Esta 5:1-14

  • Esta aenda mbele ya mfalme (1-8)

  • Hasira na kiburi cha Hamani (9-14)

5  Siku ya tatu+ Esta akavaa mavazi yake ya kifalme na kusimama katika ua wa ndani wa nyumba ya* mfalme, sehemu iliyotazamana na nyumba ya mfalme, naye mfalme alikuwa ameketi kwenye kiti chake cha ufalme ndani ya nyumba ya mfalme akitazama langoni. 2  Mara tu mfalme alipomwona Malkia Esta akiwa amesimama kwenye ua, akafurahi kumwona, naye mfalme akamnyooshea Esta fimbo yake ya ufalme ya dhahabu+ iliyokuwa mkononi mwake. Basi Esta akakaribia na kuigusa ncha ya fimbo hiyo. 3  Mfalme akamuuliza: “Malkia Esta, kuna nini? Niambie unachotaka. Hata ukiomba nusu ya ufalme wangu utapewa!” 4  Esta akajibu: “Mfalme akipenda na aje leo pamoja na Hamani+ kwenye karamu ambayo nimemwandalia.” 5  Basi Mfalme akawaambia watumishi wake: “Mwambieni Hamani aje haraka, kama Esta anavyoomba.” Basi, mfalme na Hamani wakaenda kwenye karamu ambayo Esta alikuwa ameandaa. 6  Karamu ya divai ilipokuwa ikiendelea, mfalme akamwambia Esta: “Una ombi gani? Utapewa utakachoomba! Na unataka nini? Hata ukiomba nusu ya ufalme wangu, utapewa!”+ 7  Esta akamjibu: “Hili ndilo ombi langu na jambo ninalotaka, 8  Ikiwa nimepata kibali chako Ee mfalme, nawe mfalme ukipenda kutimiza ombi langu na kunipa ninachotaka, naomba mfalme uje pamoja na Hamani kwenye karamu ambayo nitawaandalia kesho; na kesho nitafanya kama unavyosema mfalme.” 9  Siku hiyo Hamani aliondoka akiwa na shangwe na uchangamfu moyoni. Lakini Hamani alipomwona Mordekai katika lango la mfalme na kutambua kwamba hakusimama wala kutetemeka alipomwona, Hamani alimkasirikia sana Mordekai.+ 10  Hata hivyo, Hamani akajizuia na kwenda nyumbani kwake. Kisha akawatuma watu wawaite marafiki zake na pia Zereshi+ mke wake. 11  Hamani akajigamba kuhusu utajiri wake mwingi, wanawe wengi,+ na jinsi mfalme alivyompandisha cheo na kumkweza juu ya wakuu na watumishi wa mfalme.+ 12  Hamani akaendelea kusema: “Isitoshe, Malkia Esta hakumwalika mtu mwingine yeyote isipokuwa mimi nimsindikize mfalme kwenye karamu aliyoandaa.+ Kesho pia amenialika mimi ili niwe naye pamoja na mfalme.+ 13  Lakini mambo hayo yote hayaniridhishi ninapoendelea kumwona Mordekai Myahudi akiwa ameketi kwenye lango la mfalme.” 14  Ndipo Zereshi mke wake na marafiki zake wote wakamwambia: “Agiza mti wenye kimo cha mikono 50* usimamishwe. Kisha asubuhi umwambie mfalme kwamba Mordekai anapaswa kutundikwa juu yake.+ Halafu uende na mfalme kujifurahisha kwenye karamu.” Pendekezo hilo likampendeza Hamani, kwa hiyo akaagiza mti huo usimamishwe.

Maelezo ya Chini

^ Au “jumba la.”
^ Karibu mita 22.3 (futi 73). Angalia Nyongeza B14.