Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Sehemu ya 16

Masihi Afika

Masihi Afika

Yehova amtambulisha Yesu wa Nazareti kuwa Masihi aliyeahidiwa

JE, Yehova angewasaidia watu wake kumtambua Masihi? Ndiyo. Fikiria aliyofanya. Karne nne baada ya Maandiko ya Kiebrania kumalizika, katika jiji linaloitwa Nazareti, eneo la kaskazini la Galilaya, mwanamke kijana anayeitwa Maria alitembelewa na mgeni asiye wa kawaida. Malaika anayeitwa Gabrieli alimtokea na kumwambia kwamba ijapokuwa yeye ni bikira, Mungu angetumia nguvu zake za utendaji, roho takatifu, kumfanya azae mwana. Mwana huyo ndiye Mfalme aliyeahidiwa zamani, yule ambaye angetawala milele! Mtoto huyo angekuwa Mwana wa Mungu mwenyewe. Mungu angeuhamisha uhai wake kutoka mbinguni na kuutia katika tumbo la uzazi la Maria.

Maria alikubali kwa unyenyekevu mgawo huo wa pekee. Mchumba wake, seremala anayeitwa Yosefu, alimwoa baada ya Mungu kumtuma malaika amhakikishie chanzo cha uja-uzito wa Maria. Hata hivyo, unabii uliosema kwamba Masihi angezaliwa Bethlehemu ungetimizwa jinsi gani? (Mika 5:2) Jiji hilo dogo lilikuwa umbali wa kilomita 140 hivi kutoka Nazareti!

Mtawala Mroma aliagiza watu wahesabiwe. Watu walipaswa kujiandikisha katika miji ya nyumbani kwao. Inaonekana kwamba Bethlehemu kulikuwa nyumbani kwa Yosefu na Maria, kwa hiyo Yosefu na mke wake wakasafiri hadi huko. (Luka 2:3) Maria alizalia zizini, na kumlaza mtoto wake katika hori. Kisha Mungu akatuma malaika wengi wakawaambie wachungaji waliokuwa mlimani kwamba mtoto ambaye amezaliwa ndiye Masihi, au Kristo, aliyeahidiwa.

Baadaye, wengine pia walishuhudia kwamba Yesu ndiye Masihi aliyeahidiwa. Nabii Isaya alitabiri kwamba mtu fulani angetokea na kutayarisha njia kwa ajili ya kazi muhimu ya Masihi. (Isaya 40:3) Mtu huyo ni Yohana Mbatizaji. Alipomwona Yesu, alipaaza sauti: “Ona, Mwana-Kondoo wa Mungu ambaye huondolea mbali dhambi ya ulimwengu!” Baadhi ya wanafunzi wa Yohana wakamfuata Yesu mara moja. Mmoja wao akasema: “Tumempata Masihi.”—Yohana 1:29, 36, 41.

Kulikuwa na ushuhuda zaidi. Yohana alipombatiza Yesu, Yehova mwenyewe alisema kutoka mbinguni. Akitumia roho takatifu, alimweka rasmi Yesu kuwa Masihi na kusema: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa, ambaye nimemkubali.” (Mathayo 3:16, 17) Masihi aliyeahidiwa akawa amefika!

Hilo lililotokea wakati gani? Mwaka wa 29 W.K., wakati ambapo ile miaka 483 iliyotabiriwa na Danieli ilipokamilika. Ndiyo, utimizo huo ni mojawapo ya ushuhuda wenye kuthibitisha kwamba Yesu ndiye Masihi, au Kristo. Hata hivyo, alitangaza ujumbe gani alipokuwa duniani?

—Inatoka kwenye Mathayo, sura ya 1 hadi 3; Marko, sura ya 1; Luka, sura ya 2; Yohana, sura ya 1.