Ayubu 24:1-25

  • Ayubu aendelea kujibu (1-25)

    • ‘Kwa nini Mungu haweki wakati wa hukumu?’ (1)

    • Asema kwamba Mungu ameruhusu uovu (12)

    • Watenda dhambi wanapenda giza (13-17)

24  “Kwa nini Mweza-Yote haweki wakati wa hukumu?+ Kwa nini wale wanaomjua hawaioni siku yake?*  2  Watu husogeza alama za mipaka;+Wanaiba mifugo kwa ajili ya malisho yao.  3  Huwachukua punda wa mayatimaNa kumchukua ng’ombe dume wa mjane kuwa dhamana ya mkopo.*+  4  Huwasukuma maskini waondoke barabarani;Watu wasio na uwezo duniani hulazimika kujificha kwa sababu yao.+  5  Maskini hutafuta chakula kama punda mwitu+ nyikani;Huwatafutia watoto wao chakula jangwani.  6  Wanalazimika kuvuna shamba la mtu mwingine*Na kuokota masalio katika shamba la mizabibu la mwovu.  7  Wanalala uchi usiku, bila nguo;+Hawana cha kujifunika ili wasipigwe na baridi.  8  Wanaloweshwa na mvua za milimani;Wanashikilia miamba kwa nguvu kwa sababu hawana mahali pa kujificha.  9  Mtoto asiye na baba hunyakuliwa kutoka kwenye matiti ya mama yake;+Na mavazi ya maskini huchukuliwa kuwa dhamana ya mkopo,+ 10  Na kuwalazimisha kutembea uchi, bila nguo,Wakiwa na njaa, huku wakibeba masuke ya nafaka. 11  Hufanya kazi ngumu kwenye matuta yaliyo milimani katika joto la mchana;*Hukanyaga mashinikizo ya divai, lakini wanaona kiu.+ 12  Wanaokufa wanaendelea kulia kwa uchungu jijini;Waliojeruhiwa vibaya sana hulilia msaada,+Lakini Mungu haoni jambo hilo kuwa baya.* 13  Kuna wale wanaoasi nuru;+Hawatambui njia zake,Nao hawafuati vijia vyake. 14  Muuaji huamka wakati wa mapambazuko;Huwaua wasio na uwezo na maskini,+Naye huiba wakati wa usiku. 15  Macho ya mzinzi husubiri giza linapoingia,+Akisema, ‘Hakuna atakayeniona!’+ Naye huufunika uso wake. 16  Wakati wa giza wanavunja nyumba;Wakati wa mchana wanajifungia ndani. Wanaepuka nuru.+ 17  Kwa maana kwao, asubuhi ni kama giza zito;Wamezoea vitisho vya giza zito. 18  Lakini wanabebwa upesi na maji.* Fungu lao la ardhi litalaaniwa.+ Hawatarudi kwenye mashamba yao ya mizabibu. 19  Kama theluji iliyoyeyuka inavyokaushwa na ukame na joto,Ndivyo Kaburi* linavyowachukua waliotenda dhambi!+ 20  Mama yake atamsahau;* naye ataliwa na mabuu. Hatakumbukwa tena.+ Na uovu utakatwa kama mti. 21  Humwinda mwanamke tasa,Na kumtesa mjane. 22  Mungu atatumia nguvu zake kuwaangamiza wenye nguvu;Hata wakiinuka, hawana uhakika wa kuishi. 23  Mungu anawaacha wawe na uhakika na wajihisi salama,+Lakini macho yake yanatazama kila jambo wanalotenda.*+ 24  Wanakwezwa kwa muda mfupi, kisha wanatoweka.+ Wanashushwa chini+ na kukusanywa kama watu wengine wote;Wanakatwa kama masuke ya nafaka. 25  Sasa ni nani anayeweza kuthibitisha kwamba mimi ni mwongoAu kupinga neno langu?”

Maelezo ya Chini

^ Yaani, siku yake ya hukumu.
^ Au “rehani.”
^ Au labda, “kuvuna chakula cha mifugo shambani.”
^ Au labda, “Hukamua mafuta katikati ya kuta za matuta.”
^ Au labda, “Mungu hamhukumu yeyote kwa kutenda mabaya.”
^ Tnn., “Yeye ni mwepesi juu ya maji.”
^ Au “Sheoli.” Angalia Kamusi.
^ Tnn., “Tumbo la uzazi litamsahau.”
^ Tnn., “njia zao.”