Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Wanawake Milioni 79 “Wametoweka”

Uchunguzi uliotegemezwa na UM kuhusu “India, Pakistan, Bangladesh, Nepal, Sri Lanka, Bhutan na Visiwa vya Maldives ulisema kwamba wanawake milioni 79 ‘wametoweka katika Asia Kusini’ kwa sababu ya ubaguzi dhidi ya wanawake, kabla na baada ya kuzaliwa,” yasema ripoti ya shirika la habari la Reuters. Wanawake “wametoweka” kwa sababu ya utoaji-mimba na vilevile “kuuawa kwa watoto wachanga na kupendelewa kwa watoto wa kiume katika eneo hilo wakati wa kugawa chakula.” Watoto wa kiume hupendelewa hata wanapokuwa watu wazima, hivyo watoto wa kike wanapata matatizo mabaya ya kukosa lishe. Kuna “idadi kubwa ya vifo vya wasichana na wanawake walio katika umri wa kupata watoto,” ikasema ripoti hiyo. Takwimu hiyo ya milioni 79 ilitegemea uwiano wa wanawake 94 tu kwa wanaume 100 katika eneo hilo, ilhali uwiano wa ulimwenguni kote ni wanawake 106 kwa wanaume 100.

Barabara Ndefu Zaidi ya Chini ya Ardhi Yafunguliwa

Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung laripoti kwamba barabara ndefu zaidi ya chini ya ardhi ilifunguliwa nchini Norway. Barabara ya Chini ya Ardhi ya Laerdal ina urefu wa kilometa 24.5 na huunganisha majiji makuu mawili ya Norway, Oslo na Bergen. Awali, madereva walikuwa wakichagua kutumia ama barabara yenye kujipinda-pinda ya mlimani au kusafiri kwa kutumia feri inayovuka kivuko cha bahari. Usalama umezingatiwa sana katika njia hiyo mpya ya chini ya ardhi. Ina nafasi ya kutosha kuruhusu magari kugeuka baada ya kila meta 500, feni kubwa zisizoweza kushika moto zinazoweza kuondoa moshi na gesi zenye sumu kupitia mtaimbo wa kuingiza hewa, na mifumo ya hali ya juu ya wakati wa dharura. Kwa sababu watu wengi huogopa barabara ndefu za chini ya ardhi, maegesho makubwa yamegawanya Barabara ya Chini ya Ardhi ya Laerdal katika sehemu nne. Kuta za maegesho hayo zinamulikwa kwa taa za samawati ili kutokeza mandhari ya mwangaza wa mchana na hewa safi. Hata hivyo, uchunguzi ulionyesha kwamba asilimia 25 ya wenyeji wa Norway hawatatumia barabara hiyo ya chini ya ardhi kwa sababu ya kuogopa aksidenti au moto.

Wanyama Walio Hatarini Wanarudi Israel

Makala moja katika gazeti la Israel la Haaretz ilisema kwamba wanyama wengi waliotoweka Israel wameanza kurudi. Mbweha na makundi ya mbwa mwitu yamerudi Negeb na kwenye eneo la Golan Heights. Walipohesabiwa mara ya mwisho, idadi ya tai kaskazini mwa Israel ilikuwa imeongezeka kufikia tai 450. Hata chui ameonekana huko Galilee. Iliaminika kuwa chui wametoweka katika eneo hilo, na mbweha walikuwa hatarini. Lakini sasa wanyama hao wawindaji wamerudi na vilevile wanyama wanaowindwa kama swara, mbuzi-mwitu, na kulungu. Ingawa wanyama fulani wamerudi wenyewe, wengine wamerudishwa kwenye makao yao ya zamani. Wanyama waliorudishwa ni kutia ndani punda-mwitu. Sasa zaidi ya punda-mwitu 100 wanaishi Negeb.

Kuna Faida Nyingi Zaidi za Kunyonyesha Mtoto

“Je, unataka kuongeza uwezo wa akili wa mtoto wako mchanga?” lauliza gazeti la Psychology Today. “Yaweza kuwa rahisi sana kama kuchagua maziwa ya matiti badala ya maziwa ya watoto ya dukani.” Yaonekana asidi mbili zenye mafuta zinazopatikana katika maziwa ya matiti, yaani, asidi ya docosahexaenoic (DHA) na asidi ya arachidonic (AA) hutokeza tofauti katika ustawi wa mfumo wa neva. Majaribio yalionyesha kuwa “watoto wanaotumia DHA na AA walifanya vema kuliko wengine kwa habari ya kukumbuka mambo, kutatua matatizo na kusitawisha ustadi wa lugha,” lasema gazeti hilo. Hiyo inaonyesha kwamba maziwa ya matiti ndiyo bora zaidi.

“Uchunguzi unafunua ni kwa nini watu hupenda sana vyakula vya jamii yao,” lasema gazeti la Science. “Wanawake waliokunywa maji ya karoti walipokuwa wajawazito au walipokuwa wakinyonyesha waliwafanya watoto wao kupenda karoti. . . . Uchunguzi huo waonyesha kwamba kutumia maziwa ya matiti ni bora kuliko kutumia maziwa ya watoto ya dukani, kwa sababu huwafanya watoto wakubali vyakula vipya” na huwafundisha “vyakula vilivyo salama—hiyo ikionyesha umuhimu wa akina mama wajawazito na wale wanaonyonyesha kupata lishe yenye afya.”

Kazi Nzuri Bado Inatamaniwa

“Kazi Nzuri kwa Ajili ya Watu Wote—Bado Inatamaniwa,” ndicho kilichokuwa kichwa kimoja cha habari cha gazeti la Ujerumani la Hannoversche Allgemeine Zeitung. Gazeti hilo lilikuwa likiripoti juu ya kongamano la “Mazungumzo ya Ulimwenguni Kote,” lililofanywa kwenye maonyesho ya ulimwengu ya EXPO 2000 huko Hannover. Ingawa sheria ya kuwapa wanaume na wanawake kazi sawa na kuwalipa mshahara sawa iliwekwa mwaka wa 1951 na kuwaajiri watoto kukapigwa marufuku mwaka wa 1973, watu milioni 150 ulimwenguni kote hawana kazi, milioni 850 hawalipwi mshahara wa kutosha, na watoto 250 milioni wanalazimika kufanya kazi. Nusu ya idadi ya watu ulimwenguni hupata mshahara usiozidi dola mbili za Marekani kwa siku. Na licha ya jitihada nyingi, pengo kati ya matajiri na maskini limezidi kupanuka badala ya kupungua. Pia, mahangaiko ya nchi tajiri yanatofautiana sana na yale ya nchi maskini. Wanasiasa wa nchi za Ulaya huzungumzia mipango ya haki za ununuzi wa bidhaa na uvutano wa vyama vya wafanyakazi, ilhali wanasiasa wenzao katika nchi zinazositawi huzungumzia mambo ya msingi, kama elimu ya msingi kwa ajili ya wote na jinsi ya kutokeza kazi kwa ajili ya kizazi kinachokua.

Masada Hatarini?

“Masada haipaswi kuanguka tena!” ni usemi uliowachochea Wayahudi walipokuwa wakijenga taifa la kisasa la Israel. “Lakini Masada yaweza kuanguka tena kwa sababu ya hali za asili,” yasema ripoti moja ya habari ya shirika la televisheni la NBC. Sehemu hiyo inayopendwa na watalii “iko karibu na mojawapo ya nyufa zinazopanuka haraka zaidi duniani: Bonde la Ufa la Bahari ya Chumvi.” Majabali ya mlima huo yamevunjika-vunjika katika visehemu vingi. Visehemu vingine vyaweza kuangushwa na tetemeko la ardhi. Kwa kweli, uchanganuzi wa kompyuta waonyesha kwamba majabali fulani upande wa mashariki unaoitwa Snake Path yalikuwa karibu kuanguka, na tayari yameimarishwa kwa fito za chuma zenye urefu wa meta 18. Hata hivyo, mabaki ya kasri iliyojengwa na Mfalme Herode kwenye upande wa kaskazini wa Masada “yako juu ya eneo linalotikisika” na yanahitaji kuimarishwa. Kufikia sasa, sehemu hiyo haijaanza kurekebishwa kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Ilikuwa katika Masada, kilometa 100 kutoka Yerusalemu, ambapo kikundi cha Wayahudi waasi 967 kilihimili upinzani mkali kwa miaka miwili kilipozingirwa na jeshi la Waroma miaka 2,000 hivi iliyopita. Usiku uliotangulia siku ambayo Waroma walivunja ngome yao, yasemekana kwamba Wayahudi waliamua kujiua badala ya kusalimu amri.

Jihadhari na Jua

Kukaa kwa muda mrefu katika jua bila kinga ya kutosha kwaweza kusababisha kansa ya ngozi, yasema makala moja katika gazeti la El Universal la Mexico. Kulingana na daktari wa ngozi Adriana Anides Fonseca, mnururisho wa jua husababisha athari inayodumu ambayo kwa kawaida hutokeza ugonjwa hatari mtu afikiapo umri wa miaka 50. Anapendekeza kutumia krimu inayolinda ngozi dhidi ya miale ya jua dakika 30 kabla ya kujianika juani na kujipaka tena krimu hiyo kila saa tatu au nne baada ya kuingia majini, au unapotokwa jasho sana. Watu weupe wanahitaji krimu ya kiwango cha nguvu kinachozidi namba 30 au 40; na watu weusi wanahitaji ya kiwango cha namba 15 hadi 30. Hata hivyo, yapasa kukumbukwa kuwa krimu inayolinda ngozi dhidi ya miale ya jua haizuii ngozi kabisa isiharibiwe na mnururisho. Pia, losheni za kubadili rangi ya ngozi zaweza kufanya mambo yawe mabaya zaidi kwa kusababisha majeraha ya kuungua ndani sana ngozini. Watoto wanahitaji utunzaji wa kipekee ili kuwalinda dhidi ya kuchomwa na jua moja kwa moja, kwa kuwa mifumo yao ya kukinga ngozi dhidi ya miale ya jua haijasitawi kabisa.

Upendezi wa Kuwa Padri Umekwisha

Wazazi Wakatoliki “hawaoni tena ni fahari kusema ‘mwanangu ni padri,’” lasema gazeti la The New York Times. ‘Viongozi Wakatoliki wanajua kwamba upungufu wa mapadri umesababishwa hasa na idadi kubwa ya wazazi Wakatoliki ambao hawataki kuwatia moyo watoto wao wafikirie kufanya kazi ya upadri.’ Mojawapo ya sababu zilizotolewa ni kwamba katika familia za Kikatoliki zenye watoto wachache, ‘ni vigumu kukubali mwana wa pekee kuwa mmoja wa mapadri wasiooa,’ makala hiyo ilisema. “Kwa kuongezea, wazazi walipohojiwa walisema kwamba cheo cha upadri kimeshushwa katika mwongo uliopita kwa sababu ya ripoti nyingi kuhusu mapadri wanaowatendea vibaya watoto.” Uchunguzi kuhusu Wakatoliki wanaojihusisha sana katika dini, ulioagizwa na Kongamano la Kitaifa la Maaskofu Wakatoliki, ulifunua kwamba theluthi mbili ya wazazi hawawezi kuwatia moyo watoto wao kuwa mapadri au watawa wa kike. Edward J. Burns, ambaye ni padri na mwakilishi wa kikundi hicho, asema kwamba kwenye kikusanyiko cha familia, wenzi wawili wasiofunga ndoa hawatashutumiwa wakisema kuwa wanaishi pamoja. Hata hivyo, kijana anayefikiria kuwa padri ataulizwa na washiriki wa familia, “Je, una hakika unajua kile unachofanya?”