Kitabu cha Pili cha Samweli 4:1-12

  • Ish-boshethi auawa (1-8)

  • Daudi aagiza waliomuua Ish-boshethi wauawe (9-12)

4  Ish-boshethi+ mwana wa Sauli aliposikia kwamba Abneri amekufa huko Hebroni,+ alipoteza ujasiri* na Waisraeli wote wakashikwa na wasiwasi.  Kulikuwa na wanaume wawili waliosimamia makundi ya wavamizi ya mwana wa Sauli: mmoja wao aliitwa Baana na mwingine aliitwa Rekabu. Walikuwa wana wa Rimoni Mbeerothi, wa kabila la Benjamini. (Kwa maana awali Beerothi+ pia lilihesabiwa kuwa sehemu ya Benjamini.  Wabeerothi walikimbilia Gitaimu,+ nao wamekuwa wakaaji wageni katika eneo hilo mpaka leo.)  Sasa Yonathani+ mwana wa Sauli alikuwa na mwana aliyelemaa miguu.*+ Alikuwa na umri wa miaka mitano wakati habari kuhusu Sauli na Yonathani zilipofika kutoka Yezreeli,+ mlezi wake akambeba na kukimbia, lakini alipokuwa akikimbia kwa woga, mwana huyo alianguka na kulemaa. Mwana huyo aliitwa Mefiboshethi.+  Rekabu na Baana, wana wa Rimoni Mbeerothi, walienda nyumbani kwa Ish-boshethi mchana wakati wa jua kali, alipokuwa akipumzika adhuhuri.  Wakaingia nyumbani mwake kana kwamba wamekuja kuchukua ngano, wakampiga tumboni; kisha Rekabu na Baana+ ndugu yake wakakimbia.  Walipoingia nyumbani, alikuwa amelala kitandani mwake katika chumba chake cha kulala, wakampiga na kumuua, kisha wakamkata kichwa. Halafu wakakichukua na kutembea usiku kucha kwenye barabara inayoenda Araba.  Wakamletea Daudi kichwa cha Ish-boshethi+ huko Hebroni na kumwambia mfalme: “Ndicho hiki kichwa cha Ish-boshethi mwana wa Sauli adui yako+ aliyetaka kukuua.+ Leo hii Yehova amekulipizia kisasi bwana wangu mfalme dhidi ya Sauli na wazao wake.”  Hata hivyo, Daudi akamjibu hivi Rekabu na Baana ndugu yake, wana wa Rimoni Mbeerothi: “Kwa hakika kama Yehova anavyoishi, aliyeniokoa* kutoka katika taabu zote,+ 10  mtu fulani aliponiambia, ‘Sauli amekufa,’+ akifikiri ananiletea habari njema, nilimkamata na kumuua+ kule Siklagi. Hayo ndiyo malipo ya mjumbe aliyopokea kutoka kwangu! 11  Itakuwaje wakati wanaume waovu wamemuua mtu mwadilifu nyumbani mwake mwenyewe akiwa katika kitanda chake? Kwa nini nisidai damu yake kutoka mikononi mwenu+ na kuwaangamiza kutoka duniani?” 12  Kisha Daudi akawaamuru vijana wake wawaue.+ Wakawakata mikono na miguu yao na kuwatundika+ kando ya kidimbwi kilicho Hebroni. Lakini wakachukua kichwa cha Ish-boshethi na kukizika katika kaburi la Abneri huko Hebroni.

Maelezo ya Chini

Tnn., “mikono yake ikalegea.”
Au “kiwete.”
Au “aliyeikomboa nafsi yangu.”