Ayubu 30:1-31

  • Ayubu aeleza jinsi maisha yake yalivyobadilika (1-31)

    • Adhihakiwa na watu wasiofaa kitu (1-15)

    • Yaonekana ni kama Mungu hamsaidii (20, 21)

    • “Ngozi yangu imekuwa nyeusi” (30)

30  “Sasa wananicheka+—Wanaume wenye umri mdogo kuliko mimi,Ambao baba zao ningekataaKuwaweka pamoja na mbwa waliolinda kondoo wangu.  2  Nguvu za mikono yao zilikuwa na faida gani kwangu? Nguvu zao zimekwisha.  3  Wamedhoofika kwa sababu ya umaskini na njaa;Wanaguguna ardhi iliyokaukaAmbayo ilikuwa tayari imeharibiwa na kuachwa ukiwa.  4  Wanakusanya mmea wenye chumvi kutoka vichakani;Chakula chao ni mizizi ya miretemu.  5  Wanafukuzwa kutoka katika jamii;+Watu wanawapigia kelele kama wanavyompigia kelele mwizi.  6  Wanaishi kwenye miteremko ya mabonde,*Kwenye mashimo ardhini na katika miamba.  7  Wanalia kwa sauti kutoka vichakaniNa kujikunyata pamoja katikati ya upupu.  8  Kama wana wa watu wapumbavu na wasio na jina,Wamefukuzwa* kutoka nchini.  9  Lakini sasa wananidhihaki hata katika nyimbo zao;+Nimekuwa kitu cha kudharauliwa nao.*+ 10  Wananichukia na kukaa mbali nami;+Hawasiti kunitemea mate usoni.+ 11  Kwa sababu Mungu amenidhoofisha* na kuninyenyekeza,Wanafanya watakavyo* mbele zangu. 12  Wanainuka upande wangu wa kulia kama umati;WananikimbizaNa kuweka vizuizi vya maangamizi kwenye njia yangu. 13  Wanaharibu barabara zanguNa kuzidisha msiba wangu,+Na hakuna yeyote anayewazuia.* 14  Wanakuja kana kwamba wanapita kwenye ufa mpana ukutani;Wanamiminika ndani katikati ya magofu. 15  Hofu inanilemea;Heshima yangu inapeperushwa mbali kama upepo,Na wokovu wangu unatoweka kama wingu. 16  Sasa uhai wangu unatoweka taratibu;+Siku za mateso+ zinashikamana nami. 17  Maumivu yanatoboa mifupa yangu* usiku;+Na maumivu yanayonitafuna hayaishi kamwe.+ 18  Kwa nguvu nyingi vazi langu limechakazwa;*Hunikaba kama ukosi wa vazi langu. 19  Mungu ameniangusha chini kwenye matope;Nimebaki mavumbi na majivu tu. 20  Ninakulilia unisaidie, lakini hunijibu;+Ninasimama, lakini unaniangalia tu. 21  Umenigeukia kwa ukatili;+Kwa nguvu zote za mkono wako, unanishambulia. 22  Unaniinua juu na kunipeperusha katika upepo;Kisha unanitupa huku na huku katika dhoruba.* 23  Kwa maana ninajua kwamba utanishusha katika kifo,Katika nyumba ambamo watu wote walio hai watakutana. 24  Lakini hakuna yeyote anayeweza kumshambulia mtu anayetaabika*+Anapolilia msaada wakati wa msiba. 25  Je, sijawalilia wale ambao wamekabili nyakati ngumu?* Je, sijawahuzunikia maskini?+ 26  Ingawa nilitumaini mema, mabaya yalikuja;Nilitarajia nuru, lakini giza likaja. 27  Msukosuko uliokuwa ndani yangu haukukoma;Siku za mateso zilinikabili. 28  Ninatembeatembea kwa huzuni;+ hakuna mwangaza wa jua. Ninasimama na kulilia msaada katika kusanyiko. 29  Nimekuwa ndugu ya mbwamwituNa rafiki ya mabinti wa mbuni.+ 30  Ngozi yangu imekuwa nyeusi na imebambuka;+Mifupa yangu inaungua kwa sababu ya joto.* 31  Kinubi changu kinatumika kwa ajili ya maombolezo tu,Na zumari* yangu kwa ajili ya sauti ya kilio.

Maelezo ya Chini

^ Au “makorongo.”
^ Tnn., “Wamepigwa mijeledi na kufukuzwa.”
^ Tnn., “methali; msemo kwao.”
^ Tnn., “amelegeza kamba ya upinde wangu.”
^ Tnn., “Wanatupilia mbali lijamu.”
^ Au labda, “Na hakuna yeyote anayewasaidia.”
^ Tnn., “Mifupa yangu inatobolewa.”
^ Au labda, “Mateso yangu makali yanauharibu mwili wangu.”
^ Au labda, “unaniyeyusha kwa kishindo.”
^ Tnn., “kushambulia rundo la magofu.”
^ Au “walio na siku ngumu?”
^ Au labda, “homa.”
^ Au “filimbi.”