Matendo ya Mitume 23:1-35

  • Paulo azungumza mbele ya Sanhedrini (1-10)

  • Bwana amtia nguvu Paulo (11)

  • Njama ya kumuua Paulo (12-22)

  • Paulo apelekwa Kaisaria (23-35)

23  Paulo akaikazia macho Sanhedrini, akasema: “Wanaume, akina ndugu, nimetenda kwa dhamiri safi kabisa+ mbele za Mungu mpaka leo hii.”  Ndipo kuhani mkuu Anania akawaagiza wale waliosimama kando yake wampige kofi mdomoni.  Paulo akamwambia: “Mungu atakupiga wewe, ewe ukuta uliopakwa chokaa. Je, unaketi kunihukumu kulingana na Sheria na wakati uleule unaivunja Sheria hiyo kwa kuamuru nipigwe?”  Wale waliosimama kando wakamuuliza: “Je, unamtukana kuhani mkuu wa Mungu?”  Paulo akasema: “Akina ndugu, sikujua yeye ni kuhani mkuu. Kwa maana imeandikwa, ‘Usiseme vibaya kuhusu mtawala wa watu wako.’”+  Sasa Paulo, akijua kwamba sehemu moja ilikuwa Masadukayo na nyingine Mafarisayo, akasema kwa sauti kubwa katika Sanhedrini: “Wanaume, akina ndugu, mimi ni Farisayo,+ mwana wa Mafarisayo. Ninahukumiwa kwa sababu ya tumaini la ufufuo wa wafu.”  Baada ya kusema hivyo, kukatokea mtengano kati ya Mafarisayo na Masadukayo, na kusanyiko likagawanyika.  Kwa maana Masadukayo husema hakuna ufufuo wala malaika wala roho, lakini Mafarisayo huyakubali* hayo yote.+  Basi kukawa na vurugu, na baadhi ya waandishi wa chama cha Mafarisayo wakasimama na kuanza kubishana kwa ukali, wakisema: “Hatuoni kosa lolote katika mtu huyu, lakini ikiwa roho au malaika alizungumza naye+—.” 10  Basi mzozo ulipozidi kuongezeka, kamanda wa jeshi akaogopa kwamba watamrarua-rarua Paulo, akaamuru wanajeshi washuke wamnyakue kutoka kati yao kisha wamlete kwenye makao ya wanajeshi. 11  Lakini usiku uliofuata Bwana akasimama kando yake na kumwambia: “Jipe moyo!+ Kwa maana kama vile ambavyo umekuwa ukitoa ushahidi kamili kunihusu katika Yerusalemu, ndivyo utakavyotoa ushahidi huko Roma pia.”+ 12  Ilipofika mchana, Wayahudi wakafanya hila na kujifunga kwa kiapo cha laana, wakisema hawatakula wala kunywa mpaka watakapomuua Paulo. 13  Kulikuwa na watu zaidi ya 40 waliofanya hila hiyo iliyofungwa kwa kiapo. 14  Watu hao wakaenda kwa wakuu wa makuhani na wazee na kusema: “Tumejifunga kabisa kwa laana* kwamba hatutakula chochote mpaka tutakapomuua Paulo. 15  Basi ninyi pamoja na Sanhedrini mwambieni kamanda wa jeshi amshushe kwenu kana kwamba mnataka kuchunguza zaidi kesi yake. Lakini kabla hajafika, tutakuwa tayari kumuua.” 16  Hata hivyo, mwana wa dada ya Paulo akasikia kuhusu mpango wao wa kumvizia, akaingia kwenye makao ya wanajeshi na kumjulisha Paulo. 17  Kisha Paulo akamwita mmoja wa maofisa wa jeshi na kumwambia: “Mpeleke kijana huyu kwa kamanda wa jeshi, kwa maana ana jambo la kumweleza.” 18  Basi akampeleka kwa kamanda wa jeshi na kusema: “Mfungwa Paulo aliniita na kuniomba nimlete kijana huyu kwako, kwa sababu ana jambo la kukuambia.” 19  Kamanda wa jeshi akamshika mkono akampeleka faraghani na kumuuliza: “Unataka kuniambia nini?” 20  Akasema: “Wayahudi wamekubaliana kukuomba umshushe Paulo kwenye Sanhedrini kesho, kana kwamba wanataka kupata habari zaidi kuhusu kesi yake.+ 21  Lakini usikubali wakushawishi, kwa maana kuna wanaume zaidi ya 40 kati yao walio tayari kumvizia, nao wamejifunga kwa laana* kwamba hawatakula wala kunywa mpaka watakapomuua;+ na sasa wako tayari, wakisubiri ruhusa kutoka kwako.” 22  Basi yule kamanda wa jeshi akamwacha kijana huyo aende baada ya kumwagiza: “Usimwambie mtu yeyote kwamba umenijulisha jambo hili.” 23  Akawaita maofisa wawili wa jeshi na kuwaambia: “Wekeni tayari wanajeshi 200 waende moja kwa moja mpaka Kaisaria, pia wapanda farasi 70 na watu 200 wenye mikuki, saa tatu usiku.⁠ 24  Pia, andaeni farasi kwa ajili ya Paulo ili asafiri salama mpaka kwa gavana Feliksi.” 25  Naye akaandika barua yenye ujumbe huu: 26  “Klaudio Lisia kwa Mtukufu, Gavana Feliksi: Salamu! 27  Mwanamume huyu alikamatwa na Wayahudi nao walikuwa karibu kumuua, lakini nikaja haraka pamoja na wanajeshi wangu na kumwokoa,+ baada ya kujua kwamba ni Mroma.+ 28  Nilitaka kujua kwa nini walikuwa wakimshtaki, basi nikampeleka kwenye Sanhedrini yao.+ 29  Nikatambua kwamba ameshtakiwa kuhusu maswali ya Sheria yao,+ lakini hajashtakiwa kwa jambo lolote linalostahili kifo au kufungwa gerezani. 30  Lakini kwa sababu nimejulishwa njama iliyopangwa dhidi ya mwanamume huyu,+ ninamtuma kwako mara moja, na kuwaamuru wale wanaomshtaki wamshtaki mbele yako.” 31  Basi wale wanajeshi wakamchukua Paulo+ usiku kama walivyoagizwa wakamleta mpaka Antipatri. 32  Siku iliyofuata wakawaruhusu wapanda farasi waende pamoja naye, nao wakarudi kwenye makao ya wanajeshi. 33  Wale wapanda farasi wakaingia Kaisaria, wakamkabidhi gavana ile barua na kumleta Paulo mbele yake. 34  Basi akaisoma na kuuliza ametoka mkoa gani, akajua kwamba alikuwa ametoka Kilikia.+ 35  Akasema: “Nitasikiliza kesi yako kwa makini wale wanaokushtaki watakapofika.”+ Naye akaamuru awekwe chini ya ulinzi katika jumba la kifalme la Herode.

Maelezo ya Chini

Au “huyatangaza hadharani.”
Au “kiapo.”
Au “kiapo.”