 19:15.

 • Shohamu.

  Jiwe lenye thamani ya wastani, aina ngumu ya jiwe la akiki, au jiwe la kalkedoni lenye matabaka mbalimbali. Jiwe la shohamu lina matabaka meupe katikati ya matabaka meusi, ya kahawia, mekundu, ya kijivu, au ya kijani. Jiwe hilo lilitumiwa kwenye mavazi ya pekee ya kuhani mkuu.—Kut 28:9, 12; 1Nya 29:2; Ayu 28:16.

 • Shubiri.

  Ni kipimo cha urefu ambacho kwa wastani kinaanzia kwenye ncha ya kidole gumba hadi ncha ya kidole kidogo, kiganja kikiwa kimepanuliwa. Kwa msingi wa kipimo cha mkono cha sentimita 44.5 (inchi 17.5), shubiri ina urefu wa sentimita 22.2 (inchi 8.75). (Kut 28:16; 1Sa 17:4)—Angalia Nyongeza B14.

 • Si safi.

  Usemi huo unaweza kumaanisha kuwa mchafu kimwili au kuvunja sheria za maadili. Hata hivyo, katika Biblia mara nyingi neno hilo linamaanisha kitu kisichokubalika, au kisicho safi, kulingana na Sheria ya Musa. (Law 5:2; 13:45; Mt 10:1; Mdo 10:14; Efe 5:5)—Tazama SAFI.

 • Siku ya Hukumu.

  Siku hususa, au kipindi hususa, wakati ambapo vikundi fulani, mataifa, au wanadamu kwa ujumla watawajibika mbele za Mungu. Huenda wakati huo wale watakaohukumiwa kuwa wanastahili kifo watauawa, au huenda hukumu hiyo ikawapa baadhi ya watu nafasi ya kuokolewa na kupata uzima wa milele. Yesu Kristo na mitume wake walirejelea “Siku ya Hukumu” inayokuja itakayowahusisha si watu walio hai tu bali pia waliokufa zamani.—Mt 12:36.

 • Siku ya Kufunika Dhambi.

  Siku takatifu iliyo muhimu zaidi kwa Waisraeli, inaitwa pia Yom Kippur (maneno hayo yanatokana na neno la Kiebrania yohm hak·kip·pu·rimʹ, “siku ya kufunika”), inayofanywa tarehe 10 ya mwezi wa Ethanimu. Ndiyo siku pekee ya mwaka ambayo kuhani mkuu aliingia Patakatifu Zaidi katika hema la ibada. Humo alitoa damu ya dhabihu kwa ajili ya dhambi zake, dhambi za Walawi wengine, na dhambi za watu wote. Ulikuwa wakati wa kusanyiko takatifu na kufunga, na pia ilikuwa siku ya sabato, wakati ambapo watu hawakupaswa kufanya kazi za kawaida.—Law 23:27, 28.

 • Siku ya Matayarisho.

  Jina la siku iliyotangulia Sabato, ambayo ilitumiwa na Wayahudi kufanya matayarisho muhimu. Siku hiyo ilifikia mwisho jua lilipotua siku ambayo leo inaitwa Ijumaa, kisha siku ya Sabato ilianza. Kulingana na Wayahudi, siku ilianza jioni na kufikia mwisho jioni iliyofuata.—Mk 15:42; Lu 23:54.

 • Siku za mwisho.

  Maneno haya na mengine yanayofanana nayo, kama vile “kipindi cha mwisho cha zile siku,” yanatumiwa katika unabii wa Biblia kurejelea wakati ambapo matukio ya kihistoria yatafikia kilele chake. (Eze 38:16; Da 10:14; Mdo 2:17) Ikitegemea unabii unaohusika, huenda kikawa kipindi cha miaka michache tu au mingi. Biblia hasa hutumia maneno hayo kurejelea “siku za mwisho” za mfumo huu wa mambo, wakati wa kuwapo kwa Yesu kusikoonekana.—2Ti 3:1; Yak 5:3; 2Pe 3:3.

 • Silaha.

  Vifaa vya kujilinda vilivyovaliwa na wanajeshi, yaani, kofia, koti la vita, mshipi, vyuma vya kukinga miundi ya miguu, na ngao.—1Sa 31:9; Efe 6:13-17.

 • Sinagogi.

  Neno linalomaanisha “kukusanya pamoja; kusanyiko,” lakini katika maandiko mengi, linarejelea jengo au mahali ambapo Wayahudi walikusanyika kwa ajili ya usomaji wa Maandiko, mafundisho, mahubiri, na sala. Katika siku za Yesu, kila mji mkubwa wa Israeli ulikuwa na sinagogi, na majiji makubwa zaidi yalikuwa na masinagogi kadhaa.—Lu 4:16; Mdo 13:14, 15.

 • Siri takatifu.

  Sehemu ya kusudi la Mungu ambayo chanzo chake ni Mungu, hubaki ikiwa siri mpaka wakati wa Mungu wa kuifunua ufikapo, naye huwafunulia tu wale anaochagua.—Mk 4:11; Kol 1:26.

 • Siria; Wasiria.

  Tazama ARAMU; WAARAMU.

 • Sirti.

  Ghuba mbili kubwa zenye kina kifupi zilizo kwenye pwani ya Libya, Afrika Kaskazini, zilizoogopwa na mabaharia wa kale kwa sababu zilikuwa na mchanga hatari uliokuwa ukihamishwa-hamishwa na mawimbi. (Mdo 27:17)—Angalia Nyongeza B13.

 • Sivani.

  Jina la mwezi wa tatu katika kalenda takatifu ya Wayahudi baada ya kutoka uhamishoni Babiloni na jina la mwezi wa tisa katika kalenda iliyotumiwa na watu wote. Mwezi huo ulianzia katikati ya mwezi wa Mei mpaka katikati ya mwezi wa Juni. (Est 8:9)—Angalia Nyongeza B15.

 • Suria.

  Mke wa ziada ambaye kwa kawaida alikuwa kijakazi.—Kut 21:8; 2Sa 5:13; 1Fa 11:3.

 • T

 • Takatifu; Utakatifu.

  Sifa asilia ya Yehova; hali ya kuwa na usafi kamili kimaadili na utakato. (Kut 28:36; 1Sa 2:2; Met 9:10; Isa 6:3) Linapotumiwa kuwahusu wanadamu (Kut 19:6; 2Fa 4:9), wanyama (Hes 18:17), vitu (Kut 28:38; 30:25; Law 27:14), mahali (Kut 3:5; Isa 27:13), vipindi vya wakati (Kut 16:23; Law 25:12), na kazi (Kut 36:4), neno la awali la Kiebrania huwasilisha wazo la hali ya kutengwa, upekee, au kutakaswa kwa ajili ya Mungu mtakatifu; hali ya kuwekwa kando kwa ajili ya utumishi wa Yehova. Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, maneno “takatifu” na “utakatifu” huonyesha pia hali ya kuwekwa kando kwa ajili ya Mungu. Maneno hayo hutumiwa pia kurejelea usafi katika mwenendo wa mtu.—Mk 6:20; 2Ko 7:1; 1Pe 1:15, 16.

 • Talanta.

  Kipimo kikubwa zaidi cha uzito kilichotumiwa na Waebrania na pia kilitumiwa kama pesa. Kilikuwa na uzito wa kilogramu 34.2. Talanta ya Wagiriki ilikuwa ndogo zaidi, ilikuwa na uzito wa karibu kilogramu 20.4. (1Nya 22:14; Mt 18:24)—Angalia Nyongeza B14.

 • Tamuzi.

  (1) Jina la mungu aliyeliliwa jijini Yerusalemu na wanawake Waebrania walioasi imani. Inasemekana kwamba mwanzoni Tamuzi alikuwa mfalme ambaye alifanywa kuwa mungu baada ya kifo chake. Katika maandishi ya Wasumeri, Tamuzi anaitwa Dumuzi, naye anatajwa kuwa malkia au mpenzi wa Inanna mungu mke wa uzazi (yaani, Ishtari wa Wababiloni). (Eze 8:14) (2) Jina la mwezi wa nne katika kalenda takatifu ya Wayahudi baada ya kutoka uhamishoni Babiloni na jina la mwezi wa kumi katika kalenda iliyotumiwa na watu wote. Mwezi huo ulianzia katikati ya mwezi wa Juni mpaka katikati ya mwezi wa Julai.—Angalia Nyongeza B15.

 • Tanuru.

  Jiko la kuyeyushia mawe yenye madini au kuyeyushia chuma; hutumiwa pia kuchomea vyombo vya udongo na vyombo vingine vya kauri. Katika nyakati za Biblia, matanuru yalitengenezwa kwa matofali au mawe. Tanuru la kuchomea vyombo vya udongo na vya kauri na chokaa au saruji linaitwa kalibu.—Mwa 15:17; Da 3:17; Ufu 9:2.

 • Tarshishi, meli za.

  Mwanzoni neno Tarshishi lilitumiwa kurejelea meli ambazo zilisafiri kwenda katika eneo la kale la Tarshishi (leo ni Hispania). Inaonekana kwamba hatimaye neno hilo lilirejelea meli kubwa zilizoweza kusafiri mbali. Sulemani na Yehoshafati walitumia meli hizo kufanya biashara.—1Fa 9:26; 10:22; 22:48.

 • Tartaro.

  Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, Tartaro ni hali ya kushushwa hadhi kama ya mfungwa gerezani; malaika walioasi katika siku za Noa walitupwa katika hali hiyo. Kitenzi tar·ta·roʹo (“kutupa ndani ya Tartaro”) kinachotumiwa katika 2 Petro 2:4 hakimaanishi kwamba “malaika waliofanya dhambi” walitupwa ndani ya Tartaro inayotajwa katika hekaya za wapagani (yaani, gereza lililo chini ya ardhi na mahali penye giza pa miungu midogo). Badala yake, kitenzi hicho kinaonyesha kwamba Mungu aliwashusha kutoka mahali pao mbinguni na kutoka katika mapendeleo yao na kuwaweka katika hali ya giza zito sana la kiakili kuhusiana na makusudi maangavu ya Mungu. Hatimaye watawekwa katika giza halisi, ambalo Maandiko yanaonyesha kwamba ni maangamizi ya milele, yatakayowapata wao pamoja na mtawala wao, Shetani Ibilisi. Kwa hiyo, Tartaro inafananisha hali ya kushushwa hadhi kabisa ya malaika hao walioasi. Tartaro ni tofauti na “shimo refu lisilo na mwisho” (abiso) linalotajwa katika Ufunuo 20:1-3.

 • Tarumbeta.

  Ala inayopulizwa ambayo imetengenezwa kwa chuma, nayo hutumiwa kutoa ishara na pia katika muziki. Katika Hesabu 10:2, Yehova alitoa maagizo kwamba tarumbeta mbili za fedha zitengenezwe ili zipigwe kwa miito fulani hususa kwa ajili ya kuwakusanya watu, kuvunja kambi, au kutangaza vita. Inaelekea kwamba tarumbeta hizo hazikuwa zimepinda, tofauti na “ala za pembe” zilizopinda ambazo zilitengenezwa kutokana na pembe za wanyama. Tarumbeta ambazo Biblia haisemi kihususa jinsi zilivyotengenezwa zilikuwa pia miongoni mwa ala za muziki zilizotumiwa hekaluni. Kwa kawaida sauti za tarumbeta huambatana kwa njia ya mfano na matangazo ya hukumu za Yehova au matukio mengine muhimu ambayo chanzo chake ni Mungu.—2Nya 29:26; Ezr 3:10; 1Ko 15:52; Ufu 8:7–11:15.

 • Tauni au ugonjwa hatari.

  Ugonjwa wowote wa kuambukiza unaoenea kwa kasi ambao unaweza kuathiri wengi na kusababisha vifo. Mara nyingi unahusianishwa na kutekelezwa kwa hukumu ya Mungu.—Hes 14:12; Eze 38:22, 23; Am 4:10.

 • Tebethi.

  Jina la mwezi wa kumi katika kalenda takatifu ya Wayahudi baada ya kutoka uhamishoni Babiloni na jina la mwezi wa nne katika kalenda iliyotumiwa na watu wote. Mwezi huo ulianzia katikati ya mwezi wa Desemba mpaka katikati ya mwezi wa Januari. Kwa kawaida mwezi huo unaitwa “mwezi wa kumi.” (Est 2:16)—Angalia Nyongeza B15.

 • Terafimu.

  Miungu ya familia au sanamu, nyakati nyingine ilitumiwa kutafuta ishara za ubashiri. (Eze 21:21) Baadhi ya terafimu zilikuwa na ukubwa na umbo la mwanadamu, na nyingine zilikuwa ndogo. (Mwa 31:34; 1Sa 19:13, 16) Vitu vya kale vilivyopatikana Mesopotamia vinaonyesha kwamba yule aliyekuwa na sanamu za terafimu angepokea urithi wa familia. (Jambo hili linatusaidia kuelewa ni kwa nini Raheli alichukua terafimu za baba yake.) Inaonekana kwamba Waisraeli hawakuwa na desturi hiyo, ingawa hivyo terafimu zilitumiwa katika ibada ya sanamu katika siku za waamuzi na pia wafalme, nazo zilikuwa miongoni mwa vitu vilivyoharibiwa na Mfalme Yosia aliyekuwa mwaminifu.—Amu 17:5; 2Fa 23:24; Ho 3:4.

 • Tia mafuta.

  Neno la Kiebrania ambalo kimsingi linamaanisha “kupaka kitu kilicho majimaji.” Mtu au kitu kilipakwa mafuta ili kuonyesha kwamba kimewekwa wakfu kwa ajili ya utumishi wa pekee. Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, neno hilo linatumiwa pia kuhusiana na kumiminwa kwa roho takatifu juu ya wale waliochaguliwa kwa ajili ya tumaini la kwenda mbinguni.—Kut 28:41; 1Sa 16:13; 2Ko 1:21.

 • Tishri.

  Tazama ETHANIMU na Nyongeza B15.

 • Toba.

  Katika Biblia, neno hili hutumiwa kumaanisha kubadili akili na kujuta kutoka moyoni kwa sababu ya njia ya awali ya maisha, matendo yasiyofaa, au kwa sababu ya mambo ambayo mtu alikosa kufanya. Toba ya kweli huzaa matunda, humfanya mtu abadili mwenendo wake.—Mt 3:8; Mdo 3:19; 2Pe 3:9.

 • Tohara.

  Tendo la kuondoa govi la kiungo cha kiume. Tohara ilifanywa kuwa takwa kwa Abrahamu na wazao wake, lakini si takwa kwa Wakristo. Neno hilo linatumiwa kwa njia ya mfano katika maandiko mbalimbali.—Mwa 17:10; 1Ko 7:19; Flp 3:3.

 • Toleo la kinywaji.

  Toleo la divai lililomiminwa kwenye madhabahu na kutolewa pamoja na nyingi ya zile dhabihu nyingine. Paulo anatumia maneno hayo kwa njia ya mfano kuonyesha utayari wake wa kujitoa kabisa kwa ajili ya Wakristo wenzake.—Hes 15:5, 7; Flp 2:17.

 • Toleo la kutikiswa.

  Katika toleo hili inaonekana kwamba kuhani aliweka mikono yake chini ya mikono ya mwabudu aliyekuwa amebeba dhabihu iliyopaswa kutolewa, kisha kuhani aliitikisa mikono ya mwabudu huyo kwenda mbele na nyuma; au kuhani mwenyewe alilitikisa toleo hilo. Kwa kufanya hivyo ni kana kwamba walikuwa wakimtolea Yehova matoleo ya dhabihu.—Law 7:30.

 • Towashi.

  Kihalisi neno hilo linamaanisha mwanamume aliyehasiwa. Kwa kawaida wanaume hao waliwekwa katika makao ya wafalme ili wawe watumishi au watunzaji wa malkia na masuria. Neno hilo pia linamrejelea mwanamume ambaye kihalisi hakuwa towashi, bali alikuwa ofisa aliyepewa majukumu mbalimbali katika makao ya mfalme. Linatumiwa kwa njia ya mfano kumrejelea ‘towashi kwa ajili ya Ufalme,’ mtu ambaye anajidhibiti ili ajitoe kikamili zaidi katika utumishi wa Mungu.—Mt 19:12; Est 2:15; Mdo 8:27.

 • U

 • Ua.

  Eneo lililokuwa wazi kuzunguka hema la ibada na ambalo lilikuwa na uzio; baadaye ua huo ulirejelea mojawapo ya maeneo yaliyokuwa wazi yenye kuta yaliyozunguka jengo kuu la hekalu. Madhabahu ya dhabihu za kuteketezwa ilikuwa katika ua wa hema la ibada na katika ua wa ndani wa hekalu. (Angalia Nyongeza B5, B8, B11.) Biblia inataja pia nyua inapozungumzia nyumba za watu na majumba ya wafalme.—Kut 8:13; 27:9; 1Fa 7:12; Est 4:11; Mt 26:3.

 • Uadilifu.

  Katika Maandiko, uadilifu ni jambo lililo sawa kulingana na viwango vya Mungu vya mema na mabaya.—Mwa 15:6; Kum 6:25; Met 11:4; Sef 2:3; Mt 6:33.

 • Uajemi; Waajemi.

  Nchi na watu wanaotajwa mara nyingi pamoja na Wamedi, ni wazi kwamba wana uhusiano nao. Katika historia yao ya mapema, Waajemi walimiliki tu eneo lililo upande wa kusini magharibi wa uwanda wa Irani. Chini ya Koreshi Mkuu (ambaye kulingana na wanahistoria fulani wa kale alizaliwa na baba Mwajemi na mama Mmedi), Waajemi walikuwa na mamlaka kuliko Wamedi, ingawa milki hiyo iliendelea kuwa na falme mbili. Koreshi aliishinda Milki ya Babiloni katika mwaka wa 539 K.W.K. naye akawaruhusu Wayahudi waliokuwa utekwani warudi katika nchi yao. Milki ya Uajemi ilianzia kwenye Mto Indus upande wa mashariki mpaka kwenye Bahari ya Aegea upande wa magharibi. Wayahudi walikuwa chini ya utawala wa Waajemi mpaka Aleksanda Mkuu alipowashinda Waajemi katika mwaka wa 331 K.W.K. Danieli aliona mapema Milki ya Uajemi katika maono, nayo inatajwa pia katika vitabu vya Biblia kama vile Ezra, Nehemia, na Esta. (Ezr 1:1; Da 5:28)—Angalia Nyongeza B9.

 • Uasherati.

  Neno hili linatokana na neno la Kigiriki por·neiʹa, ambalo ni neno la ujumla la ngono zote haramu. Linatia ndani uzinzi, ukahaba, ngono kati ya watu ambao hawajafunga ndoa, ngono kati ya watu wa jinsia moja, na kufanya ngono na wanyama. Linatumiwa kwa njia ya mfano katika kitabu cha Ufunuo kueleza jinsi kahaba wa kidini anayeitwa “Babiloni Mkubwa” anavyoshirikiana na watawala wa ulimwengu huu kupata mamlaka na utajiri. (Ufu 14:8; 17:2; 18:3; Mt 5:32; Mdo 15:29; Gal 5:19)—Tazama KAHABA.

 • Uasi imani.

  Katika Kigiriki neno hili (a·po·sta·siʹa) linatokana na kitenzi ambacho kihalisi kinamaanisha “kusimama mbali na.” Nomino hiyo inamaanisha “kuondoka, kuacha, au kuasi.” Katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, neno “uasi imani” hutumiwa hasa kuwarejelea wale ambao wameasi ibada ya kweli.—Met 11:9; Mdo 21:21; 2Th 2:3.

 • Ubani.

  Utomvu uliokaushwa wa miti na vichaka vya jamii fulani ya mimea inayoitwa Boswellia. Ubani huo ulipochomwa, ulitoa harufu nzuri sana. Ulikuwa mojawapo ya viungo vya uvumba mtakatifu uliotumiwa katika hema la ibada na hekaluni. Ulitolewa pia pamoja na matoleo ya nafaka, nao uliwekwa juu ya kila safu ya mikate ya wonyesho ndani ya Patakatifu.—Kut 30:34-36; Law 2:1; 24:7; Mt 2:11.

 • Ubatizo; Batiza.

  Kitenzi “batiza” kinamaanisha “zamisha,” au tumbukiza ndani ya maji. Yesu alifanya ubatizo uwe takwa kwa wafuasi wake. Maandiko yanataja pia ubatizo uliofanywa na Yohana, kubatizwa kwa roho takatifu, kubatizwa kwa moto, na ubatizo mwingineo.—Mt 3:11, 16; 28:19; Yoh 3:23; 1Pe 3:21.

 • Ufalme wa Mungu.

  Maneno hayo yanatumiwa hasa kumaanisha enzi kuu ya Mungu inayowakilishwa na serikali ya kifalme ya Mwana wake, Kristo Yesu.—Mt 12:28; Lu 4:43; 1Ko 15:50.

 • Ufilisti; Wafilisti.

  Nchi iliyo kwenye pwani ya kusini ya Israeli ambayo baadaye iliitwa Ufilisti. Wahamiaji kutoka Krete ambao waliishi katika nchi hiyo waliitwa Wafilisti. Daudi aliwashinda, lakini waliendelea kuwa huru na daima walikuwa maadui wa Israeli. (Kut 13:17; 1Sa 17:4; Am 9:7)—Angalia Nyongeza B4.

 • Ufufuo.

  Kuinuka kutoka katika kifo. Neno la Kigiriki a·naʹsta·sis kihalisi linamaanisha “kuinuka; kusimama.” Biblia ina masimulizi tisa ya ufufuo, kutia ndani simulizi kuhusu Yehova Mungu akimfufua Yesu. Ingawa Eliya, Elisha, Yesu, Petro, na Paulo waliwafufua watu, ni wazi kwamba walifanya miujiza hiyo kwa nguvu za Mungu. Ufufuo wa “waadilifu na wasio waadilifu pia” utakaofanyika duniani ni muhimu katika kutimiza kusudi la Mungu. (Mdo 24:15) Biblia inataja pia ufufuo wa kwenda mbinguni, unaoitwa ufufuo “wa mapema” au “wa kwanza,” ambao ni ufufuo wa ndugu za Yesu waliotiwa mafuta kwa roho.—Flp 3:11; Ufu 20:5, 6; Yoh 5:28, 29; 11:25.

 • Ujitoaji-kimungu.

  Heshima, ibada, na utumishi unaotolewa kwa Yehova Mungu, na ushikamanifu kwa enzi yake kuu ya ulimwengu mzima.—1Ti 4:8; 2Ti 3:12.

 • Ukaldayo; Wakaldayo.

  Awali maneno hayo yalirejelea nchi na watu walioishi katika eneo la mlango bahari wa Mto Tigri na Mto Efrati; baada ya muda maneno hayo yalitumiwa kurejelea eneo lote la Babilonia na watu wake. Neno “Wakaldayo” lilitumiwa pia kuwahusu watu fulani wasomi waliojifunza sayansi, historia, lugha, na elimu ya nyota lakini ambao walizoea pia kufanya uchawi na unajimu.—Ezr 5:12; Da 4:7; Mdo 7:4.

 • Ukoma; Mwenye ukoma.

  Ugonjwa mbaya sana wa ngozi. Ukoma unaotajwa katika Maandiko haulingani sana na ugonjwa unaoitwa ukoma leo, kwa maana zamani ugonjwa huo uliwaathiri wanadamu na pia mavazi na nyumba. Mtu mwenye ugonjwa huo anaitwa mtu mwenye ukoma.—Law 14:54; Lu 5:12.

 • Ulozi.

  Matumizi ya nguvu zinazojulikana kwamba zinatoka kwa roho waovu.—2Nya 33:6.

 • Umalizio wa mfumo wa mambo.

  Kipindi cha wakati kinachotangulia mwisho wa mfumo wa mambo, au hali ya mambo, kipindi ambacho kinaongozwa na Shetani. Kinaenda sambamba na kuwapo kwa Kristo. Chini ya mwongozo wa Yesu, malaika ‘watawatenganisha waovu kutoka kwa waadilifu’ na kuwaangamiza. (Mt 13:40-42, 49) Wanafunzi wa Yesu walitaka kujua wakati ambapo “umalizio” huo ungekuja. (Mt 24:3) Kabla ya kurudi mbinguni, Yesu aliwaahidi wafuasi wake kwamba angekuwa pamoja nao mpaka wakati huo.—Mt 28:20.

 • Unabii.

  Ujumbe ulioongozwa na roho takatifu, iwe ni ufunuo kuhusu mapenzi ya Mungu au tangazo la mapenzi yake. Unabii unaweza kuwa fundisho la maadili lililoongozwa na roho takatifu, amri ya Mungu au hukumu, au tangazo la jambo litakalotokea.—Eze 37:9, 10; Da 9:24; Mt 13:14; 2Pe 1:20, 21.

 • Upatanisho.

  Tazama KUFUNIKA DHAMBI.

 • Upendo mshikamanifu.

  Kwa kawaida usemi huo unatafsiriwa kutokana na neno la Kiebrania cheʹsedh, linalomaanisha upendo unaochochewa na uwajibikaji au ujitoaji, utimilifu, ushikamanifu, na kufungamana kwa dhati. Mara nyingi usemi huo unatumiwa kurejelea upendo wa Mungu kwa wanadamu, lakini pia wanadamu wanaweza kuwa na upendo huo kati yao.—Kut 34:6; Ru 3:10.

 • Urimu na Thumimu.

  Ni vitu vilivyotumiwa na kuhani mkuu kama kura ili kujua mapenzi ya Mungu maswali muhimu ya kitaifa yalipohitaji majibu kutoka kwa Yehova. Urimu na Thumimu viliwekwa ndani ya kifuko cha kifuani cha kuhani mkuu alipoingia katika hema la ibada. Inaonekana kwamba vitu hivyo havikutumiwa tena Wababiloni walipoharibu Yerusalemu.—Kut 28:30; Ne 7:65.

 • Ushahidi.

  Kwa kawaida “Ushahidi” ni zile Amri Kumi zilizoandikwa kwenye mabamba mawili ya mawe ambayo Musa alipewa.—Kut 31:18.

 • Ushuru.

  Malipo ambayo Taifa au mtawala alimpa mwingine ikiwa ishara ya ujitiisho, ili kudumisha amani au kupata ulinzi. (2Fa 3:4; 18:14-16; 2Nya 17:11) Neno hilo pia linatumiwa kumaanisha kodi ambayo mtu mmoja mmoja alitozwa.—Ne 5:4; Ro 13:7.

 • Utangulizi.

  Maneno yanayopatikana mwanzoni mwa zaburi ambayo yanamtambulisha mwandishi, yanaeleza habari za ziada kuhusu zaburi hiyo, yanatoa maagizo ya kimuziki, au yanaonyesha wakati zaburi hiyo ilipoimbwa au kusudi lake.—Angalia utangulizi wa Zaburi 3, 4, 5, 6, 7, 30, 38, 60, 92, 102.

 • Utete wa kupimia.

  Utete wa kupimia ulikuwa na urefu wa mikono sita. Kulingana na kipimo cha kawaida cha mkono, utete huo ulikuwa na urefu wa mita 2.67 (futi 8.75); kulingana na kipimo cha mkono mrefu, ulikuwa na urefu wa mita 3.11 (futi 10.2). (Eze 40:3, 5; Ufu 11:1)—Angalia Nyongeza B14.

 • Utete.

  Neno linalotumiwa kurejelea mimea mingi ambayo kwa kawaida inakua katika sehemu zenye umajimaji. Mmea unaoitwa utete katika Maandiko mengi ni Arundo donax. (Ayu 8:11; Isa 42:3; Mt 27:29; Ufu 11:1)—Tazama UTETE WA KUPIMIA.

 • Utumishi mtakatifu.

  Huduma, au kazi, iliyo takatifu, ambayo inahusiana moja kwa moja na ibada ambayo mtu anamtolea Mungu.—Ro 12:1; Ufu 7:15.

 • Uvumba.

  Mchanganyiko wa utomvu wa aina mbalimbali wenye harufu nzuri na zeri unaoungua polepole na kutokeza harufu yenye manukato. Uvumba wa pekee wenye viungo vinne ulitengenezwa ili utumiwe katika hema la ibada na hekaluni. Ulifukizwa asubuhi na usiku kwenye madhabahu ya uvumba ndani ya Patakatifu, na katika Siku ya Kufunika Dhambi, ulifukiziwa ndani ya Patakatifu Zaidi. Ulifananisha sala zinazokubalika za watumishi waaminifu wa Mungu. Wakristo hawakuwa chini ya takwa la kutumia uvumba.—Kut 30:34, 35; Law 16:13; Ufu 5:8.

 • Uzinzi.

  Ni ngono inayofanywa kwa hiari kati ya mwanamume aliyeoa na mwanamke ambaye si mke wake au kati ya mwanamke aliyeolewa na mwanamume ambaye si mume wake.—Kut 20:14; Mt 5:27; 19:9.

 • V

 • Vyetezo.

  Vifaa vilivyotengenezwa kwa dhahabu, fedha, au shaba, ambavyo vilitumiwa katika hema la ibada na hekalu kufukizia uvumba na kuondolea makaa ya mawe kwenye madhabahu ya dhabihu na tambi zilizoungua za taa kutoka katika vinara vya taa vya dhahabu.—Kut 37:23; 2Nya 26:19; Ebr 9:4.

 • W

 • Waamuzi.

  Wanaume waliowekwa na Yehova ili kuwaokoa watu wake kabla ya kipindi cha wanadamu waliotawala wakiwa wafalme wa Israeli.—Amu 2:16.

 • Wafuasi wa chama cha Herode.

  Tazama HERODE; WAFUASI WA CHAMA CHA.

 • Wakfu, ishara takatifu ya.

  Bamba linalong’aa la dhahabu safi lililochongwa maneno haya ya Kiebrania, “Utakatifu ni wa Yehova.” Liliwekwa upande wa mbele wa kilemba cha kuhani mkuu. (Kut 39:30)—Angalia Nyongeza B5.

 • Wakili Mkuu.

  Katika Kigiriki, kimsingi neno hili linamaanisha “Kiongozi Mkuu.” Linaonyesha jukumu muhimu la Yesu Kristo la kuwaweka huru wanadamu waaminifu kutoka katika madhara yanayoangamiza ya dhambi na kuwaongoza kwenye uzima wa milele.—Mdo 3:15; 5:31; Ebr 2:10; 12:2.

 • Walinzi wa Mfalme.

  Kikundi cha wanajeshi Waroma kilichoanzishwa ili kumlinda maliki wa Roma. Kikundi hicho kilikuja kuwa na ushawishi mkubwa sana wa kisiasa katika kumuunga mkono au kumwondoa maliki.—Flp 1:13.

 • Wamedi; Umedi.

  Wazao wa Madai, mwana wa Yafethi; waliishi katika eneo lenye milima la uwanda wa Irani ambalo lilikuja kuwa nchi ya Umedi. Wamedi walijiunga na Wababiloni ili kuwashinda Waashuru. Wakati huo, nchi ya Uajemi ilikuwa mkoa wa Umedi, lakini Koreshi aliasi na nchi ya Umedi ikaungana na Uajemi zikatokeza Milki ya Umedi na Uajemi ambayo ilishinda Milki mpya ya Babiloni katika mwaka wa 539 K.W.K. Wamedi walikuwa Yerusalemu katika siku ya Pentekoste ya mwaka wa 33 W.K. (Da 5:28, 31; Mdo 2:9)—Angalia Nyongeza B9.

 • Wana wa Haruni.

  Wazao wa Haruni, mjukuu wa Lawi; Haruni alichaguliwa kuwa kuhani mkuu wa kwanza chini ya Sheria ya Musa. Wana wa Haruni walitekeleza majukumu ya kikuhani katika hema la ibada na hekaluni.—1Nya 23:28.

 • Wanafalsafa Waepikurea.

  Wafuasi wa mwanafalsafa Mgiriki aliyeitwa Epicurus (341-270 K.W.K.). Falsafa yao ilitegemea wazo la kwamba lengo kuu maishani mwa mtu ni kupata raha.—Mdo 17:18.

 • Wanafalsafa Wastoa.

  Jamii ya wanafalsafa Wagiriki walioamini kwamba furaha inahusisha kuishi kulingana na mambo ya asili na kutumia akili. Kulingana na maoni yao, mtu aliyekuwa na hekima ya kweli, alipuuza maumivu na furaha.—Mdo 17:18.

 • Wanefili.

  Wana wakatili waliozaliwa baada ya malaika waliojivika miili ya kibinadamu kufanya ngono na mabinti wa wanadamu kabla ya Gharika.—Mwa 6:4.

 • Wanethini.

  Watumishi au wahudumu wa hekaluni ambao hawakuwa Waisraeli. Kihalisi neno la Kiebrania linamaanisha “Waliotolewa,” kuonyesha kwamba walikuwa wametolewa kwa ajili ya utumishi wa hekaluni. Inaelekea kwamba Wanethini wengi walikuwa wazao wa Wagibeoni, ambao Yoshua alikuwa amewafanya kuwa “wakusanyaji wa kuni na watekaji wa maji kwa ajili ya Waisraeli na kwa ajili ya madhabahu ya Yehova.”—Yos 9:23, 27; 1Nya 9:2; Ezr 8:17.

 • Wasamaria.

  Mwanzoni neno hili lilirejelea Waisraeli wa ufalme wa kaskazini wa makabila kumi, lakini baada ya nchi ya Samaria kushindwa na Waashuru katika mwaka wa 740 K.W.K., neno hilo lilitia ndani wageni walioletwa na Waashuru. Katika siku za Yesu, neno hilo halikuhusianishwa na jamii fulani au siasa, badala yake, kwa kawaida lilimaanisha wafuasi wa madhehebu ya kidini ambayo yalikuwa karibu na jiji la kale la Shekemu na Samaria. Wafuasi wa madhehebu hayo walifuata mafundisho fulani yaliyokuwa tofauti sana na ya dini ya Kiyahudi.—Yoh 8:48.

 • Wimbo wa maombolezo.

  Wimbo wa maneno au wa ala, wenye hisia za huzuni kubwa, kama huzuni inayoonyeshwa na mtu aliyefiwa na rafiki yake au na mpendwa wake; wimbo wa majonzi.—2Sa 1:17; Zb 7:Utangulizi.

 • Wimbo wa Safari za Kupanda.

  Maneno ya utangulizi ya Zaburi 120-134. Ingawa watu wana maoni mbalimbali kuhusu maana ya maneno hayo, wengi wanaamini kwamba zaburi hizo 15 ziliimbwa na waabudu Waisraeli wenye shangwe walipokuwa ‘wakipanda’ kwenda Yerusalemu, jiji lililokuwa juu katika milima ya Yuda, ili kuhudhuria sherehe tatu kuu za kila mwaka.

 • Y

 • Yakobo.

  Mwana wa Isaka na Rebeka. Baadaye Mungu alimpa jina Israeli, naye akawa mzee wa ukoo wa watu wa Israeli (ambao pia waliitwa Waisraeli na baadaye, Wayahudi). Alikuwa baba ya wana 12 ambao, pamoja na wazao wao, walifanyiza makabila 12 ya taifa la Israeli. Jina Yakobo liliendelea kutumiwa kurejelea taifa la Israeli au watu wa Israeli.—Mwa 32:28; Mt 22:32.

 • Yeduthuni.

  Maana ya neno hili linalopatikana katika utangulizi wa Zaburi 39, 62, na 77 haijulikani vizuri. Inaonekana kwamba utangulizi huo ni maagizo ya kuimba zaburi hizo, labda yanatambulisha mtindo au ala ya muziki. Kulikuwa na mwanamuziki Mlawi aliyeitwa Yeduthuni, kwa hiyo huenda mtindo wa Yeduthuni au ala ya kuimba kwa mtindo huo ilihusianishwa naye au wanawe.

 • Yehova.

  Kwa kawaida jina hili ni tafsiri ya Kiswahili ya Tetragramatoni (zile herufi nne za Kiebrania za jina la kibinafsi la Mungu), nalo linapatikana zaidi ya mara 7,000 katika tafsiri hii.—Angalia Nyongeza A4 na A5.

 • Yuda.

  Mwana wa nne wa Yakobo aliyezaliwa na mke wake Lea. Katika unabii aliotoa alipokuwa akikaribia kufa, Yakobo alitabiri kwamba mtawala mkuu na wa kudumu angetoka katika ukoo wa Yuda. Akiwa mwanadamu, Yesu alitoka Yuda. Pia, jina Yuda linarejelea kabila hilo na baadaye lilirejelea ufalme ulioitwa kwa jina hilo. Ufalme wa Yuda unatajwa pia kuwa ufalme wa kusini, na ulifanyizwa na makabila haya ya Israeli, yaani, kabila la Yuda na la Benjamini, na pia makuhani na Walawi. Kabila la Yuda liliishi upande wa kusini wa nchi iliyotia ndani Yerusalemu na hekalu.—Mwa 29:35; 49:10; 1Fa 4:20; Ebr 7:14.

 • Z

 • Zaburi.

  Wimbo wa kumsifu Mungu. Zaburi zilitungwa kama muziki na kuimbwa na waabudu, kama wakati ambapo watu walimwabudu Yehova Mungu katika hekalu lake kule Yerusalemu.—Lu 20:42; Mdo 13:33; Yak 5:13.

 • Zawadi za rehema.

  Zawadi zilizotolewa ili kumsaidia mtu mwenye uhitaji. Zawadi hizo hazitajwi moja kwa moja katika Maandiko ya Kiebrania, lakini Sheria iliwapa Waisraeli maagizo hususa kuhusu wajibu wao wa kuwasaidia maskini.—Mt 6:2.

 • Zeu.

  Mungu mkuu wa Wagiriki walioabudu miungu mingi. Kule Listra, Barnaba aliitwa kimakosa Zeu. Maandishi ya kale yaliyochongwa yaliyopatikana karibu na Listra yanataja “makuhani wa Zeu” na “mungu-jua Zeu.” Meli alimosafiria Paulo kutoka katika kisiwa cha Malta ilikuwa na sanamu ya “Wana wa Zeu,” juu upande wa mbele, yaani, ndugu mapacha Castor na Pollux.—Mdo 14:12; 28:11.

 • Zivu.

  Jina la awali la mwezi wa pili katika kalenda takatifu ya Wayahudi na jina la mwezi wa nane katika kalenda iliyotumiwa na watu wote. Mwezi huo ulianzia katikati ya mwezi wa Aprili mpaka katikati ya mwezi wa Mei. Unaitwa Iyari katika Talmudi ya Wayahudi na pia katika maandishi mengine baada ya Wayahudi kutoka uhamishoni Babiloni. (1Fa 6:37)—Angalia Nyongeza B15.

 • Ziwa la moto.

  Mahali pa mfano ‘panapowaka moto na kiberiti,’ panafafanuliwa pia kuwa “kifo cha pili.” Watenda dhambi wasiotubu, Ibilisi, na hata kifo na Kaburi (au, Hadesi) vinatupwa humo. Kwa kuwa kiumbe wa roho na pia kifo na Hadesi, vitu ambavyo haviwezi kuathiriwa na moto, vinatajwa kuwa vinatupwa humo, hilo linaonyesha kwamba ziwa hili ni mfano, si mfano wa mateso ya milele, bali ni mfano wa maangamizi ya milele.—Ufu 19:20; 20:14, 15; 21:8.

 •