Yona 1:1-17

  • Yona ajaribu kumkimbia Yehova (1-3)

  • Yehova aleta dhoruba kali (4-6)

  • Yona ndiye chanzo cha taabu (7-13)

  • Yona atupwa ndani ya bahari iliyochafuka (14-16)

  • Samaki mkubwa ammeza Yona (17)

1  Neno hili la Yehova lilimjia Yona*+ mwana wa Amitai:  “Inuka, nenda Ninawi+ lile jiji kubwa, ukatangaze hukumu dhidi ya jiji hilo kwa sababu nimeona uovu wao.”  Lakini Yona akainuka na kwenda Tarshishi ili amkimbie Yehova; akashuka kwenda Yopa, akakuta meli inayokwenda Tarshishi. Basi akalipa nauli na kupanda meli ili asafiri nao kwenda Tarshishi, amkimbie Yehova.  Ndipo Yehova akavumisha upepo mkali baharini, dhoruba* kali sana ikatokea baharini hivi kwamba meli ikawa karibu kuvunjika-vunjika.  Mabaharia wakaogopa sana hivi kwamba kila mmoja wao akaanza kumlilia mungu wake amsaidie. Nao wakaanza kutupa baharini vitu vilivyokuwa melini ili kupunguza uzito wa meli.+ Lakini Yona alikuwa ameshuka chini ndani ya meli,* ambamo alikuwa amelala na kushikwa na usingizi mzito.  Nahodha wa meli akamkaribia na kumuuliza: “Kwa nini unalala? Amka, mwombe mungu wako! Huenda Mungu wa kweli atatuhurumia, nasi hatutaangamia.”+  Ndipo mabaharia wakaambiana: “Njooni, tupige kura+ ili tujue chanzo cha taabu hii.” Basi wakapiga kura, na kura zikamwangukia Yona.+  Wakamuuliza: “Tafadhali tuambie, ni nani anayetusababishia taabu hii? Unafanya kazi gani, na unatoka wapi? Unatoka nchi gani, na wewe ni mtu wa kabila gani?”  Akawajibu: “Mimi ni Mwebrania, nami namwogopa* Yehova Mungu wa mbinguni, Aliyeumba bahari na nchi kavu.” 10  Waliposikia hayo, wanaume hao wakazidi kuogopa, wakamuuliza: “Umefanya nini?” (Watu hao wakagundua kwamba alikuwa akimkimbia Yehova, kwa sababu Yona aliwaambia.) 11  Basi wakamuuliza: “Tukufanye nini ili bahari itulie kwa ajili yetu?” Kwa sababu bahari ilizidi kuchafuka. 12  Akawajibu: “Nibebeni mnitupe baharini, na bahari itatulia kwa ajili yenu; kwa maana najua kwamba dhoruba hii kali imewapata kwa sababu yangu.” 13  Hata hivyo, wanaume hao wakapiga makasia kwa nguvu* ili kuirudisha meli kwenye nchi kavu, lakini wakashindwa kwa sababu dhoruba ilizidi kuwa kali. 14  Kisha wakamlilia Yehova wakisema: “Jamani, sasa, Ee Yehova, tafadhali, tunakusihi usituangamize kwa sababu ya mtu huyu!* Usituadhibu kwa sababu ya damu isiyo na hatia, kwa kuwa umefanya upendavyo, Ee Yehova!” 15  Basi wakambeba Yona na kumtupa baharini; na bahari ikatulia. 16  Kisha wanaume hao wakamwogopa sana Yehova,+ nao wakamtolea Yehova dhabihu na kumwekea nadhiri. 17  Kisha Yehova akamtuma samaki mkubwa ammeze Yona, basi Yona akakaa ndani ya tumbo la samaki huyo kwa siku tatu, mchana na usiku.+

Maelezo ya Chini

Maana yake “Njiwa.”
Au “tufani.”
Au “chombo chenye sitaha.”
Au “namwabudu.”
Au “wakajitahidi kutafuta njia.”
Au “kwa sababu ya nafsi ya mtu huyu.”