Yoshua 2:1-24

  • Yoshua atuma wapelelezi wawili Yeriko (1-3)

  • Rahabu awaficha wapelelezi (4-7)

  • Rahabu apewa ahadi (8-21a)

    • Ishara ya kamba nyekundu (18)

  • Wapelelezi warudi kwa Yoshua (21b-24)

2  Kisha Yoshua mwana wa Nuni akawatuma kwa siri wanaume wawili wapelelezi kutoka Shitimu,+ akawaambia: “Nendeni mkaipeleleze nchi, hasa jiji la Yeriko.” Basi wakaenda na kufika nyumbani kwa mwanamke mmoja kahaba aliyeitwa Rahabu,+ wakakaa humo.  Mfalme wa Yeriko akaambiwa: “Wanaume Waisraeli wameingia humu leo usiku ili kuipeleleza nchi.”  Ndipo mfalme wa Yeriko akawatuma wajumbe kwa Rahabu, akisema: “Watoe nje wanaume waliokuja nyumbani mwako, kwa sababu wamekuja kuipeleleza nchi nzima.”  Lakini mwanamke huyo alikuwa amewaficha wanaume hao wawili. Basi akasema: “Ni kweli, wanaume hao walikuja kwangu, lakini sikujua walikotoka.  Giza lilipoingia, waliondoka kabla ya lango la jiji kufungwa. Sijui walikokwenda, mkiwafuatia haraka, mtawafikia.”  (Lakini alikuwa amewaficha juu ya paa katikati ya majani ya kitani yaliyopangwa paani.)  Basi watu hao wakawafuatia kwenye vivuko vya Yordani,+ na mara tu walipotoka, lango la jiji likafungwa.  Kabla wapelelezi hao hawajalala, Rahabu akaenda kuwaona kwenye paa.  Akawaambia: “Najua kwamba Yehova atawapa nchi hii+ na tumeshikwa na hofu kwa sababu yenu.+ Wakaaji wote wa nchi wamevunjika moyo kwa sababu yenu,+ 10  kwa maana tumesikia jinsi Yehova alivyoyakausha maji ya Bahari Nyekundu* mbele yenu mlipotoka Misri+ na mambo mliyowatendea wale wafalme wawili wa Waamori, yaani, Sihoni+ na Ogu,+ waliokuwa ng’ambo ya* Yordani, mliowaangamiza kabisa. 11  Tuliposikia hayo, tulikufa moyo,* na hakuna yeyote aliye na ujasiri kwa sababu yenu, kwa kuwa Yehova Mungu wenu ni Mungu juu mbinguni na chini duniani.+ 12  Sasa, tafadhalini, niapieni kwa Yehova kwamba, kwa kuwa nimewatendea kwa upendo mshikamanifu, ninyi pia mtaitendea familia ya baba yangu kwa upendo mshikamanifu; nipeni ishara inayoaminika* kwamba mtatimiza ahadi yenu. 13  Nanyi hamtawaangamiza baba yangu na mama yangu, ndugu zangu na dada zangu, na watu wetu wote, mtatuokoa tusife.”*+ 14  Ndipo wanaume hao wakamwambia: “Tutakufa badala yenu!* Ikiwa hamtatoa habari kuhusu mambo yaliyotuleta, tutawatendea kwa upendo mshikamanifu na kwa uaminifu Yehova atakapotupatia nchi hii.” 15  Basi akawashusha kwa kamba kupitia dirishani, kwa kuwa nyumba yake ilikuwa imejengwa kwenye ukuta wa jiji.+ 16  Naye akawaambia: “Nendeni milimani mkajifiche huko kwa siku tatu ili wale wanaowafuatia wasiwapate. Kisha wakirudi mnaweza kwenda zenu.” 17  Wanaume hao wakasema: “Hatutakuwa na hatia kuhusiana na kiapo ulichotuapisha+ 18  isipokuwa, tutakapokuja katika nchi hii, utakuwa umefunga kamba hii nyekundu katika dirisha ambamo utatuteremshia. Wakusanye baba yako, mama yako, ndugu zako, na familia yote ya baba yako ndani ya nyumba hii.+ 19  Ikiwa mtu yeyote atatoka nje ya nyumba yako, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe, nasi hatutakuwa na hatia. Lakini mtu yeyote aliye ndani ya nyumba yako pamoja nawe akifa, damu yake itakuwa juu ya vichwa vyetu. 20  Lakini ukitoa habari kuhusu mambo yaliyotuleta,+ hatutakuwa na hatia kuhusiana na kiapo chako ulichotuapisha.” 21  Naye akasema: “Na iwe kama mlivyosema.” Kwa hiyo akawaruhusu waende zao, nao wakaondoka. Baadaye, akafunga ile kamba nyekundu dirishani. 22  Basi wakaondoka na kuelekea milimani, wakakaa huko kwa siku tatu, mpaka wale waliokuwa wakiwafuatia waliporudi. Waliwatafuta katika kila barabara lakini hawakuwapata. 23  Kisha wapelelezi hao wawili wakaondoka milimani, wakavuka mto na kwenda kwa Yoshua mwana wa Nuni. Wakamsimulia mambo yote yaliyowapata. 24  Halafu wakamwambia hivi Yoshua: “Yehova ametupatia nchi yote.+ Na kwa hakika wakaaji wote wa nchi wamevunjika moyo kwa sababu yetu.”+

Maelezo ya Chini

Au “Bahari ya Shamu.”
Yaani, upande wa mashariki wa.
Tnn., “mioyo yetu iliyeyuka.”
Au “inayotegemeka.”
Au “mtaokoa nafsi zetu.”
Tnn., “Nafsi zetu zitakufa badala ya nafsi zenu!”