Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Cyril Lucaris—Mtu Aliyeithamini Biblia

Cyril Lucaris—Mtu Aliyeithamini Biblia

Cyril Lucaris—Mtu Aliyeithamini Biblia

Ilikuwa siku ya kiangazi mwaka wa 1638. Wavuvi katika Bahari ya Marmara karibu na Constantinople (Istanbul ya siku hizi), jiji kuu la Milki ya Uturuki, walipigwa na butwaa kuona maiti ikielea majini. Walipoichunguza kwa ukaribu zaidi, walishtuka walipotambua kwamba maiti hiyo iliyokuwa imenyongwa ilikuwa ya askofu mkuu wa Constantinople, kiongozi wa Kanisa Othodoksi. Huo ndio uliokuwa mwisho wenye kuhuzunisha wa Cyril Lucaris, kiongozi mashuhuri wa kidini wa karne ya 17.

LUCARIS hakuishi muda mrefu vya kutosha kuona tamaa yake kuu—kutolewa kwa tafsiri ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo katika Kigiriki cha kimazungumzo—ikitimizwa. Lucaris alikuwa na tamaa nyingine ambayo pia haikutimizwa—ile ya kuona Kanisa Othodoksi likirejelea “mafundisho sahili ya gospeli.” Mtu huyo alikuwa nani? Alipata vipingamizi vipi katika jitihada hizo?

Afadhaishwa na Ukosefu wa Elimu

Cyril Lucaris alizaliwa mwaka wa 1572, katika Candia (ambayo leo ni Iráklion) iliyokaliwa na Venice, Krete. Kwa kuwa alikuwa na vipawa, yeye alisomea Venice na Padua nchini Italia, kisha akasafiri sana katika nchi hiyo na nchi nyinginezo. Akiwa amechukizwa na mizozo ya vikundi ndani ya kanisa na kuvutiwa na harakati za mageuzi ya kidini katika Ulaya, yaelekea alizuru Geneva, ambako wakati huo mafundisho ya Calvin yalifuatwa sana.

Alipokuwa akizuru Poland, Lucaris aliona kwamba kwa sababu ya ukosefu wa elimu hali ya kiroho ya Waothodoksi, makasisi na pia watu wa kawaida, ilikuwa mbaya sana. Aliporudi Aleksandria na Constantinople, alishtuka kuona kwamba hata mimbari—ambapo Maandiko yalisomwa—zilikuwa zimeondolewa katika makanisa fulani!

Katika mwaka wa 1602, Lucaris alienda Aleksandria, ambapo alirithi uaskofu kutoka kwa mtu wa ukoo, Askofu Meletios. Kisha akaanza kuandikiana barua na wanatheolojia kadhaa wa Ulaya waliopendelea mageuzi. Katika mojawapo ya barua hizo, alisema kwamba Kanisa Othodoksi lilidumisha mazoea mengi yenye makosa. Katika barua nyinginezo, alikazia uhitaji wa kanisa kufundisha “mafundisho sahili ya gospeli” badala ya ushirikina na pia uhitaji wa kutegemea mamlaka ya Maandiko pekee.

Lucaris pia alishtuka kwamba mamlaka ya kiroho ya Waandishi wa Kanisa ilionwa kuwa sawa na maneno ya Yesu na mitume. “Siwezi kuvumilia tena kusikia watu wakisema kwamba maneno ya mapokeo ya wanadamu yana umuhimu sawa na Maandiko,” akaandika. (Mathayo 15:6) Aliendelea kusema kwamba kulingana na maoni yake ibada ya sanamu inaleta msiba. Alisema kwamba kusali kupitia “watakatifu” ni kumfedhehesha Mpatanishi, Yesu.—1 Timotheo 2:5.

Cheo cha Askofu Chauzwa

Kwa sababu ya maoni hayo pamoja na kulichukia sana Kanisa Katoliki, Lucaris alichukiwa na kunyanyaswa na Wajesuti na waumini wa Kanisa Othodoksi waliopendelea kushirikiana na Wakatoliki. Licha ya upinzani huo, Lucaris alichaguliwa kuwa askofu wa Constantinople mwaka wa 1620. Wakati huo, uaskofu wa Kanisa Othodoksi ulikuwa chini ya mamlaka ya Milki ya Uturuki. Serikali ya Uturuki ingemwondoa askofu mara moja na kuweka mwingine mpya wakipewa pesa.

Adui za Lucaris, hasa Wajesuti na kundi la Congregatio de Propaganda Fide (Kundi la Kueneza Imani) la papa lenye nguvu na lenye kuogofya, waliendelea kumchongea na kula njama dhidi yake. “Ili kutimiza lengo hilo Wajesuti walitumia kila njia—hila, usingiziaji, kurairai na, zaidi ya yote, rushwa ambayo ndiyo iliyokuwa njia nzuri zaidi ya kupata upendeleo wa watawala wa [Uturuki],” chasema kitabu Kyrillos Loukaris. Hivyo, katika mwaka wa 1622, Lucaris akahamishiwa kisiwa cha Rhodes, na Gregory wa Amasya akanunua uaskofu kwa sarafu za fedha 20,000. Lakini Gregory alishindwa kulipa pesa zote alizoahidi, hivyo Anthimus wa Adrianople akanunua uaskofu, lakini akajiuzulu baadaye. Kwa kushangaza, Lucaris alirudishwa awe askofu.

Lucaris aliazimia kutumia fursa hii mpya kuelimisha makasisi wa Othodoksi na watu wa kawaida kwa kuchapisha tafsiri ya Biblia na trakti za kidini. Ili kutimiza jambo hilo, alipanga matbaa iletwe Constantinople chini ya ulinzi wa balozi wa Uingereza. Lakini matbaa hiyo ilipowasili Juni 1627, adui za Lucaris walimshtaki kwamba anaitumia kwa makusudi ya kisiasa, na hatimaye wakafanya iharibiwe. Sasa ilimbidi Lucaris atumie matbaa zilizokuwa Geneva.

Tafsiri ya Maandiko ya Kikristo

Lucaris alistahi sana Biblia na uwezo wa Biblia wa kuelimisha, jambo lililochochea tamaa yake ya kuifanya iwe rahisi zaidi kwa mtu wa kawaida kuisoma. Alitambua kwamba lugha iliyotumiwa katika hati za awali za Biblia ya Kigiriki iliyopuliziwa haikueleweka na watu wa kawaida. Hivyo, Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo ndicho kitabu cha kwanza ambacho Lucaris aliagiza kitafsiriwe katika Kigiriki cha wakati wake. Maximus Callipolites, mtawa mwenye elimu, alianza kukitafsiri Machi 1629. Waothodoksi wengi waliona kutafsiriwa kwa Maandiko kuwa kitendo kiovu, hata kama ilikuwa vigumu kadiri gani kwa wasomaji kuyaelewa maandishi hayo. Ili kuwaridhisha, Lucaris aliagiza maandishi ya awali na yale yaliyotafsiriwa yachapwe katika safu sambamba, yakiongezwa maneno machache tu. Kwa kuwa Callipolites alikufa punde tu baada ya kuwasilisha tafsiri hiyo, nakala hizo zilisahihishwa na Lucaris mwenyewe. Tafsiri hiyo ilichapwa muda mfupi baada ya kifo cha Lucaris mwaka 1638.

Licha ya tahadhari ambazo Lucaris alichukua, maaskofu wengi walipinga vikali tafsiri hiyo. Upendo wa Lucaris kwa Neno la Mungu ulikuwa dhahiri kabisa katika dibaji ya tafsiri hiyo ya Biblia. Aliandika kwamba Maandiko, yakiandikwa katika lugha ambayo watu huzungumza, ni “ujumbe wenye kupendeza, tuliopewa kutoka mbinguni.” Aliwashauri watu “wajue na kufahamu maandiko yote ya [Biblia]” na kusema kwamba hakuna njia nyingine ya kujifunza “mambo yanayohusiana barabara na imani . . . ila kupitia Gospeli takatifu ya Mungu.”—Wafilipi 1:9, 10.

Lucaris aliwashutumu vikali wale waliozuia watu wasijifunze Biblia, na pia wale waliokataa kutafsiriwa kwa maandishi ya awali: “Tukizungumza au kusoma bila kuelewa, ni kama kusema hewani tu.” (Linganisha 1 Wakorintho 14:7-9.) Akimalizia dibaji yake, yeye aliandika: “Nyote mnaposoma tafsiri hii ya Gospeli ya Mungu iliyo takatifu katika lugha yenu wenyewe, zingatieni manufaa zinazotokana na kuisoma, . . . na Mungu awawezeshe sikuzote kuelewa yaliyo mema.”—Mithali 4:18.

Taarifa ya Confession of Faith

Baada ya kuanzisha kutafsiriwa huko kwa Biblia, Lucaris alichukua hatua nyingine ya ujasiri. Katika mwaka wa 1629 alichapisha taarifa ya Confession of Faith jijini Geneva. Hiyo ilikuwa taarifa yake kuhusu itikadi ambazo alitumaini zingekubaliwa rasmi na Kanisa Othodoksi. Kwa mujibu wa kitabu The Orthodox Church, taarifa hiyo ya Confession “hufanya fundisho la Othodoksi kuhusu ukasisi na utawa lisiwe na umaana wowote, na inashutumu kutukuzwa kwa sanamu na kusali kupitia watakatifu kuwa aina za ibada ya sanamu.”

Taarifa hiyo ya Confession ina kanuni 18. Kanuni yake ya pili hutaarifu kwamba Maandiko yamepuliziwa na Mungu na kwamba mamlaka yake yanapita yale ya kanisa. Kanuni hiyo yasema: “Twaamini tulipata Maandiko Matakatifu kutoka kwa Mungu. . . . Twaamini kwamba mamlaka ya Maandiko Matakatifu yanapita mamlaka ya Kanisa. Kufundishwa na Roho Mtakatifu ni tofauti kabisa na kufundishwa na mwanadamu.”— 2 Timotheo 3:16.

Kanuni ya nane na ya kumi zasema kwamba Yesu Kristo tu ndiye Mpatanishi, Kuhani wa Cheo cha Juu, na Kichwa cha kutaniko. Lucaris aliandika: “Twaamini kwamba Bwana wetu Yesu Kristo ameketi mkono wa kuume wa Baba Yake na akiwa hapo Yeye hutuombea, akiwa mtekelezaji pekee wa kazi ya kuhani wa cheo cha juu, aliye wa kweli na halali, na ya mpatanishi.”—Mathayo 23:10.

Kanuni ya 12 yatangaza kwamba kanisa linaweza kukosea, na kufikiria kimakosa kwamba uwongo ndio kweli, lakini nuru ya roho takatifu yaweza kuliokoa kupitia jitihada za wahudumu waaminifu. Katika kanuni ya 18, Lucaris asisitiza kwamba purgatori ni dhana iliyotungwa tu: “Ni dhahiri kwamba Purgatori iliyotungwa haipasi kukubaliwa.”

Nyongeza ya Confession hiyo ina maswali na majibu kadhaa. Kwenye nyongeza hiyo, Lucaris anakazia kwanza kwamba Maandiko yapaswa kusomwa na kila mwumini na kwamba ni hatari kwa Mkristo kutosoma Neno la Mungu. Kisha anaendelea kusema kwamba vitabu vya Apokrifa viepukwe.—Ufunuo 22:18, 19.

Swali la nne lauliza: “Twapaswa kuzionaje Sanamu?” Lucaris ajibu: “Tumefundishwa na Maandiko ya Mungu yaliyo Matakatifu, ambayo husema wazi, ‘Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani; usivisujudie, wala kuviabudu; [Kutoka 20:4, 5]’ kwa kuwa twapaswa kuabudu, si kiumbe, bali Muumba na Mfanyi wa mbingu na dunia, na kusujudu Yeye pekee. . . . Kama ambavyo ibada na kutumikia [sanamu] zimekatazwa . . . katika Maandiko Matakatifu, sisi pia tunazikataa, tusije tukasahau, na badala ya kuabudu Muumba na Mfanyi, tuabudu rangi, sanaa, na viumbe.”—Matendo 17:29.

Ingawa Lucaris hakuweza kufahamu kabisa mafundisho yote yenye makosa katika enzi ya giza la kiroho alimoishi, * alifanya jitihada nzuri za kufanya Biblia iwe na mamlaka juu ya mafundisho ya kanisa na kuelimisha watu juu ya mafundisho yake.

Punde tu baada ya taarifa hiyo ya Confession kutolewa, upinzani ulianza tena dhidi ya Lucaris. Katika mwaka wa 1633, Cyril Contari, aliyekuwa askofu wa Beroea (sasa Aleppo), adui ya Lucaris ambaye aliungwa mkono na Wajesuti, alijaribu kujadiliana na Waturuki juu ya bei ya kununua uaskofu. Hata hivyo, mpango huo ulikosa kufaulu Contari aliposhindwa kulipa pesa zilizotakiwa. Lucaris akabaki mamlakani. Mwaka uliofuata, Athanasius wa Thesalonike akalipa sarafu za fedha zipatazo 60,000 kununua uaskofu. Na kwa mara nyingine Lucaris akaondolewa mamlakani. Lakini akarudishwa tena baada ya mwezi mmoja. Kufikia wakati huo, Cyril Contari alikuwa amekusanya sarafu za fedha 50,000. Wakati huu Lucaris alihamishiwa Rhodes. Baada ya miezi sita, rafiki zake wakaweza kumrudisha tena mamlakani.

Hata hivyo, katika mwaka wa 1638 Wajesuti na Waothodoksi walioshirikiana nao walimshtaki Lucaris kuwa alitaka kupindua Milki ya Uturuki. Wakati huu sultani akaamuru auawe. Lucaris akakamatwa, na mnamo Julai 27, 1638, akapandishwa kwenye mashua ndogo kana kwamba anahamishwa. Lucaris alinyongwa mara tu mashua hiyo ilipofika baharini. Mwili wake ulizikwa karibu na ufuo, kisha ukafukuliwa na kutupwa baharini. Wavuvi waliupata mwili huo na baadaye rafiki zake wakauzika.

Mambo Tunayojifunza

“Yapasa kuzingatiwa kwamba mojawapo ya mradi mkuu wa [Lucaris] ulikuwa kuelimisha na kuinua kiwango cha elimu cha makasisi na waumini, ambacho katika karne ya kumi na sita na mapema katika karne ya kumi na saba kilikuwa kimeshuka sana,” asema msomi mmoja. Lucaris alipata vizuizi vingi asiweze kufikia mradi wake. Aliondolewa uaskofu mara tano. Miaka 34 baada ya kifo chake, sinodi moja katika Jerusalem ililaani itikadi zake kuwa uzushi. Walitangaza kwamba Maandiko “hayapaswi kusomwa na kila mtu, lakini yapaswa kusomwa na wale wenye kuchunguza mambo ya roho yenye kina baada ya kufanya utafiti ufaao”—yaani, wale makasisi waliodhaniwa kuwa na elimu.

Kwa mara nyingine tena, viongozi wa kanisa walikandamiza jitihada za kufanya Neno la Mungu lipatikane kwa waumini wao. Walinyamazisha kwa ujeuri mtu aliyewaonyesha baadhi ya makosa ya itikadi zao zisizotokana na Biblia. Viongozi hao wakawa adui wakubwa zaidi wa uhuru wa ibada na kweli. Kwa kusikitisha, mtazamo huu umedumu katika njia mbalimbali hata wakati wetu. Mtazamo huo ni kikumbusha kinachofanya mtu afikirie yale yanayotukia wakati njama zenye kuchochewa na makasisi zinapozuia uhuru wa kufikiri na wa kusema.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 24 Katika taarifa yake ya Confession, yeye anaunga mkono Utatu na fundisho la kuamuliwa kimbele yatakayompata mtu na la nafsi isiyoweza kufa—yote yakiwa mafundisho yasiyotokana na Biblia.

[Blabu katika ukurasa wa 29]

Lucaris alifanya jitihada nzuri za kufanya Biblia iwe na mamlaka juu ya mafundisho ya kanisa na kuelimisha watu juu ya mafundisho yake

[Picha/Sanduku katika ukurasa wa 28]

Lucaris na Codex Alexandrinus

Mojawapo ya vitu vyenye thamani vya Jumba la Maktaba ya Uingereza ni Codex Alexandrinus, hati ya Biblia ya karne ya tano W.K. Kurasa 773 kati ya kurasa zake 820 zimehifadhiwa.

Lucaris alipokuwa askofu wa Aleksandria, Misri, alikusanya vitabu vingi sana. Alipowekwa askofu wa Constantinople, alibeba hati ya Codex Alexandrinus. Katika mwaka wa 1624 alimpa balozi wa Uingereza nchini Uturuki hati hiyo ikiwa zawadi kwa Mfalme wa Uingereza, James wa Kwanza. Ilikabidhiwa mwandamizi wake, Charles wa Kwanza, miaka mitatu baadaye.

Katika mwaka wa 1757 Maktaba ya Kifalme ilikabidhiwa taifa la Uingereza, na sasa kodeksi hiyo bora imewekwa kwa ajili ya maonyesho katika sehemu iitwayo John Ritblat Gallery kwenye Maktaba mpya ya Uingereza.

[Hisani]

Gewerbehalle, Vol. 10

From The Codex Alexandrinus in Reduced Photographic Facsimile, 1909

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]

Bib. Publ. Univ. de Genève