Kitabu cha Pili cha Samweli 14:1-33

  • Yoabu na mwanamke Mtekoa (1-17)

  • Daudi agundua njama ya Yoabu (18-20)

  • Absalomu aruhusiwa kurudi (21-33)

14  Sasa Yoabu mwana wa Seruya+ akatambua kwamba moyo wa mfalme ulitamani kumwona Absalomu.+  Kwa hiyo Yoabu akatuma watu huko Tekoa+ wamlete mwanamke mwerevu, akamwambia hivi: “Tafadhali, jifanye kana kwamba unaomboleza, nawe uvae nguo za kuomboleza, na usijipake mafuta.+ Jifanye kama mwanamke ambaye amekuwa akiomboleza kwa siku nyingi kwa sababu ya kufiwa.  Kisha uende kwa mfalme na kumwambia hivi.” Basi Yoabu akamwambia mambo ya kusema.*  Mwanamke huyo Mtekoa akaenda kwa mfalme, akaanguka chini kifudifudi, akainama na kusema: “Ee mfalme, nisaidie!”  Mfalme akamuuliza: “Kuna shida gani?” Mwanamke huyo akasema: “Mimi ni mjane; mume wangu amekufa.  Nami, mtumishi wako, nilikuwa na wana wawili, nao wakapigana walipokuwa shambani. Hapakuwa na mtu wa kuwatenganisha, mwana mmoja akampiga mwenzake na kumuua.  Sasa watu wote wa familia wako dhidi yangu, mimi mtumishi wako, nao wanasema, ‘Mtoe yule aliyemuua ndugu yake, ili tumuue kwa sababu ya uhai wa* ndugu yake ambaye alimuua,+ hata kama tutamwangamiza mrithi wake!’ Watakuwa wamezima kaa langu la mwisho linalowaka,* na mume wangu hatakuwa na jina wala mzao* duniani.”  Ndipo mfalme akamwambia mwanamke huyo: “Nenda nyumbani kwako, nami nitatoa agizo kukuhusu.”  Mwanamke huyo Mtekoa akamwambia mfalme: “Ee bwana wangu mfalme, hatia na iwe juu yangu na juu ya nyumba ya baba yangu, lakini wewe mfalme na kiti chako cha ufalme hakina hatia.” 10  Mfalme akamwambia: “Mtu yeyote akizungumza nawe tena, mlete kwangu, naye hatakusumbua tena kamwe.” 11  Lakini mwanamke huyo akasema: “Tafadhali mfalme, mkumbuke Yehova Mungu wako, ili mtu anayelipiza kisasi cha damu+ asilete maangamizi zaidi kwa kumuua mwanangu.” Mfalme akasema: “Kwa hakika kama Yehova anavyoishi,+ hakuna hata unywele mmoja wa mwana wako utakaoanguka chini.” 12  Ndipo mwanamke huyo akasema: “Tafadhali, niruhusu mimi mtumishi wako, nikwambie neno moja, bwana wangu mfalme.” Basi mfalme akasema: “Niambie!” 13  Mwanamke huyo akasema: “Kwa nini, basi, umefikiria kuwatendea watu wa Mungu jambo kama hilo?+ Mfalme akisema jambo kama hilo, anajitia katika hatia, kwa sababu mfalme hamrudishi mwana wake aliyefukuzwa.+ 14  Hakika tutakufa na kuwa kama maji yanayomwagwa chini, ambayo hayawezi kuzolewa. Lakini Mungu haondoi uhai,* naye hufikiria sababu za kumrudisha yule aliyefukuzwa. 15  Nimekuja kukwambia jambo hili bwana wangu mfalme kwa sababu watu walinitia woga. Basi mimi mtumishi wako nikasema, ‘Tafadhali, niruhusu nizungumze na mfalme. Huenda mfalme atatimiza ombi langu, mimi mtumwa wake. 16  Huenda mfalme akasikiliza na kuniokoa mimi mtumwa wake kutoka mikononi mwa mtu anayetaka kuniangamiza mimi na mwanangu wa pekee kutoka kwa urithi ambao Mungu alitupatia.’+ 17  Kisha mimi mtumishi wako nikasema, ‘Acha neno la bwana wangu mfalme linitulize,’ kwa maana bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu wa kweli katika kutofautisha jambo lililo jema na lililo baya. Yehova Mungu wako awe pamoja nawe.” 18  Basi mfalme akamwambia mwanamke huyo: “Tafadhali, usinifiche jambo lolote nitakalokuuliza.” Mwanamke huyo akamwambia: “Tafadhali, sema bwana wangu mfalme.” 19  Basi mfalme akamuuliza: “Je, Yoabu ndiye aliyekuambia ufanye hivi?”+ Mwanamke huyo akajibu: “Kwa hakika kama unavyoishi, Ee bwana wangu mfalme, ni kama tu ulivyosema bwana wangu mfalme, kwa kuwa Yoabu mtumishi wako ndiye aliyeniagiza mimi mtumishi wako na kuniambia niseme maneno hayo yote.* 20  Mtumishi wako Yoabu amefanya hivyo ili mambo yaonekane tofauti, lakini wewe bwana wangu una hekima kama ya malaika wa Mungu wa kweli na unajua mambo yote yanayotendeka nchini.” 21  Basi mfalme akamwambia Yoabu: “Sawa, nitafanya jambo hilo.+ Nenda ukamlete kijana Absalomu.”+ 22  Ndipo Yoabu akaanguka chini kifudifudi, akainama na kumsifu mfalme. Yoabu akasema: “Leo mimi mtumishi wako ninajua kwamba nimepata kibali machoni pako, Ee bwana wangu mfalme, kwa maana wewe mfalme umetimiza ombi langu, mimi mtumishi wako.” 23  Kisha Yoabu akaondoka kwenda Geshuri+ na kumleta Absalomu Yerusalemu. 24  Hata hivyo, mfalme akasema: “Acha arudi nyumbani kwake, lakini hatauona uso wangu.” Basi Absalomu akarudi nyumbani kwake, naye hakuuona uso wa mfalme. 25  Sasa katika Israeli yote, hakuna mwanamume yeyote aliyesifiwa kwa sura yake nzuri kama Absalomu. Hakuwa na kasoro yoyote, kuanzia wayo wa mguu mpaka utosi wa kichwa chake. 26  Aliponyoa kichwa chake—kwa maana alikinyoa mwishoni mwa kila mwaka kwa sababu nywele zake zilikuwa nzito sana—nywele hizo zilikuwa na uzito wa shekeli 200* kulingana na mizani ya kifalme.* 27  Absalomu alizaa wana watatu+ na binti mmoja ambaye aliitwa Tamari. Alikuwa mwanamke mrembo sana. 28  Absalomu akaendelea kuishi Yerusalemu kwa miaka miwili kamili, lakini hakuuona uso wa mfalme.+ 29  Basi Absalomu akamwita Yoabu ili amtume kwa mfalme, lakini Yoabu akakataa kuja. Kisha akatuma mtu amwite kwa mara ya pili, lakini bado akakataa kuja. 30  Mwishowe akawaambia watumishi wake: “Shamba la Yoabu liko kando ya shamba langu, nalo lina shayiri. Nendeni mkalichome moto.” Basi watumishi wa Absalomu wakalichoma moto shamba hilo. 31  Yoabu akaenda nyumbani kwa Absalomu na kumuuliza: “Kwa nini watumishi wako walilichoma moto shamba langu?” 32  Absalomu akamjibu Yoabu: “Tazama! nilikutumia ujumbe huu, ‘Njoo nikutume kwa mfalme, umuulize: “Kwa nini niliondoka Geshuri?+ Afadhali ningekaa huko. Sasa acha nikauone uso wa mfalme, na ikiwa nina hatia, basi aniue.”’” 33  Kwa hiyo Yoabu akaenda kwa mfalme na kumwambia. Kisha akamwita Absalomu, naye akaja kwa mfalme na kuanguka chini kifudifudi, mbele ya mfalme. Kisha mfalme akambusu Absalomu.+

Maelezo ya Chini

Tnn., “akayatia maneno hayo kinywani mwake.”
Au “nafsi ya.”
Yaani, tumaini la mwisho la kupata wazao.
Tnn., “baki.”
Au “nafsi.”
Tnn., “kutia maneno hayo yote katika kinywa changu.”
Karibu kilogramu 2.3. Angalia Nyongeza B14.
Huenda ilikuwa mizani yenye kipimo hususa iliyotumiwa katika jumba la mfalme au shekeli ya “kifalme” iliyokuwa tofauti na shekeli ya kawaida.