Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tii Onyo!

Tii Onyo!

Tii Onyo!

PUU! Mnamo Juni 3, 1991, Mlima Fugen nchini Japani ulilipuka kwa mshindo mkubwa wenye ngurumo ukimwaga gesi na majivu ya volkano. Mchanganyiko huo uliokuwa moto sana ulitiririka chini ya mlima. Mlipuko huo ulisababisha vifo vya watu 43. Wengi walioponea chupuchupu walikuwa wamechomeka vibaya. “Maji, maji, tafadhali,” wengine wakalia. Zimamoto na polisi wakaenda mbio sana kuwasaidia.

MAWE yaliyoyeyuka yalikuwa yameonekana kwenye kilele cha Mlima Fugen majuma mawili hivi awali, kwa hiyo wenye mamlaka na wakazi walikuwa macho. Kwa muda wa zaidi ya juma moja kabla ya msiba huo, watu walikuwa wameshauriwa waondoke kwenye eneo hilo. Siku moja tu kabla ya mlipuko huo, polisi walikuwa wamewaomba waandishi wa habari wasiingie katika eneo hilo marufuku. Lakini, alasiri hiyo yenye msiba watu 43 walikufa katika eneo hilo la hatari.

Kwa nini watu wengi hivyo walijasiria kuingia katika eneo hilo au kubaki humo? Wakulima fulani waliokuwa wamehama nyumba zao walirudi kutazama mali zao na mashamba yao. Wataalamu watatu wa mambo ya volkano walikuwa wakijaribu kuikaribia volkano hiyo kwa kadiri iwezekanavyo ili waridhishe tamaa yao ya kitaaluma. Waandishi kadhaa wa habari na wapiga-picha walithubutu kuvuka mpaka wa eneo marufuku kwa sababu walitaka kutoa habari motomoto juu ya mlipuko huo. Madereva watatu wa teksi zilizokuwa zimekodishwa na waandishi wa habari walikuwa katika eneo hilo. Polisi na zimamoto wa kujitolea walikuwa kazini. Kila mmoja wao alikuwa na sababu yake ya kuingia katika eneo la hatari—na matokeo yakawa kifo.

Je, Wewe Uko Katika Eneo la Hatari?

Huenda si wote wanaishi karibu na volkano yenye kulipuka. Lakini, namna gani kama tungekabili msiba mkubwa wa ulimwenguni pote, ukituweka sote katika eneo la hatari linalohusu ulimwengu mzima? Kitabu ambacho kimekuwa chanzo chenye kutegemeka cha habari za kiunabii chatuonya juu ya msiba wa ulimwenguni pote na kuufafanua hivi: ‘Jua litatiwa giza, nao mwezi hautatoa nuru yao, nazo nyota zitaanguka kutoka mbinguni, nazo nguvu za mbingu zitatikiswa. Makabila yote ya dunia yatajipiga yenyewe kwa maombolezo.’ (Mathayo 24:29, 30) Hapa matukio ya ajabu ya mbingu yanayoukumba ulimwengu wote yanaonyeshwa kuwa yanapata “makabila yote ya dunia.” Yaani, unabii huo wahusiana na msiba mkubwa utakaoathiri kila mmoja wetu.

Biblia ndiyo kitabu hicho cha unabii wenye kutegemeka. Jambo la kutokeza ni kwamba muktadha wa andiko ambalo limetajwa juu wafafanua kinaganaga mambo yatakayotangulia msiba huo mkubwa wa ulimwenguni pote. Kama vile myeyuko wa mawe na ishara nyinginezo zilivyowafanya maofisa wa jiji la Shimabara watenge eneo la hatari, Biblia hutupa sababu za kuwa macho na za kujitayarisha kwa ajili ya kuokoka. Tunaweza kujifunza somo fulani kutokana na msiba wa Mlima Fugen na kufahamu uzito wa mambo yatakayotukia karibuni.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 2]

COVER: Yomiuri/Orion Press/Sipa Press

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

Yomiuri/Orion Press/Sipa Press