Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Dhihirisheni Imani Katika Nuru”

“Dhihirisheni Imani Katika Nuru”

“Dhihirisheni Imani Katika Nuru”

MARA nyingi Maandiko huhusianisha nuru na Muumba wake. Mtunga-zaburi alisema: “Wewe, BWANA, Mungu wangu, umejifanya mkuu sana; umejivika heshima na adhama. Umejivika nuru kama vazi.” (Zaburi 104:1, 2) Tangazo hilo lapatana vizuri na maelezo ya Ezekieli ya mambo aliyoona katika ono: “Nikaona kana kwamba ni rangi ya kaharabu, kama kuonekana kwa moto ndani yake pande zote, tangu kuonekana kwa viuno vyake na juu; na tangu kuonekana kwa viuno vyake na chini, naliona kana kwamba ni kuonekana kwa moto; tena palikuwa na mwangaza pande zake zote. Kama kuonekana kwa upinde wa mvua, ulio katika mawingu siku ya mvua, ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwa mwangaza ule pande zote. Ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwake mfano huo wa utukufu wa BWANA.” (Ezekieli 1:27, 28) Karne nyingi awali, udhihirisho kidogo tu wa utukufu huo ulifanya uso wa Musa ung’ae.—Kutoka 33:22, 23; 34:29, 30.

“Mungu ni nuru na hakuna giza kamwe katika muungano na yeye.” (1 Yohana 1:5) Yeye ni mwadilifu, mnyoofu, na mtakatifu, na hatendi mambo mapotovu na yasiyo safi ambayo kwa kawaida huhusianishwa na giza. (Kumbukumbu la Torati 32:4; Ufunuo 4:8) Basi watu wanaotembea gizani kwa kuwachukia ndugu zao na wasioifuata kweli hawawezi kamwe kuwa katika muungano na yeye.—1 Yohana 1:6; 2:9-11.

Yehova ndiye “Baba wa mianga ya kimbingu.” (Yakobo 1:17) Yeye ‘huwapa watu jua, ili kuwa nuru wakati wa mchana, na amri za mwezi na nyota, ili kuwa nuru wakati wa usiku,’ na zaidi yeye ndiye Chanzo cha nuru yote ya kiroho. (Yeremia 31:35; 2 Wakorintho 4:6) Sheria yake, maamuzi yake ya hukumu, na neno lake ni nuru kwa wale wanaopenda waongozwe nazo. (Zaburi 43:3; 119:105; Mithali 6:23; Isaya 51:4) Mtunga-zaburi alitangaza hivi: “Katika nuru yako tutaona nuru.” (Zaburi 36:9) Kama vile jua huzidi kung’aa tangu mapambazuko hata “mchana mkamilifu,” ndivyo na njia ya wenye haki, inayoangazwa na hekima ya Mungu, izidivyo kung’aa. (Mithali 4:18) Kufuata njia anayotaja Yehova ni kutembea katika nuru yake. (Isaya 2:3-5) Kwa upande mwingine, mtu atazamapo mambo kwa njia isiyo safi au kwa lengo bovu, yeye yumo katika giza kubwa la kiroho. Kama Yesu alivyosema: “Ikiwa jicho lako ni bovu, mwili wako wote utakuwa wenye giza. Ikiwa kwa kweli nuru iliyo katika wewe ni giza, jinsi lilivyo kubwa giza hilo!”—Mathayo 6:23.

Nuru na Mwana wa Mungu.

Tangu afufuliwe na kwenda mbinguni, Kristo Yesu, “Mfalme wa wale watawalao wakiwa wafalme na Bwana wa wale watawalao wakiwa mabwana,” ‘akaa katika nuru isiyokaribika.’ Nuru hiyo ni tukufu sana hivi kwamba macho dhaifu ya wanadamu hayawezi kumwona. (1 Timotheo 6:15, 16) Hata mtu mmoja, Sauli (Paulo) wa Tarso, alipofushwa na nuru kutoka mbinguni aliyoona wakati Mwana wa Mungu aliyetukuzwa alipojifunua kwa mnyanyasi huyo wa wafuasi wa Yesu.—Matendo 9:3-8; 22:6-11.

Wakati wa huduma yake hapa duniani Yesu Kristo alikuwa nuru, akiandaa nuru ya kiroho kuhusu makusudi ya Mungu na mapenzi yake kwa wale ambao wangepokea upendeleo wa Mungu. (Yohana 9:5) Mwanzoni, ni “kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli” tu waliopokea manufaa ya “nuru kubwa.” (Isaya 9:1, 2; Mathayo 4:13-16; 15:24) Lakini nuru ya kiroho haikuwa ibaki tu kwa Wayahudi wa asili na wageuzwa-imani. (Yohana 1:4-9; linganisha Matendo 13:46, 47.) Yesu alipopelekwa hekaluni akiwa kitoto kichanga, Simeoni mzee alimtaja kuwa “nuru ya kuondoa shela kwa mataifa.” (Luka 2:32) Kama Paulo alivyowaeleza Waefeso, watu wasio Wayahudi ambao hawakutahiriwa walikuwa gizani kuhusu Mungu na makusudi yake: “Hapo zamani nyinyi mlikuwa watu wa mataifa kwa habari ya mwili; ‘kutotahiriwa’ ndivyo mlivyoitwa na kile kiitwacho ‘kutahiriwa’ kifanywacho katika mwili kwa mikono— kwamba kwenye wakati huo maalumu mlikuwa bila Kristo, mkifanywa wageni kwa dola la Israeli na mkiwa watu wasiojulikana kwa maagano ya ahadi, nanyi mlikuwa hamna tumaini na mlikuwa bila Mungu katika ulimwengu.” (Waefeso 2:11, 12) Hata hivyo, watu wasio Wayahudi walipohubiriwa habari njema kuhusu Kristo, wale waliokubali ‘waliitwa kutoka katika giza na kuingia katika nuru ya Mungu ya ajabu.’ (1 Petro 2:9) Lakini wengine waliendelea kumruhusu yule ambaye hujigeuza kuwa “malaika wa nuru” (2 Wakorintho 11:14), “mungu wa huu mfumo wa mambo,” awapofushe ili ‘mmuliko wa habari njema yenye utukufu juu ya Kristo usipate kung’aa kwa kupenya.’ (2 Wakorintho 4:4) Walipendelea giza, kwa sababu walitaka kuendelea kufuata mwendo wao wenye ubinafsi.—Linganisha Yohana 3:19, 20.

Wafuasi wa Kristo Wapata Kuwa Nuru.

Wale waliokuwa na imani katika Kristo Yesu wakiwa “nuru ya ulimwengu” na kuwa wafuasi wakawa “wana wa nuru.” (Yohana 3:21; 8:12; 12:35, 36, 46) Waliwajulisha wengine matakwa ya kupata upendeleo wa Mungu na uhai, wakifanya hivyo “katika nuru,” yaani, waziwazi. (Mathayo 10:27) Vivyo hivyo, Yohana Mbatizaji alitumikia akiwa nuru “akihubiri ubatizo katika ufananisho wa toba” na kutaja kuja kwa Mesiya. (Luka 3:3, 15-17; Yohana 5:35) Pia, kupitia kazi zao nzuri, na kwa maneno na mfano, wafuasi wa Kristo huangaza nuru yao. (Mathayo 5:14, 16) “Matunda ya nuru huwa yana kila namna ya wema na uadilifu na kweli.” Kwa hiyo, nuru hufunua chanzo cha matendo yenye aibu ya gizani (uasherati, ukosefu wa usafi wa kila aina, pupa, na kadhalika) yanayotendwa na “wana wa kutotii.” Matokeo ni kwamba kazi hizo huonekana jinsi zilivyo kihalisi na, katika maana ya kudhihirishwa kuwa mambo yanayoshutumiwa na Mungu, yenyewe huwa nuru. (Waefeso 5:3-18) Wakiwa na “silaha za nuru,” silaha za kiroho zitokazo kwa Mungu, Wakristo hupigana vita “dhidi ya serikali, dhidi ya mamlaka, dhidi ya watawala wa ulimwengu wa giza hili, dhidi ya majeshi ya roho waovu katika mahali pa kimbingu” nao huwezeshwa kusimama imara wakiwa watumishi waliokubaliwa wa Mungu.—Waroma 13:12-14; Waefeso 6:11-18.