Hesabu 23:1-30

  • Maneno ya kwanza ya kishairi ya Balaamu (1-12)

  • Maneno ya pili ya kishairi ya Balaamu (13-30)

23  Kisha Balaamu akamwambia Balaki: “Jenga madhabahu saba mahali hapa,+ nawe unitayarishie ng’ombe dume saba na kondoo dume saba.” 2  Mara moja Balaki akafanya kama Balaamu alivyomwambia. Kisha Balaki na Balaamu wakatoa dhabihu ya ng’ombe dume mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.+ 3  Halafu Balaamu akamwambia Balaki: “Kaa hapa karibu na dhabihu yako ya kuteketezwa, nami nitaenda. Labda Yehova atawasiliana nami. Jambo lolote atakalonifunulia, nitakwambia.” Basi akaenda juu ya kilima kilicho wazi. 4  Ndipo Mungu akawasiliana na Balaamu,+ Balaamu akamwambia: “Nilijenga safu za madhabahu saba na kutoa dhabihu ya ng’ombe dume mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.” 5  Yehova akatia maneno haya katika kinywa cha Balaamu:+ “Rudi kwa Balaki, na hili ndilo utakalosema.” 6  Basi akarudi na kumkuta Balaki na wakuu wote wa Moabu wakiwa wamesimama karibu na dhabihu yake ya kuteketezwa. 7  Kisha akasema maneno haya ya kishairi:+ “Balaki mfalme wa Moabu amenileta kutoka Aramu,+Kutoka katika milima ya mashariki: ‘Njoo umlaani Yakobo kwa niaba yangu. Naam, njoo uwashutumu Waisraeli.’+  8  Ninawezaje kuwalaani watu ambao Mungu hajawalaani? Ninawezaje kuwashutumu wale ambao Yehova hajawashutumu?+  9  Kutoka juu ya miamba ninawaona,Na kutoka vilimani ninawatazama. Wanaishi peke yao kama taifa;+Hawajioni kuwa sawa na mataifa mengine.+ 10  Ni nani anayeweza kuhesabu chembe za mavumbi ya Yakobo+Au hata kuhesabu robo ya Waisraeli? Acha nife kifo cha watu wanyoofu,Na mwisho wangu uwe kama wao.” 11  Ndipo Balaki akamwambia Balaamu: “Kwa nini umenitendea hivi? Nilikuleta ili uwalaani maadui wangu, lakini badala yake umewabariki tu.”+ 12  Balaamu akasema: “Je, sipaswi kusema neno lolote ambalo Yehova anatia kinywani mwangu?”+ 13  Balaki akamwambia: “Tafadhali, twende mahali pengine ambapo unaweza kuwaona. Utaona baadhi yao; hutawaona wote. Ukiwa huko walaani kwa niaba yangu.”+ 14  Kwa hiyo akampeleka kwenye uwanja wa Sofimu, juu ya Pisga,+ naye akajenga madhabahu saba na kutoa dhabihu ya ng’ombe dume mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.+ 15  Kisha Balaamu akamwambia Balaki: “Kaa hapa karibu na dhabihu yako ya kuteketezwa ninapoenda pale kuwasiliana Naye.” 16  Basi Yehova akawasiliana na Balaamu na kutia neno hili kinywani mwake:+ “Rudi kwa Balaki, na hili ndilo utakalosema.” 17  Basi akarudi na kumkuta Balaki akisubiri karibu na dhabihu yake ya kuteketezwa, na wakuu wa Moabu walikuwa pamoja naye. Balaki akamuuliza: “Yehova amesema nini?” 18  Kisha Balaamu akasema maneno haya ya kishairi:+ “Inuka, Balaki, usikilize. Nisikilize, ewe mwana wa Sipori. 19  Mungu si mwanadamu anayesema uwongo,+Wala si binadamu anayebadili nia yake.*+ Akisema jambo, je, hatalitenda? Akinena jambo, je, hatalitimiza?+ 20  Tazama! Nimeletwa ili nibariki;Sasa Yeye amebariki,+ nami siwezi kubadili.+ 21  Havumilii nguvu zozote za uchawi dhidi ya Yakobo,Wala haruhusu taabu yoyote impate Israeli. Yehova Mungu wake yuko pamoja nao,+Nao humsifu kwa sauti kubwa kuwa mfalme wao. 22  Mungu anawatoa Misri.+ Yeye ni kama pembe za fahali mwitu.+ 23  Kwa maana hakuna ishara za msiba dhidi ya Yakobo,+Wala hakuna uaguzi* wowote dhidi ya Israeli.+ Sasa inaweza kusemwa hivi kumhusu Yakobo na Israeli: ‘Tazameni mambo ambayo Mungu ametenda!’ 24  Watu hawa watainuka kama simba,Na kama simba, watajiinua.+ Hawatalala chini mpaka wale mawindoNa kunywa damu ya waliouawa.” 25  Ndipo Balaki akamwambia Balaamu: “Ikiwa huwezi kamwe kuwalaani, basi usiwabariki pia.” 26  Balaamu akamwambia Balaki: “Je, sikukwambia, ‘Nitafanya mambo yote ambayo Yehova anasema’?”+ 27  Ndipo Balaki akamwambia Balaamu: “Tafadhali njoo nikupeleke mahali pengine. Labda Mungu wa kweli atakubali uwalaani kwa niaba yangu kutoka mahali hapo.”+ 28  Basi Balaki akampeleka Balaamu juu ya Mlima Peori, unaoelekeana na Yeshimoni.*+ 29  Kisha Balaamu akamwambia Balaki: “Jenga madhabahu saba mahali hapa, nawe unitayarishie ng’ombe dume saba na kondoo dume saba.”+ 30  Kwa hiyo Balaki akafanya kama Balaamu alivyomwambia, naye akatoa dhabihu ya ng’ombe dume mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.

Maelezo ya Chini

^ Au “anayejuta.”
^ Au “ubashiri.”
^ Au labda, “jangwa; nyika.”