Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ni Nani Wanaotumia Dawa za Kulevya?

Ni Nani Wanaotumia Dawa za Kulevya?

Ni Nani Wanaotumia Dawa za Kulevya?

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AFRIKA KUSINI

“KILA mtu hutumia dawa za kulevya.” Usemi huo wa kawaida unaweza kuwashawishi wale wasio na busara waonje dawa haramu za kulevya. Ikitegemea jinsi tunavyoelewa neno “dawa za kulevya,” usemi huo ni wa kweli kwa kadiri fulani.

Neno “dawa za kulevya” linafafanuliwa kuwa: “Kitu chochote chenye kemikali, kiwe ni cha asili au cha sanisia, ambacho kinaweza kuvuruga uwezo wa kufikiri, hisia au hali nyingine za kisaikolojia.” Ufafanuzi huo muhimu sana hutumiwa na wengi kurejezea dawa zinazoathiri uwezo wa kufikiri ingawa hauhusu dawa nyingi za matibabu.

Kupatana na ufafanuzi huo, pombe ni dawa ya kulevya. Hatari huzuka watu wanapokunywa pombe kupita kiasi. Ni wazi kwamba tatizo hilo linaongezeka. Uchunguzi mmoja uliofanywa katika vyuo na vyuo vikuu katika nchi moja ya Ulaya ulifunua kwamba “sherehe za ulevi ni tatizo kubwa sana katika vyuo hivyo.” Uchunguzi huo ulifunua kwamba asilimia 44 ya wanafunzi ni walevi. *

Kama pombe, sigareti imeidhinishwa kisheria ijapokuwa ina sumu kali sana ya nikotini. Shirika la Afya Ulimwenguni, linasema kwamba watu wapatao milioni nne hufa kila mwaka kwa sababu ya uvutaji wa sigareti. Lakini, wauzaji mashuhuri wa sigareti ni watu matajiri wanaoheshimiwa katika jamii. Uvutaji wa sigareti husababisha uraibu, labda hata kuliko dawa nyingi haramu za kulevya.

Katika miaka ya karibuni, nchi nyingi zimepiga marufuku matangazo ya sigareti na kuweka vizuizi vingine. Lakini watu wengi wanaona kuvuta sigareti kuwa jambo linalokubaliwa na jamii. Watayarishaji wa sinema hutukuza uvutaji wa sigareti kana kwamba ni jambo zuri sana. Uchunguzi mmoja uliofanywa na Chuo Kikuu cha California huko San Francisco kuhusu sinema zilizovuma sana kati ya mwaka wa 1991 na 1996, ulifunua kwamba asilimia 80 ya waigizaji wakuu wa sinema hizo walionyeshwa wakivuta sigareti.

Vipi Kuhusu Dawa “Zisizodhuru”?

Bila shaka dawa za kitiba zimewasaidia watu wengi, lakini zinaweza kutumiwa vibaya. Nyakati nyingine madaktari huwapa wagonjwa dawa ovyoovyo, au wanashurutishwa na wagonjwa kuwapa dawa zisizohitajiwa. Daktari mmoja alisema hivi: “Mara nyingi madaktari hawachanganui kisababishi cha ugonjwa. Ni rahisi kusema, ‘Meza kidonge hiki.’ Lakini kisababishi cha ugonjwa hakishughulikiwi.”

Hata dawa zinazotumiwa bila maagizo ya daktari, kama vile aspirini na paracetamol (Tylenol, Panadol), zinaweza kuwa hatari sana kwa afya zikitumiwa vibaya. Zaidi ya watu 2,000 ulimwenguni pote hufa kila mwaka kwa sababu ya kutumia vibaya dawa ya paracetamol.

Kulingana na ufafanuzi wetu wa awali, kemikali ya kafeini iliyo katika chai na kahawa ni dawa ya kulevya pia, ingawa hatufikiri hivyo tunapokunywa chai au kahawa tunayopenda wakati wa kiamsha-kinywa. Na haingefaa kulinganisha vinywaji vinavyokubaliwa kama chai au kahawa na dawa kali za kulevya kama heroini. Kufanya hivyo kungekuwa kama kulinganisha kitoto cha paka na simba mkali. Hata hivyo, wataalamu fulani wa afya wanasema kwamba ukizoea kunywa zaidi ya vikombe vitano vya kahawa au vikombe tisa vya chai kwa siku, unaweza kupata madhara. Isitoshe, ukipunguza ghafula kiasi kikubwa unachokunywa, unaweza kusumbuliwa na dalili za kuacha kama zile zilizompata mnywaji mmoja wa chai. Alianza kutapika, kupata maumivu makali ya kichwa, na kuathiriwa na mwangaza.

Vipi Kuhusu Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya?

Jambo ambalo limezusha ubishi mkali zaidi ni matumizi ya dawa za kulevya michezoni. Jambo hilo lilitukia katika mashindano ya baiskeli ya Tour de France mwaka wa 1998, wakati waendeshaji tisa wa baiskeli wa timu iliyokuwa ikiongoza walipofukuzwa mashindanoni kwa sababu ya kutumia dawa zinazoongeza nguvu mwilini. Wanariadha wamebuni njia mbalimbali za kuepuka kunaswa wakati wanapopimwa kuhusiana na matumizi ya dawa za kulevya. Gazeti Time laripoti kwamba baadhi ya wanariadha hata huenda “‘kutiwa mkojo wa mtu mwingine,’ yaani mkojo ‘usio na dawa za kulevya’ hutiwa kwenye kibofu chao kupitia kifaa maalumu kiitwacho katheta. Kwa kawaida mtu huhisi maumivu makali sana.”

Bado hatujazungumzia aina mbalimbali za dawa haramu za kulevya zinazotumiwa kama “kiburudisho.” Zatia ndani bangi, ecstasy (methylenedioxy-methamphetamine, au MDMA), LSD (lysergic acid diethylamide), dawa zinazochochea utendaji wa mwili kama vile kokeini na amphetamines, dawa zinazopumbaza akili (za kutuliza wasiwasi), na heroini. Hatupaswi pia kusahau zoea linalopendwa na vijana wengi la kupumua mvuke wa gundi na petroli. Bila shaka, bidhaa hizo zenye mvuke hazijapigwa marufuku na zinapatikana kwa urahisi.

Maoni ya kawaida ya kwamba waraibu wa dawa za kulevya walionyong’onyea hujifungia katika chumba kichafu na kujidunga mishipani sindano zenye dawa za kulevya huenda yasiwe sahihi. Waraibu wengi wa dawa za kulevya huishi maisha ya kawaida tu, ijapokuwa uraibu wao huathiri maisha yao kwa kadiri fulani. Hata hivyo, hatuwezi kupuuza hatari ya dawa za kulevya. Mwandishi mmoja aeleza kwamba watumiaji fulani wa kokeini “wanaweza kujidunga sindano nyingi sana za kokeini kwa muda mfupi tu, kiasi cha kwamba mwili wao unajaa majeraha mengi sana ya sindano yanayovuja damu.”

Matumizi haramu ya dawa za kulevya yalipungua sana mwishoni mwa miaka ya 1980, lakini sasa yanaongezeka tena ulimwenguni pote. Gazeti la Newsweek lilisema hivi: “Wenye mamlaka hawajui la kufanya kwa sababu ya kuenea sana kwa ulanguzi na matumizi ya dawa mbalimbali za kulevya. Hawana pesa—wala habari—za kupambana na ulanguzi na matumizi ya dawa hizo za kulevya.” Gazeti la The Star la Johannesburg, Afrika Kusini, lilisema kwamba takwimu za serikali zinaonyesha kwamba “mkazi mmoja kati ya kila wakazi wanne wa Afrika Kusini ni mraibu wa pombe au wa dawa za kulevya.”

Taasisi ya UM ya Utafiti wa Maendeleo ya Kijamii ilisema kwamba “watengenezaji na walanguzi wa dawa za kulevya . . . wametapakaa ulimwenguni pote nao hurundika katika mabenki pesa nyingi wanazopata kutokana na biashara ya dawa hizo. Wao huchagua mabenki yanayotoa huduma za siri ambayo hulipa faida kubwa sana. . . . Hivi sasa walanguzi wa dawa za kulevya wanaweza kuhalalisha pesa wanazopata kwa njia haramu kwa kuhamisha pesa hizo kwenye mabenki mengineyo ulimwenguni kupitia mifumo ya kompyuta bila kudhibitiwa na serikali.”

Yamkini Wamarekani wengi hugusa kokeini kila siku pasipo kujua. Makala moja katika gazeti Discover ilieleza kwamba noti nyingi za mabenki ya Marekani zina madoa ya kokeini.

Ukweli ni kwamba watu wengi wanakubali na hata wanaona utumizi wa dawa za kitiba na hata dawa haramu za kulevya kuwa jambo la kawaida tu. Tuzingatiapo athari zinazotangazwa kote za dawa haramu za kulevya, sigareti na pombe, swali lifaalo ni, Kwa nini watu hutumia dawa za kulevya? Tunapotafakari swali hilo, inafaa pia kuchunguza maoni yetu wenyewe kuhusu dawa hizo za kulevya.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Ulevi ulifafanuliwa kuwa ‘kunywa chupa tano au zaidi za pombe kwa wanaume, na chupa nne au zaidi kwa wanawake.’

[Picha katika ukurasa wa 3]

Sherehe za ulevi ni tatizo kubwa sana katika vyuo vingi

[Picha katika ukurasa wa 5]

Watu wengi hudhani sigareti na dawa za kulevya “za kujiburudisha” hazina madhara