Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Je, Wajua?

Kwa nini Wayahudi walikuwa wametawanyika sana katika siku za Yesu?

Yesu alipowaambia wasikilizaji wake kwamba mahali alipokuwa akienda hawangeweza kwenda, Wayahudi waliulizana: “Mtu huyu anakusudia kwenda wapi . . . ? Je, anakusudia kwenda kwa Wayahudi waliotawanyika katikati ya Wagiriki?” (Yohana 7:32-36) Muda mfupi baadaye, wamishonari Wakristo walihubiri habari njema kati ya Wayahudi waliotawanyika kotekote katika eneo la Mediterania.—Matendo 2:5-11; 9:2; 13:5, 13, 14; 14:1; 16:1-3; 17:1; 18:12, 19; 28:16, 17.

Wayahudi walitawanyika walipochukuliwa mateka na mataifa yaliyowashinda—kwanza Waashuru mnamo 740 K.W.K., kisha Wababiloni, mnamo 607 K.W.K. Ni Wayahudi wachache tu waliorudi Israeli. (Isaya 10:21, 22) Wengine walibaki katika maeneo walimoishi.

Hiyo ndiyo sababu katika karne ya tano K.W.K., Wayahudi walipatikana katika wilaya za utawala 127 katika Milki ya Uajemi. (Esta 1:1; 3:8) Baada ya muda, jitihada za Wayahudi za kuwageuza watu wafuate dini ya Kiyahudi ziliwafanya watu wengi wamjue Yehova na Sheria aliyowapa Wayahudi. (Mathayo 23:15) Wayahudi kutoka mataifa mbalimbali walikuwa huko Yerusalemu kwa ajili ya Sherehe ya Pentekoste ya mwaka wa 33 W.K., nao wakasikia habari njema kumhusu Yesu. Kwa hiyo, kutawanyika kwa Wayahudi kotekote katika Milki ya Roma kulichangia kuenea haraka kwa Ukristo.

Mfalme Sulemani alikuwa na dhahabu nyingi kadiri gani?

Maandiko yanasema kwamba Hiramu mfalme wa Tiro, alimpa Sulemani tani nne za dhahabu, na malkia wa Sheba akampa kiasi kama hicho, na meli za Sulemani zilileta zaidi ya tani 15 za dhahabu kutoka Ofiri. Simulizi hilo linasema: “Uzito wa dhahabu iliyoletwa kwa Sulemani katika mwaka mmoja ulijumlika kuwa talanta 666 za dhahabu,” au zaidi ya tani 25. (1 Wafalme 9:14, 28; 10:10, 14) Je, hilo ni kweli? Siku hizo, hazina za dhahabu za wafalme zilikuwa kubwa kadiri gani?

Bamba la kale lenye maandishi ambalo wasomi wanaliona kuwa la kweli, linasema kwamba Farao Thutmose wa Tatu wa Misri (aliyeishi miaka 3,500 hivi iliyopita) alitoa tani 13.5 za dhahabu kwa ajili ya hekalu la Amun-Ra huko Karnaki. Katika karne ya nane K.W.K., Mfalme wa Ashuru, Tiglath-pilesa wa Tatu alipokea zaidi ya tani 4 za dhahabu kama kodi kutoka Tiro, na Mfalme Sargoni wa Pili akatoa kiasi kama hicho cha dhahabu kuwa zawadi kwa miungu ya Babiloni. Inaripotiwa kwamba kila mwaka Mfalme Filipo wa Pili wa Makedonia (359-336 K.W.K.) alichimbua zaidi ya tani 28 za dhahabu kutoka kwa migodi ya Pangaeum huko Thrake.

Inasemekana kwamba mwana wa Filipo, Aleksanda Mkuu (336-323 K.W.K.) alipoteka jiji la Uajemi la Susa, alichukua tani 1,180 hivi za dhahabu kutoka huko na karibu tani 7,000 kutoka kwa eneo lote la Uajemi. Kwa hiyo, kwa kulinganisha na ripoti hizo, ufafanuzi wa Biblia kuhusu kiasi cha dhahabu ya Mfalme Sulemani haujatiliwa chumvi.