Zekaria 5:1-11

  • Maono ya 6: Kitabu cha kukunjwa kinachopaa angani (1-4)

  • Maono ya 7: Kikapu cha kupimia (5-11)

    • Kina mwanamke anayefananisha Uovu (8)

    • Kikapu hicho chapelekwa Shinari (9-11)

5  Nikatazama juu tena, nikaona kitabu cha kukunjwa kikipaa.  Akaniuliza: “Unaona nini?” Nikamjibu: “Ninaona kitabu cha kukunjwa chenye urefu wa mikono 20* na upana wa mikono 10 kikipaa.”  Kisha akaniambia: “Hii ndiyo laana inayotoka kwenda juu ya dunia yote, kwa sababu kila mtu anayeiba,+ kama ilivyoandikwa upande mmoja, hajaadhibiwa; na kila mtu anayeapa kwa uwongo,+ kama ilivyoandikwa upande wa pili, hajaadhibiwa.  ‘Nimeituma laana hiyo,’ asema Yehova wa majeshi, ‘nayo itaingia katika nyumba ya mwizi na katika nyumba ya mtu anayeapa kwa uwongo katika jina langu; nayo itakaa katika nyumba hiyo na kuiharibu kabisa na pia mbao zake na mawe yake.’”  Ndipo malaika aliyekuwa akizungumza nami akaja na kuniambia: “Tafadhali, tazama juu, uone kitu kinachotoka.”  Kwa hiyo nikamuuliza: “Ni kitu gani hicho?” Akanijibu: “Ni chombo cha efa kinachotoka.”* Kisha akaniambia: “Hivyo ndivyo wanavyoonekana duniani kote.”  Nami nikaona kwamba kifuniko chake cha mviringo cha madini ya risasi kilikuwa kimeinuliwa, na kulikuwa na mwanamke aliyekuwa ameketi ndani ya chombo hicho.  Kwa hiyo malaika akasema: “Huu ni Uovu.” Kisha akamsukuma mwanamke huyo ndani ya chombo hicho cha efa na kukifunika kwa nguvu kwa kile kifuniko kizito cha madini ya risasi.  Halafu nikatazama juu na kuwaona wanawake wawili wakija, nao walikuwa wakipaa katika upepo. Walikuwa na mabawa kama ya korongo. Nao wakakiinua kile chombo na kuruka nacho kati ya dunia na mbingu. 10  Basi nikamuuliza malaika aliyekuwa akizungumza nami: “Wanakipeleka wapi chombo cha efa?” 11  Akanijibu: “Katika nchi ya Shinari*+ ili wamjengee nyumba mwanamke huyo; na itakapokuwa tayari, atawekwa humo mahali panapomfaa.”

Maelezo ya Chini

Mkono mmoja ulilingana na sentimita 44.5 (inchi 17.5). Angalia Nyongeza B14.
Tnn., “Ni efa inayotoka.” Efa inatumiwa hapa kurejelea chombo au kikapu kilichotumiwa kupima kipimo cha efa. Efa ya nafaka ilikuwa karibu kilogramu 13. Angalia Nyongeza B14.
Yaani, Babilonia.