Kitabu cha Kwanza cha Samweli 21:1-15

  • Daudi ala mikate ya wonyesho kule Nobu (1-9)

  • Daudi ajifanya mwenda wazimu kule Gathi (10-15)

21  Baadaye Daudi akafika Nobu+ kwa kuhani Ahimeleki. Ahimeleki alianza kutetemeka alipokutana na Daudi, akamuuliza: “Kwa nini uko peke yako na hujaja na mtu yeyote?”+  Daudi akamjibu kuhani Ahimeleki: “Mfalme aliniagiza nifanye jambo fulani, lakini akaniambia, ‘Usimjulishe mtu yeyote kazi niliyokutuma kufanya na maagizo niliyokupa.’ Nilikubaliana na vijana wangu tukutane mahali fulani.  Sasa ikiwa una mikate mitano, nipe tu, au chochote kinachopatikana.”  Lakini kuhani akamwambia Daudi: “Kwa sasa hakuna mikate ya kawaida, lakini kuna mikate mitakatifu+—ninaweza kukupa tu ikiwa vijana wako wamejiepusha na wanawake.”*+  Daudi akamwambia hivi kuhani: “Kwa hakika tumejitenga kabisa na wanawake kama tulivyofanya awali nilipoenda vitani.+ Ikiwa miili ya vijana hawa ni mitakatifu hata katika shughuli za kawaida, je, si mitakatifu zaidi leo?”  Basi kuhani akampa mikate mitakatifu,+ kwa sababu hakukuwa na mikate mingine isipokuwa mikate ya wonyesho iliyokuwa imeondolewa mbele za Yehova na mikate mipya kuwekwa siku hiyo.  Basi mmoja wa watumishi wa Sauli alikuwa hapo siku hiyo, akiwa amezuiliwa mbele za Yehova. Aliitwa Doegi+ Mwedomu,+ mkuu wa wachungaji wa Sauli.  Basi Daudi akamuuliza Ahimeleki: “Je, una mkuki au upanga hapa? Sikubeba upanga wangu wala silaha zangu kwa sababu kazi ya mfalme ilipaswa kufanywa haraka.”  Ndipo kuhani akamwambia: “Nina upanga wa Goliathi+ yule Mfilisti, uliyemuua katika Bonde la* Ela,+ nao umefungwa kwa kitambaa nyuma ya efodi.+ Ikiwa unataka kuuchukua, uchukue, kwa sababu ndio upanga pekee ulio hapa.” Daudi akamwambia: “Hakuna upanga mwingine kama huo. Nipe upanga huo.” 10  Siku hiyo Daudi akaondoka na kuendelea kumkimbia+ Sauli, hatimaye akafika kwa Mfalme Akishi wa Gathi.+ 11  Watumishi wa Akishi wakamuuliza Akishi: “Je, huyu si Daudi mfalme wa ile nchi? Je, si yeye waliyeimba kumhusu walipocheza dansi, wakisema, ‘Sauli ameua maelfu yake,Na Daudi makumi yake ya maelfu’?”+ 12  Daudi akayaweka maneno hayo moyoni mwake, naye akamwogopa sana+ Mfalme Akishi wa Gathi. 13  Kwa hiyo akajifanya hana akili timamu+ mbele yao na kutenda kama mwenda wazimu kati yao.* Alikuwa akitia alama kwenye milango ya lango na kuacha mate yake yatiririke kwenye ndevu zake. 14  Mwishowe Akishi akawaambia watumishi wake: “Hamwoni kwamba mtu huyu ni mwenda wazimu? Kwa nini mmemleta kwangu? 15  Je, nimepungukiwa na wenda wazimu hivi kwamba nahitaji mtu huyu atende kiwazimu mbele yangu? Kwa nini ameingia nyumbani mwangu?”

Maelezo ya Chini

Au “hawajafanya ngono.”
Au “Nchi Tambarare ya Chini ya.”
Tnn., “mikononi mwao.”