Kitabu cha Pili cha Samweli 19:1-43

19  Yoabu akaletewa habari hii: “Mfalme analia na kumwombolezea Absalomu.”+  Basi siku hiyo ushindi* uligeuka na kuwa maombolezo kwa watu wote, kwa sababu walisikia kwamba mfalme alikuwa akimwombolezea mwana wake.  Siku hiyo watu wakarudi jijini kimyakimya+ wakiona aibu kama watu waliokimbia kutoka vitani.  Mfalme aliufunika uso wake na kuendelea kulia kwa sauti kubwa: “Mwanangu Absalomu! Absalomu mwanangu, mwanangu!”+  Kisha Yoabu akaingia nyumbani kwa mfalme na kumwambia: “Leo umewaaibisha watumishi wako wote ambao siku ya leo waliokoa uhai wako,* uhai wa* wana wako,+ mabinti wako,+ wake zako, na masuria wako.+  Unawapenda wale wanaokuchukia na kuwachukia wale wanaokupenda, kwa maana leo umeonyesha wazi kwamba wakuu wako na watumishi wako hawana maana kwako, kwa sababu nina hakika kwamba ikiwa Absalomu angekuwa hai leo na sisi sote tuwe tumekufa, ingekuwa sawa kwako.  Sasa inuka, toka nje ukawatie moyo* watumishi wako, kwa sababu naapa kwa jina la Yehova kwamba usipotoka nje, hakuna mtu atakayebaki pamoja nawe usiku wa leo. Hili litakuwa jambo baya zaidi kwako kuliko madhara yote yaliyokupata tangu ulipokuwa kijana mpaka sasa.”  Basi mfalme akainuka na kwenda kuketi kwenye lango la jiji, na watu wote wakaambiwa hivi: “Sasa mfalme ameketi langoni.” Kisha watu wote wakaja mbele ya mfalme. Lakini Waisraeli walikuwa wamekimbia, kila mmoja kwenda nyumbani kwake.+  Watu wote katika makabila yote ya Israeli walikuwa wakibishana, wakisema: “Mfalme alituokoa kutoka mikononi mwa maadui wetu,+ naye alituokoa kutoka mikononi mwa Wafilisti; lakini sasa ameikimbia nchi kwa sababu ya Absalomu.+ 10  Na Absalomu, tuliyemtia mafuta ili atutawale,+ amekufa vitani.+ Basi sasa, kwa nini hamfanyi lolote kumrudisha mfalme?” 11  Mfalme Daudi akatuma ujumbe huu kwa Sadoki+ na Abiathari+ waliokuwa makuhani: “Waambieni wazee wa Yuda,+ ‘Kwa nini muwe wa mwisho kunirudisha mimi mfalme nyumbani kwangu, wakati ujumbe wa Waisraeli wote umenifikia nyumbani kwangu? 12  Ninyi ni ndugu zangu; ninyi ni mfupa wangu na nyama yangu.* Kwa nini muwe wa mwisho kunirudisha mimi mfalme?’ 13  Nanyi mnapaswa kumwambia Amasa,+ ‘Je, wewe si mfupa wangu na nyama yangu? Basi Mungu na aniadhibu, tena vikali, ikiwa hutakuwa mkuu wa jeshi langu kuanzia sasa na kuendelea badala ya Yoabu.’”+ 14  Kwa hiyo aliiteka* mioyo ya watu wote wa Yuda wakawa kama mtu mmoja, wakamtumia mfalme ujumbe huu: “Rudi, wewe na watumishi wako wote.” 15  Mfalme akaanza safari ya kurudi, akafika Yordani, na watu wa Yuda wakaja Gilgali+ ili kumpokea mfalme na kumsindikiza kuvuka Yordani. 16  Ndipo Shimei+ mwana wa Gera, Mbenjamini kutoka Bahurimu, akashuka haraka pamoja na watu wa Yuda ili kumpokea Mfalme Daudi, 17  naye alikuwa na wanaume 1,000 kutoka Benjamini. Pia Siba,+ mtumishi wa nyumba ya Sauli, pamoja na wanawe 15 na watumishi wake 20 wakashuka haraka kwenye Mto Yordani kabla mfalme hajafika. 18  Naye akavuka* kivuko ili kuivusha nyumba ya mfalme na kufanya lolote alilotaka. Lakini Shimei mwana wa Gera akaanguka mbele ya mfalme kifudifudi mfalme alipokuwa karibu kuvuka Mto Yordani. 19  Akamwambia mfalme: “Bwana wangu usinione kuwa na hatia, nawe usikumbuke kosa ambalo mimi mtumishi wako nilifanya+ siku ambayo bwana wangu mfalme ulitoka Yerusalemu. Mfalme, usiweke jambo hilo moyoni mwako, 20  kwa sababu mimi mtumishi wako najua vizuri kwamba nimetenda dhambi; kwa hiyo leo mimi ndiye wa kwanza kutoka katika nyumba yote ya Yosefu kushuka hapa kuja kukupokea bwana wangu mfalme.” 21  Papo hapo Abishai+ mwana wa Seruya+ akasema: “Je, Shimei hapaswi kuuawa kwa sababu hii, kwa kuwa alimtukana mtiwa-mafuta wa Yehova?”+ 22  Lakini Daudi akasema: “Jambo hili linawahusuje, ninyi wana wa Seruya,+ kwamba mtende kinyume cha matakwa yangu? Je, mtu yeyote anapaswa kuuawa leo katika Israeli? Je, sijui kwamba leo mimi ndiye mfalme wa Israeli?” 23  Kisha mfalme akamwambia Shimei: “Hutakufa.” Naye mfalme akamwapia.+ 24  Mefiboshethi,+ mjukuu wa Sauli, akashuka pia kuja kumpokea mfalme. Hakuwa ameosha miguu wala kukata kucha zake wala hakuwa amenyoa masharubu yake wala kufua mavazi yake tangu siku ambayo mfalme aliondoka mpaka siku aliyorudi kwa amani. 25  Alipofika* Yerusalemu kumpokea mfalme, mfalme alimuuliza: “Mefiboshethi, kwa nini hukwenda pamoja nami?” 26  Akamjibu: “Bwana wangu mfalme, mtumishi wangu+ alinidanganya. Kwa maana mimi mtumishi wako nilikuwa nimesema, ‘Acha niweke matandiko juu ya punda wangu ili nipande juu yake na kwenda pamoja na mfalme,’ kwa maana mimi mtumishi wako ni kilema.+ 27  Lakini alinichongea kwako bwana wangu mfalme.+ Hata hivyo, wewe bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu wa kweli, basi fanya jambo lolote unaloona ni jema kwako. 28  Kwa maana wewe bwana wangu mfalme ungeiangamiza nyumba yote ya baba yangu, lakini uliniruhusu mimi mtumishi wako niwe miongoni mwa wale wanaokula mezani pako.+ Basi nina haki gani ya kuendelea kumlilia mfalme?” 29  Hata hivyo, mfalme akamwambia: “Kwa nini unaendelea kusema hivyo? Nimeamua kwamba wewe na Siba mgawane lile shamba.”+ 30  Ndipo Mefiboshethi akamwambia mfalme: “Acha achukue shamba lote, kwa sababu sasa bwana wangu mfalme umerudi kwa amani nyumbani kwako.” 31  Kisha Barzilai+ Mgileadi akashuka kutoka Rogelimu mpaka Yordani ili amsindikize mfalme hadi Yordani. 32  Barzilai alikuwa mzee sana, mwenye umri wa miaka 80, naye alimpa mfalme chakula alipokuwa akikaa Mahanaimu,+ kwa maana alikuwa tajiri sana. 33  Basi mfalme akamwambia Barzilai: “Vuka pamoja nami, nami nitakuandalia chakula huko Yerusalemu.”+ 34  Lakini Barzilai akamwambia mfalme: “Ni siku ngapi* zilizobaki za maisha yangu hivi kwamba niende nawe mfalme mpaka Yerusalemu? 35  Leo nina umri wa miaka 80.+ Je, ninaweza kutofautisha kati ya jema na baya? Je, mimi mtumishi wako ninaweza kuonja ladha ya kile ninachokula na kile ninachokunywa? Je, bado ninaweza kusikia sauti za waimbaji wa kiume na wa kike?+ Basi kwa nini mimi mtumishi wako nikuongezee mzigo bwana wangu mfalme? 36  Mimi mtumishi wako nimeridhika kukuleta wewe mfalme mpaka Yordani. Kwa nini, mfalme, unilipe thawabu hii? 37  Tafadhali, niruhusu mimi mtumishi wako nirudi, na acha nife katika jiji letu karibu na kaburi la baba yangu na mama yangu.+ Lakini mtumishi wako Kimhamu ndiye huyu.+ Acha avuke pamoja nawe bwana wangu mfalme, nawe umtendee unaloona ni jema.” 38  Basi mfalme akasema: “Kimhamu atavuka pamoja nami, nami nitamtendea ninaloona ni jema; nitakutendea wewe jambo lolote utakaloniomba.” 39  Sasa watu wote wakaanza kuvuka Yordani, na mfalme alipovuka alimbusu Barzilai+ na kumbariki; kisha Barzilai akarudi nyumbani. 40  Mfalme alipovuka kwenda Gilgali,+ Kimhamu alivuka pamoja naye. Watu wote wa Yuda na nusu ya watu wa Israeli wakamvusha mfalme.+ 41  Kisha wanaume wote wa Israeli wakaja kwa mfalme na kumuuliza: “Kwa nini ndugu zetu watu wa Yuda walikuiba na kukuleta wewe mfalme na nyumba yako ng’ambo ya Yordani, pamoja na wanaume wako wote?”+ 42  Wanaume wote wa Yuda wakawajibu hivi wanaume wa Israeli: “Kwa sababu mfalme ni mtu wa jamaa yetu.+ Kwa nini jambo hili linawakasirisha? Je, tumekula chochote ambacho kimemgharimu mfalme, au je, tumepewa zawadi?” 43  Hata hivyo, wanaume wa Israeli wakawajibu hivi wanaume wa Yuda: “Tuna makabila kumi na kwa hiyo tuna haki zaidi kumhusu Mfalme Daudi kuliko ninyi. Kwa nini, basi, mmetutendea kwa dharau? Je, hatukupaswa kuwa wa kwanza kumrudisha mfalme wetu?” Lakini maneno ya wanaume wa Yuda yalikuwa makali zaidi kuliko maneno ya wanaume wa Israeli.

Maelezo ya Chini

Au “wokovu.”
Au “nafsi yako.”
Au “nafsi ya.”
Tnn., “ukazungumze na moyo wa.”
Tnn., “nina uhusiano wa damu nanyi.”
Tnn., “aliikunja.”
Au labda, “Nao wakavuka.”
Au labda, “Alipotoka.”
Tnn., “Ni siku ngapi za miaka.”