Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Miti ya Yew Katika Maeneo ya Makaburi Huko Uingereza

Miti ya Yew Katika Maeneo ya Makaburi Huko Uingereza

Miti ya Yew Katika Maeneo ya Makaburi Huko Uingereza

Na Mwandishi Wa Amkeni! Nchini Uingereza

MNAMO mwaka wa 1656, kasisi mmoja wa Kanisa la Anglikana aliandika hivi: ‘Babu zetu walihifadhi kwa uangalifu sana miti aina ya Yew katika maeneo ya makaburi ya makanisa, kwa sababu ilionwa kuwa mifano mizuri ya kutoweza kufa kwa nafsi kwa sababu majani yake yalidumu mwaka mzima bila kunyauka.’ Mapokeo yasema hivyo. Lakini, je, hivyo ndivyo ilivyo?

Kuhusisha mimea yenye majani yasiyonyauka na kutokufa kwa nafsi ni dhana iliyoanza zamani za kale. Huko Wales mti wa yew ulionwa kuwa mfano wa kutokufa kwa nafsi kulingana na imani na desturi za Druid. (Hao Druid walikuwa makasisi-wachawi Waselti) Huko Uingereza, miti hiyo ilipandwa kwenye mahekalu ya wapagani muda mrefu kabla ya enzi ya Ukristo, na hatimaye ikawa “mfano mtakatifu” wa kanisa. Ijapokuwa wale wasiofuata kanisa hawakuendeleza desturi hiyo, bado miti hiyo hupandwa kwenye maeneo ya makaburi ya kisasa huko Uingereza.

Biblia inasema nini kuhusu kutokufa kwa nafsi? Biblia haihusishi kamwe neno “kutokufa” na neno “nafsi.” Katika hotuba yenye kichwa “Uelewevu wa Kanisa Juu ya Maisha na Kifo,”Askofu Mkuu wa York huko Uingereza alionyesha tofauti kati ya “mawazo yasiyo kamili juu ya jinsi ambavyo nafsi hutoka katika mwili” na kweli ya Biblia. “Hakuna chochote ambacho hutoka kwa njia fulani katika miili yetu tunapokufa,” akasema.

Yew Ni Mti wa Aina Gani?

Mti aina ya yew wa Uingereza [Taxus baccata] ni mti wenye majani ya sindano yasiyonyauka, unaokua polepole na kufikia urefu wa meta 10 hivi. Miti mingi mikubwa sana huko Uingereza ni miti miwili au mitatu iliyounganika pamoja na kufunikwa na maganda hivi kwamba ikawa mti mmoja tu. Imegunduliwa kwamba mti mmoja wa yew huko Scotland ambao una mzingo wa meta 17, ni miti miwili ambayo imeungana kwa njia hiyo.

Miti hiyo inaweza kudumu kwa mamia ya miaka, hata kwa maelfu ya miaka kulingana na vitabu kadhaa. Miti mingi ya kale ya yew huko Uingereza ilikua katika vijiji vya Enzi za Kati, na sasa vijiji hivyo haviko tena lakini miti hiyo imedumu na vijiji vipya vimejengwa katika mazingira yake.

Mbegu zilizokomaa za mti huo zina utando laini mwekundu wenye umbo la kikombe. Lakini mbegu hizo zina sumu, kama vile majani yake ya sindano na ganda la mti huo. Wanyama wanaofugwa wanaweza kufa wakiruhusiwa kulisha karibu na miti hiyo na kula majani na mbegu zake. Zamani watu waliamini kwamba mtu wa familia angekufa ikiwa nyumba ingepambwa kwa mti huo.

Mbao ya yew ina nyuzinyuzi nyembamba, nayo hufanana na mkangazi. Mbao ya sehemu ya ndani ya mti huo ina rangi ya manjano iliyoiva na hutumiwa kutengenezea vyombo vya nyumbani vyenye kudumu. Mbao hizo nyumbufu na zenye nguvu zilitumiwa kutengenezea nyuta katika Enzi za Kati. Wapiga mishale Waingereza walitumia kwa stadi sana nyuta hizo vitani.

Huko Uingereza na vilevile katika eneo la Normandy, lililotawaliwa na Uingereza zamani, ni jambo la kawaida kuona miti ya yew katika maeneo ya makaburi ya makanisa ya kale. Katika eneo la makaburi la kanisa moja huko Uingereza kuna miti 99 ya aina hiyo, lakini hilo si jambo la kawaida. Mara nyingi miti miwili ilipandwa katika eneo la kaburi. Mmoja ulipandwa kwenye lango la eneo la makaburi na ule mwingine karibu na mlango wa kanisa. Siku hizi, huenda ukaona safu mbili ya miti aina ya yew ya Ireland iliyopunguzwa matawi, ambayo imepandwa kandokando ya njia inayoanzia kwenye lango la makaburi na kuelekea hadi mlango wa kanisa, na miti mingine karibu na makaburi yenyewe.

Hata hivyo, fundisho la kutokufa kwa nafsi ni fundisho la kipagani la Ugiriki ambalo linahusisha mafundisho ya Plato. Zawadi ya Mungu kwa wanadamu ni ufufuo wa wafu na tumaini la kuishi milele duniani, wakati ambapo kifo hakitakuwapo tena.—Yohana 5:28, 29; Ufunuo 21:4.

[Picha katika ukurasa wa 31]

Mti aina ya “yew” wenye umri wa miaka 1,000 katika eneo la makaburi la kanisa la St. Andrew, Totteridge, Hertfordshire

[Picha katika ukurasa wa 31]

Kulia: Utando wenye rangi nyangavu—lakini mbegu ni zenye sumu

Kulia kabisa: Miti aina ya “yew” ya Ireland iliyopunguzwa matawi katika eneo la makaburi la kanisa la St. Lawrence, Little Stanmore, Middlesex