Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Wauguzi Nimekuwa muuguzi kwa miaka mitatu hivi. Bila shaka, kushughulika moja kwa moja na magonjwa na kuteseka si kazi rahisi. Lilikuwa jambo zuri kama nini kusoma jinsi wengine wanavyothamini kazi yetu katika ule mfululizo wa makala “Wauguzi—Tungefanyaje Bila Wao?” (Novemba 8, 2000) Ile ahadi ya Biblia kwamba karibuni wauguzi hawatahitajiwa inatia moyo hata zaidi.—Isaya 33:24.

J.S.B., Brazili

Mimi na mume wangu tuna zahanati, na mfululizo huo ulitutia moyo sana. Mfululizo huo ulitusaidia kuboresha mtazamo wetu kuelekea kazi yetu na kuelekea wagonjwa wanaokuja kupata msaada wetu. Hongera!

S. S., Ujerumani

Nilikuwa nikifikiri kuwa wauguzi walikuwa wasaidizi tu. Lakini makala hizo zilinisaidia kuelewa kwamba wauguzi husaidia kukomesha mateso ya kiakili, na huandaa huruma na utegemezo ambao mara nyingi madaktari wenye kazi nyingi hawawezi kuandaa. Nilituma nakala kadhaa za gazeti hilo kwa baadhi ya wanadarasa wenzangu wa zamani ambao sasa wanasomea uuguzi.

F. G., Italia

Asanteni kwa makala hizo zenye kugusa hisia. Kazi ya uuguzi imenisaidia kukomaa katika njia mbalimbali. Ni mojawapo ya mambo yaliyonifanya nitafakari kuhusu kusudi la uhai na kujifunza Biblia. Toleo hilo la Amkeni! ndilo tamko zuri zaidi la shukrani ambalo nimewahi kupokea. Litanitia moyo kwa muda mrefu!

J. D., Jamhuri ya Cheki

Asanteni kwa mfululizo huo. Nimekuwa muuguzi aliyesajiliwa kwa miaka mingi. Mimi huwahurumia sana wagonjwa hivi kwamba ninapowatia dawa ya matone machoni, mimi hutokwa na machozi. Nina hakika kwamba wauguzi ulimwenguni pote watafurahia gazeti hilo la Amkeni!

L.A.R., Marekani

Meno ya Vitoto Kazi yangu katika ofisi ya daktari wa meno hutia ndani kuwafundisha akina mama jinsi ya kutunza meno ya vitoto vyao. Makala “Kuyalinda Meno Dhaifu” (Novemba 22, 2000) imenisaidia sana kwa sababu inaeleza hatari za meno kuoza kwa sababu ya bakteria na vitu vinavyochachuka. Sasa akina mama wote wanaoniomba mawaidha hupata nakala moja, na matokeo yamekuwa mazuri sana!

T.C.S., Brazili

Miguu Isiyotulia Nimetoka tu kusoma makala yenu “Je Una Miguu Isiyotulia?” (Novemba 22, 2000) Nimeteseka kwa miaka 18 kwa sababu ya tatizo hilo, na nilifikiri kuwa ni mimi tu ninayeumia. Nimelia mara nyingi kwa sababu ya kuvunjika moyo na kukosa usingizi, na nimetumia dawa za kila aina. Bila shaka, suluhisho kamili ni Ufalme wa Yehova tu.

S. T., Scotland

Niliposoma makala hiyo, nilishangaa kwa kuwa ilieleza kabisa dalili nilizokuwa nazo. Ijapokuwa hali yangu haijatambuliwa rasmi kuwa Ugonjwa wa Miguu Isiyotulia, nimefarijiwa baada ya kujua kwamba wengine wanavumilia tatizo hilohilo. Sasa ninajifunza namna ya kustahimili vyema zaidi tatizo hilo kuliko zamani. Kwa sababu sasa ninajua namna ya kushughulikia hisia hizo zisizopendeza, ninahisi vizuri zaidi.

A. K., Japani

Nina umri wa miaka 43 na bado mimi huamka usiku kwa sababu ya kuhisi mitambao hiyo kwenye miguu na mikono yangu. Kabla ya kusoma makala hiyo, nilifikiri kuwa ni mimi tu niliyekuwa katika hali hiyo. Sikujua kuwa wengine wanateseka sana kama mimi. Asanteni sana kwa kuchapisha makala kama hizo ili kuwafahamisha wengine kuhusu hali hizo zisizojulikana sana.

D. L., Kanada