Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SEHEMU YA 9

Waisraeli Wataka Mfalme

Waisraeli Wataka Mfalme

Sauli, mfalme wa kwanza wa Israeli, akosa kutii. Daudi, ambaye Mungu afanya pamoja naye agano la ufalme wa kudumu, atawala baada yake

BAADA ya siku za Samsoni, Samweli alikuwa nabii na mwamuzi katika taifa la Israeli. Waisraeli walikuwa wakimwambia kwamba wanataka kuwa kama mataifa mengine, na kuwa na mfalme wa kibinadamu. Ijapokuwa ombi hilo halikumpendeza Yehova, alimwagiza Samweli alitekeleze. Mungu alimchagua mwanamume mnyenyekevu anayeitwa Sauli awe mfalme. Hata hivyo, baada ya muda, Mfalme Sauli alibadilika na kuwa mwenye kiburi na mkaidi. Yehova alimkataa na kumwambia Samweli amteue mwingine—kijana anayeitwa Daudi. Hata hivyo, miaka kadhaa ilipita kabla ya Daudi kuanza kutawala.

Yamkini akiwa katika miaka ya utineja, Daudi aliwatembelea ndugu zake waliokuwa katika jeshi la Sauli. Jeshi zima lilikuwa limebabaishwa na askari mmoja adui, jitu linaloitwa Goliathi, lililokuwa likimdhihaki Mungu wao. Akiwa na ghadhabu, Daudi alijitolea kupigana na jitu hilo. Akiwa na kombeo na mawe matano, kijana huyo alikwenda kukutana na mpinzani wake, aliyekuwa na urefu wa karibu mita tatu. Goliathi alipomdhihaki, Daudi alijibu kwamba amejihami kuliko jitu hilo kwa kuwa anapigana kwa jina la Yehova Mungu! Daudi alilipiga na kuliangusha jitu hilo kwa jiwe moja tu kisha akauchukua upanga wa jitu hilo na kulikata kichwa. Jeshi la Wafilisti likakimbia kwa hofu.

Mwanzoni, Sauli alipendezwa sana na ujasiri wa Daudi na kumweka aongoze jeshi lake. Hata hivyo, mafanikio ya Daudi yalimfanya Sauli awe na wivu mbaya. Daudi alilazimika kukimbia aokoe uhai wake. Aliishi akiwa mkimbizi kwa miaka mingi. Hata hivyo, Daudi alibaki mshikamanifu kwa Sauli aliyekuwa akijaribu kumuua, akijua kwamba Mfalme Sauli aliwekwa na Yehova Mungu. Hatimaye, Sauli akafa vitani. Muda mfupi baadaye, Daudi akatawazwa, kama vile Yehova alivyokuwa ameahidi.

“Nitakifanya imara kiti cha ufalme wake mpaka wakati usio na kipimo.”—2 Samweli 7:13

Akiwa mfalme, Daudi alitamani sana kumjengea Yehova hekalu. Lakini Yehova akamwambia Daudi kwamba mmoja wa wazao wake ndiye atakayefanya hivyo. Mzao aliyepata pendeleo hilo ni Sulemani, mwana wa Daudi. Hata hivyo, Mungu alimthawabisha Daudi kwa kufanya pamoja naye agano lenye kusisimua: Familia yake ingetokeza ukoo wa kifalme usio na kifani. Hatimaye, Mkombozi, au Uzao ulioahidiwa katika shamba la Edeni ungetokea kupitia ukoo huo. Mkombozi huyo angekuwa Masihi, yaani, “Mtiwa Mafuta,” aliyewekwa rasmi na Mungu. Yehova aliahidi kwamba Masihi huyo angekuwa Mtawala wa Ufalme au serikali ambayo ingedumu milele.

Akiwa na shukrani nyingi, Daudi alikusanya vifaa vingi sana vya ujenzi na madini ya thamani kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa hekalu. Pia, aliongozwa na roho kuandika zaburi nyingi. Alipokuwa akikaribia kufa, Daudi alikiri hivi: “Roho ya Yehova ndiyo iliyosema kupitia mimi, na neno lake lilikuwa kwenye ulimi wangu.”—2 Samweli 23:2.

—Inatoka kwenye 1 Samweli; 2 Samweli; 1 Nyakati; Isaya 9:7; Mathayo 21:9; Luka 1:32; Yohana 7:42.