Ayubu 4:1-21

  • Elifazi azungumza kwa mara ya kwanza (1-21)

    • Adhihaki utimilifu wa Ayubu (7, 8)

    • Asimulia ujumbe kutoka kwa kiumbe wa roho (12-17)

    • ‘Mungu hana imani na watumishi wake’ (18)

4  Kisha Elifazi+ Mtemani akajibu:   “Mtu akijaribu kuongea nawe, je, utakosa subira? Kwa maana ni nani anayeweza kujizuia kuongea?   Ni kweli, umewarekebisha wengi,Nawe ulikuwa ukiimarisha mikono iliyo dhaifu.   Maneno yako yalimwinua yeyote aliyejikwaa,Nawe uliwatia nguvu waliokuwa na magoti dhaifu.   Lakini sasa yamekupata wewe, nawe unalemewa;* Yanakugusa, nawe unashuka moyo.   Je, hofu yako kwa Mungu haikupi ujasiri? Je, njia yako ya utimilifu+ haikupi tumaini?   Kumbuka, tafadhali: Ni mtu gani asiye na hatia ambaye amewahi kuangamia? Tangu lini wanyoofu wakaangamizwa?   Jambo ambalo nimeona ni kwamba wale wanaolima* madharaNa wale wanaopanda taabu watavuna mambo hayohayo.   Kwa pumzi ya Mungu wanaangamia,Na kwa mlipuko wa hasira yake wanafikia mwisho wao. 10  Simba hunguruma, na mwanasimba hurindima,Lakini hata meno ya simba wenye nguvu* huvunjwa. 11  Simba hufa kwa kukosa mawindo,Na wanasimba hutawanyika. 12  Sasa niliambiwa neno kwa siri,Na sikio langu lilisikia mnong’ono wake. 13  Katika maono ya usiku yenye kufadhaisha,Watu wanapolala usingizi mzito, 14  Nilitetemeka kwelikweli,Mifupa yangu yote ikajaa hofu. 15  Roho fulani alipita mbele ya uso wangu;Nywele za mwili wangu zikasimama. 16  Kisha akasimama tuli,Lakini sikutambua sura yake. Umbo fulani lilikuwa mbele ya macho yangu;Kulikuwa na utulivu, kisha nikasikia sauti: 17  ‘Je, mwanadamu anayeweza kufa anaweza kuwa mwadilifu kuliko Mungu? Je, mtu anaweza kuwa safi kuliko Muumba wake?’ 18  Tazama! Hana imani na watumishi wake,Naye huona kwamba malaika* wake wana kasoro. 19  Sembuse wale wanaokaa katika nyumba za udongo,Ambao msingi wao umo mavumbini,+Wanaopondwa kwa urahisi kama nondo!* 20  Wanapondwa kabisa kuanzia asubuhi mpaka jioni;Wanaangamia milele, na hakuna yeyote anayetambua hilo. 21  Je, wao si kama hema ambalo kamba yake imeng’olewa? Wanakufa bila hekima.

Maelezo ya Chini

Tnn., “nawe unachoka.”
Au “wanaotunga.”
Au “wanasimba wenye manyoya marefu shingoni.”
Au “wajumbe.”
Aina fulani ya wadudu waharibifu.