Esta 1:1-22

  • Karamu ya Mfalme Ahasuero kule Shushani (1-9)

  • Malkia Vashti akataa kutii (10-12)

  • Mfalme ashauriana na wanaume wake wenye hekima (13-20)

  • Barua za agizo la mfalme zatumwa (21, 22)

1  Katika siku za Ahasuero,* yaani, Ahasuero aliyetawala mikoa 127*+ kuanzia India mpaka Ethiopia,*  siku hizo Mfalme Ahasuero alipokuwa akiketi kwenye kiti chake cha ufalme katika ngome ya* Shushani,*+  katika mwaka wa tatu wa utawala wake aliwafanyia karamu wakuu na watumishi wake wote. Jeshi la Uajemi+ na Umedi,+ watu mashuhuri, na wakuu wa mikoa* walikuwa mbele yake,  na kwa siku nyingi, siku 180, akawaonyesha utajiri wa ufalme wake wenye utukufu, na pia ukuu, heshima, na fahari yake.  Baada ya siku hizo kwisha, mfalme akawafanyia karamu kwa siku saba watu wote waliokuwa katika ngome ya* Shushani,* wakubwa kwa wadogo, katika bustani ya jumba la mfalme.  Kulikuwa na vitambaa vya kitani, pamba bora, na vitambaa vya bluu vilivyofungwa kwa kamba za kitambaa laini, sufu ya zambarau iliyofungwa kwa pete za fedha, nguzo za marumaru, na makochi ya dhahabu na fedha kwenye sakafu ya mawe mekundu, lulu, na marumaru nyeupe na nyeusi.  Walipewa divai katika vikombe vya* dhahabu; kila kikombe kilikuwa tofauti na vikombe vingine, na divai ya kifalme ilikuwa nyingi sana, kulingana na mali ya mfalme.  Walikunywa kulingana na sheria ya kwamba hakuna mtu aliyelazimishwa,* kwa maana mfalme alikuwa amepanga na maofisa wa jumba la mfalme kwamba kila mtu afanye kama alivyopenda.  Pia, Malkia Vashti+ akawafanyia wanawake karamu katika nyumba ya kifalme ya* Mfalme Ahasuero. 10  Siku ya saba, moyo wa mfalme ulipokuwa umechangamka kwa sababu ya divai, akawaambia Mehumani, Biztha, Harbona,+ Bigtha, Abagtha, Zethari, na Karkasi, maofisa saba wa makao ya mfalme waliokuwa wahudumu wake binafsi, 11  wamlete Malkia Vashti mbele ya mfalme akiwa na taji la* malkia, ili awaonyeshe watu na wakuu urembo wake, kwa maana alikuwa mrembo sana. 12  Lakini Malkia Vashti akaendelea kukataa kuja, hakutii agizo la mfalme alilopewa na maofisa wa makao ya mfalme. Basi mfalme akakasirika sana, na ghadhabu yake ikawaka. 13  Kisha mfalme akazungumza na wanaume wenye hekima waliokuwa na ujuzi kuhusu desturi* (kwa maana hivyo ndivyo habari za mfalme zilivyoletwa kwa wale wote walioifahamu sheria na kesi za kisheria, 14  na watu waliokuwa karibu zaidi na mfalme walikuwa Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena, na Memukani, wakuu saba+ wa Uajemi na Umedi, walioingia kwa mfalme na waliokuwa na vyeo vya juu zaidi katika ufalme). 15  Mfalme akauliza: “Kulingana na sheria, Malkia Vashti anapaswa kutendewaje kwa sababu hajatii agizo la Mfalme Ahasuero aliloambiwa na maofisa wa makao ya mfalme?” 16  Ndipo Memukani akajibu hivi mbele ya mfalme na wakuu: “Malkia Vashti hajamkosea mfalme peke yake,+ bali pia amewakosea wakuu wote na watu wote walio katika mikoa yote ya* Mfalme Ahasuero. 17  Kwa maana jambo alilofanya malkia litajulikana kwa wanawake wote walioolewa, nao watawadharau waume zao wakisema, ‘Mfalme Ahasuero aliamuru Malkia Vashti aletwe mbele yake, lakini akakataa kuja.’ 18  Leo hii mabinti wa wakuu wa Uajemi na Umedi wanaojua jambo alilofanya malkia, watawaambia wakuu wote wa mfalme, na hilo litasababisha dharau na hasira nyingi. 19  Basi mfalme akipenda, na atoe amri ya kifalme itakayoandikwa katika sheria za Uajemi na Umedi, zisizoweza kubadilishwa,+ kwamba Vashti asije tena kamwe mbele ya Mfalme Ahasuero, na mfalme ampe cheo chake cha umalkia mwanamke aliye bora kuliko yeye. 20  Na amri hiyo itakaposikiwa katika milki yake yote kubwa, wanawake wote watawaheshimu waume zao, kuanzia mkubwa mpaka mdogo zaidi.” 21  Pendekezo hilo likamfurahisha mfalme na wakuu, naye mfalme akafanya kama alivyosema Memukani. 22  Basi akatuma barua kwa mikoa yote ya ufalme,*+ kila mkoa* kwa mwandiko wake wenyewe* na kwa kila kikundi cha watu katika lugha yao wenyewe, kwamba kila mume awe bwana mkubwa* wa nyumba yake mwenyewe na azungumze lugha ya watu wake mwenyewe.

Maelezo ya Chini

Inaaminiwa kwamba ni Shasta wa Kwanza, mwana wa Dario Mkuu (Dario Histaspisi).
Au “wilaya 127 za utawala.”
Au “Kushi.”
Au “jumba la mfalme lililokuwa.”
Au “Susa.”
Au “wilaya za utawala.”
Au “jumba la mfalme la.”
Au “Susa.”
Au “vyombo; bilauri za.”
Au “aliyezuiwa.”
Au “jumba la kifalme la.”
Au “kilemba cha.”
Au “taratibu.” Tnn., “nyakati.”
Au “wilaya zote za utawala za.”
Tnn., “wilaya zote za utawala za mfalme.”
Au “wilaya ya utawala.”
Au “mtindo wake wenyewe wa kuandika.”
Au “mkuu.”