Kutoka 37:1-29

  • Kutengeneza sanduku la agano (1-9)

  • Meza (10-16)

  • Kinara cha taa (17-24)

  • Madhabahu ya uvumba (25-29)

37  Kisha Bezaleli+ akatengeneza sanduku la agano+ kwa mbao za mshita. Lilikuwa na urefu wa mikono miwili na nusu* na upana wa mkono mmoja na nusu na kimo cha mkono mmoja na nusu.+  Akalifunika ndani na nje kwa dhahabu safi na kutengeneza ukingo wa dhahabu kulizunguka.+  Kisha akalitengenezea pete nne za dhahabu na kuzifunga sehemu ya juu ya miguu yake minne, pete mbili upande mmoja na pete mbili upande wa pili.  Halafu akatengeneza fito za mshita na kuzifunika kwa dhahabu.+  Akazitia fito hizo kwenye zile pete zilizo pande mbili za Sanduku hilo ili zitumiwe kulibeba.+  Akatengeneza kifuniko cha dhahabu safi.+ Kilikuwa na urefu wa mikono miwili na nusu na upana wa mkono mmoja na nusu.+  Kisha akatengeneza makerubi wawili+ wa dhahabu kwa nyundo kwenye miisho miwili ya kifuniko hicho.+  Kerubi mmoja alikuwa kwenye mwisho mmoja, na yule kerubi mwingine kwenye mwisho wa pili wa kifuniko. Alitengeneza makerubi hao kwenye pande zote mbili za kifuniko.  Makerubi hao walikuwa wamenyoosha mabawa yao kuelekea juu, na hivyo kukifunika kifuniko hicho kwa mabawa yao.+ Walielekeana huku nyuso zao zikitazama kifuniko.+ 10  Kisha akatengeneza meza ya mbao za mshita.+ Ilikuwa na urefu wa mikono miwili, upana wa mkono mmoja, na kimo cha mkono mmoja na nusu.+ 11  Akaifunika kwa dhahabu safi na kutengeneza ukingo wa dhahabu kuizunguka. 12  Kisha akatengeneza utepe wenye upana wa kiganja kimoja* kuizunguka na ukingo wa dhahabu kuzunguka utepe huo. 13  Pia, akaitengenezea pete nne za dhahabu na kuzitia kwenye pembe nne za miguu yake minne. 14  Pete hizo zilikuwa karibu na utepe ili fito za kubebea meza hiyo zitiwe humo. 15  Halafu akatengeneza fito za mshita na kuzifunika kwa dhahabu ili zitumiwe kubebea meza hiyo. 16  Baada ya hayo akatengeneza sahani, vikombe, magudulia, na mabakuli ya meza hiyo kwa dhahabu safi ili yatumiwe kumimina matoleo ya vinywaji.+ 17  Halafu akatengeneza kinara cha taa kwa dhahabu safi.+ Alikitengeneza kinara hicho cha taa kwa nyundo. Sehemu yake ya chini, shina lake, matawi yake, vikombe vyake, matumba yake, na maua yake yalitengenezwa kwa kipande kimoja cha dhahabu.+ 18  Kinara hicho kilikuwa na matawi sita, matawi matatu upande mmoja na matawi matatu upande wa pili. 19  Kila tawi lilikuwa na vikombe vitatu vyenye umbo la maua ya mlozi, na kila kikombe kilikuwa na ua na tumba lake. Hivyo ndivyo matawi hayo sita yalivyotengenezwa kwenye shina la kinara hicho cha taa. 20  Shina la kinara lilikuwa na vikombe vinne vyenye umbo la maua ya mlozi, kila kikombe kilikuwa na ua na tumba lake. 21  Kulikuwa na tumba chini ya jozi ya kwanza ya matawi hayo sita, tumba chini ya jozi ya pili, na tumba chini ya jozi ya tatu. 22  Matumba na matawi yake na kinara chote cha taa kilitengenezwa kwa kipande kimoja cha dhahabu safi, kwa kutumia nyundo. 23  Kisha akatengeneza taa saba+ pamoja na koleo zake na vyetezo vyake kwa dhahabu safi. 24  Alitumia talanta moja* ya dhahabu safi kutengeneza kinara hicho na vifaa vyake vyote. 25  Kisha akatumia mbao za mshita kujenga madhabahu ya kufukizia uvumba.+ Ilikuwa ya mraba, yenye urefu wa mkono mmoja, upana wa mkono mmoja, na kimo cha mikono miwili. Pembe zake zilikuwa sehemu ya hiyo madhabahu.+ 26  Aliifunika kwa dhahabu safi sehemu yake ya juu, pande zote kuizunguka na pia pembe zake, na kutengeneza ukingo wa dhahabu kuizunguka. 27  Akaitengenezea pete mbili za dhahabu chini ya ukingo wake kwenye pande zake mbili zinazoelekeana ili zishikilie fito za kubebea madhabahu. 28  Baada ya hayo akatengeneza fito za mshita na kuzifunika kwa dhahabu. 29  Alitengeneza pia mafuta matakatifu ya kutia mafuta+ na uvumba safi uliotiwa manukato+ na kuchanganywa kwa ustadi.*

Maelezo ya Chini

Mkono mmoja ulilingana na sentimita 44.5 (inchi 17.5). Angalia Nyongeza B14.
Karibu sentimita 7.4 (inchi 2.9). Angalia Nyongeza B14.
Talanta moja ilikuwa na uzito wa kilogramu 34.2. Angalia Nyongeza B14.
Au “kama anavyofanya mtengenezaji wa manukato.”