Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maporomoko ya Maji ya Niagara Yalinistaajabisha

Maporomoko ya Maji ya Niagara Yalinistaajabisha

Maporomoko ya Maji ya Niagara Yalinistaajabisha

HIVI karibuni nilipata fursa ya kuyatazama Maporomoko ya Maji ya Niagara nikiwa karibu sana. Sijawahi kuyatazama nikiwa karibu hivyo. Nawahakikishia kuwa ilikuwa pindi yenye kustaajabisha. Mimi na rafiki zangu tulitembelea Maporomoko ya Maji ya Horseshoe huko Kanada. Tangu nilipotembea huko mara ya kwanza mnamo mwaka wa 1958, nimewahi kurudi tena mara kadhaa. Lakini kuna jambo moja ambalo sikuwahi kufanya—sikuwahi kamwe kusafiri kwenye mto kwa kutumia mashua ili kuyakaribia sana maporomoko hayo ya maji. Hata hivyo, watu wamekuwa wakifanya hivyo tangu mashua zinazoitwa Maid of the Mist zilipoanza kutumiwa kuwasafirisha watalii mnamo mwaka wa 1848. Mamilioni ya watu wamefunga safari hiyo yenye kusisimua. Sasa ilikuwa zamu yangu.

Mashua huanza safari kwa ukawaida kutoka pande zote mbili za mto, upande wa Marekani na vilevile upande wa Kanada. Foleni haziishi. Tuliwaona watu wa umri mbalimbali, hata watoto wadogo, wakiwa wamevaa makoti mepesi ya mvua ya rangi ya samawati ambayo yanawakinga na rasharasha. (Wale wanaotembelea Maporomoko ya Maji ya American kwenye upande ule mwingine, huvaa makoti ya rangi ya manjano.) Mashua inayoitwa Maid of the Mist ya Saba, yaweza kubeba abiria 582. Mashua hiyo ina uzito wa tani 132, urefu wa meta 24 na upana wa meta 9. Kwa sasa kuna mashua nne zinazotumiwa, mashua ya Maid of the Mist ya Nne, ya Tano, ya Sita, na ya Saba.

Zamu Yetu ya Kulowa

Tulipanga foleni pamoja na umati wa watu. Mara tu abiria waliokuwa wamelowa chepechepe waliposhuka kutoka kwenye mashua ya Maid of the Mist ya Saba, tuliingia kwenye mashua hiyo. Nilijua kuwa safari yetu ingesisimua. Kilometa moja hivi mbele yetu, maji yalikuwa yakiporomoka kwa kishindo kwa zaidi ya meta 52 kutoka kwenye ncha ya maporomoko hayo na kuingia ndani ya bonde la mto lenye kina cha meta 55. Mashua yetu ilisonga mbele mtoni na kufika upande wa Marekani ambapo tulipenya kwa nguvu mawimbi yaliyo chini ya Maporomoko ya Maji ya American. Maji hayo huporomoka kwa jumla ya meta 54. * Sehemu yenye kupendeza zaidi ilikuwa ingali mbele yetu.

Wasiwasi uliongezeka tulipozidi kukaribia maporomoko hayo ya maji. Punde si punde, ikawa vigumu kupiga picha kwa sababu ya upepo na rasharasha. Ilionekana ni kana kwamba nahodha wa mashua hiyo alichukua mwaka mzima kusogeza mashua hiyo karibu na mahala ambapo maji ya meta mchemraba 168,000 huporomoka kila dakika na kuanguka kwenye sehemu ya chini ya maporomoko, mbele tu ya mashua! Kulikuwa na kishindo kikubwa. Hata hungeweza kujisikia ukipiga kelele. Moyo wangu ulipigapiga kwa nguvu. Maji ya Niagara yaliyo baridi lakini safi yaliingia kinywani mwangu. Pasipo shaka, hilo lilikuwa tukio bora zaidi maishani mwangu!

Mwishowe, nahodha wetu aliondoa mashua yetu ya Maid polepole kutoka kwenye sehemu hiyo hatari na kuiongoza kulingana na uelekeo wa mto. Nilipumua. Tulikuwa tumefaulu. Lakini hatukuwa na shaka yoyote kuhusu jambo hilo. Kampuni inayoendesha mashua hizo ina sifa nzuri ya kutopata aksidenti. Emil Bende, meneja mkuu wa kampuni hiyo ya mashua zinazotumia mvuke, alituhakikishia kwamba kila mashua ina majaketi ya kuokolea na vyelezo vinavyotosha idadi kamili ya abiria katika mashua. Hatuwezi kurudia makosa yaliyosababisha meli ya Titanic kuzama!

Maporomoko ya Maji Yanarudi Nyuma!

Naam, mmomonyoko umeathiri maporomoko hayo ya maji. Inakadiriwa kuwa katika kipindi cha miaka 12,000 iliyopita, maporomoko ya Niagara yamerudi nyuma kwa kilometa 11 kufikia mahala yalipo sasa. Kuna wakati ambapo mmomonyoko uliyarudisha maji nyuma kwa meta moja kila mwaka. Sasa mmomonyoko umepungua na unayarudisha maji nyuma kwa sentimeta 36 kila miaka kumi. Ni nini kinachosababisha mmomonyoko huo?

Maji hupita kwenye tabaka gumu la juu la mawe ya chokaa ya marumaru. Tabaka hilo huwa juu ya matabaka ya mawe-mchanga laini na mwambatope. Matabaka hayo ya chini humomonyoka na mawe ya chokaa huvunjika na kuanguka ndani ya bonde la mto.

Maji Hayapotei Bure

Maji yanayotiririka kwenye Mto mfupi wa Niagara (wenye urefu wa kilometa 56) hutoka kwenye Maziwa Makuu manne kati ya yale matano. Mto huo hutiririka kuelekea upande wa kaskazini kutoka Ziwa Erie hadi Ziwa Ontario. Mto huo unapotiririka kati ya maziwa hayo, unatumiwa kutokeza nguvu za umeme zinazotumiwa na Kanada na Marekani. Mto huo husemekana kuwa mojawapo ya vyanzo vikuu vya nguvu za umeme ulimwenguni. Mitambo ya Kanada na Marekani ya kutokeza nguvu za umeme hutokeza kilowati 4,200,000. Maji yanayoendesha injini za mitambo hutolewa kwenye Mto Niagara kabla mto huo haujafika kwenye maporomoko ya maji.

Fungate na Taa Zinazowaka Usiku

Wenzi wengi walio kwenye fungate hupenda kufika kwenye Maporomoko ya Maji ya Niagara. Jambo hilo lilianza kuonekana sana baada ya filamu ya Niagara ya mwaka wa 1953. Wakati wa usiku maporomoko hayo ya maji humulikwa kwa taa zenye rangi zinazoongeza uzuri na fahari ya sehemu hiyo ya pekee duniani. Bila shaka, safari yako ya Kanada na Marekani haiwezi kuwa kamili bila kutembelea sehemu hiyo ya ajabu duniani. Na ikiwa unapenda kujasiria mambo, usisahau kusafiri kwa mashua! Hutajuta kamwe wala hutasahau pindi hiyo.—Imechangwa.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 “Kwenye Maporomoko ya Maji ya American, maji huporomoka kwa meta 21 hadi 34 (futi 70 hadi 110) mpaka kwenye [mi]amba iliyo chini ya maporomoko hayo.”—Ontario’s Niagara Parks.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]

KIGARI CHA WAYA CHA MHISPANIA CHA NIAGARA

Kilometa 4.5 kutoka kwenye maporomoko ya maji, kuna dimbwi la maji yanayozunguka haraka ‘lililofanyizwa chini ya Maporomoko, mahala ambapo lile Korongo Kubwa (Great Gorge) hujipinda kuelekea kaskazini-mashariki. Maji hayo ya rangi ya kijani inayong’aa huzunguka-zunguka ili kupita kwenye mtaro mwembamba kwenye korongo hilo.’—Ontario’s Niagara Parks.

Njia nzuri ya kuona ukubwa wa dimbwi hilo la ajabu ni kutumia Kigari cha Waya cha Mhispania cha Niagara. Kigari hicho kinachoning’inia kwenye waya huvuka juu ya dimbwi hilo na kinamwezesha mtu kuona mandhari za kuvutia za mto, mahala mkondo wa maji unakotoka na unakoelekea. Lakini kwa nini kinaitwa Kigari cha Waya cha “Mhispania”? Kilibuniwa na kuundwa na mhandisi Mhispania, aliyeitwa Leonardo Torres Quevedo (1852-1936), na kimetumiwa tangu mwaka wa 1916. Ni kigari kisicho na kifani.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 26]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

MMOMONYOKO umesababisha maporomoko ya maji kurudi nyuma kwa meta 300 au zaidi tangu mwaka wa 1678

1678

1764

1819

1842

1886

1996

[Hisani]

Kutoka kwa: Niagara Parks Commission

[Ramani katika ukurasa wa 27]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

KANADA

MAREKANI

KANADA

MAREKANI

Ziwa Erie

Maporomoko ya Maji ya Niagara

Mto Niagara

Ziwa Ontario

[Picha katika ukurasa wa 25]

Maporomoko ya Maji ya American

Maporomoko ya Maji ya Horseshoe huko Kanada

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mandhari ya maporomoko hayo ya maji katika majira ya baridi kali yanapomulikwa kwa taa usiku