Ayubu 19:1-29

  • Jibu la Ayubu (1-29)

    • Akataa kukemewa na “rafiki” zake (1-6)

    • Asema kwamba ameachwa (13-19)

    • “Mkombozi wangu yuko hai” (25)

19  Ayubu akajibu:  2  “Mtaendelea kunikasirisha* mpaka lini,+Na kuniponda kwa maneno?+  3  Mmenikemea* mara kumi sasa;Mnanitesa bila aibu.+  4  Na ikiwa kwa kweli nilifanya kosa,Ni kosa langu mimi mwenyewe.  5  Ikiwa mnasisitiza kujikweza juu yangu,Mkidai kwamba mna haki ya kunishutumu,  6  Basi, jueni kwamba Mungu ndiye amenipotosha,Naye ameninasa katika wavu wake wa kuwindia.  7  Tazameni! Naendelea kulia kwa sauti, ‘Ukatili!’ lakini sijibiwi;+Naendelea kulilia msaada, lakini hakuna haki.+  8  Ameziba kijia changu kwa ukuta wa mawe, siwezi kupita;Amezifunika njia zangu kwa giza.+  9  Amenivua utukufu wanguNa kunivua taji kichwani. 10  Hunibomoa kila upande na kuniangamiza;Anang’oa tumaini langu kama mti. 11  Hasira yake huwaka dhidi yangu,Naye huniona kuwa adui yake.+ 12  Majeshi yake hukusanyika na kunizingira,Nayo hupiga kambi kuzunguka hema langu. 13  Ndugu zangu wenyewe amewafukuza mbali nami,Na wale wanaonijua wamegeuka na kuniacha.+ 14  Rafiki zangu wa karibu* wametoweka,Na wale niliowajua vema wamenisahau.+ 15  Wageni walio nyumbani mwangu+ na vijakazi wangu wananiona kuwa mgeni;Mimi ni mgeni machoni pao. 16  Ninamwita mtumishi wangu, lakini hajibu;Namsihi kwa kinywa changu anihurumie. 17  Pumzi yangu mwenyewe inamchukiza mke wangu,+Nami ni uvundo kwa ndugu* zangu wenyewe. 18  Hata watoto wachanga wananidharau;Ninaposimama, wanaanza kunifanyia mzaha. 19  Rafiki zangu wote wa karibu wananichukia,+Na wale niliowapenda wamenigeuka.+ 20  Mifupa yangu inashikamana na ngozi yangu na mwili wangu,+Nami ninaponyoka kwa ngozi ya meno yangu. 21  Nionyesheni rehema, rafiki zangu, nionyesheni rehema,Kwa maana mkono wa Mungu mwenyewe umenigusa.+ 22  Kwa nini mnaendelea kunitesa kama Mungu anavyonitesa,+Mkinishambulia bila kuacha?*+ 23  Laiti maneno yangu yangeandikwa,Laiti yangeandikwa katika kitabu! 24  Laiti yangechongwa milele kwenye mwamba,Kwa kalamu ya chuma na risasi! 25  Kwa maana najua vizuri kwamba mkombozi wangu+ yuko hai;Atakuja baadaye na kuinuka juu ya dunia.* 26  Baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi,Nikiwa bado hai, nitamwona Mungu, 27  Ambaye mimi mwenyewe nitamwona,Ambaye macho yangu mwenyewe yatamwona, si ya mwingine.+ Lakini ndani kabisa ninahisi nimelemewa!* 28  Kwa maana mnauliza, ‘Tunamtesa kwa njia gani?’+ Kwa maana mimi ndiye mzizi wa tatizo hili. 29  Ninyi wenyewe ogopeni upanga,+Kwa kuwa upanga huwaadhibu wakosaji;Mnapaswa kujua kwamba kuna mwamuzi.”+

Maelezo ya Chini

^ Au “kuikasirisha nafsi yangu.” Angalia Kamusi.
^ Au “Mmenitukana.”
^ Au “Watu wangu wa ukoo.”
^ Tnn., “wana wa tumbo langu la uzazi,” yaani, tumbo lililonibeba (tumbo la mama yangu).
^ Tnn., “Na hamtosheki na mwili wangu?”
^ Tnn., “juu ya (kwenye) mavumbi.”
^ Au “Figo zangu zimeacha kufanya kazi.”